Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Viwanda na Biashara

MHE. MAULID S. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nakushukuru kwa kunipa fursa hii adhimu nami kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu lakini vilevile nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia uzima na salama. Pia nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wka kazi kubwa na juhudi yake na hasa kutuelekeza katika Tanzania ya viwanda. Hakika Tanzania ya viwanda inawezekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waswahili tuna msemo wetu “mzigo mzito mpe Mnyamwezi” na sina shaka Waziri wa Wizara hii ni Mnyamwezi. Namwombea kila la heri afanye kazi hii tukimtegemea kwamba atatuoa hapa tulipo. Ushauri tu; Mheshimiwa Waziri Wabunge wenzangu wengi wamesema akae na wadau, lakini naanza kusema Mzee wangu akae na wafanyakazi wake, Wakuu wake wa Idara. Kuna tatizo limetokea wakati mwingine mabwana wakubwa hawatoi nafasi za kutosha kwa wataalam wetu kutoa ushauri. Sasa haya yote yaliyosemwa na Wabunge ni vizuri wakaenda wakakaa na wataalam, naamini wataalam wana njia ya kututoa hapa tulipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuja hapa na kilio chetu cha watu wa Dar es Salaam. Dar es Salaam kilikuwa ni kitovu chetu cha biashara, lakini leo iko wapi Dar es Salaam yetu ya biashara? Iko wapi Kariakoo yetu? Namtaka Mheshimiwa Waziri aturejeshee Kariakoo yetu ya Wanyarwanda, ya Warundi, ya Waganda na Wakongo. Kariakoo ambayo tulikuwa tunafanya biashara na mimi kama Mbunhge wa Kinondoni nanufaika sana na biashara inapochangamka katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakuwaje na biashara katika Jiji la Dar es Salaam kama hatuna miundombinu inayoweza kutuwezesha kufanya biashara? Nichukue fursa hii kuwapa pole Wanadar es Salaam wote kwa mafuriko yaliyotokea kutokana na mvua kubwa iliyonyesha. Dar es Salaam barabara zetu zinapitika kiangazi tu. Juzi tu hapo barabara ya Jangwani imefungwa kwa sababu ya mafuriko, barabara ya Mkwajuni imefungwa kwa sababu ya mafuriko na niseme kwamba tunawaomba sana wenzetu wa Wizara ya Fedha, ule mpango wa DMDP waliokubali kutuongezea Dola milioni 100 kwa ajili ya kufanya mabadiliko, kujenga daraja vizuri pale, kufanya Dar es Salaam ipitike mpango ule ufanyike, kwa sababu haya ndiyo yanayoiua Dar es Salaam yetu na haya ndiyo yanayoiua Kariakoo yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Kariakoo ilikuwa ni kitovu cha uchumi, ilikuwa ndiyo Dubai yetu, lakini leo wapi haipo tena. Kwa hiyo namtaka Mheshimiwa Waziri asiulize tufanyeje kwa sababu ni jambo lililokuwa wazi kwamba Kariakoo imedorora, milango iko wazi, frame hazina wapangaji, biashara haifanyiki, Watanzania wanakwenda kuchukua mzigo kutoka Uganda, it is shamefull. Unatoka hapa unakwenda kufuata mzigo Uganda watu ambao hawana bahari, kwa nini? Kwa sababu bandari yetu inasemekana kodi kubwa, watu wanapita Mombasa, wanapeleka mzigo Uganda. Sasa mambo haya mengine maana yake ni lazima tuyafanyie kazi. Haiwezekani Kariakoo inakufa ndani ya mikono yetu, haiwezekani.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, nataka nizungumzie watu wangu wa sanaa (COSOTA); COSOTA wanasimamia hati miliki na hati shiriki, leo vijana wangu wacheza filamu, vijana wangu waimba muziki, vijana wangu wafanya sanaa kazi zao zinafilisiwa, kazi zao zinaporwa, zinadhulumiwa, wameingizwa mikataba ya Chief Mangungu. Msanii anakwenda kwa mtu ambaye anamtazama kama sponsor, anamwambia kazi hii bwana kwa vile umeileta kwangu unataka nikudhamini, sasa hii kazi itakuwa ya kwangu na wewe utakuwa msimamizi, hiyo ndiyo mikataba walioingia vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo kazi zao zote zinasomeka ni kazi za mtu mmoja haiwezekani na Sheria ilikuwepo ya mwaka 1999. Ifike mahali Serikali iwatetee hawa watoto wa kimaskini, kazi zao zirejeshwe kwao wenyewe. Haiwezekani kama mtu ameingizwa mkataba wa kitapeli unasema aliuza mwenyewe, aliuza akiwa na uelewa? Aliuza kwa usahihi? Kama ameuza, ana mkataba wa kuuza? Hakuna. Mkataba uliokuwepo ni kwamba yeye, msimamizi na mjanja mmoja anajiita yeye ndiyo mmiliki.

Mheshimiwa Naibu Spika, ifike mahali Serikali yetu iwe na uwezo wa kutoa maamuzi na hasa tunapowatetea vijana wetu wanyonge. Haiwezekani vijana wanyonge wanafanya kazi zao kwa jasho lao, halafu hawapati matunda ya kazi zao, haiwezekani. Lazima ifike mahali vijana wetu wapate matunda kutokana na jasho lao, siyo kurubuniwa rubuniwa. Hili jambo mimi kwa kweli nina-appeal kwa Mheshimiwa Waziri na COSOTA lazima ifanye jambo ambalo vijana watahisi kwamba Serikali ipo pamoja nao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema biashara; biashara lazima iwe na miundombinu. Hivi sisi leo tuna biashara za viwanda, viwanda lazima uuze. Leo nimeona kwenye kitabu saruji zinakwenda nje, lakini sijaona nondo. Hivi kweli Congo, Nchi za nje zinachukua saruji zinashindwa kuchukua nondo, lakini tunawezaje kupeleka nondo Congo kama hatujatengeneza miundombinu ya kutoka hapa Tanzania kwenda Congo? Tunawezaje kulitumia soko la Congo? Tunapokuwa sisi hatutengenezi miundombinu kwenda kulifuata soko, nilitegemea viwanda vyetu vinavyozalisha cement ile cement ipite iende mahali ikafanye biashara. Mimi nategemea Wachina wanaingiza nondo Tanzania siyo kwa ajili ya soko la Tanzania, iwe ni transit, ipite kwa ajili ya kwenda kwenye masoko mengine na haiwezi kwenda kwenye masoko haya mengine lazima sisi tutengeneze miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo miundombinu ya kwenda Congo ni muhimu sana kwa sababu kuna soko kubwa, soko ambalo linaweza likawa ni suluhisho la biadhaa zetu za nondo, biadhaa zetu za cement, mahindi yetu, mchele wetu na bidhaa zote zinazozalishwa. Sasa tunapokosa kutengeneza hii miundombinu na kutengeneza kwamba vitu vinavyoingia viwe vinapita vitajaa hapa na vikijaa hapa badala yake vinaleta mzigo mkubwa kwa viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nimengalia kwenye kitabu hapa kuna watu tunafanya biashara India, sijaona biashara Uturuki kitabu hiki hakijasema na Watanzania wengi sasa hivi wanachukua biashara Uturuki, lakini kitabu hiki hakijaeleza kwamba biashara ya Tanzania na Uturuki ikoje...

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mtulia kengele ya pili imeshagonga, ahsante sana.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)