Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Ester Michael Mmasi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia kwa dakika hizi chache ambazo umenipatia. Nina heshima ya pekee kabisa na ninasimama kwa unyenyekevu mkubwa nikiwapongeza Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii husika, lakini pia na kwa taarifa yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda kukita mchango wangu kwenye vipengele viwili. Kama ambavyo imewasilishwa, kuongelewa na kujadiliwa na Wabunge wengi hapa ndani suala la Liganga na Mchuchuma, nami nitapenda nijielekeze huko kwa maslahi mapana ya ajira kwa vijana wetu wa Kitanzania. Pia nataka kuongelea ushiriki wa vijana mathalan graduates wa nchi hii katika muktadha mzima wa masuala ya biashara na ujenzi wa viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, hapa nimesimama nimeshika kitabu kilichoandikwa na Wizara ambayo wamewasilisha hapo mbele. Nitapenda nirejee ukurasa wa 15. Ninaongea haya kwa masikitiko makubwa na sijui; ninaongea kwa sababu kaka yangu Mheshimiwa Kakunda wewe ni Mheshimiwa Waziri ambaye ni mmoja wa wajumbe ambao nimekuwa nikizunguka na ninyi kwenye programu zangu za vijana. Kwa hiyo, unafahamu fika maneno waliyokuwa wanakwambia vijana wale. Nimezunguka na wewe mikoa mingi tu na umeniahidi tutazunguka mikoa mingi ukasikilize changamoto za wanafunzi wa Vyuo Vikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana mama yangu, Mheshimiwa Ndalichako ambaye ni mlezi wa wazo langu hili pamoja na kaka yangu Mheshimiwa Olenasha, nawashukuruni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ninaongea ikiwa hii ni sauti ya wanafunzi wa Vyuo Vikuu. Nikiangalia ukurasa wa 15 pale Section No. 29, kwa heshima na unyenyekevu mkubwa ninaomba Mheshimiwa Waziri ikibidi ondoa huu utata hapa. Naongea hivi nikiwaomba hata wasaidizi wenu wanisikilize na waamini kwamba Wabunge tunasoma. Waamini hata taarifa zilizotolewa na Mheshimiwa Spika kwamba, hili ni moja ya Bunge mahiri ambalo vijana na Wabunge wote tunajituma katika kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nitapenda urejee hapa, nawe ni Mwanasheria, utanisaidia na utaniongoza pamoja na Kiti chako hapo mbele. Hapa tunaambiwa moja ya changamoto iliyosababisha mkwamo wa project hii ya Liganga na Mchuchuma ni pamoja na pale ambapo mwekezaji yule alitokea kudai additional incentives, yaani vivutio vya ziada. Hii ilisababisha kukwama kwa mradi huu kwa maana ya kwamba, baada ya kupitishwa na Bunge lako hili Tukufu sheria zile mbili za kulinda na kuhifadhi maliasili ya nchi hii (Natural Wealth Resources Permanent Sovereign Act na Natural Wealth Resources Renegotiation of Unconscionable Terms 2017) ndiyo ilisababisha kukwama kwa mradi huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninasikitika kusema huu ni uwongo mkubwa na sijui kwa nini tunaandikiana vitu kama hivi, kwa sababu moja. Hapa wanasema, kwenye section 29 kwamba, wakati majadiliano yanaendelea kuhusu vivutio hivyo vya ziada, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kupitisha sheria hizi mbili na ili kukidhi matakwa ya Ibara ya 27 ya Azimio la Umoja wa Mataifa ya sheria hizi mbili, mikataba yote ya nyuma ya aina hiyo, yaani ya Liganga na Mchuchuma pamoja na Liganga, yaani zile sheria mbili za kulinda na kuhifadhi maliasili ya nchi hii zilisababisha kuwa ni sharti la kimkataba kwamba Mradi wa Liganga na Mchuchuma ukapitiwe vipengele vile.

Mheshimiwa Naibu Spika, ikumbukwe masharti ya sheria zote hizi mbili ni pale ambapo tunaona mikataba hii ilikuwa na masharti hasi. Haikuwahi kuandikwa mahali popote kwamba baada ya kupitisha sheria zile, basi Liganga na Mchuchuma ilitakiwa iende ikapitiwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutapitia Liganga na Mchuchuma kama pale ambapo tumeona kulikuwa na masharti hasi. Pengine upande wa Wizara unafahamu masharti hayo hasi yako wapi, lakini hii sidhani kama ni kweli. Nasema hivi kwa sababu, wanasema pia ati mchakato wa kupitia upya mkataba huo unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nimrudishe Mheshimiwa Waziri na nirejee haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, katika sheria zile ikumbukwe tunaambiwa katika Part Two, Ibara ya 4(1) inasema, “For effective performance of the oversight and advisory functions stipulated under article 63(2) of the Constitution, The National Assembly may review any arrangement or agreement made by the Government relating to natural resources.”

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda kwenye Article 5, ukienda kwenye section 5 ya Sheria ile ya Renegotiation for Unconscionable Terms inasema, “Where the National Assembly consider that certain terms of arrangements and/ or agreement of the natural wealth and resources of the entirely arrangement or agreement of natural resources made before the coming into force of this Act and for the interest of the people of The United Rupublic of Tanzania, the reason of Unconscionable terms it may by resolution advise the Government to initiate renegotiation.”

Mheshimiwa Naibu Spika, yaani inamaanisha hivi, pale ambapo itabainika kuna masharti hasi, ni Bunge hili litapeleka, litapitisha azimio (resolution). Likishapitisha azimio Wizara husika ndani ya siku 30 itaenda kwa mwekezaji na kumpa matakwa ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema huu ni uwongo kwa sababu hakuna azimio lolote lililowahi kupitishwa na Bunge lako hili Tukufu kupitia Mkataba wa Liganga na Mchuchuma, hakuna mahali popote. Tunachukia sana, nami binafsi sipendi kuandikiwa taarifa ambayo nikiisoma ninaona huu ni upotoshaji. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ESTER M. MMASI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninadiriki kusema kwamba ninafikiri Wizara ijipange kutuambia pale kuna kufidia. Kuna fidio lile ambalo mlifanya tathmini mwaka 2017, pengine hizi ndiyo tuziite masharti hasi. Siamini kwamba eti sheria hizi mbili zimesababisha kwamba Liganga na Mchuchuma isimame kwa sababu tu sheria hii ina matakwa hayo ya kisheria. Bunge hili halijawahi kupitisha azimio mahali popote. (Makofi)