Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Julius Kalanga Laizer

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Monduli

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. JULIUS K. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, na Wizara hii nina maslahi nayo, kwa hiyo naomba dakika zangu ziwekwe vizuri kumi ili niweze kusema vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri na watumishi wote wa Wizara kwa juhudi wanazofanya katika kusaidia Wizara hii ambayo ina changamoto nyingi. Nikiri kwamba tangu tumeanza Bunge hili na mpaka sasa kuna improvement kubwa na juhudi kubwa ambazo tunaona Wizara inafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekutana na changamoto nyingi, na tangu dunia iumbwe na nchi hii ianze, tangu mimi nimeanza kuwa mtu mzima mpaka leo sijawahi kusikia mahali ambapo Waziri wa Mifugo amesimama upande wa wafugaji bila kujali kwamba Serikali inatakiwa kuwajibika kwa wakati mmoja, nakushukuru sana Mheshimiwa Waziri kwa kazi ambazo unazifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ninaomba Mheshimiwa Waziri asipende sana maduhuli kuliko utu wa Watanzania wanaofuga. Wizara hii ukiondoa tozo na faini haikusanyi chochote kwa samaki wala kwa ng’ombe, na nadhani inaweza ikawa ni Wizara inayoongoza kwa tozo na faini kwa wananchi wake. Mimi sijawahi kuona mahali ambapo Wizara, na nadhani nadhani inaweza ikawa ni Wizara ya kwanza imevuka lengho la makusanyo; lakini ukiangalia makusanyo yenu asimilia karibu 50 ni faini na tozo. Hata hivyo ng’ombe hawa hawakuja kwa ajili tozo peke yake na faini, ni rasilimali ambayo lazima tujiulize kama kuna uvunjaji mkubwa wa sheria kwa nini wafugaji wanavunja sheria, ili changamoto zilizopo mziondoe ili muweze kupata kilicho halali yenu mnachokusanya si halali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijasema ninaomba niseme mambo mawili kuhusiana na jimboni kwangu. Asilimia 70 ya watu wa Monduli ni wafugaji. Nimeangalia majosho unayokarabati mzee hakuna hata josho moja Monduli. Ninapata mashaka au kwa sababu bado hamjafika, lakini na sisi ni sehemu ya wafugaji wa nchi hii. Naomba wakati unahitimisha utuambie unafanyaje eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili, mmetuweka kwenye kundi la halmashauri ambao wanapaswa kunyima wasikusanye tozo ya wafugaji kama hawajaboresha majosho; mtuondoe huko, sisi tumevuka mbali, tumejenga majosho zaidi ya matano na tumekarabati zaidi ya majosho sita. Kwa hiyo aliyokupa taarifa nadhani amekupa wrong information, mtuondolee kwenye kundi la kutuzuia kutokukusanya tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba naomba nimpe challenge Mheshimiwa Waziri. Kama anasema halmashauri wasikusanye tozo zinazotokana na mifugo kwa sababu hawajakarabati majosho, wao Wizara wanaokusanya zaidi ya bilioni 64 kutoka kwetu wanaturejeshea nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ni muhimu tukakubaliana, kwamba kama halmashauri wanapaswa kutoa na ninyi toeni; tuwekeane asilimia; ninyi Wizara mtupe asilimia 30, halmashauri watupe asilimia 20 sisi tupate asilimia 50 tuboreshe miundombinu ya wafugaji. Haiwezekani, ukavuna pasipo kupanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niwape challenge, ukisoma ilani ya uchaguzi ya CCM inasema yafuatayo:-

Inasema katika ule ukurasa wa 15 hoja ya kwanza inasema kwamba Serikali itajenga visima zaidi ya 300, lakini inasema itajenga mabwawa kutoka 1,300 kwenda mabwawa 2,000, pia inasema itatenga maeneo ya malisho na kuyawekea Sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka atuambie mpaka sasa kwa mujibu wa ilani mmechimba visima vingapi na mabwawa mangapi mapya ambayo yameboreshwa kwa ajili ya wafugaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi naomba niseme challenge ambazo Wizara mkiziondoa itasaidia ninyi kupata fedha kwa haki yenu. Jana nilikuwa napitia kwenye Sekta ya Maziwa. Sekta ya Maziwa ili mtu awe na kiwanda mpaka amalize utaratibu anapaswa awe ameilipa Serikali zaidi ya milioni 30. Usajili tu wa kampuni 400,000, ukaguzi wa eneo la kujenga 120,000, kibali cha ujenzi 300,000, ukaguzi wa kiwanda 350,000, usajili wa leseni ya biashara milioni 3,000,000, namba ya mlipa kodi ya kwanza 500,000, usajili na ukaguzi wa mitambo 245, 000, tathimini ya mazingira milioni 1500, 000, ukaguzi wa kiwanda 350,000, ukaguzi wa usajili wa magari 250,000, ukaguzi wa usalama 400,000 na mengine na mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa mnafahamu kabisa mchakato wa ng’ombe hizi gharama anabeba mfugaji; kwamba ukiweka gharama katika uendeshaji wa kiwanda cha maziwa maana yake bei ya maziwa kule kwa mfugaji inashuka. Sasa hamuwezi kupunguza mifugo kama hatuna utaratibu unaomuhamasisha mfugaji kufuga kwa tija, ukiwa na bei nzuri ya maziwa maana yake utakuwa na ng’ombe bora wa maziwa mengi ili uweze kuuza. Kwa hiyo angalieni hizi tozo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niseme kuhusu mgogoro wetu na ninyi Namanga. Mheshimiwa Waziri unajua kabisa hakuna sheria ya utaifishaji wa ng’ombe; lakini naomba uniambie mchakato wa kutambua kwamba mfugo huu umekosa mwenyewe ukoje, kwa mujibu wa sheria? na mkatangaze na mkabandike. Watu wenu wanatuibia, watu wenu wanatunyang’nya ng’ombe kwa nguvu. Mtu anakamata mbuzi saa mbili asubuhi saa nne anauliza anasema ng’ombe, mbuzi wamekosa mwenyewe. Ni Mmasai gani anatelekeza mifugo? nani kwenye dunia hii? Sisi tuko tayari kuwafa kwanza mifugo ipone. Yet wewe unakamata mbuzi wangu saa nne saa tano unauza unaniambia umekosa mwenyewe! Hapana bwana! Hapana! Hapana!

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri tunataka kwa mchakato wenu huu tuelekezeni sharia, watu wenu wanatuonea. kwa Namanga watu wanaovunja sheria wachukuliwe hatua lakini msituonee, fuateni sharia; na CAG nanyi mfuatilie, ni mifugo mingapi ambayo imeuzwa kwa kukosa wenyewe Namanga? Halafu mimi niambiwe kwamba Mmasai ameacha mbuzi, ameacha ng’ombe kwa kuogopa faini ya 500,000? si kweli, lakini inaonekana mnatunyang’anya mnatumia mgongo huo kwa sababu sheria hairuhusu kutaifisha, lakini mmetaifisha mifugo ya wafugaji kwa sabaubu tu mnasema imekosa mwenyewe kwa sababu sheria hairuhusu kutaifisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri umetusaidia mengi lakini naomba utusaidie Namanga hali yetu ni mbaya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga hoja mkono.