Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Maria Ndilla Kangoye

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. MARIA N. KANGOYE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia fursa ya kuchangia hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri wanayofanya ya kumsaidia Mheshimiwa Rais kusimamia Wizara kwa uaminifu mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba ya Wizara ya Viwanda na Biashara imekaa vyema na imeelezea mikakati mizuri ya Serikali ya kuhakikisha tunaijenga Tanzania ya Viwanda. Pamoja na mipango hiyo, bado ipo haja ya WIzara kuhakikisha inakaa na wadau wengine wa viwanda kama Wizara ya Kilimo, Wizara ya Fedha na Taasisi mbalimbali kama NDC, OSHA, NEMC, TFDA, TBS, TRA na nyingine ili kuhakikisha dhamira na mipango mikakati iliyoainisha ndani ya hotuba hii inafanikiwa, kwani kwa asilimia kubwa taasisi hizi kwa namna moja ama nyingine zinakwamisha jitihada za kuijenga Tanzania ya Viwanda kwa kodi na tozo nyingi pamoja na urasimu mrefu wa kupata vibali vya biashara bila kusahau Wizara ya Fedha inayotoa bajeti ndogo ama kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kila leo tunakumbushana kuhusu kilimo kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania lakini mara zote tumekuwa tukijisahau kuimarisha biashara ya kilimo ambayo inatuingizia mapato makubwa na kuongeza ajira kwa Watanzania tena kwa uhakika. Nasema hivyo kwa kumekuwa na changamoto ya wafanyabiashara wa bidhaa za kilimo, wanaouza bidhaa nje ya Bara la Afrika kwa kulazimika kwenda Nairobi ama Holland kupeleka bidhaa zao kwa ajili ya kuthibitishiwa ubora katika maabara zinazokidhi vigezo vya Kimataifa. Pamoja na yote, Tanzania bado haijawa na maabara ya kupima ubora wa bidhaa kama mbogamboga na maua zilizothibitishwa Kimataifa. Ombi langu ni kuwa Serikali iwekeze katika maabara za aina hiyo ili kupunguza adha za wafanyabiashara hao.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ukosefu wa maabara hizo, bado kuna changamoto za ukosefu wa ndege za kutosha kwa ajili ya usafirishaji wa mboga mboga na maua ambapo wafanyabiashara wengi wamelazimika kusafirisha bidhaa zao kupitia Jomo Kenyatta Airport. Naomba Serikali ihakikishe inaweka mipango ya kuhakikisha kwamba inaweka mazingira ya ndege za aina hiyo kutua nchini kwa wingi kwa ajili ya bidhaa zetu kusafirishwa kwenda katika masoko ya nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana naunga mkono hoja.