Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuja kuhitimisha hoja yangu jioni ya leo. Nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha, kutupa afya njema ili kuweza kuhitimisha majukumu ya Wizara yangu kama ambavyo ilivyo ada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja hii kwa kuzungumza na kwa maandishi. Waliochangia kwa maandishi idadi yao ni 29 na waliochangia kwa kuzungumza idadi yao ni 15 ukiwajumuisha Mheshimiwa Mwakyembe, Mheshimiwa Jenista Mhagama na Mheshimiwa Waitara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kujibu hoja kwa hoja za Kamati; kwa kiwango kikubwa Kamati imejielekeza katika kuiombea Wizara ya Ulinzi iweze kupata fedha za kutosha kutekeleza majukumu yake. Tunashukuru kwa hilo na hatuna shaka yoyote kwamba kadri hali ya uchumi inavyoimarika Serikali inaona umuhimu wa kuongeza fedha kwa Wizara yetu ili majukumu yetu ambayo ni ya msingi kabisa ya ulinzi wa nchi yaweze kufanyika kikamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hivyo Kamati ya NUU (Nje, Ulinzi na Usalama) imeshauri kuongezwa kwa ukomo wa bajeti ya Wizara ya Ulinzi, Serikali ione umuhimu wa kuongeza kasi ya ulipaji madeni ya kimkakati kwa kutenga fedha zaidi kwenye miradi ya maendeleo, Serikali itoe fedha za maendeleo zilizoidhinishwa kwa Fungu 38 kwa mwaka wa fedha unaoisha, Serikali ione umuhimu wa kuongeza fedha za maendeleo zilizotengwa, Serikali itoe fedha zote zilizoidhinishwa kwa ajili ya kugharamia mafunzo na usalama na utambuzi, Serikali itoe fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya utunzaji wa zana, magari, mitambo na Serikali itoe fedha zilizoidhinishwa kwa ajili ya kuboresha mfumo wa mawasiliano salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ujumla karibu hotuba nzima ya Kamati ilijikita katika uona umuhimu wa kuweza kupata bajeti stahili ya kutekeleza majukumu yetu na sisi tunasema ahsanteni sana na Serikali kwa kweli nia hii ipo, kadri uwezo unavyoongezeka na Wizara hii inaweza kupata mgao unaostahili kwa majukumu yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hao, naomba sasa niingie kwenye hoja za Kambi ya Upinzani na nianze kwa kusema leo nimesikitishwa sana kwa kauli zilizokuwa zinatolewa kuhusu Jeshi letu. Tumezoea kusikia kwamba ndani ya Bunge hili kila mtu anaunga mkono kazi nzuri zinazofanya na Jeshi letu. Yanapotokea maneno aidha ya kukashifu au kukejeli kwa kweli huwa napata taabu sana kwa sababu Waheshimiwa Wabunge, sisi sote ni mashahidi juu ya kazi nzuri inayofanywa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu tuangalie tu majirani zetu wapi kuko salama kama tulivyo sisi. Sasa tusichukulie kwamba amani hii tuliyokuwa nayo ipo tu imekuja yenyewe, kuna watu wanafanya kazi usiku na mchana. Kwa hivyo, naomba niwasihi sana ndugu zangu katika suala la ulinzi wa nchi tusiingize sana siasa. Tukiingiza siasa tutaharibu kwa sababu ulinzi ndiyo kila kitu. Bila ya ulinzi, bila ya amani hamuwezi kufanya kingine chochote. Kwa hiyo, bila shaka tutarekebisha kauli zote zilizotolewa ambazo kwa kweli hazikuwa na sababu ya kutolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na hili la hali za wanajeshi wastaafu hususan cheo cha private hadi Brigadier General hazilingani na uzito wa kazi wanazozifanya. Niseme tu Serikali inathamini kwa kiwango kikubwa kazi zinazofanywa na zilizofanywa na wanajeshi wastaafu. Serikali imehakikisha wanalipwa mafao yao ya kustaafu kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo za utumishi wa JWTZ. Aidha, Serikali imeendelea kupitia upya mafao ya wanajeshi wastaafu wote ili aweze kuendelea kulipwa kwa kuzingatia hali ya uchumi ilivyo kwa lengo la kuboresha maslahi haya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilieleze Bunge lako tukufu kwamba mpango wa kuboresha maslahi kwa wanajeshi wanaostaafu upo na tunaenda hatua kwa hatua, Jeshi hili ni kubwa. Huwezi kufanya watu wote wapate mara moja. Ilianza ngazi ya Major General mpaka Jenerali, itafuata ngazi nyingine na hatimae tutakamilisha Jeshi lote lakini maadam nia na dhamira ipo, hali ya uchumi ikiruhusu jambo hili litatekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja kutoka Kambi ya Upinzani kwamba nyongeza ya mishahara kwa wanajeshi, wao waliita annual increment haipo kwa maana walisema wanajeshi hawapati annual increment kwa kipindi chote cha Serikali ya Awamu ya Tano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaeleze kwamba statement hiyo sio kweli, Serikali inaendelea kutoa annual increment kila mwaka kwa ngazi za vyeo husika. Serikali imekuwa ikitoa nyongeza za mishahara kwa maana annual increment kwa kipindi chote cha Serikali ya Awamu ya Tano na inaendelea kufanya hivyo. Aidha, hakuna malimbikizo yoyote ya annual increment ambayo hayajalipwa au wanajeshi wanadai. Pia hakuna posho zilizofutwa, bali zilizopo zimeendelea kuboreshwa zaidi mfano, kwa mwaka wa fedha 2018/2019 posho za wanajeshi zimeboreshwa kwa asilimia 15 ikilinganishwa na posho za mwaka uliopita. Kwa hiyo, hapa tunachozungumzia ni kwamba kila mwaka kwa kila cheo kuna increment wanayopata kwenye mishahara yao. Lakini vilevile posho zinazotolewa kwa mfano Ngome Allowance ile ya makazi fedha za maji, fedha za umeme, fedha za taaluma zote zimekuwa zikipata increment na kama nilivyosema kwa kiwango cha asilimia 15. Kwa hiyo, ningeomba sana kwamba hizi statement zinazotolewa pengine ni vyema watu wakathibitisha kabla ya kuzisema ndani ya Bunge lako. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu posho ya chakula kwa wanajeshi yaani ration allowance, Kambi ya Upinzani imesema imegeuzwa kuwa ada ya kulipia mafunzo katika shule na vyuo vya kijeshi kwa wanajeshi wanaokwenda mafunzoni. Nataka niwaeleze ndugu zangu kwamba ration allowance ni fedha zinazotolewa kwa ajili ya kumlisha mwanajeshi na kila mwanajeshi anapata fedha hizo kupitia kwenye akaunti yake pamoja na mshahara wake. Kwa hiyo ukisema kwamba umepewa fedha za chakula halafu umekwenda kwenye mafunzo unataka ulishwe, hiyo sio sawa. Cha msingi hapa ni kwamba kuna maeneo machache ambayo watu wanaopata ration allowance bado wanapewa na chakula, nayo ni katika operations, siyo kwenye mafunzo ya kawaida. Kwa hiyo, operations na kazi za mipakani, kule wanalishwa na wanapata ration allowance, lakini kwa wengine wote wanatakiwa wajilishe kwa sababu fedha hizo wameshaingiziwa kwenye akaunti zao. (Makofi)

Kuhusu suala la JWTZ kuingilia utendaji wa kazi za Jeshi la Polisi, mimi nadhani tu niliweke sawa hili ili Waheshimiwa waelewe, vyombo hivi vya ulinzi na usalama haviwezi vikafanya kazi kila kimoja peke yake, hiyo itakuwasiyo kazi ya ulizi. Kazi ya ulinzi inataka vyombo vishirikiane, kwa sababu matishio ni tofauti. Unaposema kwamba jeshi la wananchi libaki mipakani, wakati kuna ugaidi, unategemea itakuwaje. Inapokuwakuna suala la ugaidi lazima Jeshi la Polisi, Jeshi la Wananchi, Usalama wa Taifa na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vishirikiane, ndicho kinachoanyika. (Makofi)

Kwa hiyo, JWTZ na Jeshi la Polisi ni Vyombo vya Ulinzi na Usalama ambavyo vimeundwa kwa sheria na mipaka ya majukumu yao ya kiutendaji ipo wazi, na hakuna mwingiliano wowote. JWTZ itanedelea kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria za nchi yetu na bila kuingilia mamlaka ya vyombo vingine vya ulinzi na usalama, ni masikitiko na bahati mbaya sana kwa Kambi ya Upinzani kudiliki kusema, kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi anaingilia Mamlaka ya Jeshi la Polisi, hii siyo sahihi, hata kidogo na tunaikataa kwa nguvu zote, kwa sababu kwanza tutambue kwamba Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, ndiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Vyombo vya Ulinzi na Usalama. Kwa hiyo, Mkuu wa Majeshi anayo haki kuzungumzia vyombo vyote kwa ujumla wake, akiwa kama Mwenyekiti. (Makofi)

Kwa hiyo, nadhani hoja hii siyo sahihi na tuendelee kuamini kwamba bila ya kuwa na Jeshi kushirikiana na vyombo vingine, kuna baadhi ya kazi zitashindikana kufanyika! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa kuna hoja ya kwamba Serikali haiwekezi kwenye shughuli za ugunduzi na utafiti katika JWTZ. Nataka niwaeleze ndugu zangu kwamba ukienda Nyumbu, ukienda Mzinga, utakuta kuna baadhi ya tafiti zinafanyika hadi leo, ni kweli tunakiri kwamba fedha za kuwawezesha kufanya tafiti kubwa bado hazijapatikana, lakini hii haikuwakatisha tamaa, wamekuja na mpango mkakati, taasisi zote mbili hizi; Nyumbu, wao wamekuja na mpango wa miaka 10, wenye bajeti ya shilingi bilioni 227 na kwa miaka mitano ya kwanza bilioni 105. Fedha hizi zikipatikana kupitia bajeti zetu kwa sababu sasa hivi hili suala liko katika majadiliano Serikalini, Shirika hili litaweza kufanya kazi zake za utafiti inavyotakiwa na vilevile Mzinga wana mpango wa miaka mitano, wenye bajeti ya shilingi bilioni 152 ambao na wenyewe fedha hizi zikianza kutiririka katika bajeti zao kwa miaka inayokuja, wataweza kufanya tafiti kubwa zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mchakato wa manunuzi ya sare za Jeshi, kwamba uchunguzwe. Walisema Kambi ya Upinzani, kwamba taratibu za ununuzi wa mavazi ya Jeshi hufuata taratibu kwamba hauendi, yaani una walakini, lakini pia wanajeshi wanavaa mavazi ambayo hayawatoshi, kwamba kuna mavazi madogo au makubwa wanapewa. Sasa tuweke sawa kwanza kuhusu mchakato wa manunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna utata wowote katika utaratibu wa manunuzi ya mavazi ya Jeshi. Tender zinatolewa kama kawaidia, watu wanashindanishwa kama kawaida na wanaoleta mavazi hayo basi wanakuwa wamweshinda kitaratibu zinazohusika, sasa sijui Kambi ya Upinzani wanalitoa hili wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu mavazi kutowatosha wavaaji, nalo ni maelezo ambayo yana kasoro. Niseme tu kwamba mavazi yote ya Jeshi, yote, wanajeshi kila mtu anapimwa isipokuwa kombati, kwa hiyo, ukiwaonaleo wanajeshi wote wamevaa mavazi yanayowatosha, kwa sababu wanapimwa. Kombati peke yake ndiyo zinaletwa kwa size mbalimbali, kuna ndogo, medium, large na extra-large. Sasa kuna mtu yeye ni size yake ni small amepewa extra-large, kunahaja gani ya kulalamika, si kurudisha tu ili aweze kupewa kwa size yake. (Makofi)

Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa, ndugu zangu Kambi ya Upinzani, msiyachukue maneno haya kijumlajumla, haya ni maneno yenye lengo la kugombanisha, nadhani si sawa sisi tukayabeba kwa ujumla namna hiyo. Mimi sioni tatizo lolote, kamasize zipo kuanzia small mpaka extra-large, kwa nini usipate size yako, kama umepewa siyo, ni kiasi cha kubadilisha tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maboresho ya Sheria ya Ulinzi wa Taifa; Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea kufanya majadiliano ya ndani yenye lengo la kuboresha Sera ya Ulinzi na kama tulivyosema siku za nyuma, hatimaye tumepata mapendekezo au tuseme maoni ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na vilevile baada ya kupitiwa na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na wenyewe wametoa maoni yao, kazi inayofanyika sasa hivi ni kutayarisha rasmu ya kwenda kwenye Balaza la Mawaziri ili hatiye hii sera iweze kukamilika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya ulinzi na usalama kwenye mipaka yetu ya nchi; Wizara inasema zoezi la kurejesha alama za mipaka kimataifa linahitaji fedha na utayari wa nchi husika. Hapa hoja ilikuwa ni kwamba mipaka hakuna alama na kwamba Wizara husika hazijashughulikia tatizo la mipaka kwa maana ya beacons na kadhalika. Mheshimiwa Masoud hili suala amekuwa akilizungumza kila mwaka, lakini tushukuru tu na niseme kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa na katika mpaka wetu wa Kenya kazi hii imefanyika, katika mpaka wetu wa Uganda, kazi hii imefanyika na katika mpaka wetu wa Burundi kazi hii imefanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipaka mingine tutaendelea kwa kadri fedha zinavyopatikana na mtambue tu, kwamba kazi hii ni kazi ya Wizara nyingi, Wizara ya Ardhi, Wizara ya Mambo ya Nje, Wizara ya Ulinzi na kadhalika. Kwa hiyo, ni vyema tushukuru kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa na tumeanza sasa kuboresha mipaka yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu maeneo ya wananchi yaliyochukuliwa na Jeshi Serikali kushindwa kulipa fidia; hii imekuwa ni hoja kwa siku nyingi sana, na naomba nieleze kidogo kuhusu hoja hii kwamba Serikali inatambua umuhimu wa kuhakikisha kwamba wananchi wote wanalipwa fidia kwa kadri uwezo unavyopatikana. Mwaka huu tunaomaliza, tulitenga bajeti ya shilingi bilioni 20.9 kwa ajili ya kulipa fidia katika maeneo mbalimbali. Tumeshafanikiwa kulipa eneo moja la Kilwa, lakini tumeanza kulipa Kakonko kule, na tumeanza vilevile kulipa maeneo kadhaa.

Kwa hiyo, ninachoweza kusema hapani kwamba, sasa hivi Wizara ya Fedha imeshaweka/imeshatenga shilingi bilioni 16 ili tuendelee kulipa maeneo mengine yaliyobaki. Tathmini, uhakiki ulishafanyika katika katika baadhi ya maeneo, samahani, tathmini ilishafanyika, lakini uhakiki ndiyo unaoendelea sasa. Kwa hiyo, kuna eneo la Ilemela kule, maeneo mawili katika Wilaya ile, lakini vilevile kuna maeneo ya Tarime, kuna maeneo ya Makoko, kuna maeneo kadhaa ambayo yanafanyiwa uhakiki, ili fedha zile zianze kulipwa kwa wahusika.

Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, tuvute subira wakati mchakato huu wa uhakiki wa fedha zilizofanyiwa uthamini unaendelea ili tuweze kukamisha ulipaji. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro ya ardhi baina ya wananchi na Jeshi, kama vile kubomolewa nyumba, kukatwa mazao ya wananchi na kadhalika; yamezungumzwa sana humu ndani, lakini mimi napenda niseme mambo mawili; kwanza tutambue kwamba maeneo ya jeshi ni maeneo ambayo wananchi wakiambiwa wasikae karibu ni kwa maslahi yao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na ningekuwa nayasema haya bila ya matukio yaliyotokea siku za nyuma, pengine ningeonekana nasema tu, lakini tuna mifano hai, yalitokea pale Gongo la Mboto, yalitokea pale Mbagala, kwa nini wananchi waendelee kukaa katika maeneo haya.

Sasa watu tunatofautiana, kuna watu unaweza ukawaambia mnatakiwa kuhama wakahama, kuna watu wengine hawaelewi lugha hiyo, kwa hiyo, lazima hatua zichukuliwe, na ndiyo maama hatua zinapochukuliwa, basi tusiwe tunapiga kelele ni kwa sababu ya maslahi yao wenyewe, haya maeneo mengine ni hatari kwa watu kukaa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kikubwa zaidi ni kuangalia nani mwenye haki, unapokuwa umevamia katika eneo la Jeshi lililopimwa, lenye mipaka. Kuna njia gani zaidi ya kuzungumza zaidi ya kumwambia mtu atake asitake lazima aondoke, kwa hiyo, ndicho kinachofanyika. Kwa hiyo, sioni kama hili suala tulichukulie kisiasa, tulichukulie kwamba watu wameonewa, watu hawajaonewa, na mpaka haya yametokea, wameshapewa warning mara kadhaa, kila aina ya juhudi zinafanyika na nimwambie tu ndugu yangu aliyezungumia suala hili la kukatwa hii mipapai, ni kwamba Serikali za Mitaa ile, za Vijiji vile, zilitumika kuwashawishi, kuwaambia wananchi wahame, lakini baada ya mbinu zote kushindikana, basi lazima tutumie njia hizi, hakuna njia nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushiriki wa amani nje ya nchi, Waheshimiwa Wabunge kwenye upande wa Upinzani walitaka kujua idadi ya wanajeshi waliopoteza maisha na vilevile na stahili wanazopaswa kupewa endapo wanapoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwanajeshi anapoumia au kufariki akiwa katika ulinzi wa amani huwa anapewa malipo ya sehemu mbili, sehemu ya kwanza anapata malipo ambayo yanatiolewa na Umoja wa Mataifa na sehemu ya pili hutolewa na Seikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuzingatia kanuni zilizowekwa za pensheni kwa Majeshi ya Ulinzi.

Kwa hiyo, hakuna utata katika mafao ya wanaopoteza masiha wakiwa katika ulinzi wa amani, fedha hizo zinatolewa kwa pande zote mbili na niseme tu malipo yanayotolewa na Umoja wa Mataifa ni dola za kimarekani 70,000 na fedha za rambirambi ambazo hutolewa na Mkuu wa Majeshi ikiwa ni mishahara ya miezi sita na familia zinasafirishwa pamoja na mizigo kwenda nyumbani. Kwa hiyo, hakuna utata kabisa katika eneo hili na mara zote yanapotokea maafa ya kupoteza watu katika maeneo hayo, Serikali imekuwa ikitoa taarifa na taarifa ziko wazi za idadi ambao wamepoteza maisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hili nizungumzia pia wajane wa wanajeshi waliofariki, hoja ilikuwa ni kwamba hawatunzwi, ni kwamba wajane wa hawa waopoteza maisha, Serikali imekuwa ikihakikisha kuwa wanatunzwa, wajane na mayatima na kuwapa stahiki zao kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ya jeshi katika kupambana na matukio ya kigaidi nchini; Kitengo cha Usalama na Utambuzi (Military Intelligence) kitumike kusaidia Jeshi la Polisi kubaini na kukabiliana na vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na watu wasiojulikana, mfano kutekwa kwa watu ambao wamewataja. Sasa niseme tu, ni Kambi hii hii ya Upinzani katika hoja yao walisema Jeshi lisiingilie kazi za Polisi, halafu Kambi hii hii inasema, military intelligence isaidie Polisi. Sasa tunachoweza kusema hapa ni kwamba vyombo hivi lazima vifanye kazi kwa pamoja. Military Intelligence lazima iasaidie jeshi la polisi katika masuala ya ugaidi, masuala ya uharamia, masuala ya usafirishaji haramu wa watu na kadhalika, hizo kazi lazima zifanywe kwa pamoja, kwa hiyo, msione kwamba jeshi linaingilia kazi wa vyombo vingine, ni wajibu wao kufanya kazi hizi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafasi ya Jeshi la Kujenga Taifa katika kuongeza uchumi wa viwanda nchini. Hili linatambulika, Jeshi la Kujenga Taifa linafanya kazi ya viwanda, linafanya kazi ya kilimo, ufugaji na kadhalika. Nia na madhumuni ni kwamba tuhakikishe wanachangia katika ukuaji wa uchumi na wana viwanda kadhaa kama ambavyo nimevitaja katika hotuba yangu vikiwemo Kiwanda cha Mahidi - Ruvuma, Kiwanda cha Kutengenezea Bidhaa za Ngozi - Dar es Salaam, Kiwanda cha Kokoto, Kiwanda cha Kutengeneza Samani - Chang’ombe, Kiwanda cha Maji - Dar es Salaam na kadhalika. Kwa hiyo, viwanda viko vingi, wanaendelea kufungua na biashara mbalimbali, ikiwemo ulinzi na kadhalika, ili tuweze kuchochea uchumi kupitia Jeshi letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ajira Jeshini, wanasema vijana wengi wa JKT kutoajiriwa na Jeshi, nadhani hii niitolee ufafanuzi kidogo. Tunachukua vijana wa kujitolea wengi, kwa mwaka wanaweza wakafika 20,000; hatuwezi kuwaajiri vijana wote hawa, na ieleweke kwamba anayeingia katika Jeshi la Kujenga Taifa, si kwa madhumuni ya kutafuta ajira, ni kwa madhumuni ya kupata stadi za kazi, ni kwa madhumuni ya kupewa stadi za ulinzi wa nchi yake, na hili ni Jeshi la Akiba. Kwa hiyo, hawa huwa wanapewa mafunzo yale ya kijeshi, lakini baadaye wanapewa mafunzo ya stadi za kazi. Wanaobahatika kuajiriwa wanaajiriwa na ambao hawabahatiki wanatakiwa wakajiajiri baada ya kupata stadi za kazi hizo.

Kwa hiyo, vijana wengi wamekuwa wakilalamika lakini nataka ieleweke, kwamba ukijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa, siyo kwamba unaingia kwenye ajira, ni kwamba unakuja kuoata mafunzo ya stadi za kazi na ukakamavu za uzalendo, ili hatimaye uweze kuwa jeshi la akiba kwa ajili ya nchi yako. Kuna baadhi ya nchi ni watu wote lazima wapiti huko. Kwa hiyo, ilie hoja ya kwamba mnawafundisha kutumia dhana za kivita halafu hamuwapi ajira, wala siyo hoja, kwa sababu kuna nchi, kwa mfano Israel, kila mtu, lazima apate mafunzo hayo. Madhumini yake ni nini, madhumuni yake ni kwamba hili ni Jeshi la Akiba, wanapohitajika wakati wa vita, lazima watu hawa wawe wana ujuzi wa kutumia silaha ili waweze kuisaidia nchi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, muda wa saa za kazi jeshini bado unalalaikiwa, Waheshimiwa Wabunge, mimi nadhani tusiingie huku, wanajeshi wanatakiwa wawe kazini, wawe tayari masaa 24, jeshini hakuna suala la saa za kazi, saa 24 uwe tayari. Ukiwa una mapumziko ni kutokna na kitengo ambacho upo au maeneo ya kazi ambayo unafanya au una majukumu maalum, lakini kwa mara zote inatakiwa masaa 24 watu wawe kazini. Kwa hiyo, hili suala la kulalamikiwa kwa masaa 12, mimi nadhani wala siyo la msingi na tusiingilie kama wanasiasa, tuwaache wenyewe kwa kanuni zao na taratibu zao za kijeshi watekeleze majukumu yao. (Makofi)

Mimi nadhani haitakuwa busara twende na vile mnavyotaka kwamba watu saa tisa wasiwepo, limetokea tatizo, itakuwa sisi wa kwanza kulaumu kwamba Jeshi halikutekeleza wajibu wake, ndiyo maama watu wote wanatakiwa wawe kazini muda wote na tumwachie Mkuu wa Majeshi apange taratibu za kazi kwa wanajeshi wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu upandeshwaji vyeo kwamba kuna mizengwe, kuna nini, mimi nadhani hizi kauli tujiepushe nazo, hakuna mizengwe, kuna taratibu. Taratibu kupandishwa vyeo JWTZ au tuseme Jeshi kwa ujumla, utaratibu wa kupandisha vyeo maafisa na askari unazingatia mambo yafuatayo; kufanya kazi, kufanya kozi kwa cheo husika, tabia na mwenendo mzuri, utendaji kazi mzuri na kujituma, tabia yake kiusalama, nafasi katika muundo kama ikama ipo, kutimiza muda wa kukaa na cheo kimoja. Sasa haya yote yanafuatwa, asitokee mtu akaja kwa Mbunge akasema kwamba mimi sijapandishwa cheo na kozi nimefanya, kozi siyo kigezo pekee, nimetaja vigezo vingapi hapo, kuna vigezo vingi! (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo, tujiepushe na kuchukua maneno haya kutoka kwa vijana hawa au kwa watu ambao hawalitakii mema Jeshi. Mimi nataka nikupeni ushahidi wangu, kwa kipindi nilichokaa katika Wizara hii, watu wamepanda vyeo ninawaona kila wakati. Watu wamepanda vyeo kila wakati kwa sabbu jeshi hili linaendeshwa kwa taratibu na kanuni zinazotakiwa na ndiyo maana tuko vizuri, hata ulinzi wetu uko vizuri, kama ingekuwa kuna matatizo hayo simgeona kuna migomo na vitu kama hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge wengine, Mheshimiwa Richard Ndassa alitaka Kambi ya JKT Kanda ya Ziwa, hili limepokelewa litafanyiwa kazi na bila shaka na sisi tunataka hilo litokee. (Makofi)

Mheshimiwa Fakharia alitaka nyumba za wanajeshi ziboreshwe, ni kweli, tunatambua kwamba tuna changamoto ya kuchoka kwa nyumba nyingi za Jeshini, na ndiyo maana tukawa tuna ule mradi wa nyumba mpya. Nyumba mpya zile zimejengwa zaidi ya 6,000, hazitoshelezi, nyumba za zamani kuna bajeti ndogo Wizarani, kuna bajeti ndogo Ngome kwa ajili ya kukarabati nyumba zile, lakini kwa sababu ya upungufu wa bajeti, hatuwezi kufika kote zikawa nzuri kwa wakati mmoja. Tunaomba tuvumilie wakati utaratibu unaendelea awamu kwa awamu kuboresha nyumba na ukarabati wa nyumba za wananchi.

Kuhusu suala la fidia kwa wanaodai, hili nimeshalizungumza, fidia za ardhi, suala la ajira, lini watapata ajira kama alivyosema Mheshimiwa Rais, tunalifanyia kazi liko katika mchakato wa kupanga wale ambao Mheshimiwa Rais alisema wapatiwe ajira, watapata ajira hizo kama ilivyoagizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haki za wastaafu kusumbuliwa, hili Mheshimiwa Fakharia naweza nikasema kwamba tumelipokea, tunaona ugumu wa mtu ambaye amestaafu hajapata mafao kwenda Makao Mkuu kila mara kunaweza kukamgharimu sana. Tutatafuta utaratibu mzuri zaidi wa documents zote kuwekwa sehemu moja pale Zanzibar ili wazijaze na baadae baada ya kukamilisha mchakato huo zipelekwe Makau Makuu ndipo muhusika atakiwe kwenda kule ili kumalizia mchakato.

Mheshimiwa Anatropia alizungumzia bima ya afya, na sisi tunakubaliana kwamba ni muhimu tupate bima ya afya kwa wanajeshi na mchakato wa kuanzisha bima ya afya kwa wanajeshi unaendelea. Sisi kama Wizara tunataka bima ya afya ya wanajeshi itayoendeshwa na wanajeshi na hili tunasababu ya kutaka kufanya hivyo, kwa sababu fedha zitakazopatikana tutaweza kuboresha vituo vyetu, kujenga vipya na kutumia na hospitali nyingine kutoa huduma. Kwa hiyo watu wasiwe na wasiwasi kwamba labda mna vituo vichache hapana, vituo vingine vitatumika ambavyo siyo vya jeshi tukiwa na bima ya afya.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, SUMA kujiingiza kwenye mikataba mibovu, hili lilishazungumzwa Tanzansino, Cami SUMA, Equator wote hawa tulishatolea ufafanuzi katika bajeti zilizopita, mikataba hii imesitishwa kwa sababu haikuwa mizuri na ni nia ya Serikali kuondoa mikataba yote mibovu na sasa hivi mikataba mingine yote tunayoingia tunahakikika inakwenda vizuri ilituweze kupata masilahi kutokana na mikataba hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ile Kampuni ya URSUS, Mheshimiwa Anatropia nikueleze tu kwamba URSUS haifanyi kazi na SUMA JKT, inafanya kazi na NDC, wanakwenda vizuri matreka tunayaona wanaendelea kama kawaida. URSUS hawapo upande wa SUMA. (Makofi)

Mheshimiwa Maryam Msabaha, kuhusu viatu kwamba havina viwango vinavyotakiwa; nieleze tu kwamba viatu sasa vinanunuliwa nchini humuhumu, SUMA JKT wana kiwanda kidogo cha viatu, lakini kuna kampuni zinazozalisha ndani zinanunuliwa humu ndani. Kwa hiyo siyo kweli kwamba tunaendelea kununua kutoka China vyenye kiwango kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uhakiki wa mipaka nilishalitolea maelezo Mheshimiwa Rehani anataka mafunzo ya JKT yawajenge vijana kujitegemea, hili ndiyo tunalolifanya, tunawafundisha stadi za kazi ili waweze kujitegemea na kuna programu chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya uwezeshaji. Ni matumaini yetu kwamba tukiziunganisha hizi baada ya kupata stadi za kazi na kuwezeshwa vijana hawa wataweza kujitegemea wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, JKT lijitegemee kwa chakula ndiyo nia yetu, ni kweli tunayo maeneo makubwa ya kilimo na ufugaji, tunataka tuwawezeshe JKT kifedha kwa maana kibajeti ili waweze kulima, waweze kufuga wajitegemee wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Ras Mshindo kwamba ijengwe karakana na bandari ya uvuvi, hilo liko katika nia yetu kuweza kuweka karakana pale nzuri kwa ajili ya meli za kijeshi na meli za kiraia, vilevile ikiwezekana kuweka bandari ya uvuvi ili kuweza kupata kipato kwa ajili ya kuendesha Jeshi na Serikali kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Malembeka Serikali iangalie jinsi ya kuajiri vijana wa JKT, hili nilishalitolea ufafanuzi Waheshimiwa Wabunge vijana hawa ni wengi, hatuwezi kuwachukua wote, lakini vyombo vyote vya ulinzi na usalama vimetakiwa kuchukua kutoka JKT. Kwa hiyo, baada ya kuchukuliwa na vyombo vyote vya ulinzi na usalama bado wanabaki wengi ni lazima watafutiwe njia nyingine za kujiajiri.Kwa hiyo wasitegemee kwamba wote watapata ajira katika vyombo vya ulinzi na usalama.

Kuhusu Waziri atoe taarifa ya kupigwa watu kule Afrika ya Kusini, hili lilishatolewa ufafanuzi na Waziri wa Mambo ya Nje kwamba atalitolea maelezo yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Jeshi Welezo kwamba haliendani na mandhari ya pale na vitu vinavyofanyika siyo vizuri, hili limeshazingatiwa na limefanyiwa kazi kwa kweli yale mambo ambayo yalikuwa yanaharibu taswira pale yameshaondolewa.

Mheshimiwa Kanali Masoud, Serikali iongeze pensheni kwa wastaafu; hili liko katika mkakati kama nilivyosema awamu kwa awamu, mipaka fedha nyingi za upimaji na fidia hazitoshi Serikali iongeze, tunakubaliana na kadri bajeti itavyoruhusu tutaendelea kupima ili kuondoa migogoro ambayo kila mara inajitokeza. Kuhusu Nyumbu na Mzinga yaboreshwe, nimeshatoa ufafanuzi kwamba wana mipango mikakati sasa ili kuweza kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Salim Jeshi limetumika kiutemi kufyeka mipaka nilishalisemea. Wanajeshi hawalipwi overtime, hakuna Jeshi duniani wanaolipwa overtime, Jeshi dunia nzima wanafanya kazi muda wote. Kwahiyo hakuna suala la overtime jeshini, wanakatwa kodi kwenye mishahara ndivyo utaraibu, Serikali inajiendesha kwa kodi za watu wote, hakuna upendeleo katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mishahara haina tofauti na watumishi umma, hii siyo kweli wana viwango vyao ni tofauti, hawana bima za afya ndiyo kama tulivyozungumza kuhusu bima ya afya na fedha zitumike kwenyepiece keeping ili kupata fedha. Piece keeping tunafanya na hizo re- embracement tunazipata, na tunaweza kuboresha Jeshi kupitia re-embracement hizo.

Mheshimiwa Musukuma ametaka Wabunge wapate mafunzo pale NDC, ni wazo zuri na mimi ninashauri kwa kila mwenye nafasi na atakayependa anaweza ku-apply pale NDC aweze kupata mafunzo kwa kweli itabadilisha taswira au uelewa wa ulinzi katika nchi yetu.

SUMA JKT wapewe ulinzi wa migodi watafanya kazi ya kwenda kushawishi migodi iwape kazi kwa sababu ni uwamuzi wao kumpa wanaemtaka lakini SUMA JKT watafanya kazi hii. Kuhusu bima ya afya, Mheshimwa Mlinga tulishaitolea ufafanuzi, Mheshimiwa Getere alitaka matreka ya SUMA JKT pale kilimo kwanza yaondolewe au wakulima warudishie, hili limepokelewa na Mkuu wa JKT atalifanyia kazi ili kuhakikisha kwamba tatizo hilo linaondoka kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo hoja nyingine kuhusu maeneo mengi ya Jeshi kuvamiwa na wananchi kuanzia sasa au tumeshatoa utaratibu wa kwanza kupima maeneo ya Jeshi ili kuweka mipaka. Nadhani hii ndiyo itaondoa tatizo lote, kwa miaka mingi Jeshi lilikuwa lina maeneo ambayo hayajapimwa hiyo ilitoa nafasi kwa watu kuyavamia, lakini sasa yatapimwa na yatapewa hati miliki, ili kuondoa utata huu wa kuvamiwa mara kwa mara na kuleta migogoro.

Vilevile tutaweka mapango kwa sasa wakati utaratibu huo wa kutafuta fedha za kupima na kupata hati miliki mapango yatawekwa, miti itapandwa ili kuondoa utata wa mipaka ilipo na wananchi waache kuyavamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakuu wa Vikosi wamepewa maelekezo ya kufanya doria mara kwa mara ii watu wasiachiwe wanajenga wanamaliza halafu ndiyo wanakuja kubomolewa, hii iwe inafanyika pale wanapoanza ili kuondoa malalamiko yanayotokana na watu ambao wameshajenga au wameshawekeza vya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fedha za mikataba kwamba Serikali itenge fedha za kutosha katika fungu la maendeleo ili kulipa madeni ya mikataba. Hii imekuwa ikifanyika awamu kwa awamu, fedha zote karibu zote ambazo zinawekwa katika bajeti yetu ya maendeleo madhumuni yake ni hayo kulipa mikataba ambayo tumeingia, si rahisi kuilipa yote kwa kipindi kimoja na ndiyo maana kila mwaka tumekuwa tunafanya hivo awamu kwa awamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la Mzinga na Nyumbu, nilishatolea ufafanuzi kwamba mashirika haya yana mipango mikakati ili yawezeshwe na yakiwezeshwa yatafanya kazi nzuri zaidi kuliko ambavyo inafanyika sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu fedha za chakula kwa wanajeshi kwamba Serikali itenge fedha za kula za kutosha na ziongezwe kiwango, hii hoja imepokelewa, tunaendelea mazungumzo na Hazina ili kuona uwezekano, bila shaka hili linategemea na mapato ya Serikali, lakini kila mapato yakiongezeka na uwezekano ukipatikana kwa sababu tumetoka mbali, hatukuanzana hii fedha ambayo inatolewa sasa hivi tulianza shilingi 3,000 ikaja shilingi 5,000, ikaja shilingi 8,000 sasa shilingi 10,000. Kwa hiyo, bila shaka Serikali itaendelea kuboresha hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Sera ya Ulinzi ya Taifa, nimeshalitolea maelezo kwamba mchakato wake sasa umefika hatua nzuri sana na muda si mrefu tutafikisha katika mamlaka husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Serikali itenge fedha kwa ajili ya shughuli za Jeshi ikiwemo barabara, vikosini na barabara za mipakani; kwa kweli mpaka sasa hivi hakuna sera maalum ya barabara za mipakani na fedha hizo haziji katika Wizara ya Ulinzi, fedha hizo bado zinapelekwa Halmashauri, ni wajibu wa halmashauri kuhakikisha kwamba wanaziboresha barabara hizo.

Waheshimiwa wengi walichangia kuhusu vijana wa JKT kuwezeshwa ili waweze kujiajiri. Niseme tu kwamba JKT linaendelea kutoa mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana wakujitolea, kupitia shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na ufundi. Aidha, kupitia mashamba darasa yaliyopo makambini vijana wanajifunza utaalam mbalimbali wa kilimo na ufugaji utakaopelekea kuwezakujitegemea mara wanapomaliza mkataba.

Vilevile JKT iliingia mkata na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ikilenga kuwafundisha elimu ya ujasiliamali wakufunzi wanaotoa mafunzo kwa vijana wa JKT; mafunzo hayo yameongeza uwezo vijana kupata elimu iliyoboresha ya stadi za kazi na ujasiriamali. Pamoja na hatua hizo JKT ipo katika mpango wa kujenga Vocational Training Center, Kongwa, Dodoma ili kuweza kuongeza uwezo wa mafunzo ya stadi za kazi kwa vijana ili waweze kujiajiri wenyewe baada ya kuhitimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mkazo tuweke hapa kwamba hawa vijana wawezeshwe baada ya kupata stadi za kazi wajiajiri kwa sababu si kweli kwamba wote wanaweza kuajiriwa na Jeshi na sasa hivi imekuwa malalamiko mengi, lakini ni kutojua pale wanapojiunga kwamba si wote watakaopata ajira na bila shaka wakiwezeshwa kimafunzo wataweza kujitegemea wao wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo kero ambazo zilielezwa hapa na baadhi ya Waheshimiwa Wabunge kuhusu kumbi za burudani katika Kambi za Jeshi kutumiwa na wananchi badala ya wanajeshi na kuwa chanzo cha ugomvi kati ya wanajeshi na wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa tueleze tu kwamba mwanajeshi anapokuwa nje ya kazi akifanya makosa anashtakiwa kwa mujibu wa sheria bila kujali kwamba yeye ni mwanajeshi. Kwa hiyo isichukuliwe kwamba kwa kuwa ni mwanajeshi basi anaweza akavunja sheria anavyotaka hilo halipo na tunaweza kueleza hapa kwamba mara nyingi yakitokea matatizo kama haya hata Jeshi lenyewe linachukua sheria, linachukua taratibu za kinidhamu dhidi yao na bila shaka taarifa zikitolewa basi utaratibu wa kisheria na kikanuni utachukuliwa dhidi ya wanaovunja maadili ya kijeshi wanapokuwa nje ya maeneo ya kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mbunge alitaka wanajeshi kwamba walipwe mishahara maalum; jibu ni kwamba wanajeshi wote wanapoandikishwa kwa ajili ya ulinzi wa Taifa hulipwa mishahara maaum yaani specific salary na Serikali kila mwezi kwa kuzingatia cheo na muda wa kukaa na cheo hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nadhani mengi nitakuwa nimeyatolea maelezo ya ujumla na yale ambayo sijayatolea maelezo moja moja basi kama kawaida yetu tutayapanga ili Waheshimiwa Wabunge waweze kupata maelezo ya maandishi kwa kila hoja ili waweze kujiridhisha na majibu yetu kwa wale ambao pengine majibu yao maswali yao nitakuwa sijaweza kuyatolea ufafanuzi wa kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii na baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.