Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

Hon. Peter Ambrose Lijualikali

Sex

Male

Party

CHADEMA

Constituent

Kilombero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021 – Ofisi ya Waziri Mkuu

MHE. PETER A. P. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, tangu mwanzo wa Bunge hili linaanza 2015 nimekuwa nikizungumzia sana ujenzi wa barabara yetu ya Ifakara - Kidatu ambayo inatakiwa itoboe iende mpaka Songea. Hii barabara inafadhiliwa na wafadhili katika mradi wa Sagoti wafadhili kama wanne hivi USA Aid na wengine.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Dkt. Magufuli Rais wetu mwaka 2017 aliweka na akasema anaamini hizi km 75 ndani ya miaka mitatu itakuwa zimeisha yaani ilitakiwa mwezi huu 4 barabara iwe imeisha. Lakini mpaka dakika hii barabara imefanyiwa kazi kwa almost asilimia tano au sita. Leo ni miaka mitatu wafadhili wanalipia kila kitu asilimia 98 ni ufadhili serikali ya Tanzania inatakiwa itoe asilimia mbili tu kwa ajili ya fidia kwa wananchi.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, mpaka leo barabara inasuasua na juzi nikamwona RAS baada ya daraja kuwa limekatika pale kutokana na hizi mvua, anakwenda anamshutumu mkandarasi, anasema mkandarasi ni mzembe, anazembea, Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga barabara hii iishe lakini wewe mkandarasi unazembea kitu ambacho siyo kweli, anajua ukweli. Ukweli ni kwamba Serikali yetu inataka mkandarasi yule atoe kodi (VAT) wakati mikataba haitaki kodi kutoka. Kumekuwa na ubishani wa kodi itoke au isitoke, tangu mwaka 2017 mpaka leo miaka mitatu, kitu ambacho tunapewa bure. Yaani wazungu wanatuambia wanataka watujengee barabara na fedha wanatupa, wazungu, mabeberu, ninyi hamtaki barabara ijengwe mnataka kodi. Hii ni aibu kabisa, ni aibu na ni kitu kibaya na sielewe commitment ya Serikali katika hili maana yake ni nini. Yaani tafsiri ni nini! Hapa napata mashaka hivi ni kweli wizara zinaweza zikagombana na mkandarasi kama Mheshimiwa Rais Magufuli hajui, kweli!

Mheshimiwa Spika, wnataka watu wa Kilombero tuamini kwamba nyuma ya kwenye huu mpango, kwenye huu ukwamishwaji Mheshimiwa Rais yupo? Kwa sababu kama Mheshimiwa Rais amekuja kuzindua barabara na akasema ndani ya miaka mitatu barabara iishe, leo ni asilimia tano na Mheshimiwa Rais ana vyombo vyake, ana watu wake wote. Ana Mawaziri, ana Waziri Mkuu, ana Wakuu wa Majeshi, ana TAKUKURU, ana vyombo vyote, kweli hajui. Hivi kweli nyie hamjui!

Mheshimiwa Spika, kwa kweli hili ni jambo la aibu na hiyo commitment ya Awamu ya Tano wanayosema wao wapo hapa kutetea maslahi ya watu yako wapi kwenye hili jambo. Barabara yetu hiyo sisi huo ni uchumi, sisi kwetu ni uchumi ule.

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi, Mheshimiwa Kamwele tafadhali.

WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO: Mheshimiwa Spika, naomba kumpa taarifa Mheshimiwa Lijualikali ambaye ana dakika za kuendelea kuchangia katika bajeti hii ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, barabara ya Kidatu-Ifakara ujenzi unaendelea, lakini tulikabiliwa na changamoto za hali ya hewa. Mkoa wa Morogoro tangu tarehe Mosi Oktoba, mwaka jana, mvua ilianza kunyesha haijasimama mpaka leo na kwa asili ya ukandarasi anatumia udongo. Mvua zikishanyesha kuna moisture content inayotakiwa ili aweze kujenga barabara, sasa kutokana na hayo mazingira ameshindwa kuendelea.

Mheshimiwa Spika, tutakuwa na vitu vingi tunavyoviongea lakini sisi wasimamiaji, mimi ndiye ninayesimamia ule mradi, sehemu kubwa ambayo imefanya hii barabara isikamilike ni kwa sababu ya hali ya hewa na yale maeneo yana mvua nyingi kila wakati na yeye anaishi kule. VAT siyo sababu, VAT ni suala la kiutawala wala halina mgogoro wowote, kwa hiyo Mheshimiwa Mbunge na wananchi wa Ifakara kule niwaaminishe kwamba Serikali ina nia nzuri ya kuijenga barabara ile yote mpaka Malinyi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ndiyo maana imeshaanza lakini kutokana na hali ya hewa haiwezi ikajengwa katika kipindi cha hali ya hewa mbaya, hivyo ubora wa barabara unaotarajiwa hautapatikana na tutakuja tena kuleta lawama nyingine. Nimwombe Mheshimiwa Mbunge suala hili tusubiri mvua ikishakatika ataona speed tutakayokwenda nayo, hatuna mgogoro mwingin,e mambo mengine ni ya kiutawala tu. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali, taarifa hiyo.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, utakumbuka Bunge la mwezi wa Tisa mwaka jana nilikuwa humu peke yangu, nilikaa kiti hicho baada ya wengine kuwa wametoka nje kutokana na ambacho kimetokea, niliongea hii hoja. Nakumbuka uliniambia sasa umeona umetoa ya moyoni sasa utulie umeongea umesikika na unakumbuka, hoja ilikuwa ni hii hii. Bunge lililopita mwezi wa Kwanza nimeuliza swali na hansard zipo, Mheshimiwa Waziri kwa mdomo wake anasema tatizo ni VAT, Serikali kutaka kodi na akasema mgogoro wa kodi umeisha. Amekiri mwenyewe na hansard zipo kama ni uongo mimi leo naacha ubunge, hansard ije hapa, kama ni uongo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hatuwezi kuendesha nchi kwa ujanja ujanja, huwezi kuwa Waziri unakuwa mjanjamjanja, uongouongo hauwezekani. Majibu ya Serikali lazima yawe ya ukweli, watu wanaiamini Serikali, wanaamini jibu la Serikali; leo unapokuwa unajibu hili, kesho jibu hili maana yake commitment yako wewe haipo. Kwa hiyo niseme kwenye hili nasema wazi Mheshimiwa Waziri ametudanganya, amedanganya Bunge kwa sababu tayari kuna hansard za majibu yake akisema shida ni VAT. Haiwezekani Serikali ambayo wanasema wana fedha wanaanza kugombania fedha za msaada, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kila siku wanasema hapa, nchi hii ina fedha, nchi iko vizuri, wazungu wanatujengea barabara wao hawataki, haiwezekani, haiwezekani. Nimwambie Mheshimiwa Waziri asisingizie habari za mvua, mvua tangu mwaka 2017 mpaka leo, mwaka 2017 mpaka leo mvua gani hiyo, Mvua ya Nuhu! Ni gharika! Ni gharika nasema! (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, sisi tunaumia sana, nyie kama mnakaa huku kwenye viyoyozi barabara safi, sisi kule tuna shida hatujihisi kama tuko Tanzania. Haiwezekana halafu Mheshimiwa Waziri anakuja hapa anaongea vitu vya uongo kabisa, haiwezekani, haya mambo yanaudhi, Mheshimiwa Waziri namwomba sana aheshimu kiti alichokaa hapo na mwaka huu tunawang’oa. (Makofi)

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, mwongozo.

SPIKA: Mheshimiwa Lijualikali ni kengele ya kwanza, lakini naona yuko juu sana nataka nimpe likizo kidogo, nimrudishe baadaye ili atulie kidogo. (Kicheko)

Unaonaje dakika tano zako nikikupa baadaye.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ni sawa haina shida.

SPIKA: Ili upoe kidogo.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ni sawa haina shida.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. PETER A. LIJUALIKALI: Mheshimiwa Spika, ameniudhi.