Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. Selemani Jumanne Zedi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bukene

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. SELEMANI J. ZEDI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia taarifa hizi mbili ambazo zimewasilishwa leo hapa Bungeni. Kwa kuanzia naunga mkono taarifa ya Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) ambayo mimi pia ni Mjumbe kama ambavyo imewasilishwa na Mwenyekiti wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, mojawapo ya kazi za Kamati ya LAAC kikanuni ni kushughulikia maeneo yenye matatizo sugu katika matumizi ya fedha za umma zinazopelekwa kwenye Serikali za Mitaa. Sasa mimi nilipata bahati ya kuwa pia kwenye Kamati hii ya LAAC kwenye Bunge la Kumi na sasa hivi pia niko kwenye Kamati hii ya LAAC.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoweza kusema katika eneo hili la maeneo yenye matatizo sugu ya matumizi ya fedha za umma zinazopelekwa kwenye Serikali za Mitaa ni kwamba, pamoja na kwamba maeneo haya yenye matatizo sugu hajashughulikiwa kikamilifu yote, lakini kuna improvement kubwa sana ukilinganisha hali ilivyokuwa miaka mitatu, minne nyuma kwenye maeneo haya haya na hali ilivyo sasa pamoja na kwamba hayajakwisha kabisa lakini improvement kubwa sana ambayo inatia moyo.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitazungumzia eneo moja la mapato ya ndani, kama ambavyo tunafahamu vyanzo vikubwa viwili vya fedha kwenye Serikali za Mitaa ni fedha zinazotoka Serikali Kuu na fedha ambazo ni makusanyo ya ndani ya halmashauri yenyewe. Sasa Kamati yetu baada ya kupitia halmashauri kadhaa na kufanya mahojiano jambo ambalo limebainika wazi ni kwamba halmashauri zilizo nyingi karibu zote zina tatizo kubwa sana la kushindwa kukusanya mapato yao ya ndani kwa mujibu wa bajei zao ambazo zilikuwa zimepangwa. Ukisikia tunasema halmashauri haikuweza kukusannya mapato ya ndani maana yake ni kwamba kuna kazi ambazo zilipaswa zifanywe hazikufanywa, ndiyo maana yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano, huu mwaka wa fedha ambao tunauhoji ambao taarifa yake imewasilishwa ni mwaka wa fedha wa 2017/2018 ambako miongozo ya kibajeti ilikuwa inazitaka halmashauri zichangie kutoka mapato yake ya ndani, zichangie asilimia 60 kwenda kwenye miradi ya maendeleo. Kwa hiyo ukisikia tunasema halmashauri haikukusanya mapato yake ya ndani kwa mujibu wa bajeti maana yake ni kwamba hizi fedha zitakazopelekwa kwenye maendeleo hazikupelekwa na kama hazikupelekwa maana yake kuna kazi za maendeleo zilizokuwa zinapaswa zifanywe hazikufanyika, kuna madarasa yalikuwa yajengwe hayakujengwa, kuna zahanati zilizokuwa zijengwe hazikujengwa na shughuli nyingine mbalimbali za kimaendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo impact ni hiyo, tunaposema halmashauri zinashindwa kukusanya mapato yake ya ndani haiishi hapo maana yake tunasema kuna shughuli za kimaendeleo zilizotakiwa zifanywe hazikufanyika na hii ndiyo inafika wakati wanafunzi wanamaliza darasa la saba wamefaulu kwenda kidato cha kwanza, tunajikuta madawati hakuna, vyumba vya madarasa hakuna, ni kwamba hayo yote yaliyokuwa yafanywe hayakufanywa kwa sababu halmashauri hazikukusanya mapato ya ndani na ile asilimia iliyopaswa kwenda kwenye miradi ya maendeleo haikuweza kwenda na hili haliathiri tu miradi ya maendeleo, lakini hata matumizi ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na halmashauri kushindwa kukusanya ndiyo maana karibu halmashauri zote sasa hivi zina tatizo kubwa, Madiwani hawalipwi kwenye vikao vyao vya Kisheria na unakuta kwa mfano pale Nzega halmashauri ya Nzega DC sasa hivi hata Madiwani wanashindwa hata kupita hesabu wanadai halmashauri kiasi gani kwa sababu wakati mwingine wakienda kwenye kikao wanalipwa posho ya kikao night hawalipwi, wakati mwingi wanalipwa night posho ya kikao hawalipwi, wakati mwingine hawalipwi posho ya kikao wala hawalipwi night na wakati mwingine unakuta halmashauri ya Nzega DC ina Madiwani 52 wamefanya kikao wamemaliza wanakwenda kwenye foleni ya kulipwa posho wanalipwa mpaka Diwani wa 23 hela zinakwisha, waliobaki wengine hawalipwi, kwa hiyo ni vurugu tupu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunaposema kwamba halmashauri inashindwa kukusanya maana yake ni kwamba kuna madhara makubwa sana na hili kwa kweli ushauri wangu ni kwamba; TAMISEMI itoe maagizo mahususi kwa Wakurugenzi wa halmashauri ili kabla mabaraza hayavunjwa mwezi wa Sita hawa Madiwani wawe wamepata stahiki zao zote wanazodai ili mabaraza yanapovunjwa wawe hawadai, hata ikiwezekana kwa halmashauri kukopeshwa na TAMISEMI na watajua namna ambavyo watafidiana wao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo Kamati imebaini baada ya kuhoji halmashauri ni eneo la miradi inayotekelezwa kwa force account. Kwa ujumla wake imethibitika bila shaka yoyote kwamba miradi inayotekelezwa kwa force account inashia kuwa ni miradi yenye gharama nafuu ukilinganisha na ile miradi ambayo ilikuwa inatekelezwa na ma- Contractor. Hata hivyo, issue iko kwenye quality (ubora) na hii inatokana na halmashauri nyingi kutokuwa na Wahandisi wa kutosha wa kwenda kuzikagua kazi kadri zinavyojengwa kwa sababu force account huko vijijini kwenye kata wanaajiri ma-local Fundi, Mafundi wanaopatikana kulekule. Kwa mfano wanajenga darasa, wakijenga msingi ni lazima Mhandisi wa Wilaya aende akaukague aone uko sawa atoe go ahead, ndiyo waendelee. Sasa unakuta Wilaya kama ya Nzega vijiji 167Mhandisi mmoja vijiji vyote vinamuhitaji unakuta kijiji kinahitaji Mhandisi aje aangalie kazi atoe go ahead kina msubiri miezi mitatu, minne wamekaa hawaendelei.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, mwisho wa siku unakuta kazi iliyokuwa ifanywe kwa miezi mitatu inafanywa kwa mwaka. Kwa hiyo maana yake ni kwamba gharama inakuwa kubwa na ubora unakuwa ni compromise. Kwa hiyo eneo hili ushauri wangu ni kwamba pamoja na kwamba Mainjinia wengi walikwenda TARURA, lakini halmashauri kwa maana ya majengo na usimamizi wa hii miradi ya force account ni lazime iwezeshwe kwa kuwa na Wahandisi wa kutosha ili waweze kuzikagua kazi na kutoa go ahead na kuhakikisha miradi ya force account siyo tu kwamba inapunguza gharama, lakini inahakikisha ubora wa miradi unakuwepo kadri ambavyo tunatarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo tumebaini baada ya kuhoji halmashauri ni kwamba, halmashauri zina tatizo la kutowasilisha michango ya akiba ya uzeeni ya wafanyakazi wake kwenye mifuko husika. Hili ni hatari, sasa hivi unaweza usilione kama hatari, lakini baadaye mfanyakazi anapostaafu, akifika kule fedha zake hazipo hapati, anateseka na inakuwa kero kubwa. Kwa hiyo ushauri wangu hapa ni kwamba iwe ni kipaumbele kwa Wakurugenzi kuhakikisha kwamba makato ya akiba za uzeeni kwa wafanyakazi yanawasilishwa kwenye mifuko husika kuliko ilivyo sasa ambavyo yanakatwa lakini hayapelekwi yanatumika pale halmashauri na baadae inakuwa kero kubwa kwa wahusika.