Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Ester Alexander Mahawe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kwanza naomba tu ni-declare interest mapema kwamba mimi ni mdau wa elimu pia, ni mwalimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niipongeze Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa sera ya elimu bure ama elimu bila malipo, lakini inayogharamiwa na Serikali. Ninajua kila kitu kina mwanzo mgumu, mtoto hazaliwi leo akakimbia, hata nani angekuja na Sera hii na yeye angeweza kuyumbayumba hapa katikati. Hata ndege inapotaka kuruka huwa kuna tatizo mara nyingi na mwisho wa siku ikifika kwenye cruising point inasimama sawasawa na inakwenda. Mimi niseme tu niwatie moyo sana Mheshimiwa Waziri Mama Ndalichako pamoja na Mheshimiwa Engineer Mama Stella Manyanya, tunawaamini sana akinamama tuko nyuma yenu, pigeni mzigo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu kwamba kama inavyoeleweka elimu ni ufunguo wa maisha. Na hata neno la Mungu linasema, mkamate sana elimu asiendezake, mshike sana maana huyo ndio uzima wako. Ninaomba tu niiombe Serikali yetu sasa, hebu iwekeze sana kwenye elimu. Taifa lolote ambalo elimu yake haijakaa sawasawa linazalisha watumwa ambao watakwenda kutumia matajiri.
Kwa hiyo, mimi naomba tu Serikali yetu iendelee sasa, hii ingekuwa ni Wizara ambayo ilipaswa ipate bajeti kubwa kuliko Wizara nyingine zozote kwa umuhimu wake. Itoshe sasa walimu na ualimu kutokupewa kipaumbele katika nchi hii. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, watu waliopata division four karibu na zero ndio wanaokwenda kusoma ualimu, unategemea nini na hawa watu ndio wanaotuanzishia msingi wa elimu nchi hii. Msingi wowote, hata kama ni nyumba unajenga huwezi ukaanza na msingi mbovu huko juu ukaweka zege, hiyo nyumba ni lazima itadondoka at the end of the day. Wale aliofaulu wakapata first class ndio wanaosubiri kuwapokea hawa watoto watakapofika Chuo Kikuu wakati hawa watoto wana mwanzo mbaya. Ifike mahali walimu nao wapewe nafasi ya ku-up grade, waweze kuboresha elimu zao na wapewe nafasi ya kwenda kujiendeleza. Na ikiwezekana hata watu wanaotokea division one na two waende wakasomee ualimu kwani kuna dhambi gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo litazamwe sana, imekuwa hivyo kwa miaka mingi, tutaendelea kumtafuta mchawi, mchawi ni sisi wenyewe ambao tunaweka sera mbovu kwenye elimu, mwisho tunabakia kulalamika kila iitwapo leo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nilikuwa naomba tu nizungumzie pia, suala la mitaala. Mitaala hii imekuwa ikibadilishwa kila wakati, ifike mahali kuwe na Standing Orders kwenye Wizara ya Elimu, sio kila Waziri anayeingia anaingia na lake, tunachanganywa. Wakati tukiwa tunasoma wengi wetu tulioko hapa, nakumbuka kuna kitabu kimoja cha Kiswahili, kitabu chenye lile shairi linalosema karudi baba mmoja toka safari ya mbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka nilikuwa naimba lile shairi nikiwa darasa la kwanza japo haikuwa level yangu kwa sababu, lilikuwa linaimbwa na ndugu zangu walionitangulia, kulikuwa kuna system nzuri. Nani ametuloga tukaondoa hiyo system? Tuangalie tulikoangukia ili tuweze kuboresha elimu yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyowahi ku-declare interest, nimesema mimi ni mdau katika shule binafsi. Sheria ya Elimu ya mwaka 1978 inaeleza kwamba shule sio biashara, shule ni huduma. Mwalimu Nyerere alisema watu wa asasi za kidini na wenye mapenzi mema waweze kuisaidia Serikali katika kutoa elimu, lakini leo tunashindwa kuelewa tumekuwa maadui? Kwa nini isifike mahali Serikali ikaona sisi ni partners badala ya competitors wakati tunawasomesha Watanzania hao hao? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi peke yake ambayo shule zisizo za Serikali zinalipa kodi. Tumetembea nchi mbalimbali humu duniani, wanapata capitation grant kutoka kwenye Serikali zao, wanalipiwa walimu wao mishahara. Sisi tunafanya kila kitu wenyewe, tunakopa mikopo 24% interest kwenye mabenki, unanunua ardhi, unajenga shule, unalipa mishahara, unalisha watoto, unafanya kila kitu, leo tunaambiwa ada elekezi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hii ni sawa na kwamba mtoto wako mimba umebeba mwenyewe, mtoto umemlea mwenyewe, shule umempeleka mwenyewe, anayekuja kuoa anakupangia mahari. Sasa namna hii tutafika? Ikiwa tu bado tuna ukakasi na tuna mahitaji makubwa kwenye shule zetu za Serikali, tutakapoanza tena kuzitibua hizi zisizo za Serikali ambazo hata kwa kunukuu tu niseme, shule 50 bora mwaka jana katika kidato cha nne zilikuwa zimetoka kwa shule binafsi, yaani tunavuruga huku wakati hata huku bado hatujaweka sawasawa! Kwa kweli, hatutendewi haki. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mlolongo wa kodi. Ada elekezi si tatizo, lakini mimi nilikuwa ninaishauri Serikali ituondolee huu msururu wa kodi ili kwamba tuwasaidie hata watoto watokao kwenye mazingira magumu. Niseme tu ukweli, mimi shuleni kwangu nina watoto 67 yatima ninaowa-sponsor mwenyewe. Watoto hawa wametelekezwa, ni shule ipi ya Serikali ambayo inaangalia hawa watoto wa namna hii? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, wamiliki wa shule binafsi wanajitahidi sana kuchukua watoto hawa. Serikali iondoe hizi kodi ili tuweze kuwasaidia watoto wengi wa namna hii, tupunguze wingi wa watoto wa mitaani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunalipa kodi zifuatazo, inawezekana Wabunge hawafahamu ama wananchi huko nje hawajui; na hizi kodi unapozi-impose kwetu hakuna mwingine atakayezilipa ni mlaji ambaye ni mzazi. Iko hivi, tunalipa Land Rent, Property Tax, Business License, Sign Boards Levy, City Service Levy, Corporation Tax, SDL, Workers Compensation Fund, Work Residence Permit Fee, Fire, OSHA, taja yote tunalipa. Tunafanya biashara gani? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaisadia Serikali kusomesha Watanzania, kabla ya hapo watu walikuwa wanasomesha watoto Kenya na Uganda. Tumejitoa muhanga, wengine wamekufa kwa pressure kwa ajili ya kudaiwa na mabenki, wengine mna ushahidi hapa wameshindwa kulipa madeni ya benki mtu anakufa na pressure na wamiliki wengi wa shule wana-suffer na masuala ya pressure na sukari kwa sababu ya ugumu wa kuendesha hizi shule. Leo ni nani mwenye shule ambaye ana biashara nyingine pembeni ya uendeshaji wa shule? Kama ulikuwa unaendesha nursery school uta-up grade utafungua primary, bado ni elimu ileile! Utatoka primary utaanzisha secondary, utatoka secondary utaenda colleges! Yet tunawasomesha Watanzania hawa hawa, kwa nini Serikali isitupatie dawati pale Wizara ya Elimu, ili kwamba, na sisi tuweze kutoa maoni yetu pale? Ili kusaidia mitaala hii inayotungwa watu wakiwa wamejifungia vyumbani bila kupokea maoni ya wadau wengine?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ilifanyika semina ya walimu wa darasa la kwanza na la pili hapa Dodoma, hatukuelezwa watu wa shule binafsi kwamba, kuna semina ya namna hiyo na wakati kwenye shule zetu kuna wanafunzi wa namna hiyo. Tunatengwa, sisi tumebaki yatima, Serikali ituangalie sasa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme pia tukaambiwa tupake magari rangi ya njano, tunaongezewa gharama, gari moja ni shilingi milioni tatu mpaka tano, mwingine ana magari 50 ni shilingi ngapi hizo? Nani atazilipa kama sio mzazi wa Kitanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, basi tukubali, kama ni hiyo ada elekezi basi ije tujue kwamba ada elekezi imekuja, lakini hatulipishwi kodi za namna hii zinaumiza sana. Tuna madeni kwenye mabenki kwa ajili ya kujenga madarasa wanakosoma watoto wa Kitanzania, hata mtu akifa leo anaacha shule inaendelea kusomesha Watanzania, lakini wewe umekufa na pressure kwa ajili ya uendeshaji wa shule za namna hii. Tutaendelea hivi mpaka lini? Itafika mahali hawa wadau watafunga hizi shule zao basi turudishe watoto Kenya na Uganda kama ndicho tunachokitafuta. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano wa shule yenye watoto 350 ambao ada yake labda makusanyo kwa mwaka ni kama shilingi milioni 216, lakini shule kama hii inalipa kodi shilingi milioni 85, kwa faida ipi anayotengeneza mwenye shule? Weka tu chakula cha mtoto shilingi 10,000 hata kwa siku 90 anazokaa mtoto shuleni ni shilingi ngapi? Tunaumizwa. Ifike mahali sasa kilio chetu kisikilizwe. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nilikuwa nafikiri there is no fair play here. Wizara ya Elimu ama TAMISEMI ina shule zake, watu binafsi wana shule zao, lakini anayetu-monitor ni Wizara ya Elimu. Ni sawa na mchezaji wa simba awe referee wakati yanga na Simba wanacheza, hivi kweli hatapendelea timu yake? (Makofi)
MHE. ESTER A. MAHAWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na naunga mkono hoja.