Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Lucia Ursula Michael Mlowe

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2018 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

MHE. LUCIA M. MLOWE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili na mimi niweze kuchangia bajeti hii. Awali ya yote naomba niunge mkono hotuba ya Kambi Rasmi ya Upinzani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nina vitu kadhaa ambavyo nitachangia. Kitu cha kwanza ni suala la vitambulisho vya wajasiriamali. Suala la vitambulisho vya wajasiriamali limeleta mkanganyiko takribani nchi nzima. Jana huko Njombe wamesomewa barua makanisani, kwamba watu wote wanatakiwa kuwa na vitambulisho vya ujasirimali. Kwa mfano akina mama ntilie ambao wameajiri wafanyakazi kuwasaidia, kuosha vyombo na shughuli zingine ndogo ndogo wameambiwa wanatakiwa wawe na vitambulisho vya wajasiriamali. Watu wanaofanya kazi kwenye bustani wanatakiwa wawe na vitambulisho vya ujasiriamali, mafundi ujenzi wanatakiwa wawe na vitambulisho vya ujasiriamali. Ninaomba kujua, hivi kodi ya kichwa imerudi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli inasikitisha kwa sababu wananchi hawa wamechanganyikiwa. Wamenipigia simu mimi asubuhi wanaongea kwa masikitiko makubwa sana wamechanganyikiwa. Ninaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atupatie basi ufafanuzi na mwongozo kuwa ni watu gani wanaotakiwa kuwa na vitambulisho hivi vya mjasiriamali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la pili naomba niongelee mradi wa Liganga na Mchuchuma. Juma lililopita nilikuwa nimeuliza swali; kwa kweli wananchi wa Mkoa wa Njombe, ingawa haya madini ni ya Taifa zima lakini kwa kweli tunasikitika; kwa sababu wananchi wa Mkoa wa Njombe wamejiandaa kwa muda mrefu, wametafuta maeneo karibu na mradi, wamewekeza wanajiandaa tayari mradi uanze lakini mradi hauanzi. Kuna watu walilima mazao kama mboga mboga, matunda wakidhani kwamba sasa watapata soko, lakini mradi uko kimya; na nimeangalia katika kitabu hiki sijaona mahali popote kuhusu mradi wa Liganga na Mchuchuma. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ni fidia. Wananchi wanalia na fidia, hawajafidiwa. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kuhitimisha atuambie hao wananchi watalipwa lini fidia, kwa sababu hii kwa kweli inakatisha tamaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine naomba niongelee juu ya mashine za EFD; mashine za EFD kwa kweli ni mbovu. Nina watu kadhaa ambao wamenionesha zile mashine na zile mashine inaonekana kila inapoharibika anatakiwa kutengeneza kwa 150,000. Kwa hiyo unaweza kukuta imetengenezwa wiki hii, wiki ijayo tena inaharibika, anatakiwa atoe 150,000. Ni kwa nini Serikali isitafute kampuni ambayo inatengeneza hizi mashine imara? Nitaomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja basi atuelekeze, atutolee ufafanuzi kama kuna uwezekano wa kutafuta kampuni nyingine inayoweza kutengeneza mashine imara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine naomba niongelee suala la taulo za kike. Mwaka jana baada ya kupata msamaha wa kodi kwa taulo za kike kwa kweli wananchi walifurahi sana, hususan wanawake; lakini mwaka huu tena imerudi. Ninaomba Waziri atakapokuja atueleze ni namna gani hawa akina mama tutaenda kuwafariji? Kwa sababu mpaka sasahivi watu wameshachanganyikiwa tena, kwamba kwa nini hizo kodi zimerudi ilhali viwanda vya kutengeneza taulo hizo bado havipo?. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, ahsante sana. (Makofi)