Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi, awali ya yote, nami nimpongeze Mheshimiwa Waziri Dkt. Kigwangalla na timu yake, lakini niwapongeeze watendaji wote kwenye maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha nyuma nilibahatika kutembelea Ngorongoro kama ambavyo sifa zimekwenda kwa ndugu yetu Manongi na naomba niendelee kusema uimara wa mhifadhi huyu unaendelea kutusaidia kulihifadhi eneo lile, najua hayupo peke yake pamoja na timu nzima. Vivyo hivyo kwa mzee Kijazi wa TANAPA na wengine wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, rai yangu, eneo la utaliii kwa ujumla wake ni tofauti na maeneo mengine. Tofauti yake inakuja hapa; unatakiwa utengeneze mazingira rafiki, mazingira ya kuweza kumshawishi mtalii ili kesho aweze kurejea nyumbani kwako. Utengeneze mazingira, kwa sababu fedha ni ya kwake yaani, huyo mtalii fedha ni ya kwake, yeye ndiyo ana hiyari aitumieje, kwa hiyo usipotii kiu yake haji, mazingira yasipokuwa mazuri hutomwona mtalii, huduma zikiwa za hovyo hovyo hutomwona mtalii. Kwa hiyo ninachoomba sana, pamoja na kujisifu kwamba tuko vizuri eneo la utalii, lakini tusipotii kiu, mahitaji ya Watalii itabaki kuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazingira yasipokuwa mazuri hutomuona mtalii, huduma zikiwa za hovyo hovyo hutomuona mtalii. Kwa hiyo ninachoomba sana, pamoja na kujisifu kwamba tuko vizuri eneo la utalii, lakini tusipotii kiu, mahitaji ya watalii itabaki kuwa historia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzuri wa Sekta hii unaweza ukampata mtalii mmoja makini akakusaidia hata katika maeneo mengine. Sasa unakusudia kuwa na aina gani ya watalii hilo nalo ni jambo jingine. Kwenye fani kuna mpaka watalii wanaitwa watalii vishuka; mtalii ambaye mnaenda kugombania wote muhindi wa kuchoma na vitu vingine vya namna hiyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni sehemu ya utalii, sikatai, lakini kuna mtalii ambaye akifika hapa kwanza anajiuliza je, mna huduma ya hoteli za kueleweka? Mna huduma ya tiba? Kwamba hata ikitokea afya yake imekorofisha atapata tiba kabla ya kurudi nyumbani kwake? Je, huduma za Viwanja vya Ndege zinaeleweka? Kwa hiyo ninapoenda kuzungumzia utalii kwa ujumla wake tuyaangalie maeneo yote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru nchi kwa ujenzi ule mzuri wa Uwanja wa Ndege Terminal III, ni mlango wa kuingilia kwenye suala la utalii. Hata hivyo, ni aina gani ya watu wapo hapo? Kwa sababu kuwa na hoteli nzuri, kuwa na uwanja mzuri ni sawa lakini je, watendaji kazi wanaeleweka? Hilo nalo ni jambo linguine. Kwa hiyo naomba pia Wizara isiache kufikisha weledi kuwa na trained personnel hata katika masuala ya hoteli na maeneo mengine hayo. Kwa sababu a trained personnel yeye ni balozi wetu pia, anaanza kutuwakilisha pale, kuiuza nchi na Kuzungumzia masuala ya nchi. Pia tusiache masuala ya amani na utulivu, ni vigezo muhimu sana kwenye kuhakikisha masuala ya utalii yanachukua nafasi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mimi natoka Mkoa wa Katavi, nakuomba Mheshimiwa Waziri; nakubali viboko, mamba ni muhimu. Hata hivyo tunalo bwawa la milala, huko wamejaa viboko, wamekuwa ni tishio kwa uhai wa watu wetu, ni hatari hata kwa wanafunzi, wanakula mazao ya wananchi wetu, naomba Mheshimiwa Waziri kwa kuwa dhamana hii iko mikononi mwako katusaidie kuokoa tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana na wote kuhusu suala la Tanzania Safari Chanel, ni jambo jema. Hata hivyo Mheshimiwa Waziri muda wote biashara ni matangazo. Haya mambo yote mazuri ya Ngorongoro, sijui wapi; bila kujikita kwenye matangazo, bila Bodi ya Utalii kuwezeshwa; na hapa narudi kwenye raslimali fedha; nimesikitika kidogo kwa kupitia taarifa ukizungumzia habari ya miradi yote ya maendeleo fedha hakuna, wakati hawa watu wanazalisha kwa kiwango kikubwa; tusipowarejeshea fedha tutakuwa tumewakata miguu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipindi cha nyuma niliwahi kusema hapa, tusipowarejeshea fedha, tutawakata miguu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na la mwisho, Mheshimiwa Waziri, mimi nilikuwa naendelea kuomba, nchi hii labda tunachanganyikiwa kwa sababu tuna vitu vingi; tuna fukwe nzuri, tuna mbuga nzuri; sasa tukishaona kila kitu tunacho, lakini tusipokuwa na vipaumbele, at the end of the day tutakuwa hatuna hata kimoja tulichokifanya kwa ufasaha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa naomba sana, Mheshimiwa Waziri tuamue, kama ni fukwe basi tuzifanye kwa ufasaha, kama ni Ngorongoro yetu iendelee kulindwa. Na mafanikio bila kuyajengea wigo, bila kuyalinda hatima yake itabaki kuwa historia pia, na tukumbuke tuko kwenye dunia ya ushindani. Mtalii kama hana kitu kipya cha kuona, anaweza akaona leo kwako, lakini kama ni twiga ni huyo huyo ataenda kumuona nchi nyingine za jirani. Kwa hiyo wewe usipomtengenezea mazingira rafiki atakukimbia tu. Kwa hiyo wakati tunajipanga, kutamani kuona tunapataje fedha kwenye maeneo haya tuendelee kutengeneza mazingira ya kuimarisha maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilizungumzie suala la uwindaji wa kienyeji. Mheshimiwa Waziri nimefarijika uliposema kwamba wananchi hawa pia tutawarejeshea uwindaji wa kienyeji. Mwananchi ambaye kwa muda wote amekuwa akiwaona wanyama, akishiriki kuwahifadhi, lakini yeye awe mshangaaji tu anapunguza mori au ile ari ya kuwa mlinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kwa hiyo tunapozungumzia habari ya uwindaji wa kienyeji itatusaidia sana pia kwenye kuhakikisha kwamba watu hawa wanakuwa ni sehemu ya ulinzi wa maliasili zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo na kwa kuheshimu muda, naunga mkono hoja. (Makofi)