Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. CAN.RTD Ali Khamis Masoud

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mfenesini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuhitimisha taarifa yetu ya Kamati ya Viwanda, Biashara na Mazingira kama tulivyoiwasilisha asubuhi ya leo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa yetu imechangiwa na watu takribani 15, pia na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Naibu Waziri. Nawapongeza sana Waheshimiwa Wabunge kwa kutoa maoni yao na ushauri. Tunayathamini sana maoni yao na ushauri huo na ninaiomba Serikali, maoni na mapendekezo yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge, yachukuliwe na kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Mawaziri waliochangia, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara na Mheshimiwa Naibu Waziri wa Ofisi Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira. Wizara ya hii ya Viwanda na BIashara ndio imebeba mwelekezo wa nchi kwa sasa, katika kuipeleka azima ya uchumi wa kati kupitia viwanda. Hivyo ni vyema na tuendelee kuiomba Serikali kuiwekea umuhimu na mkazo wa hali juu katika kuwapatia fedha za maendeleo ili waweze kuifikia azima hiyo tuliyoikusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azima hii na kufikia mahali tulipokusudia yapo mambo ya msingi ya muhimu yanatakiwa yafanywe na kuwajibishwa na wananchi wote wa Tanzania. Moja ambao lazima niwepo katika nchi nchi lazima kuwe na ulinzi au amani na utulivu ndani ya Taifa letu. Wapo Waheshimiwa Wabunge ambao walichangia hapa na kusema kwamba hata utawala bora haupo. Siamini, lakini nasema utawala bora kama ungekuwa haupo tusingeona wimbi kubwa la wawekezaji wanaoingia nchi hivi sasa kwa ajili ya kuja kuwekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza azima hiyo, yapo mambo ambayo sisi kama Kamati tuliyazungumza na kuyatolea ushauri kwa Serikali. Yapo mambo tuliyafanyia kazi katika Kamati hasa katika suala la ujenzi wa jengo la TBS. Ujenzi wa jengo la TBS katika kutembelea Kamati ilishuhudia na kuingia wasiwasi na thamani kubwa ya fedha zilizotolewa kwa ajili ya ujenzi wa jengo lile. Hivyo ilishauri Wizara kuhakikisha wanafanya tathmini au kuweka Kamati Maalum itakayofuatilia na kuhakikisha waone uhalali au wafanye uhakiki wa uhakika wa kuhakikisha kwamba jengo lile lina thamani ya kiasi gani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe nizungumze suala la Liganga na Mchuchuma, limezungumzwa na Wabunge wengi. Sisi kama Kamati tumeliona, tumelijadili, tumelizungumza na tumelishauri sana Serikali kuhusu suala hili. Kweli suala hili ni la muda mrefu, lakini kwa sasa lazima tukubali kwamba Serikali baada ya kuona utata mkubwa katika mikataba ya jambo hili, waliona ni vyema sasa waanze kupitia tena mikataba na kufanya tathmini ya kuhakikisha tunakwenda kwenye mkataba ukao tusaidia kama Taifa. Kwa hiyo tunaiomba Serikali sasa ihakikishe mapitio haya yanafanyika haraka ili mradi huu uweze kufanya kazi na ulete tija kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la matrekta ya URSUS, Kamati ililiona hili na ilitoa mawazo yake na ushauri kwa Serikali kwamba kwa sasa inaonekana kampuni hiyo ya Poland imeshindwa kutekeleza wajibu wake na kutekeleza mkataba kama tulivyokubaliana. Hivyo tunaomba sasa Serikali ilichukulie uzito wake na kwa sababu Serikali imeshatoa fedha nyingi katika mradi huu, ni vizuri sasa Serikali ikalifualia kwa karibu na kwa haraka ili fedha yetu hiyo iweze kuleta tija na kutuletea maendeleo mengine hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la bandari la kuchelewesha mizigo nalo lilitufikia katika Kamati yetu kwa wadau. Wadau wengi walipokuja katika Kamati walilalamikia suala la uchelewashaji wa mzigo. Ni kweli suala hili limezungumza katika Kamati ya Miundombinu, lakini sisi kama Kamati ya Viwanda na Biashara, biashara yoyote nayo inahusisha bandari. Huwezi kufanya biashara kwa ufanisi kama huna bandari yenye uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo sisi katika ripoti tuliyotoa leo tuliweza kuishauri Serikali kuhakikisha kwamba wale wadau wanaofanya kazi bandarini hatuna uhakika ni nani anayechelewesha mizigo inaweza ikawa TASAC Inawezekana wengine, lakini ushauri wa Kamati unasema TASAC, TRA,TPA na wengine wadau wote wanaoshughulika na mizigo bandarini wakae pamoja watafakari na kuona kwa nini mzigo inachelewesha hapa bandari na wafikie muafaka wa kutatua tatizo hilo kwa haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kero za wafanyabiasha ni nyingi na nyingine tumetoa hapa vizuri na tumezielezea. Suala la VAT refund, suala la 15% ya sukari ya viwandani. Hili kwa kweli ni tatizo kubwa, sisi tunachokiomba sasa Serikali ilichukulie kwa uzito wake na kuhakikisha wanawapa faraja wafanyabiasha wetu waweze kutumia fedha zao zile kwa ajili ya maendeleo zaidi. Viwanda vingi vinapata shida ya kuendesha biashara zao kwa sababu fedha nyingi zipo Serikalini. Tunaomba sana Serikali ilichukulie hili na kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wetu wanapata faraja katika jambao hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kutekeleza majukumu yetu kama Wizara tunashukuru wenzetu wa Tan Trade kwa kweli kuna mabadiliko makubwa ya sasa hivi yanaonekana yanayaanza kutekelezwa. Sisi tunasema tunawapongeza sana Tan Trade kwa kuunda Kitengo cha Intelejensia ya kutafuta biashara na mazao mbalimbali na kuhakikisha tunatangaza biashara zetu ili kusudi tupate masoko katika kutekeleza azima hiyo tunayokusudia ya viwanda katika uchumi wakati. Naomba sana tunapojenga viwanda katika nchi vitu hivi viwili lazima viende sambamba. Viwanda viende na masoko pia tukijenga viwanda bila kupata masoko havitaleta tija wala havitatusaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaomba sana wakati wowote Tan Trade wahakikishe bidhaa zote zinazozalishwa ndani ya nchi zinapata masoko na zinauzwa ndani na nje ya nchi. Viko viwanda sasa hivi vimetia malalamiko makubwa sana ya bidhaa nyingi sana zinazozalisha ambazo zipo ndani ya magodauni na hazina wateja. Hivyo kiwanda kama hicho si vizuri kuwa nacho kwa sababu hakitatupa faida kubwa. Naomba sana wenzetu wa Tan Trade katika hili wahakikishe wanafanya kazi ya ziada ya kuhakikisha masoko ya bidhaa zetu zote zinapatikana ili waweze kuuza huko nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo lilizungumzwa hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Malizia tu Mheshimiwa.

MHE. KANALI (MST) MASOUD ALI KHAMIS - MAKAMU MWENYEKITI WA KUDUMU WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA VIWANDA, BIASHARA NA MAZINGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya maelezo hayo, naomba Waheshimiwa Wabunge wakubali taarifa ya Kamati na ushauri, iwe kama azimio la Bunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja. (Makofi)

MHE. HASNA S.K. MWILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.