Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Anatropia Lwehikila Theonest

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. ANATROPIA L. THEONEST: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru nianze kwa kueleza changamoto ambayo wakulima wa Mkoa wa Kagera hususan Wilaya ya Karagwe waliipata, Karagwe na Kyerwa katika zao lao la kahawa. Nataka tunavyopanga Mipango tuone ni namna gani tunaweza ku-rescue changamoto wanazopitia hawa wakulima ambao wamekuwa miaka yote kahawa ni kipato chao ni uchumi wao wa muda mrefu, kahawa kwao ndiyo dhahabu na ndiyo diamond. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo tunavyoongea, uchumi wa Mkoa wa Kagera, uchumi wa Wilaya za Karagwe na Kyerwa umeanguka kabisa. Kipato kidogo walichokuwa wanakipata husomesha watoto, kujenga, kutunza familia zao, kujenga nyumba kiliparaganyika. Soko la kahawa lilianguka lakini kama haitoshi, Serikali ikaanza kununua Kahawa kupitia Vyama vya Ushirika KDCU, changamoto ndiyo ilikoanzia, kabla ya hapo tulikuwa na wafanyabiashara kwa maana ya Makampuni yananunua kahawa, tumeona mikoa tofauti tofauti tukiangalia korosho, Makampuni yananunua korosho, tukiangalia pamba, Makampuni yananunua pamba, tukiangalia mazao mengine alizeti, Makampuni yananunua alizeti, lakini ikija katika Mkoa wa Kagera mnaambiwa Makampuni yasinunue na badala yake ni Vyama vya Ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vyama vya Ushirika vinatupa bei gani? Msimu uliopita kilo moja ya kahawa inanunuliwa kwa shilingi 1,100. Mkulima ambaye alitarajia kujikwamua analea Kahawa kwa miezi sita anakuja kupewa shilingi 1,100 watu wamerudi kwenye umaskini, maisha yamekuwa magumu na takwimu ziko wazi. Takwimu za Mkoa wa Kagera miaka yote inaelekea kwamba ni mkoa unaozidi kurudi nyuma, zinatajwa Wilaya kama Ngara, zinaonekana ni kati ya wilaya tano za mwisho, tatizo ni nini? Watu wanalima, ardhi ina rutuba, tuna msimu wa kutosha, lakini mazao yetu yakifikia kuuzwa, Serikali inasema msiuze kuna bei elekezi, kuna shilingi 1,100. Tatizo ni nini? Kama korosho zinaweza kuruhusiwa makampuni kununua ni kwa nini kahawa zisiruhusiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka uliopita 2017/2018 kahawa ilienda mpaka kilo moja kwa shilingi 2,000. Tunavyoongea leo 2018/2019 kahawa ni shilingi 1,100 kama nilivyokwishasema, changamoto imekuwa nini, ni kwa nini Serikali haijawasaidia wakulima hawa? Tulisikia tamko la Mheshimiwa Rais kupitia Vyombo vya habari kwamba kahawa isinunuliwe chini ya shilingi 1,400 lakini nimwambie Mheshimiwa Waziri, hakuna mkulima aliyeweza kuuza kilo kwa shilingi 1,400, tatizo ni nini? Tunaambiwa kuna tozo, ni tozo gani sisi hatuzifahamu na kwa nini tuumizwe wakulima? Kama uchumi wetu, uti wa mgongo wa wakulima wa Mkoa wa Kagera ni kahawa, kwa nini zao hili likianguka Serikali haiwazi namna ya kuwapa ruzuku? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna tangazo la Serikali nimelinukuu hapa, ambalo lilionesha kwamba wangepewa ruzuku ya Sh.100 kwa mwaka uliopita, kwa kila kilo iliyouzwa, lakini ninavyoongea hapa, hakuna hata mkulima mmoja aliyewahi kupewa ruzuku hata ya senti kwenye kahawa alizouza, ni kwa nini tunafanyiwa haya, wakulima sisi wa Mkoa wa Kagera. Ni kwa nini watu wanakatishwa tama? Ni kwa nini mnaamua kuturudisha kwenye umaskini, wakati Mungu ametupa ardhi, Mungu ametupa rutuba, Mungu ametuwezesha, ni kwa nini? Nataka nipewe majibu ni Mpango gani uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukivuka kwetu, ukisema Mlongo ni mpakani mwa kama kilomita mbili, ukitoka upande wa Tanzania ukaingia upande wa Uganda, nimekuwa surprised hata ya leo, kilo ya kahawa ninavyoongea inanunuliwa kwa zaidi ya Sh.3,000, lakini upande wa Tanzania ambao ni just kilomita moja au mbili inanunuliwa kwa shilingi 1,100 tatizo ni nini? Sisi wakulima tunasema minada imekuwa inaendeshwa Kilimanjaro, ndiyo kuna minada ya kahawa ambayo inapelekewa kwenye Soko la Dunia, ni kwa nini hiyo minada haifanyiki kwetu ambako sisi tunazalisha sana kahawa? Ni kwa nini wakulima wa Mkoa wa Kagera wanaonekana ni kama second class? Ni kwa nini wakulima wa Mkoa wa Kagera hawawezi kuonyeshwa thamani ya biashara ya zao lao la kilimo ambalo wamelitegemea muda wote? Nataka Serikali iniambie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nime-google nikaona hata prices za dunia, nikaona kwamba iko around, mfano kama arabica coffee ni dola 2.85 ambayo ni equivalent na shilingi 4,835, ukija robusta inakuja kama dola 1.75 ambayo inaweza kuja mpaka shilingi 3,000, lakini sisi kwetu, soko halipandi na hatujui hiyo KDCU inashindanishwa na nani? Ukitaka kuleta monopoly kwenye soko ujue utawaumiza wale wakulima. Unavyoamua KDCU ndiyo wanaamua kununua zao la kahawa, unaua kabisa soko, yeye atakachoamua ndiyo kitakachofanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachosikitisha, hawa wakulima hizo fedha wanalipwa kwenye akaunti, wanalipiwa kwenye akaunti benki, wanakopesha Chama, wanasubiri wiki nzima, wao wakishakusanya fedha watumiwe kwenye meseji waende wakachukue fedha. it is not fair haiwezekani, sisi watu wa Mkoa wa Kagera hatutaki, hili ni zao letu, tunataka litukomboe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, nimepitia bajeti ya kilimo, katika miaka mitatu consecutively nikaona ambavyo kilimo kimeenda kinashuka lakini na ukiangalia mchango wa kilimo katika Pato la Taifa unaona ni mdogo sana, inaoneshwa hapa kwenye taarifa ukurasa wa tano, kwamba mwaka 2016/2017, kilimo kimekua kwa asilimia 7.6. Mwaka unaofuata imekuwa asilimia 5.6, uliofuata ni asilimia 5.3. Kama hatuwekezi fedha ya kutosha kwenye sekta inayowaajiri watu wengi maana yake we are likely kuwa-starve. Ni sawa, tunaweza kuona tunafanya miradi mikubwa, lakini miradi hiyo mikubwa kama haigusi watu wengi, ni kupoteza muda na wananchi wanaendelea kuwa maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naingia kwenye hoja yangu ya mwisho, naombeni Mipango wanayoenda kupanga iguse watu wengi na siyo watu wachache. Wapange Mipango inayotekelezeka, waache ku-bust bajeti wakati bajeti haitekelezeki, roughly kwa miaka mitatu, bajeti ukifanya estimate imetekelezwa kwa asilimia 36 tu, kwa miaka mitatu ya bajeti ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa narudi kwenye mchakato wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Nataka kuwaambia hivi tunachokitengeneza leo kwa kuona Vyama vya Upinzani katika nchi ni second class citizen, tunavyotaka kuona kwamba kuna watu ni wazalendo wakiwa kwenye Chama Tawala, basi wao ni wazalendo, lakini sisi wengine siyo wazalendo, maneno kama kuunda jukwaa la wazalendo, Walimu wazalendo, tunataka kutengeneza kinachotokea South Africa, tunataka ku-turn this country into a zone of phobic country. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, South Africa unaona wanauana leo walianza kidogo kidogo kwamba huyu, huyu ni Mkaburu, sawa alikuwa na rangi yake, lakini leo nawaona hao hao weusi wanaanza kuuana wao kwa wao na sisi tunakotaka kwenda mtu ukionekana unaji-associate na Vyama vya Upinzani kama ni kazi utapoteza, kama ni promotion utakosa, kama ni kuhamishwa utahamishwa, tunachokitengeneza ni nini? Tunataka ku-burn down hii nchi kwa sababu ya madaraka na nataka kuwaambia hakuna hali ya kudumu, there is no situation which is permanent, unaweza ukajiona leo wewe uko viti vya juu lakini kesho tutakutana benchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mifano ya kudumu, tuna mifano halisia, kuna watu walikuwa Mawaziri Wakuu katika nchi hii, leo tuko nao tunalalamika, msijione leo mmekalia viti vyekundu mkadhani mtadumu kuwa hivyo, tusiangalie maslahi ya tumbo letu katika gharama ya nchi yetu, no please. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie ni namna gani tunaweza kuwaunganisha Watanzania, tuangalie namna gani siasa zinaweza kutusaidia kuipeleka nchi yetu mbele, tupishane kwa hoja tusipishane kwa Vyama vyetu, tupishane kwa miono, tusipishane kwa maslahi, mimi ninachokiona hapa ni maslahi nani atabaki kwenye nafasi gani, nani atabaki azidi kuwa katika nafasi fulani na aonekane zaidi. Hayo mambo hayatujengi na hayo mambo hayataisaidia nchi, we can torn this country into pieces kama hatutobadilika, nataka niwaambie wanasiasa wenzangu tunaweza tukaamua ni aina gani ya nchi tunataka kuijenga, aliyoiacha Mwalimu Nyerere ambayo tunaonana sisi wote ni ndugu, sisi wote ni marafiki au nchi mpya ambayo South Africa leo wanalia, au nchi mpya ambayo Rwanda imewa-cost.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema, Mipango siyo tatizo, Mipango ni matumizi, tutakuja hapa tutaongea, tutapewa posho, tutarudi Majimboni, lakini tukirudi bajeti imetekelezwa kwa asilimia 20, Bajeti imetekelezwa kwa asilimia nne. Nitoe mifano tena halisi kabisa kama muda utaniruhusu, katika mwaka wa fedha 2016/2017, Wizara ya Kilimo, katika fungu la maendeleo ilitengewa bilioni 100, ni bilioni mbili tu ziliweza kutolewa, imagine tumekaa Bunge zima hapa…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante.