Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, labda na mimi niungane na wenzangu katika kumshukuru Mwenyenzi Mungu kwa alivyotuwezesha kutupa afya njema tukaweza kuwemo katika Bunge letu leo hii siku ya tarehe 27 Mei, siku ya Ijumaa.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mara nyingine nirudie kuwapongeza wapigakura wa Jimbo langu la Tanga Mjini. Kama nilivyosema kwa kubadilisha historia ya Tanzania na kuweza kumleta Bungeni Mbunge kutoka Kambi ya Upinzani kwa mara ya kwanza. Lakini vilevile niseme kwamba katika Wizara ya Elimu naunga mkono hoja iliyotolewa na Kambi ya Upinzani asilimia mia moja.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo nianze kuchangia kama ifuatavyo; moyo na engine ya nchi ni elimu na ndio maana wanataaluma wakasema education is a life of nation. Lakini vilevile nimnukuu aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Nelson Mandela, alisema kwamba education is the most powerful weapon which you can use to change the world yaani elimu ni silaha nzito ambayo inaweza ikaibadilisha dunia lakini sisi Tanzania imekuwa ni kunyume na ninasema hivyo kwa sababu leo ukienda katika Wizara ya Elimu kuanzia elimu ya nursery kuna matatizo, ukienda katika elimu ya msingi kuna matatizo, elimu ya sekondari kuna matatizo, ukienda kwenye vyuo vikuu ndio kabisa, sasa tujiulize hivi kweli miaka 55 baada ya Uhuru mpaka leo sisi Watanzania tunajadili madawati!
Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano wenzetu nchi ya India baada ya kupata Uhuru miaka 40 tayari Wahindi walikuwa wanaweza kutengeneza pikipiki aina ya Rajdoot, tayari walikuwa wanaweza kutengeneza magari aina ya Mahindra, tayari walikuwa wanaweza kutengeneza matreni, tayari wahindi baada ya miaka 40 waliweza kutengeneza vyombo vinavyokwenda aerospace katika anga za juu. Lakini leo Tanzania twajadili madawati, twajadili matundu ya vyoo, mashuleni vyakula hakuna it is a shame. Hii ni aibu, nchi kama Tanzania yenye rasilimali zote ambazo Mwenyenzi Mungu ametujalia lakini tumeshindwa kuisimamia vizuri elimu, tumeshindwa kuiweka misingi mizuri ya kielimu matokeo yake Tanzania tunakuwa na wa mwisho katika nchi tano za Jumuiya ya Afika Mashariki na kama sio ya mwisho basi labda tutakuwa tumeishinda Southern Sudan. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tunashindwa na Burundi, Rwanda,Uganda na Kenya. Leo Burundi waliokuwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe wakauana watu milioni mbili lakini wana system ya one child onelaptop,sisi Tanzania ambao tunajisifi tuna eneo kubwa la nchi, tuna uchumi imara lakini tumeshindwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi niseme na niishauri Serikali tusichanganye siasa na elimu. Tunaposema elimu bure basi iwe bure kweli, lakini kama tunawacheza shere Watanzania Mwenyenzi Mungu atakuja kutuhukumu kesho. Leo tumesema elimu bure, lakini hivi ni kweli elimu ni bure?
Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda shule za msingi leo hata maji ya kunywa watoto hakuna, kama pana nyumba ya jirani wakimbilie nyumba ya jirani kwenda kunywa maji. Leo watoto wa kike Ashakum si matusi anapokwenda kujisaidia lazima apate maji, shule zimekatwa maji, wanategemea kwenda katika nyumba za jirani, kama kuna muhuni, mvuta bangi huko mtoto wa kike ndio anaenda kubakwa huko huko.
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hivi wenzetu hamuoni kwamba haya ni matatizo. Sisi wapinzani tuna akili gani na ninyi wenzetu wa Chama Tawala mna akili gani. Miaka 55 baada ya Uhuru leo, tunajadili matundu ya vyoo, na ukiangalia hata katika matangazo ya Haki Elimu, mwalimu anakwenda kwenye choo na wanafunzi wamepanga mstari wanasukumana, choo hakina bati, hakijapauliwa, mwalimu anakanyaga mawe, lakini tunaambiana hapa ukitaka kuwa Rais lazima upitie kwa mwalimu, ukitaka kuwa Mbunge lazima upitie kwa kwa mwalimu, ukitaka kuwa Waziri Mkuu upitie kwa mwalimu. Tuna wacheza Watanzania shere, tuwaambieni ukweli kama tumeshindwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi niseme kitu kimoja tu kwenye suala la elimu ya nursery, Mheshimiwa Waziri lazima ukasimamie vizuri kwa sababu elimu ya nursery tumeweka utaratibu kwamba mtoto haanzi standard one mpaka apite nursery school, lakini hivi Serikali imeangalia ufundishaji na mitaala ya kwenye nursery school? Hakuna kitu kila mwenye nursery school yake ana mitaala yake ana utaratibu wake wa kufundisha. Hii ni hatari kwa sababu mwingine anaweza akawa ana uwezo mzuri wa kufundisha, mwingine hana uwezo mzuri matokeo yake sasa wazazi wanapoteza fedha lakini watoto wakitoka huko kwa sababu msingi sio mzuri hakuna kitu wanapofika standard one.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi kwenye elimu ya msingi, hapa pana matatizo makubwa. Kwenye elimu ya msingi katika nchi yetu kumekuwa na utaratibu kwamba kwanza watoto wanakwenda shuleni wakati mwingine hata chakula mtoto hajapata nyumbani. Sasa matokeo yake mtoto anakwenda na njaa, na mtu mwenye njaa hafundishiki, matokeo yake mimi nilikuwa naishauri Serikali ikibidi lazima tupeleke bajeti ya chakula katika shule zetu za msingi, hata na sekondari.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu mtoto anapotoka nyumbani, anapokwenda shuleni na njaa hata mwalimu afundishe namna gani anakuwa haelewi. Amesema mwanafalsafa mmoja anaitwa Bob Marley, the hungry man is angry man, kwamba mtu mwenye njaa anakuwa na hasira, haelewi. (Makofi)
Kwa hiyo, mimi niseme tupeleke bajeti kubwa ya chakula katika shule za msingi na sekondari na vyuo. Hata wale wanaotu-supply vyakula katika vyuo vyetu na shule zetu basi walipwe kama alivyotangulia kusema msemaji aliyetangulia, kwa sababu wengine wanapelekwa mahakamani, wametoa zabuni za vyakula Serikali haijawalipa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini lingine kwenye sekondari kuna matatizo makubwa, kuna suala zima la ukosefu wa walimu wa sayansi. Hakuna walimu wa mathematics, biology, physics na chemistry. Matokeo yake mtoto anamaliza form four hata ukimuuliza what is bunsen burner hajui, ukimuuliza what is test tube hajui, na matokeo yake wanakosa katika theory na practical zote wanakosa.
Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimtake Waziri ahakikishe maabara zinazojengwa zinaambatana pamoja na vifaa. Tusiseme tu kisiasa kwamba tunajenga maabara kumbe vifaa hakuna na matokeo yake hata wanaokuwa wanachukua masomo ya sayansi, kwa mfano wanaosoma PGM ndio hao tunaotegemea kwamba watakuja kuwa marubani. Lakini kwa ukosefu wa vifaa sasa tunakosa ma-pilot katika ndege zetu, matokeo yake tunaajiri wageni tunapeleka ajira katika nchi nyingine, mimi niseme lazima tujikite katika elimu iliyo bora kweli.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukienda kwenye suala zima la vyuo vikuu. Vyuo vikuu kuna matatizo, na matatizo ni hayo ya mikopo, lakini hata na matatizo na uwezo wa wanafunzi wenyewe wengine wanaopelekwa. Lakini hata baadhi ya walimu pia nao uwezo wao sio mkubwa sana, matokeo yake sasa wanafunzi wetu wa vyuo vikuu wamekuwa nao elimu yao ikishindanishwa na nchi nyinine inakuwa sio bora.
Pia yupo Makamu Mkuu wa Chuo kimoja alisema, hata wanafunzi wa chuo kikuu hawawezi kuandika barua ya kuomba kazi, kwa kiingereza kwa sababu msingi ulikuwa ni mbovu, leo mtoto anakwenda shule ya msingi na njaa, leo mtoto anakuwa hana chakula, matokeo yake anateseka na njaa mpaka mchana, anatoka shule hana alichoelewa.