Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba nimshukuru sana Mungu kwa kunipa kibali cha kurudi tena kwenye Bunge lako Tukufu. Nakishukuru sana chama change, Chama cha Mapinduzi kwa kuniteua na baadaye kushinda uchanguzi Jimbo la Geita Mjini. Naomba kuwaahidi wananchi wa Jimbo la Geita Mjini kwamba nitaendelea kuwa mwakilishi mwaminifu sana kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais ya kufungua Bunge ukurasa wa 41 alizungumzia madini na alisema sekta ya madini imekua kutoka mchango wake katika malipo ya pato la Taifa wa shilingi bilioni 168 mpaka 527 lakini katika pato la Taifa kutoka asilimia 3.4 mpaka 5.2. Naungana na Mheshimiwa Rais kuwapongeza sana Wizara ya Madini wanafanya kazi vizuri. Mimi ambaye natoka jimbo ambalo uchumi wake kwa asilimia zaidi ya 80 unategemea sana pato la madini, naona faida ya mabadiliko ya Sheria ya Madini ya mwaka 2017 ambayo imeleta heshima katika matumizi ya fedha za CSR katika Halmashauri yangu ya Mji wa Geita. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo moja tu hapa wachimbaji wadogo investment capital yao ni kubwa kuliko faida wanayoipata. Teknolojia wanayotumia na duni na bado mitaji ni midogo. Unakuta wachimbaji wadogo wanaendelea kubahatisha. Inaweza kutokea rush wataanza kuchimba mpaka wanafika mita 60 mpaka 100 hajaanza kufanya uzalishaji lakini tunazo teknolojia. Niiombe Wizara kama makampuni yanafanya CSR na yenyewe ifanye hivyo, ileta mitambo ya kutosha ili sehemu rush zinapotokea wawaambie wachimbaji kwamba eneo hili mnalochimba dhahabu zipo au madini yapo na yapo umbali gani na mlalo wa miamba. Namna tunavyokwenda sasa hivi utakuta ni kweli tunaongeza uzalishaji wa dhahabu lakini kimsingi gharama za uzalishaji wa dhahabu hizo ni kubwa kuliko faida ambayo wachambaji wadogo wanapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini la pili katika eneo hilo, juzi Mheshimiwa Rais akiwa kule Mbogwe alisema kwamba siyo sahihi wachimbaji wakubwa wanapopata license kuamini kwamba sasa wamenunua haki ya wananchi ya ardhi na kukiuka sheria ambazo zipo. Wananchi wangu katika maeneo ya Nyakabale, Magema, Compound na Katoma wameendelea kuishi kwenye mgogoro wa takriban miaka
20. Ni kweli wako ndani ya leseni ya mgodi lakini mashamba yao ya asili sehemu ambayo mgodi haujataka kuanza kuchimba, hawaruhusiwi hata kwenda kukata kuni. Sasa hivi kuna ulinzi katika maeneo ya Magema hawaruhusiwi hata kupita nyumba moja kwenda nyumba nyingine kwa sababu ni ndani ya mgodi wa leseni. Nataka kushauri, Mheshimiwa Waziri alitolea maelekezo lakini Serikali ya Mkoa imeendelea kuweka askari pale, wananchi wameendelea kunyanyaswa tutoe mwongozo sahihi kama mgodi unataka eneo lile walipe fidia kama wananchi bado wanatakiwa kukaa pale wawaache wafanye kazi zao kwa uhuru.

Mheshimiwa Naibu Spika, niende eneo la pili kwenye ukurasa wa 27 sehemu ya kilimo. Ni kweli kwamba nchi hii inategemea ajira kwenye kilimo ambacho ni zaidi ya asilimia 80 na kimesaidia sana kudhibiti mfumuko wa bei na mimi nakubaliana na hilo. Nataka kutoa challenge kidogo hapa kwamba bado Watanzania wanalima very local na shida ya Watanzania siyo ukubwa wa mashamba. Mheshimiwa Rais anaweza kuendelea kuongeza mashamba, kubadilisha hifadhi, kubadilisha mapori ya akiba lakini shida hapa ni productivity kwenye maeneo waliyonayo wakulima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado wakulima mtu analima heka kumi anapata gunia kumi za mahindi. Nataka kuwaambia Wizara ya Kilimo twenda sambamba na hotuba ya Mheshimiwa Rais, tulime kisasa na hili linaweza likaonekana kabisa kwa macho lakini tupate mbegu za kisasa na tupate huduma za ugani za kisasa. Utasikia tu kwenye magazeti na vitabu huduma zipo lakini kimsingi wakulima wetu bado wanalima kwa kizamani sana, productivity ya heka moja ni sawasawa na mtu aliyelima nyuma ya nyumba. Niiombe Wizara hii katika kipindi cha miaka mitano iweze kufanya jambo hili kwa umakini zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitaka kuona kwamba kilimo cha kawaida hakitiliwi maanani sana wakati wa mavuno ya mazao ya biashara, maeneo yetu sisi tunalima pamba, store zote za pamba zimeoza, zimeanguka na zimegeuka kuwa nyumba za watu binafsi. Kwa hiyo, niombe Wizara iweze kujipanga vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo tunalolipata kwenye kilimo liko pia kwenye mifugo. Utona kuna uboreshaji wa matumizi ya mashamba ya NARCO, lakini bado hata walio katika NARCO kinachowafanya waonekane wanafuga kisasa ni fensi, ukiingia kwenye shamba la NARCO utakuta hakuna mashamba ya nyasi, hakuna teknolojia unaotumika lakini bado ufugaji wa mle ni local, usambazaji wa mbegu za kisasa ni wa kizamani. Kwa hiyo, utakuta wafugaji hawa hata tunazungumza tuna ng’ombe milioni 33 hazijawasaidia Watanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe sana hasa katika kipindi hiki tunachokwenda nacho mabadiliko haya yaweze kutafsiriwa kwenye level ambayo wakulima na wafugaji wa kawaida wataondokana na kufuga ng’ombe 500 zenye kilo 250 waende wafuge ng’ombe 100 zenye tani moja ambazo zinaweza kuzalisha maziwa mengi lakini teknolojia iweze kusambazwa kwa njia ya urahisi. Tumeangalia maeneo mengi sana unakuta migogoro mingi ya wakulima na wafugaji, kwa nini? Ni kwa sababu mkulima akipata eneo la kwenda kulima akinunua mifugo anahamia hapo na akihamia hapo anajenga, kesho yake anasogea mbele anapata eneo la kulima anahamia na anajenga kwa sababu anafuga ng’ombe nyingi ambazo anashindwa kuzimudu kulingana na eneo alilonalo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niiombe Wizara katika kipindi iweze kutumia muda wa kutosha kufanya mabadiliko ya kisayansi. Unayaona haya mabadiliko kwenye vitabu lakini wafugaji na wakulima tunaokaa nao sisi bado wanafuga kizamani na wanalima kizamani na hakuna mabadiliko yoyote ambayo yameendelea kuwepo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda la mwisho, nimeona juhudi kubwa za Wizara ya Nishati katika Mikoa ya Pwani, ikisambaza gesi kwa ajili ya matumizi ya majumbani. Nilitamani kujua mkakati wa Serikali wa gesi hii kuifikisha kwenye mikoa ambayo iko nje ya Pwani, kwa mfano gesi hii itafika lini Mwanza au Geita ili tuweze kuachana na matumizi ya kuni na mkaa? Ziko taasisi zinatumia zaidi ya cubic mita 40 za kuni kwa mwezi, tunafanya nini kuzibadilisha taasisi hizi ziweze kutumia nishati ya gesi asilia tuliyonayo na kuweza kuzuia misitu yetu ambayo inaharibika kila siku. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii. (Makofi)