Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge na Utawala na Serikali za Mitaa pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo

MHE. PAULINE P. GEKUL: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia hoja hii ambayo iko mbele yetu, na ninaomba nitangulie kuunga mkono hoja kwa asilimia 100, lakini pia niwapongeze Wenyeviti wa Kamati zote pamoja na Wajumbe ambao wametuletea taarifa hii ambayo imefanyiwa kazi kwa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kwamba bado saa chache, Chama chetu Chama Cha Mapinduzi kuadhimisha miaka 43 ya kuzaliwa, naomba niendelee kuitakia kheri katika kuongoz anchi yetu na taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nitachangia mambo matano. Naomba niishauri Serikali yangu mambo matano ambayo nafikiri kwamba yanaweza yakawasaidia wananchi wetu, na nitachangia zaidi TAMISEMI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza niipongeze Serikali na TAMISEMI kufikia makusanyo ya zaidi ya asilimia 69 katika halmashauri zetu. Naamini halmashauri zetu zinajitahidi kukusanya. Niishauri Serikali yangu kwamba pamoja na makusanyo haya kuna sababu ya kukaa na wakurugenzi wetu ili kuangalia vyanzo vingine vya kuwasaidia zaidi waendelee kukusanya. Lakini kama tutawashauri, ni vizuri sasa TAMISEMI pia tukae na wakurugenzi tuhakikishe zile asilimia 40 za maendeleo zinapelekwa katika miradi ya maendeleo. Nasema hili kwa sababu tukikusanya tusipopeleka kwenye miradi ya maendeleo tukaiachia Serikali kuu iwe inapeleka fedha za kukamilisha maboma ya madarasa na zahanati nafikiri Serikali Kuu itazidiwa. Kwa hiyo pamoja na kazi nzuri hii inayofanywa ya kukusanya fedha hizi, lakini sasa zirudi kukamilisha maboma na zahanati ambazo wananchi wamezinyanyua zimebakia tu finishing. Kwa hiyo naamini Serikali, hili mtaliangalia kwa karibu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo natamani sana niishauri Serikali. Hali za barabara zetu si nzuri sana; niombe, ifikie muda sasa wa Serikali yetu kufanya maamuzi ya dhati kwa TARURA kupewa asilimia 50 kuliko ambavyo sasa ni asilimia 30. Tunaiomba Serikali yetu iangalie hili. Sasa hivi TARURA wako site pamoja na hii hali ambayo si nzuri ya mafuriko; wamekuwa wakihangaika kutafuta moram na kuziba madaraja ambayo yamekatika. Ukweli ni kwamba kwa hizi asilimia 30 TARURA haitaweza kusaidia barabara hizi nyingi ambazo zimekatika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tunaelekea kwenye wakati wa bajeti. Tunaiomba Serikali iangalie gawio la 70 kwa 30, hizi asilimia zikirekebishwa naamini TARURA watafanya kazi nzuri; na hata sasa wanafanya kazi nzuri kwa asilimia 30; lakini Bunge hili tukiwasaidia TARURA wakapewa hata asilimia 30 itasaidia sana kukarabati barabara zetu. Niiombe Wizara ya TAMISEMI, sasahivi TARURA wameshaleta maoteo ya uharibifu ambao umefanyika huko kwenye barabara katika mitaa yetu, na Wizara ya Ujenzi na TARURA Taifa pia wanasema pia sasa TAMISEMI wao wameshapokea. Niiombe Serikali yangu response ya haraka sana kwa sababu katika mafuriko haya ambayo yanatokea, wananchi wameathirika, hawapiti na wanafunzi wanakwenda shule. Kwa hiyo TAMISEMI mtusaidie upesi kwamba sasa yale maoteo mliyoletewa mnaweza mkatupatia majibu lini ili wananchi kule kazi ziendelee na wanafunzi waendelee kwenda shuleni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo langu lingine la tatu ambalo nilifikiri kwamba niishauri Serikali ni suala la miradi ya kimkakati. Serikali yetu imefanya mambo mazuri sana. Niwashukuru, Mji wa Babati ni miongoni mwa miji ambayo tulipatiwa fedha za World Bank kwa ajili ya ujenzi wa barabara za lami. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI pamoja na timu yako naamini si halmashauri zote wamefikisha zile kilometa 10, mfano sisi ni kilometa 10, lakini kwenye zile kilometa 10 tumetekeleza kilometa 8.2 bado 1.8. Tunaomba sasa fedha zile ziweze kufika mapema ili zile kilometa 10 ambazo ilikuwa ndiyo azma yetu tuweze kukamilisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sambamba na hilo, Serikali yetu iliomba tupeleke tena miradi ya kimkakati kupitia TAMISEMI kwenda Wizara ya Fedha. kwa taarifa ambazo ninazo kama ile miradi sasa haijaanza na imesimamishwa baadhi, sisi Mji wa Babati tulileta mradi wa kimkakati katika halmashauri yetu, mradi wa stendi kuu ya mabasi Babati. Tunaomba sasa tupate majibu ya haraka tuweze kujua kwamba ule mradi wa stendi unaanza lini itatusaidia sana kwa sababu pia ni hitaji letu katika mkoa wetu na halmashauri yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ni suala la Wenyeviti wetu wa Serikali za Mitaa ambao wamechaguliwa hivi karibuni. Nipongeze sana Chama Cha Mapinduzi kwa kushinda kwa asilimia 99. Niiombe sasa TAMISEMI kupitia waurugenzi, wahakikishe wenyeviti wetu hawa wanapatiwa semina. Wenyeviti hawa ndiyo wanaokaa na wananchi muda wote, wenyeviti hawa ndiyo wanaotatua kero mbalimbali za wananchi muda wote. TAMISEMI sasa tunaomba halmashauri zetu zielekezwe kwa sababu hao wenyeviti tukiwaacha wakafanya kazi bila kupata mafunzo inaweza ikawawia vigumu. Kwa hiyo kote nchini mafunzo haya tuiombe TAMISEMI wasimamie ndani ya muda mfupi waweze kupewa mafunzo wenyeviti na wajumbe hao wa Serikali ambao wamechaguliwa. Halmashauri wanaweza wakasema kwamba hawana fedha za kutosha lakini haop watu ni watu muhimu sana. Kwa hiyo niiombe Serikali yetu itoe kauli juu ya mafunzo ya Wenyeviti hao ambao wameweza kuchaguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo siku ya leo ningependa kuishauri Serikal yangu ni suala la TASAF. Fedha hizi zinasimamiwa vizuri katika halmashauri zetu na zinatoka kwa wakati; kwanza niwapongeze hili linafanyika lakini niombe sasa, si wazee wote au si kaya zote maskini zile zimeweza kuingia kwenye mpango. Kwanza niombe iharakishe suala zima la wale ambao hawajaingia na wanaingia katika bajeti na mpango wa mwaka huu na kuendelea huu mchakato ukamilishwe haraka ili wale wazee ambao walikuwa wamesubiri kwa muda mrefu waweze kupata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nishauri pia kwa upendo kabisa kuhusu wazee wa Taifa letu. Niombe Serikali yangu tena wafikirie kuwaingiza wazee katika asilimia 10 za mkopo unaotolewa kwenye halmashauri zetu. Tumefanikiwa kwa vijana, akina mama na walemavu. Wazee hawa tukiwatengea asilimia mbili kama ambavyo tumetenga kwa walemavu, tukatenga kwa vijana na akina mama wazee hawa na wao wapate hilo dirisha naamini watafanya kazi na pia Watazalisha wataendelea kupata mitaji na wataendelea kuhudumia familia zao, kwa sababu si wazee wote ambao wanashindwa kufanya kazi. Umri wa mzee ni kuanzia miaka 60 na kuendelea; haimaanishi kwamba ukiwa mzee hauwezi kufanya kazi. Kama tumeweza kuwa-consider akina mama na vijana na walemavu, niiombe Serikali yangu kwa moyo wa dhati wazee sasa katika bajeti hii tunayoelekea waweze kupewa kwa sababu waliomba pension kwa muda mrefu lakini sasa kwa sababu hatukuwatimizia hili, tukiwaweka kwenye dirisha la mkopo wa halmashauri usiokuwa na riba itatusaidia sana kuondoa kero kwa wazee wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, mambo yangu matano nimemaliza. Naunga mkono hoja. (Makofi)

Whoops, looks like something went wrong.