Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Mahmoud Hassan Mgimwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nimpongeze Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango wangu kwanza nitajielekeza kwa mtindo wa maswali. La kwanza nilitaka kumwuliza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri, nini role la NDC hapa nchini?

Mheshimiwa Naibu Spika, wenzetu wa NDC tumewapa majukumu mengi sana, lakini ukiangalia hakuna hata jukumu moja katika yale tuliyowapa mpaka leo lililotekelezwa. Tukianzia na suala la Mchuchuma na Liganga, Mchuchuma na Liganga iko chini ya NDC. Mwaka 2012 tulisaini mkataba na Wachina hapa kuendeleza maeneo ya Liganga na Mchuchuma, lakini mpaka leo hakuna jambo lolote lililofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo hili yanapatikana material ya uhakika kwa ajili ya viwanda vyetu kwa maana ya chuma pamoja na makaa ya mawe. Kwenye makaa ya mawe tulikuwa tunaweza kupata umeme wa uhakika ambao tungeweza kupata umeme wa Megawati 50, lakini mpaka leo hakuna jambo lolote linalofanyika. Sasa nataka Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anakuja hapa aje kutuambia sababu zipi zilizosababisha mpaka leo hii mradi ule haujaanza?

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa namwomba ndugu yangu Mheshimiwa Mheshimiwa Rashid angetoka pale amwache Mheshimiwa Waziri atusikilize tunachokisema, kwa sababu atakuwa anamchanganya.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nilitaka kuchangia ni suala la umeme, kwa maana ya umeme wa upepo. NDC walituhakikishia kwamba tungepata umeme wa upepo maeneo ya Makambako na Singida, lakini mpaka leo hatujaona juhudi zozote zilizofanyika katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la tatu ni suala la Arusha General Tyre. Hiki kimekuwa kilio cha miaka mingi, lakini mpaka leo hakuna chochote tunachoambiwa kuhusu suala la General Tyre. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa tunataka atupe majibu ya maeneo haya manne, kwa nini hayafanyiki? Kama hakuna majibu ya kutosha, hatuna sababu ya kuendelea kuwa na NDC kwa sababu, tutakuwa tuna watu ambao tunawalipa mishahara, lakini kazi zao hatuzioni.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la pili ambalo nilitaka kulichangia ni suala la Kurasini Logistic Centre/Kurasini Logistic Hub. Eneo hili ni sentitive. Serikali ya Tanzania tumelipa shilingi bilioni 90 kwa ajili watu waondoke kwenye maeneo yale, lakini huu ni mwaka wa saba hakuna jambo lolote la maana lililofanyika pale. Ule ni mradi mkubwa ambao ulikuwa unagombewa na nchi zaidi ya kumi, lakini kwa namna ya kipekee Wachina walitufanyia upendeleo kutupa ule mradi, lakini hakuna jambo lolote la maana linalofanyika katika eneo hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, cha kusikitisha kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, hakuna hata sehemu moja ambayo amezungumzia Kurasini Logistic Centre. Kwa hiyo, nataka atuambie kwamba zile shilingi bilioni 90 zimepotea au zimekwenda wapi? Kama ingekuwa hatuzihitaji kuzitumia kwenye maeneo haya, bora tungezipeleka kwenye maeneo mengine. Mheshimiwa Waziri kanyamaza kimya, kitabu kizima hakuna hata sehemu imezungumzia habari ya Kurasini Logistic Centre. Kwa hiyo, shilingi bilioni 90 zinapotea bila utaratibu wowote.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine nataka kuzungumzia ni utekelezaji wa Mradi wa Bagamoyo SEZ. Pale napo tumelipa zaidi ya shilingi bilioni mbili kwa ajili ya kuwalipa watu fidia. Sasa kwa utaratibu ambao siyo wa kawaida, hela zitakuwa zinapotea kwa utaratibu huu. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri atuambie, sababu zipo zinasababisha hii miradi mikubwa ambayo ingeweza kuinua uchumi mkubwa wa nchi hii inapotea bila utaratibu?

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo la mwisho nililotaka kuchangia ni suala la viwanda vinavyobinafsishwa. Ifike wakati sasa, Dar es Salaam Stock Exchange ivisajili viwanda vyote vinavyobinafsishwa. Hii itasaidia ku-control tax evasion. Kwa hiyo, huyu regulator (CMSE) ni vyema akaleta sheria hapa Bungeni kwamba viwanda vyote vilivyobinafsishwa visajiliwe kusudi tuweze kuvi-control kwenye soko.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo naunga mkono hoja. (Makofi)