Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

Hon. Felista Deogratius Njau

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyoitoa wakati wa Ufunguzi wa Bunge la Kumi na Mbili, Tarehe 13 Novemba, 2020

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwanza nimshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema ambaye amenisaidia kufika mahali hapa hii leo. Naishukuru pia familia yangu ambayo kimsingi imekuwa nyuma yangu kwa muda mrefu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakwenda moja kwa moja kwenye hotuba ya Rais ambayo imeeleza kwenye ile page ya 21 namna gani wanawake na vijanawanakwenda kupata mikopo ya asilimia 10. Nimesema kuhusiana na hili linatakiwa jicho la tatu kwa sababu wanawake wengi ndiyo wanaoonekana kwenda mbele kwenye hii mikopo na wanawake hawa wamepata changamoto lukuki. Changamoto hizi hazitatuliwi kwa muda mrefu, kwa sababu wanawake hawa wanaenda kupewa vigezo ambavyo haviko kwenye utaratibu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza wanadaiwa kadi za Chama Cha Mapinduzi, kama hauna kadi ya Chama Cha Mapinduzi hupati mkopo. Lakini wanawake hawa hawa baada ya kupata mikopo hawana mtu wa kuwafundisha ni namna gani watakwenda kufanya biashara kwa kiwango kidogo wanachopewa ili kuleta tija kwenye jamii. Kikubwa zaidi hawa wanawake wanaopata mikopo au wengine wanaokosa wanakimbilia kwenye microfinance...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Felister Njau, kuna Kanuni inavunjwa. Mheshimiws Jenista Mhagama Kanuni inayovunjwa.

KUHUSU UTARATIBU

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, BUNGE, AJIRA, VIJANA NA WENYE ULEMAVU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kwenye utaratibu. Kanuni ya 71 mambo yanayokatazwa Bungeni lakini 71(1) ambacho Mbunge haruhusiwi kusema taarifa ambazo hazina ukweli, lakini kiambatane na Kifungu cha 70(4) ambacho kinamtaka kuthibitisha ni kwa kiasi gani jambo linalosemwa kwamba si sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niliambie Bunge lako Tukufu, kwa mujibu wa miongozo tuliyojiwekea inayosimamia utoaji wa mikopo kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika halmashauri zetu, kigezo cha uanachama wa mwombaji wa mikopo hakipo na hakijawahi kutumika. Halmashauri zote zimekuwa zikitoa mikopo hiyo kwa uwiano ulio sahihi kabisa. Kinachozingatiwa ni taratibu zile za kimiongozo ambazo zinatakiwa kila mwombaji mkopo aweze kuzifuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Bunge hili lisitumike kuzungumza mambo ambayo hayana uasili na uhalisia. Mara nyingi tumekuwa tukimsikia Mheshimiwa Rais akisema maendeleo ya taifa hili hayatazingatia chama, dini, ukabila wala jambo lolote ni maendeleo huru kwa Watanzania wote kwa mambo yote.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuwasilisha. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge alikuwa anachangia Mheshimiwa Felister Njau, ameeleza maelezo kuhusu mikopo inayotolewa na vigezo vinavyozingatiwa. Akasimama Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa mujibu wa Kanuni ya 71 na 70, ametoa maelezo ambayo sote tumeyasikia, sitayarejea lakini hoja ya msingi iliyotolewa hapo ni kwamba, Mheshimiwa Felister Njau wakati anachangia amezungumza taarifa kuhusu mikopo ambazo hazina ukweli kwa mujibu wa Mheshimiwa Jenista. Kanuni yetu ya 70 inatuongoza namna ya kwenda na jambo ambalo limezungumzwa hapa, lakini Mbunge ataamua sasa kusimama kama alivyofanya Mheshimiwa Jenista kuonesha kwamba jambo hilo linalosemwa halina ukweli na ametoa ufafanuzi kwa nini anasema halina ukweli.

Mheshimiwa Felista Njau, ili twende vizuri na kwa sababu sisi wengi hapa ndani ni wageni tutaelekezana tu vizuri hizi Kanuni taratibu, lakini Kanuni ya 70, Mheshimiwa Jenista ametumia fasili ya (4) na (7) inakupa fursa ya aidha kufuta kauli yako kama hilo jambo lililosemwa huna uthibitisho nalo, ama kama hutafuta hiyo kauli hapo nitatoa mimi maelekezo ya nini kifuate baada ya hapo.

Kwa hiyo, nakupa fursa kama huna uthibitisho ufute hiyo kauli, kama utakuwa hufuti kauli nitasimama tena kutoa maelekezo. Nakupa fursa ya kufuta kauli. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Sifuti kauli kwa sababu nina uthibitisho na kimsingi nilikuwa nashauri kwa sababu watu wengi wanaweza wakatumia hiyo lakini ngazi za juu hawajui. Kwa hiyo, natoa ushauri mamlaka husika ifuatilie, hilo tu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Sawa, sasa ukae Mheshimiwa Njau. Waheshimiwa Wabunge, naenda taratibu kwa sababu sisi wengi humu ndani ni wageni.

Mheshimiwa Felista Njau matakwa ya Kanuni ya 70, ukikataa kufuta kauli maana yake mimi naweza kukuelekeza uniletee ushahidi. Ushahidi utakaoniletea si wa maneno wa kuniambia kuna watu waliambiwa, hapana; utatakiwa ulete ushahidi wa kulithibitishia Bunge hili kwamba hicho ni kigezo cha mikopo mahali fulani na mahali fulani. Kwa hiyo, tuelewane vizuri Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Kwa hivyo, unavyopewa hii fursa ni fursa ya muhimu sana lakini kama unao uhakika Bunge hili kwa sasa hivi haliwezi kukulazimisha kufuta kauli kwa sababu, wewe umesema unao uthibitisho. Sasa kwa sababu ya ugeni nakupa tena fursa ya pili, kama unao uthibitisho nitatoa maelekezo. Karibu, sekunde 30, unao uthibitisho?

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kuondoa mlolongo nafuta lakini naomba… (Makofi)

NAIBU SPIKA: Haya, kaa niiweke vizuri, kaa niiweke vizuri, eeh.

Waheshimiwa Wabunge, Kanuni zetu namna zinavyotutaka kuenenda niwashauri sana sote tuzipitie, Wabunge wageni lakini sisi sote kwa sababu hili ni Bunge jipya. Kanuni hizi ni toleo jipya kwa hiyo, ziko Kanuni ambazo zimebadilika hapa na pale niwasihi sana tukazipitie.

Masharti yaliyoko humu huwa yanafuatiliwa nukta kwa koma, kwa hivyo, ukifuta kauli unafuta bila masharti. Hakuna neno lakini ama nafanya hivi, aahh-aa, isipokuwa yale uliyokuwa unayasema maelezo yako ya pili, sasa hii natoa Mwongozo; ungeweza kusema naishauri Serikali wakati wa kutoa mikopo wajaribu kuangalia hiki na hiki na hiki, lakini ukionesha kwamba kuna shida mahali ni lazima hiyo shida iletewe uthibitisho.

Waheshimiwa Wabunge, kwa muktadha huu na ili tuweze kwenda mbele, Mheshimiwa Felister Njau amefuta kauli yake. Kwa muktadha huo Mwongozo wa Kiti kuhusu huo utaratibu aliokuwa ameomba Mheshimiwa Jenista Mhagama ni kwamba taarifa hiyo haitakuwepo kwenye Taarifa Rasmi za Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Njau endelea na mchango wako.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Nakwenda kwenye kipengele kingine page number 72 ambapo kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Rais kumeeleza kulinda demokrasia, uhuru, haki za wananchi na vyombo vya Habari. Mpaka sasa navyoongea mimi nilikuwa meneja kampeni wa Jimbo la Kawe, Mheshimiwa Halima James mwana wa Mdee, haki, demokrasia, usawa havikulindwa na havikulindwa toka uchaguzi mdogo wa mwaka 2014 uliofutwa, 2019 uliofutwa, lakini 2020 kulikuwa kuna mambo ya ajabu. Mimi ni kati ya watu niliyekamata kura fake mabegi matano kwenye vyombo vingi, lakini nikasema kwa sababu tunakuja kwenye Bunge hili ni lazima tuseme ukweli, demokrasia tunayoiimba tuifuate kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mtu anajua kwenye Bunge hili amekuja vipi, ameshinda vipi, kwa njia zipi, lakini demokrasia ikaseme na mioyo yetu. Haki ya vyombo vya habari, kuna kipindi sisi tulikuwa tukisimama kwenye majukwaa mwandishi akaonekana amepiga picha, humuoni hata siku tatu, nne, ukimpigia simu anakimbia anasema nina kigugumizi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme kama ni haki tunaitangaza, kama ni demokrasia tunaisema, tuiishi kwa vitendo kwa sababu hapa kila mtu ana imani yake. Kila mtu ana imani kwenye Bunge hili kwa hiyo, tuiishi kwa vitendo tusiimbe kwenye makaratasi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa minajili hiyo kuna watu lukuki, kuna wananchi waliokamatwa kipindi cha uchaguzi…

KUHUSU UTARATIBU

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, Kuhusu Utaratibu.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Gwajima, Kanuni inayovunjwa?

MHE. ASKOFU JOSEPHAT M. GWAJIMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama kwa Kanuni ya 71(1)(a). Inasema: “Mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa ambazo hazina ukweli.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mbunge aliyekuwa anazungumza, bahati nzuri mimi ndiye Mbunge halali wa Jimbo la Kawe niliyeshinda kwa kura 194,000 dhidi ya mpinzani wangu aliyepata 30,000 peke yake. Naomba alithibitishie Bunge lako kwamba alikamata kura maboksi 50 kama alivyosema. (Makofi/kicheko)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, bahati nzuri hizi kanuni tutazifahamu tu, Bunge hili ni la miaka mitano, Mwenyezi Mungu atujalie uhai na uzima. Kanuni ya 71 inampa fursa Mbunge kusimama ukisoma fasili nyingine zinazofuata baada ya hapo na kusema kuhusu utaratibu, kwa maana ya fasili ya (2) inampa fursa Mbunge kusimama kusema Kuhusu Utaratibu ili kueleza mambo haya yasiyoruhusiwa Bungeni kwa lile ambalo linakuwa linazungumzwa.

Mheshimiwa Gwajima, Mbunge wa Kawe, amesimama kueleza kwamba taarifa zilizokuwa zinatolewa na Mheshimiwa Felista Njau za kuhusu vitu vilivyokamatwa huko Jimboni Kawe kipindi cha uchaguzi ama siku ya uchaguzi hazina ukweli. Sasa mimi siwezi kufahamu ukweli, anayeufahamu ni Mheshimiwa Felister Njau. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, kabla hamjapiga makofi, hili jengo letu hili kuna muda kuna maneno fulani hivi yanaweza kusemwa pamoja na mambo mengine kwamba hili jumba ni jumba la kisiasa, lakini hili ni jumba ambalo ndiyo maana wanasema Mheshimiwa Spika Bunge lako Tukufu. Haiyumkiniki kwamba mtu anayesimama kuchangia humu ndani atazungumza mambo ambayo yanazungumzwa bila ushahidi, bila uhakika kwa sababu kila mmoja wetu anaitwa Mheshimiwa kwa maana ya ni kiongozi anaweza kusimamia kile anachokisema, anaweza kuthibitisha kile anachokisema.

Mheshimiwa Felister Njau huu ni utaratibu wa pili kwamba Kanuni inavunjwa. Humu ndani huwa ni kawaida watu wanaweza kusimama hata mara nyingi, lakini tazama michango yako isikupeleke mahali ambapo kuna Kanuni humu ndani zinakupeleka nje ya hili Bunge. Isitokee kwamba kila unachokisema tutafika mahali pa kwenda hapo, siyo kwa maana ya utoke nje, aah-aa, kwa maana ya uende huko Kamati ikajiridhishe, ulete huo ushahidi na mambo kama hayo. (Makofi)

Kwa hivyo, kwa muktadha wa Kanuni hizi kwa sababu, sasa husemi ukweli maana yake unarudi tena kwenye 70. Kama unao uthibitisho utasema hivyo, mimi nitaagiza utoe huo uthibitisho. Kama huna uthibitisho futa kauli yako kwa mujibu wa Kanuni ya 70 kama nilivyokusomea Fasili ya (7).

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. Uthibitisho ninao na nikiambiwa nilete nitaleta uthibitisho. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Kanuni hii ya 70 inakataza Mbunge kusema uwongo…

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Tusikilizane Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane. Kanuni ya 70 inakataza kusema uongo Bungeni na fasili ya (4) ya (5) na ya (6) ukizisoma zote kwa pamoja utapata picha kwamba Kiti kitaagiza Mbunge ambaye amekataa kufuta kauli kuleta ushahidi kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge na siyo kumridhisha mtu mmoja.

Kwa muktadha huo fasili ya (6) inanitaka mimi nitoe muda wa kufanya hivyo. Mimi sitataka nimwambie alete ushahidi hapa kwa sababu naweza kumwambia alete sasa hivi ama alete baadae, kwa sababu alikamata maboksi na mabegi hataweza kuwa nayo humu ndani maana yatakuwa hayakupita pale nje kuingia humu ndani. Kwa muktadha huo, hayo mabegi, hayo masanduku yaliyokamatwa naiagiza Kamati yetu ya Maadili, itamsikiliza yeye halafu mimi nitaletewa huo ushahidi. (Makofi)

Kwa hiyo, Mheshimiwa Njau utapeleka ushahidi wako kwenye hiyo Kamati yetu. Muda ninaoutoa kwa sababu leo ni siku ya Jumatano ndiyo kwanza tumeanza Bunge jana, kufikia Jumatano ijayo huo ushahidi uwe umeshauleta na Kamati yetu ya Maadili ikae wakati huo na kabla Bunge hili halijaisha tutatoa maamuzi kuhusu jambo hilo. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naomba dakika zangu zilindwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo niombe mamlaka ambayo inaweza kushughulika, kuna vijana wengi katika kanda mbalimbali na mikoa wako ndani kwa kesi za kisiasa za uchaguzi na zinapigwa tarehe, ushahidi unakosekana. Katika kanda mbalimbali, Kanda ya Kusini 34, Kanda ya Nyasa 36, Viktoria 16, Serengeti 34, Pwani nane, wale vijana ni wa CCM na CHADEMA. Kwa hiyo, naomba mamlaka husika iwaondoe vijana hawa ndani kwa sababu shughuli au mtanange umekwisha. (Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njau, hao washauri wako wa hapo karibu wanatakiwa wakushauri mambo mengi sana ikiwa ni pamoja na mambo yaliyoko mahakamani. Mambo yaliyoko mahakamani hayatolewi maamuzi hapa ndani.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, sorry, wako mahabusu.

NAIBU SPIKA: Mambo yaliyoko mahakamani hayatolewi maamuzi hapa ndani. Mheshimiwa Esther Matiko na Ester Bulaya msimpoteze Mheshimiwa Felister Njau.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Njau malizia mchango wako.

MHE. ESTHER N. MATIKO: No, please, sasa mimi umeniingizaje hapo, I did not say anything.

MHE. ESTER A. BULAYA: Sijawasha microphone hapa, kichwa yake yeye mwenyewe iko vizuri.

MHE. FELISTER D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, samahani…

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Esther Matiko na Ester Bulaya, muacheni mchangiaji amalize mchango wake. Muacheni mchangiaji amalize mchango wake, Mheshimiwa Felista Njau.

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, Taarifa, niko huku.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunti.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru. Naomba tu nimpe Taarifa mchangiaji Mheshimiwa Njau kwamba watu anaowazungumzia ni pamoja na wakazi wa Wilaya ya Mpwapwa ambao wako 18 walikamatwa, kesi haijaenda mahakamani…

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tusikilizane vizuri. Bunge hili siyo kazi yake kuingilia michakato ya taasisi zilizoko huko nje, labda kama hapa mbele kuna hoja hiyo, tuelewane vizuri na ninyi mnazifahamu kanuni, tuelewane vizuri. Mheshimiwa Njau malizia mchango wako. (Makofi)

MHE. FELISTA D. NJAU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Kwanza nishukuru lakini niombe, wako Mawaziri wenye mamlaka hayo wasimame kidete kwa ajili ya kutetea haki za raia na tusiende kwa sababu ya itikadi au chochote. Nakushukuru sana. (Makofi)