Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa uliokusudiwa kutekelezwa na Serikali pamoja na Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2020/2021

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipatia fursa hii ili nichangie katika haya Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nitumie nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Mipango, Dkt. Mpango na Naibu wake Waziri pamoja na Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Fedha kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya. Kwa kweli inaleta matumaini makubwa sana kwa Taifa letu kwa sababu matokeo ya Mpango yanaonekana katika jamii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo linadhihirika kwa sababu huwa tunajadili kila mwaka Mpango wa mwaka mmoja mmoja lakini hii ni kwa sababu tumekwishapitisha Mpango wa Miaka Mitano wa Maendeleo ya Taifa 2016-2021. Pia Mapendekezo haya ya Mpango yanafuata pia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Ilani ya Uchaguzi Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nitumie nafasi hii kuwapongeza waandaaji wote wa Mpango huu wa Maendeleo wa mwaka mmoja wa 2020/2021. Natambua Mpango huu umechukuliwa pia pamoja na masuala mazima ya maendeleo ya Kikanda kwa maana ya East Africa, AU lakini pia SADC. Kwa hiyo, Mpango wetu unaenda sambamba na maendeleo ya Afrika na dunia kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hongereni sana waliopanga huu Mpango kwa kutumia maarifa makubwa sana kwa sababu vipaumbele vyote tulivyokuwa tumeviainisha mwanzo ni mwendelezo. Tumeona miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, katika Mpango huu tumeona ni mwendelezo wa mpango wa 2016–2021. Pia tumeona ujenzi wa reli kama Standard Gauge kutoka Dar es Salaam kuja Morogoro umeshafikia 63% ni pongezi kubwa sana. Vilevile tumeona ujenzi wa reli kutoka Dodoma kwenda Morogoro umeshafikia 16%. Hongera kwenu Mheshimiwa Waziri kwa sababu haya ni maendeleo na tunaendelea kuwekeza fedha kwa ajili ya miradi mikubwa kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tumeona ujenzi wa Bwawa kubwa la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere la ufuaji wa umeme karibu MW 2,115, tunaenda kupunguza uhaba wa umeme katika nchi yetu lakini pia tunaenda kusambaza umeme vijiji vyote nchi nzima. Kwa hiyo, suala la nishati kwa wananchi wetu vijijini na mijini litakuwa ni historia baada ya kukamilisha Mpango wetu wa mwaka 2016–2021, nawapongeza sana Waheshimiwa Mawaziri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tunaona mpango huu umejikita zaidi katika ku-link na Sera yetu ya Viwanda. Tunatambua sasa katika nchi yetu tuna Sera ya Viwanda inaenda sambamba na uwekezaji huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, binafsi napenda kuchangia upande wa kilimo. Wenzangu wamezungumza tumeona sekta zinakuwa sana kwa kasi, sekta ya ujenzi inakua kwa 16%, madini 13%, mawasiliano 10.7%, usambazaji wa maji katika nchi yetu na wenyewe unakua sana kwa kasi. Sasa naiomba Wizara hii ya Mpango, katika mapendekezo yao sasa wajikite katika kilimo. Tuwekeze zaidi kwenye kilimo kwa sababu Tanzania kama ilivyo jiografia yake haifanani, kuna maeneo mengine ni rafiki kwa kilimo na mengine siyo rafiki, kule ambako kuna urafiki kwa upande wa kilimo tuwekeze vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfano, kuna maporomoko ya maji, kipindi cha msimu wa mvua za masika inapofika mvua nyingi zinazopatikana, maji mengi yanapotea sana. Hasa kwa upande wetu sisi pale Igunga ukiangalia ule upande wa Ziba, Simbo, Choma cha Nkola na maeneo mengineyo Tanzania maporomoko ya maji ni makubwa yanapotea. Maandiko yapo katika Wizara ya Maji na Wizara ya Kilimo juu ya ujenzi wa mabwawa, skimu zile za umwagiliaji, zikijengwa hizi katika nchi yetu itawasaidia wakulima kulima mara mbili au tatu kwa mwaka kwa sababu watakuwa na maji ambayo yamehifadhiwa tofauti na kipindi ambacho maji yanamwagika hayana sehemu yanapokusanywa mwisho wa siku yanapotea. Hii ni kupoteza rasilimali lakini pia nguvu kazi na mapato katika nchi yetu kwa sababu tunapolima mara mbili mpaka mara tatu wananchi na nchi itapata kipato kwa maana ya kodi watakapokuwa wanauza. Kwa hiyo, niombe Mpango wetu sana pia ujielekeze huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango ni mzuri na mapandekezo ni mazuri shida ni utekelezaji. Niombe katika kipindi hiki ambacho tumebakiza tujikite zaidi katika kilimo, hii itasaidia kuinua kipato cha wakulima. Tunatambua karibu 70% ya Watanzania wako kwenye sekta ya kilimo, tunatambua changamoto za kupatikana kwa mbegu za mazao yetu kupatikana kwa wakati. Niombe Wizara zinazohusika zisambaze pembejeo zote ikiwa ni pamoja na mbegu ili kurahisisha wakulima kulima kwa wakati lakini pia ufanisi utakuwepo katika kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapopata ufanisi kwenye mazao yetu kwa mfano kama pamba, mpunga, korosho, kahawa, hawa wakulima wakipewa pembejeo kwa wakati wakazalisha tunaona tunapoenda kwenye mauzo tunapata foreign currency. Kwa hiyo, niombe sana Mheshimiwa Waziri Mpango muwekeze sana katika kilimo. Pia tusaidie kukuza thamani ya mazao yetu kwa sababu tunaona mazao yetu bado hatujafikia level ambayo tunaiihitaji, kwa kweli niombe sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia tukiachana na sekta hii ya kilimo, Mheshimiwa Waziri wa Mpango, amezungumza mwenzangu hapa upande huu wa TARURA kuhusu miundombinu. Naomba TARURA iongezewe fedha za kutosha katika ujenzi wa barabara. Tunahitaji barabara za vijijini ambazo ndizo zinazosafirisha mazao kutoka mashambani kuleta kwenye masoko. Tuwekeze huko fedha za kutosha ili barabara hizi ziweze kufunguliwa lakini pia ujenzi ufanyike kwa wakati. Maana leo tunaona TARURA ina fedha ndogo sana ukilinganisha na TANROADS. Katika ule mgawanyo wa fedha kutoka Road Funds karibu 70% inakwenda TANROADS, 30% wanapata TARURA, ni ndogo sana, ingewezekana ingeenda fifty-fifty au TARURA wakapata wakapata 60% TANROADS wakapata 40% kwa sababu miundombinu ya barabara kubwa sasa iko vizuri tofauti na hizi barabara za vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi Wabunge tulio wengi tumetoka vijijini, tuwekeze sana huko kwenye barabara hizo. Tuziboreshe barabara hizi ili wakulima waweze kusafirisha mizigo yao, mazao yao lakini pia tutawarahisishia hata usafiri na kufika kwa wakati katika maeneo mbalimbali. Katika mchango wangu kwa upande huo napenda ukae kwa style hiyo kwamba fedha nyingi zipelekwe kwa upande wa TARURA ili tuweze kujenga madaraja, barabara bora kwa ajili ya kusafirisha mazao yetu lakini pia itaturahishia kukuza pato la Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwapongeze sana kwenye Mpango huu wa Miaka Mitano tumeboresha sana sekta ya afya, hospitali nyingi zimejengwa, tunajenga karibu hospitali 67 na vituo vya afya zaidi ya 400 nchi nzima vimejengwa. Leo kila sehemu umeme umesambazwa, utazungumza kitu gani ambacho hatukigusi hata watumishi hewa tumedhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri Mpango maana tulikuwa na watumishi hewa wengi lakini mmeweza kupitia upya, mmeangalia na hizi nafasi leo zimekuwa fixed, tumepata watumishi ambao ni active. Pia, mishahara hewa tumeondoa kwa maana tumeshadhibiti huku. Kwa sababu tunaelekea mwishoni Mpango huu umeelekea kufanikiwa kwa kiwango kikubwa sana. Sisi ambao tunawawakilisha wananchi tunauona utekelezaji wa Mpango wa 2016 – 2021, umekwenda vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)