Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020 Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma Kuhusu Shughuli Zilizotekelezwa na Kamati Hiyo Katika Kipindi cha Mwezi Februari, 2019 Hadi Januari, 2020

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana ahsante sana kwa nafasi hii kwanza nianze kwa kusema kwamba naunga mkono hoja ya Kamati zote mbili, niipongeze sana Serikali kwa kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa mapato pale TRA, mifumo ya disbursement ya fedha na mifumo ya ripoti ya fedha kweli imekaa vizuri sana kwa sasa hivi. Isipokuwa tatizo ambalo bado naliona ni mfumo wa uwajibikaji au accountability framework bado kidogo inahitaji kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, si vizuri sana kusubiri mpaka CAG akague atoe ripoti ndio Watanzania wajue status ya thamani ya fedha kwenye miradi. Ingekuwa vizuri sana kama thamani ya fedha kwenye miradi ingekuwa inafatiliwa tangu fedha zinapopelekwa kwenye utekelezaji hadi utekelezaji unapofanyika mpaka miradi kukamilika. Kwa hiyo, nashauri tuboreshe mfumo mzima wa ufuatiliaji na tathmini ili tuweze kuboresha utekelezaji wetu. Taarifa ya utekelezaji wa bajeti nikiangalia ni nzuri sana lakini kipengele hiki cha ufatiliaji na tathmini kinachelewa kuboreshwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mawili la kwanza ni muhimu sana tuwe na sera ya ufatiliaji na tathmini ya nchi, pili mikakati ya ufatiliaji na tathmini ambayo itaboresha mpaka idara zote ambazo zinahusika na mambo ya mipango, ununuzi, uhasibu, ukaguzi wa ndani na mambo yote yanahusiana na suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani ushauri wa kuanzisha Ofisi ya Kamishna wa Mipango wa ufatiliaji na tathmini katika Wizara ya Fedha ni muhimu sana Serikali iutekeleze. Hapo mwanzo tulikuwa tunalalamikia wakandarasi sijui bei kubwa wakandarasi baadaye tukaagiza kwamba itumike force account lakini hata kwenye force account kumeanza kujitokeza matatizo ambayo yanapunguza ile thamani ya pesa kwenye mradi. Kwa hiyo, nilikuwa nafikiri tukiboresha eneo hili la ufatiliaji na tathmini tutakuwa tumeboresha sana matokeo bora ya miradi kwa wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili fedha za mfuko wa jimbo kwa mfano mwaka jana zimetoka mwezi wa nane. Kamati za mfuko wa jimbo zimekaa kupanga matumizi ya hizo fedha lakini mpaka leo hii miradi mingi ya fedha hizi za mfuko wa jimbo haijatekelezwa kwa sababu tu fedha zilipokuja hazikuwa kwenye activity bajeti, kwa hiyo miradi yake ile mpaka iombewe kibali aidha kwa Wizara ya Fedha au TAMISEMI aidha reallocation. Nilikuwa nashauri ili kuondoa matatizo hayo Kamati za mfuko wa jimbo ziwe zinakaa mwezi Januari au Februari ili miradi ambayo imepangiwa matumizi iingie moja kwa moja kwenye activity budget wakati fedha zile zikitoka ziende kwenye utekelezaji na wakati ule Kamati za mfuko wa jimbo zifanye tu ufatiliaji na tathmini ya mradi unatekelezwa, hiyo itakuwa imeboresha kwa kiasi kikubwa sana utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho napenda kutoa pongezi kubwa kwa Serikali utekelezaji wa bajeti 2018/2019, 2019/2020 kwa kweli unaondelea ni mzuri na kazi kubwa sana zimefanyika hongera sana Serikali hasa kwenye miradi ya miundombinu, miradi ya afya, miradi ya elimu na kwa kweli naomba ndani ya Bunge hili nizungumze masikitiko yangu dhidi ya barua ambayo mwenzetu mmoja ameiandika kutaka kuzuia fedha za miradi ya elimu. Ni kituko na ni aibu sana kwetu sisi Wabunge kuona mwenzetu ameandika barua ile wangekuwa wameandika watu wa NGO huko nje mimi nisingeshtuka sana lakini mwenzetu kaandika barua ile katika jimbo lake Serikali imepeleka shilingi bilioni moja kwa ajili ya kukarabati Sekondari ya Kigoma na sasa hivi sekondari ya Kigoma ni kama mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile wamepeleka zaidi ya shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kuboresha elimu, sasa anazuia dola milioni 500 zisije kwa haraka kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa kitanzania. Nadhani hilo kwa kweli nieleze masikitiko yangu makubwa sana, na nimuombe huko aliko amesoma vizuri tena amesoma hapa ndani akasoma nan je Ujerumani basi tuitumie elimu yetu kwa ajili ya kuwasaidia watoto wa Tanzania hiyo ndio rai yangu badala ya kuwacheleweshea maendeleo. Unazuia shule 1000 zingeguswa na hizo fedha watoto zaidi ya 600,000 wangefaidika na zile fedha. Nadhani kwa kweli hilo mimi nasikitika sana sana na kama ananisikia huko aliko nilitamani nipaze sauti asikie huko aliko lakini kwa sababu yupo mbali basi naachia hapo lakini ataisikia kutoka kwenye Hansard. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa nafasi hii asante sana, naunga mkono hoja. (Makofi)