Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

Hon. George Malima Lubeleje

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpwapwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali kwa Mwaka 2019 pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa kwa Mwaka 2019

MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia hoja hizi mbili, Kamati ya Hesabu za Serikali Kuu na Serikali za Mitaa. Niwapongeze wenyeviti na pamoja na wajumbe wa kamati hizi mbili. Vilevile, nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais- TAMISEMI anafanya kazi nzuri sana na hizi halmashauri nyingi ameshazitembelea. Hivi karibuni amegawa mashine za kukusanyia mapato 7227 kwa ajili ya kuboresha ukusanyaji wa mapato katika halmashauri. Ni kweli halmashauri zilinunua mashine lakini mashine nyingi zilichakachuliwa kwa hiyo walikuwa hawakusanyi mapato ya kutosha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali za Mitaa ni Serikali kamili, ukisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ibara ya 145 na 146 inatambua kwamba Tanzania kutakuwa na Serikali za Mitaa. Hapo zamani hazikuwa kwenye Katiba lakini sasa zinatambulika kikatiba. Serikali za Mitaa zinakusanya mapato na mapato ya ndani ndiyo uhai wa kila halmashauri za mitaa lakini halmashauri nyingi wanategemea ruzuku na ruzuku ya Serikali ni kidogo sana. Vyanzo vingi vya mapato vyenye kero vilifutwa kwa sababu vilikuwa ni kero sana kwa wananchi na TAMISEMI au Serikali iliahidi kuwapa ruzuku Serikali za Mitaa ili kuwaongezea mapato ili waweze kutekeleza miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kusikitisha Serikali haitoi ruzuku ya kutosha kwa halmashauri hata zile fedha ambazo zimetengwa kwa ajili ya kusaidia halmashauri hazitolewi zote. Kwa hiyo, utakuta miradi mingi imekwama, sasa hivi ukienda kila halmashauri kuna maboma, majengo ya zahanati yamekwama, majengo ya shule yamekwama. Kwa mfano katika Jimbo langu la Mpwapwa tuna zahanati tatu ambazo zimekwama mpaka sasa, zahanati ya Mugoma sasa miaka kumi haijakamilika, zahanati ya Mzase miaka kumi haijakamilika lakini kama halmashauri wangekuwa wanakusanya mapato ya kutosha na Serikali ingekuwa inatoa ruzuku ya kutosha hayo majengo yangeweza kukamilika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kudhibiti; katika utaratibu wa Local Authorities kuna Kamati ya Fedha na Mipango na Uongozi, hawa ndiyo wanaodhibiti mapato na matumizi ya halmashauri za wilaya. Bahati mbaya sana fedha nyingi za halmashauri zinakusanywa lakini hazifiki kwenye Mfuko Mkuu wa Halmashauri, kwa hiyo, zinatumika sana bila sheria ya fedha ambayo inahusika. Nilikuwa nashauri kwamba halmashauri zidhibiti mapato na matumizi na fedha zote zinazokusanywa zisitumike kabla hazifika kwenye Mfuko Mkuu wa Halmashauri na kupelekwa benki.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu ulipaji wa posho za madiwani. Posho za madiwani ni haki yao, ni suala la kisheria, siyo kwamba halmashauri ni hiari hapana lakini kuna madiwani hawalipwi vizuri. Utakuta kuna halmashauri nyingine hazijalipa posho sasa ni miezi 12, miezi 14 hawajalipwa, na hizi posho ndiyo zinalipa deni la madiwani waliokopa kwenye vyombo vya fedha NBC, NMB na CRDB. Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI wahimize hawa wakurugenzi wamalize haya madeni kabla ya mwezi wa sita la sivyo kwa kuwa madiwani wamekopa kwenye mabenki, udiwani ukishakwisha hawataandama tena halmashauri kwa sababu halmashauri ndiyo waliowadhamini hawa madiwani. Kwa hiyo, mabenki yatawaandama madiwani, watakamatiwa mali zao madiwani, ni jambo ambalo ni baya sana kwa kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri uagize halmashauri zako zote walipe posho hizi na walipe madeni ya Waheshimiwa Madiwani au benki ili wasikamatiwe mali zao baada ya udiwani kwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho ni kodi ya majengo (property tax). Property tax mimi sipingi, TRA wakusanye property tax ninachosema basi angalau wasikae mwaka mzima (miezi 12) TRA ndiyo wagawe fedha hizi kwenye halmashauri, angalau miezi sita TRA wakishakusanya angalau miezi sita waanze kuzigawa fedha hizi kweye halmashauri, wasisubiri miezi 12. Halmashauri za Wilaya, Manispaa, Majiji wana miradi yao, miradi haiwezi kusubiri fedha zibaki mpaka miezi 12 ndiyo zigawanywe kwenye halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja hizi zote mbili na naendelea kuzipongeza hizi kamati wanafanya kazi nzuri sana na sasa hati chafu zimepungua. halmashauri nyingi na Serikalini, Mashirika, Wizara nyingi zinapata hati safi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana.