Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Jesca David Kishoa

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuweza kuchangia.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuchukua fursa hii kukishukuru Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ngazi ya Kamati Kuu kwa kuniteua kuwa mgombea wa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu Baraza la Wanawake upande wa Bara. Pia nitumie nafasi hii kuwashukuru Kamati Tendaji ya Baraza Taifa ambao wamenipa ushindi wa kishindo wa asilimia 84 kwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu upande wa Bara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nichangie, na nijikite upande wa Wizara ya Nishati. Nitazungumzia upande wa TPDC hoja ambayo kwenye hotuba ya kamati imezungumzwa.

Mheshimiwa Spika, pamoja na jitihada ambazo zinaonekana kufanywa na TPDC bado kuna changamoto kubwa ambayo inaendelea kwenye Kampuni hii ya mafuta na gesi ya Taifa hili; na changamoto hii ni kukosa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mikubwa. Ni bahati mbaya sana tumekuwa na changamoto kubwa ya viongozi ambao wamekuwa wakitoa kauli za mazoea. Kuna kauli mbili ambazo zimekuwa zikitamkwa na viongozi pale ambapo wanakuwa wanaona joto la wananchi wa Tanzania lipo juu kuhusiana na utekelezaji wa miradi.

Mheshimiwa Spika, moja ya kauli ambayo wamekuwa wakiisema, wamekuwa wakisema kwamba mradi huu haujatekelezeka kwa sababu majadiliano yanaendelea, hiyo ni kauli namba moja. Kauli namba mbili wamekuwa wakisema mradi huu haujatekelezeka kwa sababu majadiliano kuchukua muda mrefu ni jambo la kawaida sana.

Mheshimiwa Spika, naomba niseme jambo moja. Si kawaida kabisa majadiliano kuchukua muda mrefu, this is very primitive thinking, haya ni mawazo mgando, ni lazima tuseme. Nilisoma jarida la The East African la mwaka jana mwezi wa 5 tarehe 15 kuna kampuni moja kubwa sana inaitwa Delloite; kati ya makampuni 4 makubwa, Delloitte ni mojawapo ambayo imeeleza specifically Tanzania imepoteza sifa ya kuwa nchi yenye vivutio vya kuwekeza kwa sababu tu ya kuchelewa (delays), kuwa na mawazo mgando, mawazo ya kujadiliana muda mrefu, majadiliano yasiyokwisha, miradi isiyotekelezeka; tumeingia kwenye rekodi kama taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi wa LNG ni moja ya mradi ambao unaonesha namna ambavyo Serikali inashindwa kuchukua maamuzi kwenye mambo mazito na makubwa kwa maslahi ya taifa. Serikali kwenye mradi wa LNG umekuwa ukitoa kauli za mara kwa mara kwamba majadiliano yanaendelea. Ni mwendo wa konokono, kwa maana ya kwamba hakuna kinachoeleweka mpaka dakika hii, miaka na miaka hakuna kinachofanyika, investment ya over 30 billion dollars katika Taifa letu, investment ambayo ni kuwa East Africa nzima hakuna lakini Serikali inashindwa kufanya maamuzi sahihi, wanakimbilia kusema kwamba kuna migogoro kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Spika, let me ask you something. Kwa muda gani tunakwenda kusubiri kuona migogoro ya wawekezaji inakwisha, what if kama migogoro yao ikichukua miaka 50? Tunakwenda kuwasubiri kwa muda kwa kiasi gani? Mlitafuta kampuni kwa ajili ya ku-negotiate on behalf of the Government kwenye mradi huu wa LNG kwa sababu ya ukubwa wake. Mmeshindwa kweli kuibana/ku-deal na kampuni hii ikaja na majibu ya uhakika ya namna gani mnavuka /mnakwenda kutekeleza mradi wa LNG kwa kuwepo na huu mgogoro ambao ni wa wawekezaji?

Mheshimiwa Spika, mambo kama haya, mradi mkubwa kama huu ambao unaangaliwa kwenye mataifa mengi ndivyo hivi vitu vinavyo-test credibility ya Serikali katika Taifa letu. Sasa ni vema Serikali ikatuambia kwenye mradi wa LNG, mradi ambao ni mkubwa sana na unakwenda kusaidia wananchi wengi sana katika Taifa letu; kampuni hii imeshindwa kweli kutekeleza/kutusaidia kuvuka hapa na tukahakikisha kwamba tunaweza kutekeleza mradi huu?

Mheshimiwa Spika, bado kuna suala la mwendo wa konokono kwenye mradi wa Bomba la Mafuta la Hoima. Nimemsikiliza Mkurugenzi wa TPDC mwaka jana mwezi wa tisa anasema mradi huu utatekelezeka lakini bado majadiliano yanaendelea; bado tupo palepale mwendo wa konokono, haya majadiliano yanakwenda mpaka lini? Haya majadiliano yanakwenda kwisha lini? Dunia inakwenda speed sana, lazima tu-cope na speed ambayo dunia inakwenda.

Mheshimiwa Spika, kuna mradi wa kiwanda cha mbolea kule Lindi (Fertilizer Plant). Kuna makampuni matatu makubwa kutoka Ujerumani ambayo yameomba kujenga kiwanda cha mbolea Mkoani Lindi na kiwanda hiki kinakwenda kutumia gesi, lakini cha kusikitisha ni kwamba pamoja na kwamba kiwanda hiki kinakwenda kuwa kikubwa Afrika nzima lakini Serikali kupitia TPDC bado inakwenda mwendo wa konokono. Ni vema tukaelewana hapa vizuri sana. Kupitia vyombo vya habari nilishuhudia Mheshimiwa Rais akiongea na Chancellor wa Ujerumani wakizungumza namna gani wanakwenda kutekeleza mradi huu lakini mpaka sasa hivi ni story tupu, hakuna kinachofanyika.

Mheshimiwa Spika, labda nizungumze kidogo kuhusiana na mradi labda mnaweza mkaelewa kuanzia hapo. Kama tunataka ku-transform Taifa hili kwenye sekta ya agriculture, hiki kiwanda hakiepukiki kwa namna yoyote ile. Hakiepukiki kwa sababu wote tunajua kwamba 75 percent ya wananchi wa Tanzania wanashiriki kwenye Sekta ya Kilimo. Serikali imekuwa ikiagiza mbolea kutoka nje; asilimia 90 inayotumika Tanzania inatoka nje.

Mheshimiwa Spika, takwimu za mwaka 2016/2017 zinaonesha Serikali iliagiza tani za mbolea takribani 150,000, lakini kama ikitokea tukakubali mradi huu/kiwanda hiki kikajengwa, tunakwenda kutengeneza tani 1,300,000 za mbolea kwa mwaka. Kwa hesabu za haraka haraka ni kwamba nchi hii ili iweze kupata mbolea ya kutosha inahitaji mbolea zaidi ya tani 580,000, kwa hiyo tukipata tani 1,300,000 tuna uhakika wa kupata mbolea ndani na tuna uhakika wa kuuza mbolea nje, tunasubiri nini? What are waiting for? Hiki kiwanda kinakwenda kutengeneza zaidi ya ajira 500,000 kwa wananchi wa Tanzania lakini shida inabaki palepale, ukiuliza unaambiwa majadiliano bado yanaendelea yaani ni mwendo wa konokono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na mimi nafikiri huu mwendo wa konokono tukawa na jambo moja, unatokana na hofu ya viongozi kwenye sekta husika, wanahofu ya kutumbuliwa. Kumekuwa kuna shida hii kubwa, maamuzi magumu ambayo yanatakiwa yafanywe kwa maslahi ya Taifa, viongozi wa Serikali wameingiwa na hofu wanashindwa kuyafanya kwa kuhofu kutumbuliwa na Mheshimiwa John Pombe Magufuli.

Mheshimiwa Spika, ninaomba kutumia fursa hii kuiomba Serikali iipe nguvu TPDC, TPDC haiwezi kufanya kazi kama hamuwezi kuipatia fedha kwa namna yoyote ile. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie na hoja ya TEITI; nilizungumza hapa mwaka jana kwamba na kwenye taarifa ya kamati imezungumzwa. TEITI iligundua kuna ubadhilifu wa zaidi ya bilioni 30 kwenye sekta ya madini; lakini tangu mwaka jana mpaka hivi ninavyozungumza hatujaona taarifa yoyote ambayo inaweza kuelezea na kudadavua suala hili. Nilipozungumza suala hili mwaka jana, Waziri wa Madini wa wakati huo Mheshimiwa Angella Kairuki alisimama na kusema suala hili lipo kwa CAG na litafanyiwa kazi mpaka kufikia mwezi wa 12... (Makofi)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. JESCA D. KISHOA:… lakini mpaka hivi ninavyozungumza hakuna tatizo…

T A A R I F A

SPIKA: Mheshimiwa Kishoa kuna taarifa unataka upewe.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nataka nimpe tu taarifa mchangiaji anayechangia sasa kwamba viongozi wa Serikali wakiwemo Mawaziri, Wabunge, RAS pamoja na RAS wa Mkoa wa Songwe Mheshimiwa Kafulila wapo vizuri hawa hofu yoyote na ndio maana nchi yetu ya Tanzania inaendelea kupaa, miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa. Sasa kama anachangia aende kwenye hoja za msingi asizungumzie suala la viongozi wana hofu, wapo vizuri, imara na wanatekeleza majukumu yao ipasavyo, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Shemeji umepewa taarifa hiyo, unasemaje? (Kicheko/Makofi)

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, kunaona kuna taarifa kupokea hapo? Kwanza nimuulize TEITI ni kitu gani, do you know what is TEITI, unajua TEITI ni kitu gani? Tunazungumzia issues, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni tunazungumzia issues, we are not doing politics here tena cheap politics; tunazungumzia masuala kwa maslahi ya Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka wakati Waziri wa Madini au Waziri wa Nishati, maana TEITI bado haijajulikana iko Wizara gani, anapokuja kuhitimisha hapa atuambie fedha zetu bilioni 30 ambazo zimeonekana zimepotea kwenye Wizara ya Madini zimekwenda wapi, kwa sababu ni taarifa ya kutoka TEITI na TEITI ni shirika la Serikali.

Mheshimiwa Spika…

SPIKA: Ngoja upokee taarifa Mheshimiwa Jesca.

T A A R I F A

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Spika, ili tumsaidie mtoa hoja, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wakati anahitimisha hoja yake, awe focused, ninataka tu nimpe taarifa msemaji na kwa kweli Mheshimiwa Angellah Kairuki wakati akiwa Waziri alilieleza vizuri sana; hakuna fedha iliyopotea. TEITI kinachotokea ni kwamba makampuni yanapeleka hesabu na wao wanakwenda kuangalia kule mnakopeleka fedha kwa ajili ya kufanya reconciliation.

Mheshimiwa Spika, kilichotokea ni kwamba yule mtu aliyekwenda kufanya reconciliation alivyokwenda kwenye source akakuta kilichoripotiwa na makampuni na kile kilicholipwa kuna difference ya hizo fedha. Na sasa kinachotokea ni kwamba kuna mahali pengine ambapo wameripoti wamelipa shilingi kumi halafu kuna mahali hiyo shilingi kumi imeripotiwa mara mbili. Kwa hiyo CAG anachokwenda kufanya ni verification ya hiyo reporting, huo sio wizi. Na kwenye ripoti hiyo imeelezwa sio wizi, ni reconciliation. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninaomba kumpa taarifa hiyo.

SPIKA: Mheshimiwa Kishoa, malizia maana yake muda hauko upande wako.

MHE. JESCA D. KISHOA: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana, napokea taarifa yake kwa sababu amekiri kwamba kuna fedha bilioni 30 hazionekani. Lakini pia kuna shida gani kumpa CAG akakagua hizi bilioni 30 zimekwenda wapi? Kwa nini suala hili limepigwa danadana toka mwaka jana, shida iko wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nafikiri hakuna sababu ya Waheshimiwa Mawaziri kuendelea kujitetea kwenye hili, ni suala la mambo kuwekwa wazi kuonekana kwamba, okay reconciliation inatakiwa ifanyike; imefanyika? Hizo fedha ambazo zimepotea zimekwenda wapi? Kwa nini maswali haya yanakosa majibu? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante, ni kengele ya pili.