Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Doto Mashaka Biteko

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukombe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

WAZIRI WA MADINI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii ya kuchangia hoja ya kamati. Na ninaomba vilevile nimpongeze sana Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Mama yangu Mama Kaboyoka, kwa kazi kubwa yeye pamoja na kamati yake akisaidiana na Mheshimiwa Aeshi Hilal kwa kuendesha kamati ile vizuri na kuja na taarifa nzuri ambayo kwa kweli, imesheheni mambo mengi ya kufanyia kazi, nawapongeza sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumetokea hoja tatu zinazohusu Shirika la madini Nchini (STAMICO). Na hoja hizo zote kwa ujumla wake kama Wizara tunazipokea na ni hoja za msingi sana ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi. naomba tu nitoe taarifa kwa kamati kwamba, yako mambo ambayo tayari tumeshaanza kuyafanyia kazi. ni kweli kwamba, shirika hili lilikuwa linakumbwa na tatizo kubwa sana la utendaji na hivyo kulifanya kutokufanya kazi nzuri zaidi ya kuzalisha kama ambavyo lilikusudiwa toka kuanzishwa kwake mwaka 1970.

Mheshimiwa Naibu Spika, STAMICO toka wakati ule haijawahi kufanya kazi yoyote ya kuipatia faida isipokuwa siku za hivi karibuni baada ya mabadiliko ambayo nitayaeleza hapa:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza utendaji uliotajwa kwenye kamati ni utendaji ambao tumeshaanza kuufanyia kazi. Shirika kwa muda mrefu halikuwa na Mwenyekiti wa Bodi. Nafurahi kusema kwamba, Mwenyekiti wa Bodi amekwishakuteuliwa na alivyoteuliwa na sisi tukaangalia menejimenti nzima ya shirika, tumeifanyia maboresho mengi sana na kumpata mtendaji ambaye kwa sasa kwa kweli, mabadiliko yanaonekana sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, shirika lilikuwa linazalisha hasara na madeni mengi sana. Wakati tunaingiza bodi mpya na kubadilisha uongozi shirika lilikuwa limekwishakuzalisha madeni yanayozidi bilioni 35; ninafurahi kuripoti mbele ya Bunge lako Tukufu kwamba, sasa shirika linafanya biashara bila kuzalisha hata deni la shilingi moja. Na mwezi uliopita shirika limefanya biashara ya bilioni 24 na ndio maana umeona hata mwaka huu ulioisha tumeweza kutoa mchango kwa Serikali, jambo ambalo halikuwahi kufanyika toka shirika kuanzishwa miaka ya 70.

Mheshimiwa Naibu Spika, limeelezwa jambo hapa la mikataba ambayo shirika linaingia na ubia na mikataba miwili ambayo imeelezwa hapa, Mkataba wa kwanza ni wa Tanzanite One pamoja na Mkataba wa Bacliff:-

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa taarifa kuwa mikataba hii yote imekwishakupitiwa na ule mkataba ambao ulikuwa unatusumbua wa Bacliff tayari tumekwishakutoa notice ya kimakosa ya kileseni, ili tuweze kufuta leseni hiyo baadaye irudi Serikalini, ili Serikali iweze kujua namna gani itaifanyia kazi leseni hiyo. Kwa kweli, ubia ule ulikuwa sio ubia wa kutupatia faida maana ilikuwa ni leseni ile inatumika na mbia mwenzetu kukopa fedha nje ya nchi na anakwenda kuwekeza mahali pengine ambapo sisi hatujui. Sasa tumeshachukua hatua na tayari tumeshatoa default notice kwa ajili ya kufuta hiyo leseni, ili Serikali iweze kuifanyia kazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ama kuhusu Mkataba wa TML tarehe 23 Disemba, mwaka wa Mheshimiwa Naibu Spika, tayari tumeshatoa Surrender Certificate ya leseni ile na sasa ninavyozungumza hapa ni mali ya Serikali. Serikali itaangalia utaratibu mzuri wa namna ya kuisimamia leseni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na hapa kwenye mkataba wa TML ndio pametuopatia matatizo mengi sana. Hata hiyo disclaimer opinion ambayo CAG ameipata ni kutokana na mbia huyo kutokuandaa vitabu vyake vya kihasibu na kutokuweka rekodi zake vizuri na kwa hiyo, CAG akienda wakati wote anakuta hakuna taarifa yoyote; kwa kweli, ulikuwa ubia ambao tusingeweza kupata faida hata tungekaanao kwa muda wa miaka 1,000. Serikali imechukua hatua baada ya maoni mbalimbali ya Serikali yakiwemo ya Wabunge wa Kamati ya Kudumu ya Nishati na Madini tumefanyia kazi na tayari leseni hiyo imerudi mikononi mwa Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo Kamati imeeleeza ni kufanya tathmini ya kujua mali za shirika:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafurahi kuieleza kamati na Bunge lako tukufu kwamba, kazi hiyo tayari imekwishakufanyika na hata muundo wenyewe wa shirika tumeanza kuupitia upya. Tulikuwa na kurugenzi nyingi ambazo hazina kazi, tumezi-consolidate ili zibaki chache ziweze kuongeza tija kwa shirika na hatimaye tuweze kupata faida.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitoe tu taarifa kuwa, shirika hili tukilipa nafasi kwa kipindi hiki na turn arround tuliyoifanya kwa kweli, imani yetu ni kwamba, tutaanza kupata faida muda si mrefu. Hata yale madeni ambayo yalikuwepo miaka mingi tuliyoyarithi na yenyewe tumeanza kuyalipa kidogokidogo kadiri ya faida tunayoifanya. Asset tuliyonayo ni kubwa na utajiri tulionao ni mkubwa, kazi iliyopo ni kuweka akili kidogo ya kuweza kugeuza hizo assets kuwa mali na baadaye kuweza kulipa faida shirika letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisingependa kuzungumza mengi, Kamati naipongeza tena kwa michango yake na kwa yale waliyotuelekeza. Wizara yetu kwa kweli, iko tayari kuyafanyia kazi na tunawatakia kila la heri baada ya kusema hayo. Nakushukuru sana. (Makofi)