Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Dr. Philip Isdor Mpango

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba nitumie fursa hiii kukushukuru kwa kunipa nafasi, lakini pia nawapongeza sana Wenyeviti wawili wote wa Kamati kwa hoja nzuri sana ambazo wamezifanyia kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naomba nichangie baadhi ya hoja ambazo zimejitokeza humu ndani. Kwanza, kulikuwa na suala la Bajeti ya Fungu Na. 7 - Msajili wa Hazina kwamba ni kidogo, wamepata asilimia 16, hivyo wawezeshwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mwaka huu peke yake ambao tunaendelea kutekeleza, mpaka mwezi Desemba kwa upande wa kuwawezesha Ofisi ya Msajili wa Hazina ili waweze kufanya kazi yao ya kufuatilia hizi Taasisi za Umma, walishapewa asilimi 92 ya OC. Nafikiri tatizo linalojitokeza ni kwa sababu kuna baadhi ya vipengele na hususan fedha kwa ajili ya mitaji ya Mashirika ya Umma, lakini pia fedha kwa ajili ya kulipia madeni ya mashirika, hizi kwa kawaida huwa tunaziweka kwenye kasma ya dharura na haionekani kule kwenye Fungu Na. 7 moja kwa moja. Ni pale tu ambapo zinahitajika ndiyo tunazitoa na zinalipwa kutoka kwenye Fungu lile la dharura.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati nzuri ni kwamba tunaenda sasa kuanza mchakato wa bajeti, nafikiri kama ni macho ya ziada kwa ajili ya changamoto zile nyingine ambazo zilisemwa juu ya Ofisi hii muhimu sana, ni kipindi chake cha kuangaliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu kampuni za simu kujiorodhesha kwenye soko letu la hisa la Dar es Salaam. Ilitolewa hoja kwamba mpaka sasa ni Vodacom peke yake ambayo imeorodheshwa wakati tulishakubaliana na sheria inataka mashirika yote ya simu yajiorodheshe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda tu niliarifu Bunge lako kwamba tuko katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa sheria. Kwa mfano, tunatarajia kwamba tigo watawasilisha documents zile zinazohitajika kwa ajili ya kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa itakapofika mwezi ujao Februari, 2020.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Halotel kama mnavyofahamu Waheshimiwa ni kwamba hii kule kwao ni kampuni ya jeshi. Kwa hiyo, panahitajika uamuzi wa wamiliki ili kuihamisha sasa ile kampuni kuwa public company ndiyo iweze kujiorodhesha kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam. Kwa hiyo, hilo linafanyika hivi sasa, tunatarajia kwamba hatua itafikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Airtel, imechelewa kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa kwa sababu kama mnavyokumbuka tulikuwa na ule mzozo wa umiliki wa hisa na sasa baada ya kutatuliwa lile, ndiyo tutaanza sasa mchakato wa kwenda sokoni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kuiwezesha TTCL kifedha, ni kweli kabisa shirika letu hili ni muhimu, tunahitaji kuboresha miundombinu yake. Utaratibu wa kwenda kununua nguzo za mitumba, hili hapana, haliruhusiwi na sheria ambayo ilitungwa na hili Bunge. Kwa aina ya teknolojia, aina ya kazi ambayo inafanywa na shirika letu hili ni muhimu sana tukahakikisha kwamba ile infrastructure inakuwa ni ya kisasa kabisa kutupeleka kwenye uchumi wa kidigitali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, tumeanza kuchukua hatua, mwezi Desemba Serikali ilitoa ridhaa kwa TTCL ambapo tuliwaruhusu waweze kukopa dola milioni 15 ambazo ni kama shilingi bilioni 34.2 hivi waweze kukopa kutoka kwenye benki za ndani kwa ajili ya kuweza kupanua miundombinu ya taasisi hii na kadri mahitaji yatakavyojitokeza, basi Serikali itayatazama kwa jicho hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na suala la marekebisho ya VAT tena kwamba yaje kwa hati ya dharura, particularly ili Serikali isidai kodi ya ongezeko la thamani kwenye miradi kama ile ya Halmashauri inayogharamiwa na fedha za Benki ya Dunia. Niseme tu tunalifanyia kazi, kwa hiyo Bunge litaarifiwa hapo baadaye, maamuzi ya Serikali kuhusu jambo hili ni nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa pia na mapendekezo ambayo yalishawahi kutolewa. Bunge hili huko nyuma liliwahi kueleza kwamba ni muhimu tunapofanya mabadiliko ya sheria zile zinazohusu ushirikiano kule Afrika Mashariki yapite kwenye Kamati ya Bajeti. Nafikiri nilishawahi kuliambia hili Bunge Tukufu kwamba sioni tatizo la kimsingi kutekeleza hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto moja iliyopo ni ya muda. Kwa mfano, mwaka uliopita mchakato wa kuchakata yale mapendekezo ambayo tulikuwa tumeyapata kutoka kwa wadau, yalipopita kwenye task force on tax reforms na baadaye kwenye think tank, siku ile ya mwisho tunafanya kikao ndiyo siku pia Kikao cha Jumuiya ya Afrika Mashariki kilikuwa kinaanza. Kwa hiyo, inakuwa ni timing disconnect kwamba tunafanyaje ili huu mchakato uwe umekamilika ili tuweze kuupitisha kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuna changamoto ya pili kwamba Serikali kwa ujumla wake hata Waheshimiwa Mawaziri wenzangu wanakuwa hawajaona hayo mapendekezo. Kwa hiyo, inakuwa ni vigumu kuyaleta kwenye Kamati kabla Serikali haijaji-pronounce.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nilitaarifu tena Bunge lako Tukufu kwamba tunapoleta yale mapendekezo kupitia Finance Bill, bado Bunge linayo nafasi ya kushauri juu ya yale ambayo tulikubaliana kule Afrika Mashariki. Kama Bunge au Mamlaka nyingine za Serikali haziridhiki na kile ambacho tulikubaliana kule, sisi tunachofanya ni kwamba huwa tunaandika barua kwa Sekretarieti ya Afrika Mashariki, tunasitisha utekelezaji wa hicho ambacho kilipeleka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niseme kulikuwa na hoja kwamba uchumi wetu uko vizuri lakini siyo kwa mtu mmoja mmoja. Nirudie tena kusisitiza kwamba mwenendo wa vigezo kuhusu viashiria vya uchumi jumla, tunakwenda vizuri sana. Yaani katika Afrika ni ukweli kabisa tunazidiwa na ncjhi chache sana, lakini ukuaji wa uchumi wa asilimia 6.9 ni ukuaji wa kasi kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hili la mmoja mmoja naomba tu nisisitize tu vitu vitatu hivi. Kwanza, ongezeko la ukuaji wa uchumi huwa linaongezeka kwanza kwenye mchango wa kila Sekta kwenye Pato la Taifa na unaona kabisa kwamba baadhi ya Sekta mchango wake kila mwaka unaongezeka, unakua kwa kasi. La muhimu kuzingatia ni kwamba wanaonufaika na ule ukuaji ni wale wanaoshiriki kwenye zile sekta ambazo zinakua haraka. Ndiyo maana msisitizo umekuwa ni kwamba ni lazima Watanzania tufanye kazi. Hilo ni la msingi sana kwa sababu vinginevyo huwezi kufaidika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, wananchi wanafaidika na ukuaji wa uchumi kupitia kwenye huduma za jamii zinazotolewa na Serikali. Kwa hiyo, ndiyo maana tunapoboresha elimu, afya, barabara na kadhalika, ndiyo njia ya pili ya kuwafaidisha wananchi kutokana na ukuaji wa uchumi. Mwananchi mmoja mmoja, lakini pia Taifa kwa ujumla. Kwa hiyo, ni muhimu sana kufanya uchambuzi vizuri kwamba hiki kinachosema mtu mmoja mmoja haonekani kufaidika ni nini hasa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa kuwezesha Sekta ya Kilimo kama tulivyofanya kwenye Sekta ya Madini, nafikiri hoja inaweza kuwa ni ya kutafakari vizuri. Kwa sababu kilicho kikubwa kwa Serikali, kwanza kwa upande wa kilimo ni lazima tuhakikishe kwamba Sera zetu za Kilimo ni nzuri na hususan kwa sababu kilimo ni private sector activity. Kwa hiyo, lazima tuhakikishe kwamba sera zile ni nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la muhimu tujielekeze sasa kwenye miundombinu ambayo inawezesha kilimo na ndiyo hilo ambalo Serikali imekuwa inafanya tena kwa kasi. Miundombinu ya usafirishaji, maghala, umeme na irrigation, hapo ndiyo tutaweza kunyanyua kilimo. Lazima pia tujielekeze kuboresha huduma za fedha kwa wakulima, lazima tujielekeze kwenye huduma za ugani na utafiti kwenye kilimo. Huo ndiyo mwelekeo wa Serikali. Ukisoma ASDP II, huko hasa ndiyo tunapolenga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia lazima tujielekeze kwenye inputs muhimu; mbolea, dawa na mbegu bora. Huo ndiyo mwelekeo na msukumo wa Serikali katika kuboresha na kukiwezesha kilimo. Nafikiri hiyo ndiyo njia sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja nyingine, nafikiri ni tahadhari muhimu juu ya mwenendo wa mfumuko wa bei. Ni kweli mwenendo wa mfumuko wa bei kwa nchi yetu hivi sasa ni mzuri kabisa, isipokuwa tunaziona hizi changamoto zinazooneshwa kwa upande wa chakula na vile vile upande wa nishati. Hili nalo ni muhimu na hasa ukizingatia wakubwa hao ambao wanatunishiana misuli, kwa hiyo, inaelekea kuleta shida kwenye bei ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, tunachukua tahadhari kama Serikali kwa maana ya kusisitiza nishati mbadala, lakini pia kuhakikisha kwamba tuna akiba ya kutosha ya chakula. Hilo ni muhimu sana ili tuhakikishe kwamba mfumuko wa bei unaendelea kubakia kwenye kiwango ambacho hakiharibu mwenendo wa uchumi wetu kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilitolewa pia hoja kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu ambayo inahangaika na maafa haikuwekewa fedha yoyote kwenye bajeti. Naomba tu nikitaarifu kikao chako kwamba kwa kawaida constitution ya nchi yetu inataka asilimia moja ya bajeti yote ya Serikali itengwe kama contingency. Kwa hiyo, endapo itatokea dharura, hatutasita kutumia contingency fund kwa ajili ya kukabiliana na maafa kama yatajitokeza, lakini Mwenyezi Mungu anatupenda, naamini atatuepusha na madhara japo yameanza kutokea kwa wananchi kwa mfano kule Lindi na unaona Serikali ya Mkoa tayari imeingia kazini na pia Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri naomba umalizie maana nimekupa mrefu.

WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwa kumalizia jambo la mwisho tu, kwa upande wa kodi ya majengo, tunapokea ushauri, tutaufanyia kazi kwamba kodi ya majengo pengine ilipiwe kupitia ankara za umeme na maji. Kuna tahadhari pia, kwa sababu siyo ankara zote za umeme ni za matumizi ya nyumba, hilo lazima lifahamike. Vile vile, hata ankara za maji, nyumba nyingi hazina ankara za maji. Kwa hiyo, tuna changamoto kubwa. Ni jambo la kuchakata vizuri tuone kama linaweza likatupa mileage. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)