Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Ezekiel Magolyo Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nashukuru na kimsingi nilikuwa nimeshasimama kwa ajili tu ya kusemea hili la maafa. Kimsingi mimi nimesimama kuunga mkono hilo wazo, lakini nilichotaka kuomba ni kwamba chochote tutakachokifanya kiwe ni kwa Tanzania nzima kwa sababu madhara yako kwa nchi nzima, isiwe kwa Kilwa peke yake. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hilo, naomba nami nirudi kwenye mada. Nazipongeza sana Kamati zote mbili, kwa niaba ya Bunge lako zimefanya kazi kubwa sana. Kipekee naomba niipongeze sana Serikali yangu kama ambavyo Waheshimiwa Wabunge wengi wamesifu, kazi zinazofanyika ni kubwa na nzuri sana.

Mheshimiwa Spika, kama ambavyo wamesema Waheshimiwa Wabunge wengi, nikianza na Sekta ya Umeme, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa rafiki yangu Dkt. Medard Kalemani na Wizara kwa ujumla, wamefanya kazi nzuri na kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nifafanue tu kidogo kwa sababu katika Jimbo langu la Msalala tulinufaika na REA II ambayo katika Kata 18, Kata 12 tayari zilishaunganishiwa umeme; na hivi sasa kwenye hii REA III utekelezaji wa mradi unaendelea lakini umeanzia upande wa Halmashauri nyingine. Namwomba tu Mheshimiwa Waziri kwamba wananchi wanalifahamu hili, lakini angalau ule mpango wa ujazilizi uende kwa kasi kidogo kwa sababu tayari kuna Kata 12 tuna umeme, lakini hata maeneo hayo ambayo umeme umeshafika kama Busangi, Segese, Lunguya na Kakora, umeme upo lakini bado haujasambazwa vya kutosha.

Mheshimiwa Spika, naomba Meshimiwa Waziri alitazame hili na ninaamini anaweza kwa sababu kama ambavyo wengi tunamwona, amefika kwangu mara mbili, amelizungumzia suala hili na ninaamini kwamba litafanikiwa kwa mapema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba kipekee nitumie muda mwingi zaidi kwenye eneo la madini. Kama ambavyo unafahamu mimi natoka ulipo mgodi wa Bulyanhulu na kwa miaka yote 15 ambayo nimekuwa Mbunge nimekuwa nalalamikia sana namna ambavyo sisi wananchi tuliopo pale ambavyo tumekuwa tukiishi na mgodi wa Bulyanhulu.

Mheshimiwa Spika, na baada ya Mheshimiwa Rais kuwa amechukua hatua hizo alizochukua hizo alizochukua mwaka 2017, nilisimama hapa Bungeni nikampongeza sana, na nilisema kwamba kiukweli kwa sisi tunaoifahamu Acacia ilivyokuwa, ilikuwa haiwezekani kuleta mabadiliko kwenye sekta ya madini bila kuwa na Rais mwenye msimamo na approach ambayo Rais Magufuli ametumia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba tu nilikumbushe Bunge lako Tukufu kwamba manung‟uniko kwenye sekta ya madini hayajaanza leo na jitihada za kurekebisha mambo yalivyo kwenye sekta hiyo haijaanzia kwa Mheshimiwa Rais Magufuli. Mwaka 2005 Mheshimiwa Rais Kikwete anaingia madarakani, moja ya vitu alivyovizungumzia na kuvifanyia kazi ni suala la madini. Alianzisha Tume ya Bomani na mimi nilikuwa mjumbe, tukafanya kazi kubwa. Baadaye ikasababisha kupendekezwa na kupitishwa Sheria ya Madini ya mwaka 2010; na tukaanza zoezi la kuwaomba hawa wawekezaji waingie kwenye platform mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lile halikuzaa matunda makubwa kwa sababu ya Acacia. Ikumbukwe kwamba Acacia ndiye mwekezaji mkubwa kwa Tanzania, ana migodi mitatu. Kwa mwaka 2012 dhahabu iliyozalishwa Tanzania wakia milioni 1.3; migodi ya Acacia ilizalisha zaidi ya asilimia 60. Kwa nguvu hiyo waliyokuwa nayo walikuwa ni kikwazo kikubwa sana katika kuleta mabadiliko kwenye sekta hii.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, miongoni mwa mambo yaliyopendekezwa na Tume ya Bomani ilikuwa ni kuhakikisha wananchi waliopo jirani na maeneo ya mgodi wanalipwa fidia stahiki. Wenzetu wa Mgodi wa Geita walifanya hivyo; Vijiji vya Mtakuja, Nyamalimbe na Katoma vikalipwa fidia. Toka mwaka 1996 mpaka leo Mgodi wa Bulyanhulu ulipoanzishwa hakuna kijiji hata kimoja kilicholipwa fidia pamoja na kwamba mgodi upo kwenye eneo la vijiji. Kisa ukiwauliza wanasema tuna MDA the issue is the government, sisi ni wawekezaji; kwa kifupi walikuwa wanagoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tukapendekeza, na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 ikapendekeza mrabaha utoke asilimia tatu hadi asilimia tano na baadaye asilimia sita; migodi mingine ikakubali wao wakawa wamekataa. Tukasema service levy isilipwe kwa lump sum ya dola laki mbili, iwe 0.3 percent migodi ya Geita GGM wakaanza kulipa, Acacia wakakataa.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kila kilichokuwa kikifanyika, Acacia walikuwa ni kikwazo. Ilikuwa haiwezekani kufanya mabadiliko kwenye Sekta ya Madini bila kuwa-engage seriously hawa. Na pale jitihada za kuwa-engage kidiplomasia kwa lugha ya kawaida ambayo wengine wanapenda zitumike, zilipofanyika ilishindikana. Ndiyo maana Mheshimiwa Rais baada ya kuja na hii approach ambayo ilisababisha dunia nzima kujua kwamba kweli Maige amekuwa akisema Acacia ni wezi, imekuja kuthibitika kwamba kweli wamekuwa wakitorosha madini.

Mheshimiwa Spika, tusingeyakamata yale makontena ambayo yapo Dar es salaam na kufanya uchunguzi wa kilichomo mle na kuitangazia dunia kitu gani kipo mle, dunia isingejua. Kwa kufanya hivyo kwa kuonesha kwamba kweli Acacia wana matatizo, ilisababisha the whole word ikawa on our side na ndio maana wao wenyewe wakaja mezani na wakawakana Acacia wakaja Barrick wanasema tuzungumze. Wangekuwa hawatendi makosa au wangekuwa hawakutenda makosa wasingekubali na tusingefika hapa tulipofika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kimsingi nampongeza sana Mheshimiwa Rais, amefanya kazi kubwa sana na Mungu azidi kumsaidia. Akifika; na wote mnajua mliofika Kakola na Bulyanhulu mnajua kilio cha wananchi wale, leo hii ukifika Kakola, Bulyanhulu na Msalala wananchi wana furaha sana hatua iliyofikiwa ni kubwa sana. Naipongeza sana Serikali na nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa hiyo hatua ambayo imefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais lakini Mheshimiwa Waziri amelisimamia vizuri sana suala hili, suala la wachimbaji wadogowadogo. Baada ya kuwa Serikali imeanza kubana hawa wawekezaji wakubwa mwaka 2015, uzalishaji wa dhahabu ukasimama Mgodi wa Bulyanhulu, tulitegemea uzalishaji wa dhahabu na mapato yanayotokana na dhahabu yashuke; lakini cha ajabu mapato yanayotokana na sekta ya madini yameongezeka kutoka bilioni 130 hadi zaidi ya bilioni 300. Nini kilichofanya matokeo hayo; ni kwa sababu ya kuruhusu wachimbaji wadogowadogo.

Mheshimiwa Spika, leo hii soko dogo la Kakola pale kwangu linauza zaidi ya kilo nne za dhahabu kila siku. Soko la Madini la Kahama linauza zaidi ya kilo 20 za dhahabu kila siku, na hizi zote zinatoka kwa wachimbaji wadogowadogo. Maeneo ambayo wakati wa nyuma yalikuwa yamezuiwa yamewekwa kwenye utafiti wa makampuni makubwa, leo wanafanya wachimbaji wadogo na hizi dhahabu tunapata na maisha yanaendelea. Nawapongeza sana Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, kwa hii dakika moja/mbili zilizobaki nizungumzie maboresho kidogo ambayo yanapaswa yafanyike. Na Mheshimiwa Waziri Biteko naomba unisikilize sana. Kwa kuwa maeneo mengi hayana proper licenses, wachimbaji wanaochimba sasa hivi ni wale wenye vikundi; kumekuwepo matatizo mawili; la kwanza kumekuja mtindo wa wasimamizi kuwa wanachukua asilimia 30 ya mawe yanayochimbwa, hili jambo linaleta mgogoro mkubwa. Hii ada ya usimamizi ili Serikali ipate asilimia saba yake, anapewa mtu asilimia 30 ya ada ya usimamizi, wapi na wapi? Ndiyo maana unakuta mgogoro pale Namba Tisa unajua nilikueleza.

Mheshimiwa Spika, wanakuja watu sasa hivi tunaanza kupambana na mabeberu wa ndani kwa sababu vile vikundi vya wananchi wa pale havipewi nafasi, wanakuja mabeberu wa ndani, na nilishakupa majina, wale watu wanapewa usimamizi. Leo hii Wisolele wanasema wachimbaji wadogo wadogo wa pale hawawezi wakapewa kibali cha kuchimba mpaka yule mtu aliyemtaja ambaye nilisema anahusiana na mtu fulani kwenye kamisheni na yule mwingine na yule mwingine. Ninatunza majina kwa sababu Mheshimiwa Waziri tulishaongea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake sasa hivi kumeanza kutokea manung‟uniko, hebu Mheshimiwa Waziri lirekebishe hili wachimbaji wadogowadogo kupitia vikundi vyao ambao wapo kwenye maeneo wapewe vibali na waendelee kuchimba, hili litatusaidia sana.

Mheshimiwa Spika, pia Mheshimiwa Waziri nijaribu tu ku-observe, kwamba hivi sasa Kamisheni ya Madini inachukua asilimia saba ya mawe, lakini pia wanapokwenda ku-process kwenye ile mialo, dhahabu inayopatikana na kwenye elusion wanapopata dhahabu nako inachukuliwa asilimia 7. Ukiangalia kiuhalisia ni kwamba kuna double royalty; tusichukue marabaha kwenye mawe.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu sasa hivi tumeshadhibiti utoroshaji wa dhahabu, tuchukue mrabaha kwenye dhahabu, haya mawe yasimamiwe vizuri, yaende kwenye proper registered sijui kiingereza wanaitaje lakini kwa Kiswahili tunaita mialo, yaende kwenye proper registered mialo, pale dhahabu ikipatikana asilimia saba ichukuliwe.

Mheshimiwa Spika, unajua wachimbaji wadogowadogo waliopo kule wengi wao unakuta wapo kwenye vikundi wanakuwa kikundi cha watu 20, wanapata mifuko 50 wakichukua mifuko 50, mifuko ya Serikali inakuwepo labda mifuko nane. Ikishachukuliwa mifuko nane wanatoa na gharama zingine unajikuta kila mchimbaji anapata mfuko mmoja au robo mfuko, wanatesema sana. Wale wachimbaji kabisa kwa maana ya wale wanaoingia kwenye mashimo.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naipongeza sana Serikali, hatua hizi ni kubwa na nzuri lakini haya madogomadogo ambayo nimeyazungumzia yaweze kurekebishwa.

Mheshimiwa Spika, la mwisho; tumefanya makubwa na tumefikia hatua kubwa ya kuanzisha hii kampuni ya Twiga. Niombe madai ya wananchi wa Bulyanhulu toka mwaka 1996 kama migogoro mingine ya wafanyakazi…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Ezekiel bahati mbaya muda haupo upande wako.

MHE. EZEKIEL M. MAIGE: Mheshimiwa Spika, sentensi moja tu. Na migogoro ya hawa wafanyakazi waliofukuzwa na wengine wagonjwa, hebu tuimalize. Mheshimiwa Waziri tulishaongea lipo kwenye hatua ya mwisho. Basi kwa hayo, naunga mkono hoja naamini Serikali itaendelea kutenda mema, ahsante sana. (Makofi)