Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

Hon. Bernadeta Kasabago Mushashu

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Kilimo

MHE. BENARDETHA K. MUSHASHU: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nampongeza Mheshimiwa Waziri na Manaibu wote wawili kwa hotuba nzuri, lakini nawapongeza hasa kwa kuleta mpango wa bima ya mazao. Hii ndiyo itakuwa mkombozi wa mkulima kwa sababu kukiwa na majanga ya ukame, mafuriko au mashamba yakavamiwa na wadudu kama viwavi jeshi mkulima akapata hasara, hasara hii itaweza kulipiwa na hii bima ya mazao. Nawapongeza sana kwa huo mpango.

Mheshimiwa Spika, msimu uliopta Mkoa wa Kagera tulipata changamoto kubwa sana katika kuuza kahawa. Wakulima waliuza kahawa lakini hawakulipwa malipo yao, lakini na malipo yaliyotolewa ya awali yakawa madogo sana, shilingi 1,000. Ikambidi Waziri Mkuu atoke hapa aje Mkoa wa Kagera akaongea na wakulima, vyama vya msingi, vyama vikuu vya ushirika, viongozi wa Serikali, wafanyabiashara, lakini vilevile akaweza kuhakikisha kwamba wakulima wameanza kulipwa; namshukuru sana.

Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nampongeza Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mheshimiwa Brigedia Jenerali Mstaafu Marko Gaguti, wakuu wa wilaya, Mrajisi wa Vyama vya Ushirika wa Mkoa ambao wamelifanya sasa agenda ya kahawa kuwa agenda ya kudumu kwenye vikao na kila mahali wanapokaa. Matokeo yake ni kwamba sasa kwa msimu uliopita wote waliouza kahawa wameweza kulipwa, hata zile arrears tunazosema malipo ya pili wamepata angalau ni kidogo KDCU wametoa shilingi 100 kwa kila kilo, KCU wametoa shilingi 150. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo langu kubwa ambalo bado naliona; bei ya kahawa bado ni ndogo sana. Mkulima amepata kati ya shilingi 1,000 na 1,150, kitu ambacho kinamfanya anakata tamaa. Natoa ushauri kwa Serikali kwamba kwanza kabisa tafuta masoko ya kuuza kahawa, nenda nje muingie mikataba na nchi ambazo ni marafiki wakulima waweze kuzalisha kufuatana na mahitaji ya soko, waunganishe na soko waweze kuuza, waruhusu wanunuzi binafsi ambao tayari wana masoko kule nje waweze kuuza, muwape vibali mapema waende kuuza kabla Brazili na Vietnam ambao ni wakulima wakubwa hawajaingiza kahawa kwenye mzunguko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile ninaomba ukija kuhitimisha utuambie ili yasijitokeze yaliyojitokeza kwenye msimu uliopoita kwa wakulima kahawa; je, kwanza tayari mmeshapata soko la kununua kahawa mwaka huu? La pili, je, kuna utaratibu gani utakaotumika kwenye msimu huu ambao umeanza tena huu mwezi wa tano, ni utaratibu gani utakaotumia katika kuuza kahawa?

Na mwisho, mtueleze, je, bei ya kahawa itaweza kupanda angalau kutoka kwenye 1,000 hadi 2,000 kwa mwaka huu kwa mkulima wa Kagera ili aweze kunufaika?

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)