Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Aloyce John Kamamba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buyungu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ALOYCE J. KAMAMBA: Mheshimiwa Naibu Spika, nishukuru kwa nafasi, lakini kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kuchangia katika Bunge lako Tukufu, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kunijalia baraka zake zote na hatimaye kuweza kuchaguliwa, lakini nikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kuniamini, lakini wananchi wa Wilaya ya Kakonko na Jimbo la Buyungu kwa ujumla kwa kunichagua kwa kura nyingi ikiwa ni pamoja na Rais na Madiwani wote wa Chama Cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja nimpongeze Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa anayoifanya ya kukiongoza chama chetu, lakini pia katika miradi mbalimbali anasimamia na nchi kwa ujumla. Vilevile niwapongeze Waheshimiwa Mawaziri ambao wameaminiwa. Wameanza vizuri sisi Wabunge tutaendelea kuwatia shime, ili muweze kufanya vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, miradi mbalimbali imeanzishwa katika nchi yetu ikiwa ni pamoja na Wilaya ya Kakonko. Katika wilaya yetu ipo miradi mbalimbali ya umeme, ipo miradi ya maji, lakini iko hospitali ya wilaya inajengwa, lakini katika uchaguzi uliopita mwaka 2015 Mheshimiwa Rais alitupatia kilometa tatu za Mji wa Kakonko, ujenzi unaendelea. Shida yangu ni ukamilishaji wa miradi inayoendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukichukua mfano stendi ya Mji wa Kakonko ambayo iliahidiwa mwaka 2015; ujenzi umeanza kwa kilometa 0.63, lakini ninavyozungumza ule mji wamekwenda wameujaza kifusi, ujenzi haujakamilika na hakuna kinachopendelea, lakini vilevile kuna stendi ambayo nimeitaja bado fedha zake hatujaweza kuzipata. Wazo la jumla ambalo naliomba ni uletaji wa fedha kwa ajili ya ukamilishaji wa miradi hiyo ikiwa ni pamoja na ufuatiliaji na ubora wa kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, elimu; nishukuru sana kwamba, Mheshimiwa Rais ameweza kuanzisha program ya mpango wa elimu bila malipo. Hii inawalenga watoto wa Watanzania, lakini ambao wanatoka katika familia maskini. Tumefanikiwa vizuri sana watoto wameandikishwa, lakini imeleta changamoto nyingine ya vyumba vya madarasa na uhitaji wa walimu. Tuna shida kubwa sana ya walimu katika shule zetu za msingi na sekondari. Hasa kwa sekondari walimu wa masomo ya sayansi, lakini kwa shule za msingi walimu katika masomo yote. Niombe tunapotekeleza program hii ya mpango wa elimu bila malipo, chonde chonde, walimu waajiriwe ili waweze kujaza kwenye upungufu ambao tunao.

Mheshimiwa Naibu Spika, wanafunzi wanaomaliza darasa la saba wapo wanaofanikiwa kwenda kidato cha kwanza, lakini wapo wanaobaki. Tunao wanafunzi wamemaliza kidato cha nne, hawafanikiwi kwenda kidato cha tano au kwenda kwenye kozi yoyote ile, hawa tunawasaidiaje? Ndio hoja inakuja ya kuwa na vyuo vya VETA. Jana katika swali la msingi liliulizwa, lakini ikatajwa kwamba, vinajengwa vyuo vya VETA. Niombe vyuo hivi vijengwe vingi na kwa haraka kwa lengo la kuwasaidia watoto hawa waweze kupokelewa katika vyuo hivyo wapate mafunzo na kozi mbalimbali ambazo zinawasaidia watoto wetu katika masomo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upangaji wa Walimu. Kuna utaratibu ambao umewekwa, inachukuliwa idadi ya wanafunzi wanagawa kwa idadi ya Walimu, wanafunzi ambao ni 40; utaratibu huo haujibu shida ya Walimu tulionao. Uandaliwe utaratibu maalum tofauti na utaratibu uliopo wa kuangalia jinsi ambavyo walimu wanaweza wakapangwa katika shule zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa kilimo; kilimo ndio uti wa mgongo na wananchi wetu wengi wanategemea kilimo, lakini pembejeo hazifiki kwa wakati. Hiyo inakwenda sambamba na mbolea, lakini Maafisa Ugani. Maafisa Ugani nao hawapo wa kutosheleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Serikali ichukue hatua za makusudi ili nao waweze kuajiriwa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha kwamba, mbolea inapatikana, lakini inapatikana kwa wakati.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna upande wa madini; madini yapo maeneo ambayo yameashabainishwa na uchimbaji unaendelea, lakini kuna maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanagundua madini katika maeneo tofauti tofauti katika nchi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe nayo Serikali ichukue hatua za makusudi pale ambapo imebainika kwamba, kuna madini yamebainishwa, basi utafiti ufanyike na hatua za ziada zichukuliwe ili uchimbaji uweze kufanyika iwe sambamba na maeneo mengine ambayo uchimbaji unafanyika katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa afya; vituo vya afya havitoshelezi. Nikitoa mfano katika wilaya yangu nina vituo vitatu tu Kituo cha Nyamtukuza, lakini Gwanumpu na Kakonko, havitoshelezi na katika kata kumi vituo hivyo havipo. Naomba sana Serikali iweze kuchukua hatua vituo hivyo viweze kujengwa haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana na naunga mkono hoja. (Makofi)