Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Ally Mohamed Keissy

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama Kuhusu Shughuli za Kamati Kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili nami nichangie. Mimi mjumbe wa Kamati ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Spika, sisi Wabunge tupo humu na baadhi ya Wabunge wapo humu hawajamaliza hata jimboni kwake kutembelea vijiji. Lakini Mheshimiwa Waziri wa Nishati na Madini na Naibu wake wametembea kila jimbo katika nchi, kila kona na wakati huo huo nao ni Wabunge na wana majimbo yao. Wapo baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wanaishia Dodoma - Dar es Salaam, hawaendi kwenye majimbo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa moja ametoka kuzungumza hapa, wa Kamati ya Madini, kwenye kamati yetu; yeye hahudhuri vikao, ni kesi mahakamani kila siku Dar es Salaam, na yeye ananiambia Mheshimiwa Keissy mpaka hela nimeishwa, anajijua. Ametoka kuchangia hapa kwa hasira na kwa kupiga kelekele lakini ukienda kwenye record katika Kamati si mhudhuriaji.

Mheshimiwa Spika REA peke yake Tanzania tuna vijiji 12,268 vinawekewa umeme. Leo anazungumza kwamba wananchi hawajapata umeme nchini; labda kwake jimboni kwake; lakini sisi tunashukuru sana; majimbo yetu ya kule Mkoa wa Rukwa na Katavi ilikuwa ni mwisho kabisa wa nchi hatukuwa na umeme, hata mara moja kwenye vijiji vyetu. Kuna sehemu ambazo hazina hata barabara lakini REA wamepeleka nguzo na wanaendelea kufanyakazi na wananchi wanapata umeme.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Heche hawezi kusema Wizara haijafanya kazi, Wizara imefanya kazi; wewe ni jela na wewe, na kwasababu haudhurii vikao, kila siku Mahamani Dar es Salaam; na hiyo itaku-cost kwenye jimbo lako.

Mheshimiwa Spika, hii sekta ya nishati na madini ndiyo itakayotusaidia sana kwenye Serikali yetu, kwa sababu hatuwezi kwenda kwenye viwanda kama hatuna umeme, haiwezekani!

Mheshimiwa Spika, umeme ndiyo nguzo kubwa ya viwanda, huwezi kujenga kiwanda bila umeme, na serikali ina umeme wa ziada na huu umeme wa Grid ya Taifa; ndiyo sababu Mikoa ya Rukwa, Katavi na Kigoma tunauomba kwa sababu serikali inapata hasara sana kwa mafuta. Ifanye jitihada ipeleke umeme wa Grid ya Taifa kwenye mikoa mitatu; kwa sababu Serikali na TANESCO inapata hasara kila mwezi mabilioni ya fedha kwa kutumia mafuta. Kwa sababu tutaokoa; kwa sababu kuna mpango kabambe wa Serikali wa kupeleka umeme wa Gridi ya Taifa kwenye mikoa yetu hivi karibuni. Serikali mpaka ikifikia mwaka 2021 itamaliza vijiji vyote katika nchi hii kupelekewa umeme, lazima tushukuru sana.

Mheshimiwa Spika, Waziri wa Madini vilevile amesaidia sana; ametembea nchi nzima, kila kwenye mgodi anafika na wamesaidia sekta ya madini mpaka sasa kuongeza pato la Serikali. sasa nashangaa anasimama hapa Mheshimiwa anasema sekta ya madini inazidi kushuka chini. Chukua data kwa Mheshimiwa Waziri, chukua data Wizarani kiasi gani tangu wewe umeingia ubunge mpaka leo hii ni kiasi gani cha pesa kimeingizwa? Wizara ya Nishati na Madini imeigiza kiasi gani? Mheshimiwa lia na lwako.

Mheshimiwa Spika, kama jimbo langu hakuna hata kijiji kimoja kitakosa umeme mpaka mwezi Juni, 2020. Vijiji vyote katika jimbo Nkasi Kaskazini vitapata umeme sasa nashangaa.

Mheshimiwa Spika, Wizara imesaidia sana Mheshimiwa Waziri. Nguzo tulikuwa tunaagiza nje, transformer tunaagiza nje, waya tunaagiza nje kila kitu tunaagiza nje; leo vyote vinatoka ndani ya nchi yetu. Tumeokoa kias gani fedha z kigeni katika nchi yetu? Hatupotezi hata senti tano kwaajili ya mambo ya umeme, vyote vinazalishwa katika nchi yetu na watu wanapata ajira katika nchi yetu. Tulikuwa kila siku tunaagiza nje, leo ndugu yangu unakaa unaiponda Wizara ya Nishati na Madini badala ya kuwasifu! Acha!

Mheshimiwa Spika, tumeingia gharama bilioni sita kwa ajili mradi wa Nyerere kule ili tupate umeme wa kuendesha reli yetu inayotumia umeme; leo unashindwa na ku-suport Serikali? Lia na lwako Mheshimiwa. Ukiona namna hiyo ujue sasa; Mheshimiwa Heche nakuonea huruma rafiki yangu, wewe ni rafiki yangu sana; wewe wasema hali ni mbaya. Ninyi wenyewe mnasema kujenga smelter ni miaka miwili; Chama chao kina miaka 28 hata ofisi hawana. Miaka 28 unasema sawa nyumba ya kawaida wewe kujenga kiofisi unatumia block 3000 na bati hakuna ukuchojenga miaka 28,…(Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Keissy!

MHE. ALLY K. MOHAMED: … hakuna, wanapanga kaofisi pale kwenye kanyumba ka kulala pale Kinondoni...

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa…

SPIKA: Mheshimiwa Keissy!

MHE. ALLY K. MOHAMED:… Makaburini pale, hata pa ku-park gari hakuna…

SPIKA: Mheshimiwa Keissy, Mheshimiwa Keissy kwa kweli kama kuna aibu kwa chama cha upinzani chenye ruzuku ya mamilioni, hata ofisi ya chumba na sebule kwa kweli? Mheshimiwa Kessy endelea bwana.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, tuna shida. Hata CUF pale Buguruni wana ghorofa.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Chief Whip, changamoto nyingine zichukue tu kazifanyie kazi, maana kunijibu itabidi utuonyeshe ofisi ilipo. Mheshimiwa Keissy tumsubiri Chief Whip atutajie ofisi yao iko wapi? Taarifa atupatie.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Eeh!

Mheshimiwa Spika, iko pale Ufipa Street, tena…

SPIKA: Ngoja kidogo basi atulie halafu uongee

MHE. ALLY K. MOHAMED: …karibu na makaburi pale Kinondoni.

SPIKA: Ngoja kidogo Mheshimiwa Keissy, unataka kuonywesha ofisi ilipo. Mheshimiwa Ester endelea.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, CHADEMA ina ofisi zaidi ya moja. Tuna ofisi kwenye kanda zetu na hatujapanga; na kwa ruzuku hiyo hiyo na tunaitumia vizuri. Tofauti yetu sisi na ninyi…

MBUNGE FULANI: Mwongo!

MHE. ESTER A. BULAYA: …mlirithi majengo ya Umma enzi ya Chama kimoja. Sisi tumejenga wenyewe na tuna mkakati wa kujenga ofisi hapa Makao Makuu ya Dodoma nyingine ya kisasa bila kutumia…

MBUNGE FULANI: Taarifa Mwenyekiti.

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba tusikilizane. Naomba tusikilizane Waheshimiwa. Taarifa hiyo anapewa Mheshimiwa Keissy. Mheshimiwa Keissy!

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, taarifa siipokei maana yake Sabodo mwenyewe aliyewapa shilingi milioni 100 wajenge ofisi, lakini hawakujenga hata msingi. Sabodo aliwapatia shilingi milioni 100 na kwenye TV mlichangia pesa…

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. ALLY K. MOHAMED: nanyi akina mama mnakatwa kila mwezi shilingi 1,200,000/=, zinakwenda wapi? Nyie wenyewe mnakuja kuniambia Mheshimiwa tutetee, tunakatwa hela!

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, taarifa, taarifa!

MHE. ALLY K. MOHAMED: Utanipaje taarifa wakati nyie wenyewe mmeliwa hela za Sabodo…

SPIKA: Naomba tusikilizane. Mheshimiwa Dkt. Mollel, tafadhali.

MHE. DKT. GODWIN O. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nilitaka kumpa taarifa mzee wangu mzuri sana, Mheshimiwa Keissy kwamba asipate shida, aendelee na msimamo huo huo kwa sababu mwenzetu pale amepata kile cheo. Alianzisha harakati ya kudai shilingi bilioni 13 ambazo hazionekani za CHADEMA. Kwa hiyo, mwisho wa siku akahongwa hicho cheo, ndiyo sasa hivi anapambana kukitetea ili asiendelee kudai shilingi bilioni 13. (Kicheko/Makofi)

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu) (Hapa Mhe.Ester A. Bulaya – Chief Whip wa Upinzani alisimama)
SPIKA: Mheshimiwa Ester wewe ni Chief Whip unajua taratibu, kwamba taarifa hiyo anayepewa ni Mheshimiwa Keissy. Kwa hiyo, mwache mwenye taarifa yake kwanza aipokee au aikatae. Kwa hiyo, tunarudi kwanza kwa Mheshimiwa Keissy aliyepewa taarifa. Mheshimiwa Keissy
MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, napokea taarifa kwa sababu CUF wana ofisi Magomeni inajulikana, ni ya ghorofa pale Buguruni; TLP wana ofisi pale Magomeni; NCCR wana ofisi pale Pangani…

MHE. JOHN W. HECHE: Mnaruhusu hii nyumba ya Watanzania inafanyiwa hivi!

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, sasa ile Ofisi pale jina la Ufipa lile makaburini, ndiyo ofisi yako. Hawana ofisi nyingine Makao Makuu, iko Ufipa. Vijana wa Ufipa!

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. ALLY K. MOHAMED: Mheshimiwa Spika, naendelea na mchango wangu kuhusu nishati na madini.

SPIKA: Endelea Mheshimiwa Keissy.

MBUNGE FULANI: Endelea, endelea, ongea na Spika. (Kicheko)

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

MHE. ALLY K MOHAMED.: Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati na Madini inafanya kazi na inajitahidi katika nchi hii, tulikuwa katika giza kwenye vijiji vyetu vyote katika nchi hii, lakini wanajitahidi na itafika mwaka 2022 hakuna hata kijiji kimoja katika nchi kitakosa umeme. Vijiji vyote vitawaka umeme. Hakuna hata kijiji kimoja kitakosa umeme!

Mheshimiwa Spika, hawaelewi. Waende mwambao mwa Ziwa Tanganyika ambapo hata barabara hakuna, lakini leo nguzo zinakwenda na wananchi wanapewa umeme na wananchi wanaishukuru sana Serikali na mtaona wenyewe mwaka wa Uchaguzi ndugu zangu umeme utatupa kura kwa kishindo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Spika, umeme utakuwa ndiyo miongoni mwa mambo ya kusema nasi tutakuwa kifua mbele kutetea kura zetu katika mwaka huu; mwezi Oktoba ni umeme katika nchi yetu. Hamwezi kuyumbisha wananchi, walikuwa ni shida. Mimi mwenyewe wakati naweka umeme katika Kijiji cha Kirando, hawa CHADEMA kwenye kampeni walisema haiwezekani labda umeme utoke DRC Congo, CHADEMA hawa! Leo ni ajabu, wanaona umeme unawaka Kirando na wameona ni waongo. Wenyewe kazi ni kuzusha vitu vya uongo; wanaweza kuwa na dhahabu wakakwambia shaba ukaamini. (Kicheko)

Sasa ndugu zangu tuwe wakweli. Leo ndugu zangu nyie umeme kwenye vijiji vyenu karibu vyote vinawaka umeme. Kaskazini huko mnakotoka nyie ndiyo mlianza kupata umeme, mkajiona nyie ndiyo safi. Sasa tunagawana kasungura kadogo kila kona. Kwa hiyo, ndugu zangu msituonee wivu, mwaka 2020 Oktoba, mtaona matokeo.

Mheshimiwa Spika, wakipita huko, wanaona kila kijiji kinang‟aa. Leo ukipaa kwenye ndege mzee hata ukienda porini unaona kijiji kinang‟aa kwa umeme. Sasa ndugu zangu tuangalie mabadiliko yanavyokuwa. Miaka hii minne hakuna vijiji visivyo na umeme. Tumeweka umeme zaidi ya 8,500. Anatoa tarakimu 2,800 ndiyo sijui ni kaya sijui nyumba wala haieleweki hesabu yake kama nilivyomwambia. Somo la hesabu mzee halidanganyiki! Hesabu haidanganyiki wala mtu hawezi kuamini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Rukwa watu wanazidi hesabu ya wenye umeme kwenye hizo nyumba zako.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Ina maana nyumba laki 460,000 ndiyo zina umeme katika nchi hii kwa hesabu yake Mheshimiwa!

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ALLY K. MOHAMED: Nyumba 4,600 ndiyo zina umeme.

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Keissy.

MHE. ALLY K. MOHAMED: …wakati kila kona ya nchi hii kuna umeme, kila kona…

SPIKA: Mheshimiwa Keissy! Ahsante sana, inatosha, muda wako umeisha.