Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

Hon. Lucy Fidelis Owenya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Kuhusu Shughuli za Kamati kwa Mwaka 2019

MHE. LUCY F. OWENYA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia na kuwa mtu wa kwanza katika mjadala wa leo. Wizara ya Viwanda na Biashara katika fedha za maendeleo mwaka 2018/2019 walitakiwa watengewe shilingi bilioni 100.02 lakini zilizotolewa ni shilingi bilioni 13.63. Mwaka 2019/2020 fedha za maendeleo zilizotengwa zilikuwa ni shilingi bilioni 51.5 pungufu ya asilimia 48.7 ya zilizotengwa za mwaka 2018/2019.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutotoa fedha za maendeleo za kutosha inachangia kutokuziwezesha taasisi ambazo ziko chini ya Wizara kama CAMARTEC, TIRDO na SIDO ili kuweza kufanya tafiti za kuweza kuendeleza vifaa vya kilimo au vifaa vya kwenye viwanda. Kwa hiyo naishauri Serikali itenge fedha za kutosha ili waweze kuendeleza shughuli za viwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niongelee suala la viwanda vilivyoko katika Mji wa Moshi. Moshi tuna viwanda vingi sana, kulikuwa na Kiwanda cha Kibo Match ambacho kilikuwa kinatengeneza vibiriti, lakini kiwanda kile mpaka leo hii kimekufa na hakijaendelezwa kwa vyovyote vile. Kiwanda kile kilikuwa kinazalisha ajira zaidi ya 600 na walikuwa wanazalisha vibiriti zaidi ya 6,000, lakini kwa sasa hivi ina maana ajira zile zimepotea na vijana wanazurura mtaani wakati kiwanda kipo pale gofu, ambapo Serikali ingeweza kuvifufua na kikafanya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kingine ni kile cha ngozi kilichoko Moshi, kinatengeneza ngozi ndiyo, lakini kwa kiwango kidogo sana. sijui ni kwa jinsi gani Wizara imeenda kuangalia suala zima la mazingira kwa sababu pale wakazi wa Pasua, Mabogini, Bomambuzi wanaanthirika sana na harufu ya ngozi inayotoka katika kiwanda cha ngozi. Sasa sijui kma wameshafanya utafiti kugundua kama ile harufu inayotoka katika kiwanda kile kama inadhuru watu au la. Ningeomba Serikali ifanye utafiti iende ikaangalie suala zima la mazingira katika kile Kiwanda cha Tanneries. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapo hapo kulikuwa na kiwanda cha magunia, mpaka leo ni gofu liko pale. hakuna chochote kinachoendelea, imekuwa ni mahali pa kuhifdhi tu vitu lakini hakuna kiwanda cha magunia pale Moshi. Sasa sijui mpaka leo hii bado tunaimba kuhusu viwanda vya magunia Moshi wakati katani zipo lakini sijui kwanini sasa viwanda vile havifufuliwi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda kingine kilichoko katika Mkoa wetu wa Kilimanjaro ni kiwanda mama cha machine tools. Tumekuwa tukipiga kelele kila siku. Kiwanda kile bado hakizalishi, vipuli vilivyoko pale ni teknolojia zile za zamani kwa hiyo wanashindwa kuzalisha viwanda kwa ajili ya viwanda vidogo vidogo. Sasa sijui lini sasa Serikali itafanya ule utafiti iliyosema inafanya na kutafuta mwekezaji ili watengeneze teknolojia mpya, wazalishe viwanda vidogo vidogo ili viweze kusaidiana na SIDO watu waweze kuzalisha na mazao yao wakiwa kule kule vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuulizia kuhusu kiwanda cha General Tyre Arusha. Kiwanda kile kilikuwa kinafanya kazi na kilikuwa kinazalisha matairi mazuri East na Central Africa kabisa lakini sasa mpaka leo hii ni zaidi ya miaka kumi tumekuwa tukikizungumzia kiwanda cha General Tyre kilikuwa kimeajiri watu wengi sana lakini bado Serikali haijaonesha ni lini sasa kiwanda kile kitaanza kwa sababu bado tuna yale mashamba yaliyoko kule Tanga ambayo yanazalisha mpira, yamekaa tu kule badala yake wamekuwa Wakenya wakienda kule wanaenda kuchukua zile rubber wanaenda kutengeneza big Nairobi na sisi ambao tungeweza kutumia ile rubber kwa ajili ya kwenda kutengenezea matairi yetu kule Arusha. Lakini mpaka leo hii Serikali haijasema ni lini sasa kiwanda cha General Tyre kitaanza kazi. Tunaomba watupe time frame ni lini kitaanza kazi ili vijana wetu waweze kupata ajira kwa sababu kiwanda kile kina nafasi ya kutosha, kimelala tu pale, vijana wanazurura lakini wangeweza kupata kazi katika kiwanda kile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kidogo nizungumzie kuhusu masoko. Mkoa wa Kilimanjaro tunalima sana ndizi na tunalima pia maparachichi. Lakini unakuta wakulima wanavuna maparachichi kwa wingi sana lakini yote yanaoza kwa sababu tu hawana masoko na wengine ni kwa sababu ya packaging na mengine unakuta…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Lucy Owenya kwa mchango wako.