Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa ninaomba nimshukuru Mungu ambaye ametuumba, ametupa uhai, hatimaye tu wazima kabisa. Vilevile naomba niwashukuru sana wananchi wa Jimbo la Nsimbo kwa kuniamini niwe Mbunge wao wa jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru kwa kunipa muda huu niweze kuchangia hotuba ya Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kwanza kabisa ninaomba nimshukuru sana Rais na kumpongeza kwa kazi kubwa sana ambayo ameifanya kuanzia mwaka 2015 mpaka 2020. Tumeona jitihada zake kubwa ambazo zimewafanya Watanzania wawe na imani kubwa sana na Rais wetu Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona katika hotuba yake alivyoendelea kusema ataendelea kuwatumikia Watanzania kwa kila hali na nguvu zote. Ninaomba niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano kwa kazi kubwa, miradi mikubwa imefanyika, tumeiona kwa macho miradi ambayo ilikuwa inaenda sambamba, miradi ya maji, miradi ya barabara, miradi ya standard gauge, bandari, kila kitu kimekwenda sambamba. Tunaomba tuipongeze sana Serikali kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wameifanya kwa muda mfupi na malengo ni mazuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wameongea na nijikite kwenye ajira. Rais amesema ataendelea kuboresha ajira na tumeona ajira nyingi sana, yupo ndani ya kampeni lakini akamuagiza Waziri Jafo aongeze staff kupitia walimu ajira 13,000 ndani ya kampeni. Ni jitihada kubwa sana. Tuliona jinsi gani anaongeza madaktari ili kuendelea kutibu wagonjwa, madaktari bingwa. Tumeona jitihada ambazo zinaendelea kupitia ajira, lakini bado tunahitaji ajira kwa sababu kila sehemu tukienda mapungufu ni mengi sana kupitia ajira.

Tunahitaji sana tuongeze ajira kwa sababu tunaendelea kujenga zahanati,tunaendelea kujenga vituo vya afya na Rais wetu ametujengea hospitali katika mikoa mingi, hospitali za mikoa zingine za kanda, hiyo ni jitihada kubwa nzuri lakini bado watenda kazi ni wachache. Tunaomba Serikali iendelee kupambanua kuhusu ajira kwani inahitajika sana kwa kipindi hiki kwa sababu tumeongeza vitu vingi, shule zetu za secondary tunaongeza siku hadi siku, shule zetu za kata tunajenga, tunafungua shule, tunahitaji watenda kazi kwa ajili ya kutufundishia watoto wetu

Mheshimiwa Naibu Spika, Rais amejitahidi sana kwenye upande wa kilimo, tulikuwa tunapata shida pembejeo viatilifu matrekta, mbegu lakini sasa hivi mkulima anakuta mbolea madukani, anakuta pembejeo madukani, mbegu madukani, kusema kweli hali ya kilimo imeendelea kuwa nzuri siku hadi siku kutokana na uwezo ambao imeonesha Serikali ya Awamu ya Tano tunaomba tuwapongeze sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, bado kidogo kwa sababu kilimo ni uti wa mgongo na tunategemea sana, kilimo kije kutusaidia kupitia viwanda, Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli anatamani sana nchi yetu ya Tanzania tuwe na viwanda ili vijana wetu waweze kupata ajira na vile vile malighafi yetu iweze kufanya kazi ndani ya nchi yetu. Kilimo ndiyo kinaweza kufanya hivyo ili tuweze kupata viwanda vingi, lakini bado kuna maeneo ambayo hatujaweza kuwafikia wakulima vizuri, tukawapa semina mbalimbali na tukawawezesha wapate matrekta ili waweze kulima kilimo bora ambacho kitaweza kuleta tija. Naomba sana Serikali kwenye kilimo tuendelee kupaweka vizuri kwa ajili ya vifaa ambavyo vitawafanya wakulima waweze kulima vizuri ili tuweze kupata viwanda ambavyo tutapata ajira na vitu vingine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakwenda kwenye ufugaji; kwenye mambo ya ufugaji leo hii tumeshuhudia kuna viwanda vya kuchakata nyama viko viwanda vya samaki, tumetoa ajira na vile vile sasa hivi tunaweza tukasafirisha wanyama wetu nje ya nchi. Naomba nipongeze kufikia hatua nzuri ambayo tumeona ndege ya Ethiopia ilishakuja hapa kubeba cargo zetu za mizigo mbalimbali ambazo zinasafirishwa nje ya nchi ili kuendelea kukuza uchumi wa Watanzania, ndiyo maana unakuta sasa hivi watu wengi wametamani kufuga ili kuweza kupata uchumi mzuri. Naomba niipongeze sana Serikali ya Awamu ya Tano, kazi ni nzuri inaonekana wazi wazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, upande wa barabara, Serikali imejipambanua sana kuhusu barabara za lami, tumeunganisha mikoa, sasa hivi hata sisi watu wa Mkoa wa Katavi tukitoka Dodoma mpaka tufike Katavi ni masaa saba, nane, tunaomba tuipongeze sana Serikali, tunakwenda kwa lami sehemu zote. Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuliamefanya kazi kubwa sana, lakini bado sisi Wabunge wa Majimbo tunaomba Serikali sasa ijikite kuongeza bajeti ya TARURA ili sasa zile malighafi ambazo zinatoka ndani ya vijiji vyetu, vijiji vyetu barabara hazipitiki kabisa, wakulima wanalima, lakini sasa kutoa mazao ndani ya vijiji vyetu ili tuweze kufisha sokoni na kipindi hiki cha mvua, inakuwa ngumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti ya mwaka jana ya TARURA sidhani kama ilitumika kabisa, kulikuwa kuna mitaro barabara zimekatika lakini hazikuweza kurekebishwa kabisa mpaka imekutana na mvua nyingine. Tunauliza shida ninini? Wanasema shida ni bajeti, kwa sababu barabara za vijiji zikitengenezwa vizuri, zikawa zinapitika ina maana malighafi zote zinazopatikana ndani ya vijiji vyetu zitatoka kwa urahisi.

Sasa hivi sisi tunasafiri vizuri, tukitaka kwenda sehemu tunakwenda, ndege zipo tunamshukuru sana Rais wetu amenunua ndege,usafiri ni mrahisi na mwepesi. Tatizo linakuja sasa ndani ya TARURA, hatujajipangia bajeti nzuri, naomba sana Serikali kwenye upande wa TARURA waongeze bajeti ili tuweze kutengeneza barabara na madaraja ndani ya maeneo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, muda umeisha?

NAIBU SPIKA: Ndiyo.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)