Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Priscus Jacob Tarimo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Moshi Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Nisikitike tu kwamba nilikuwa nimejiandaa kuongea dakika 10 na sasa tumeambiwa ni tano tano, nitajaribu kwenda kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa nafasi hii adhimu ya kuwatumikia Watanzania katika chombo hiki kitukufu cha Bunge.

Nikishukuru chama changu cha Mapinduzi lakini zaidi niwashukuru wazazi wangu baba na mama Tarimo pamoja na familia yangu, mke wangu Eveline na watoto wangu watatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kabla sijaenda mbali niseme tu kwamba naunga mkono hoja kwa asilimia 100. Nasema hivyo nikiwa nimechukua reference ya kwanza kwenye hotuba ile ya Bunge la Kumi na Moja ambayo aliitoa Mheshimiwa Rais hapa na baadaye yale aliyoyafanya kwa miaka mitano ambayo yalisababisha sasa Watanzania kutuelewa na tukapata ushindi wa kishindo kwa mwaka huu wa 2021 kwa Chama cha Mapinduzi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais yako mambo mengi ambayo nataka niyaongelee. Nianze na maslahi ya watumishi wa umma kama yalivyo kwenye ukurasa wa 8 na wa 9 wa hotuba ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli kabisa kwamba watumishi wa umma wamekuwa na malalamiko ya muda mrefu haswa walimu. Wanalalamikia madeni yao ya muda mrefu, kupandishwa kwa madaraja pamoja na mfumo mpya huu ambao umeshakuja lakini hata wastaafu wamekuwa na malalamiko ya kucheleweshewa mafao yao. Naomba Serikali iliangalie suala hili vizuri na kwa sababu liko kwenye hotuba hii basi liweze kushughulikiwa kwa haraka.

Mheshimiwa Naibu Spika, niongelee mikopo ya halmashauri hasa ile asilimia 10 kwa ajili ya akina mama, vijana na walemavu. Niishukuru na kuipongeza Serikali kwa kuamua kuibadilisha sheria ile na kuzifanya fedha zile sasa ni revolving kwa maana ya kwamba fedha zinazokopeshwa sasa zinaweza zikawekwa kwenye mfuko ambao ni revolving fund na kukopeshwa kwa vijana na akina mama wengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina mambo mawili ya kuishauri Serikali kuhusiana na mikopo hii. Wangalie uwezekano wa kukopesha fedha hizi kwa mtu mmoja mmoja na kwa sababu sasa tuna mfumo mzuri kwa kupitia vitambulisho vya NIDA, hata kama ikibidi kuwakopesha vifaa kama bodaboda ili basi ilete tija zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni katika ile sheria iliyobadilishwa na kusema kuwe na mradi wa pamoja. Nakubaliana kabisa na mawazo ya Serikali lakini nishauri pia kukopeshwa kikundi ili wakopeshane kama zamani iendelee kuruhusiwa kwa sababu iliwajenga akina mama wengi katika maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye eneo la viwanda limeelezewa vizuri na nimshukuru Mheshimiwa Rais pamoja na Serikali yake kwa kutuwekea kiwanda kiwanda kikubwa sana pale Moshi mjini lakini bado nina ombi kwa Serikali. Viko viwanda vilivyobinafsishwa ili viendelezwe vitoe ajira na kodi mfano ni kiwnada cha viberiti cha Kibo Match na kiwanda cha magunia. Katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ya Bunge la Kumi na Moja, ukurasa wa 21, alielezea dhamira yake ya kuwanyang’anya viwanda wale walioshindwa kukidhi vigezo vile. Moshi tuko tayari, tunaomba aje awanyang’anye wale waliofanya viwanda vile ni mago-down.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ukurasa wa 95 kuna marekebisho ya viwanja vya ndege 11. Naomba niikumbushe Serikali kiwanja cha ndege cha Moshi nacho kimetajwa lakini kinahitaji matengenezo ya haraka. Kiwanja hiki kina umuhimu mkubwa sana, kitabibu, kibiashara na kiutalii. Naomba kipewe kipaumbele katika viwanja vya ndege vinavyorekebishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 32 umeongelea masuala ya afya na niipongeze Serikali kwa hatua kubwa ya kujenga zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya pamoja na za mikoa na za rufaa zile za kanda. Nawaomba katika hizi 98 zinazotarajiwa kujengwa katika awamu hii tafadhali sana wawakumbuke wananchi wa Moshi Mjini na Vijijini, pote pale hakuna hospitali ya wilaya ya Serikali, tunaomba sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la elimu nililizungumzia jana kwenye swali langu na limezungumziwa sana. Hoja yangu kubwa itajikita kwenye mikopo kama nilivyosema na niendelee kusisitiza, wapo watu wanaokidhi vigezo vyote lakini hawapati mikopo ile pengine kwa sababu walisomeshwa kwa ufadhili kwenye shule za binafsi au kwa sababu nyingine zozote. Kama Mawaziri watahitaji kuniona nitawapa mifano halisi ambayo ipo na naifahamu.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile naomba msisitizo upelekwe kwenye kidato cha tano na cha sita hasa kwenye shule za kata kwenye Taifa hili. Kuna shule ambazo zina nafasi tuweke mkazo zaidi kwenye elimu inayoendelea kwa kujenga madarasa mapema badala ya kujenga mwisho baada ya watoto kumaliza shule.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 36 wa hotuba ile umeongelea wafanyabiashara wadogo. Niipongeze sana Serikali namna ambavyo imewaweka vizuri na niombe uangalizi uwekwe katika kuwapanga vizuri. Yapo maeneo wamezuia kabisa kutumia miundombinu ambayo imewekwa kama barabara. Halmashauri zinayo nafasi kubwa na sisi tunaendelea kuzishauri lakini tuweke namna bora ya kuwapanga wafanyabiashara hawa wadogo ili basi waweze kushirikiana na watumiaji wengine wa miundombinu hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukurasa wa 37 Mheshimiwa Rais ameongelea umuhimu wa kuboresha michezo. Mimi naona eneo bora zaidi la kuanzia ni kuboresha viwanja vya michezo ambavyo vinasimamiwa na halmashauri kwenye majimbo mbalimbali. Moshi Mjini tunacho kiwanja cha majengo, naomba Serikali iangalie namna ya kutusaidia na kukiboresha.

Mheshimiwa Naibu Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa kengele ya pili imeshagonga.

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kumalizia na eneo la watalii ambalo kaka yangu na baba yangu Mheshimiwa Dkt. Kimei ameliongelea lakini pia madereva…

NAIBU SPIKA: Muda wako umekwisha Mheshimiwa.

MHE. PRISCUS J. TARIMO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)