Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Naomba niipongeze sana Wizara ya Afya. Kipekee kabisa nampongeza sana Mheshimiwa Waziri pamoja na Katibu Mkuu wake. Wao wanajua ni kwa nini nawapongeza. Bila jitihada zako Mheshimiwa Ummy ukishirikiana na mama wakati akiwa TAMISEMI, sisi watu wa vijijini huko Nzera tusingekuwe na Hospitali. Nataka nikuhakikishie kazi mliyoifanya ni kubwa sana na tutawakumbuka milele. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huwa nazungumza mara nyingi, hii Wizara wakati tunaanza Ubunge ilikuwa ni Wizara ambayo kila mtu anailalamikia, lakini leo Wizara hii ukisikiliza michango ya Wabunge, nadhani mwaka ujao tutakuwa tunaijadili siku moja tu mambo yanaisha tunapitisha bajeti. Hata kama kungekuwa na tuzo ya kutunzwa Mheshimiwa Waziri anayefanya vizuri, kiukweli bila upendeleo Mheshimiwa Ummy unastahili kuwa Waziri bora kabisa katika Bunge la 2018. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, alipopita kule kwetu aliahidi hospitali, umetupa. Jimbo zima watu laki 500,000 hatuna kituo cha afya. Kwa huruma yake alipandisha vituo viwili. Tusaidiwe pesa ili tuweze kupata kituo cha afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunajenga Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita. Hii hospitali imesimama toka mwezi wa Kwanza, certificate hawataki kulipa. Lipeni certificate tuweze kujenga hospitali yetu. Kuna tatizo gani? Tunategemea hiyo hospitali ndiyo iwe hospitali ya kutukomboa sisi watu wa Geita. Tuko zaidi milioni tano na kitu. Tusaidieni kulipa hiyo certificate ili waweze kuendelea kujenga hospitali yetu ya mkoa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, kwanza nimpongeze Mheshimiwa Waziri sana kiukweli, alipofanya ziara kwenye Hospitali ya Rufaa ya Bugando alitualika Wabunge wa Kanda ya Ziwa, nami nilikuwepo. Bahati nzuri Gwajima alikuwa bado Wizarani, naye alikuwepo. Niwapongeze sana. Katika miaka yote inaoneka kweli Serikali mmekuwa serious kutukomboa sisi watu wa Kanda ya Ziwa. Ninaona kabisa jitihada za Serikali kujiona ni sehemu ya ile Hospitali ya Kanda ya Ziwa ya Rufaa ya Bungando. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pale tukiwa na Mheshimiwa Waziri tulizungukia majengo, aliyaona majengo mazuri, lakini kule ndani hakuna MRI na wagonjwa wengi wanatoka Kanda ya Ziwa. Tunamwomba Mheshimiwa Waziri aweke mpango mkakati tununuliwe MRI, watu wetu wanakufa kwa kukosa gharama za kufuata MRI Dar es Salaam. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile tunaishukuru Serikali. Tunatibu wagonjwa wa saratani. Wagonjwa wa saratani Tanzania wanaongoza toka Kanda ya Ziwa. Tunaomba mlete wataalam wakae Mwanza. Mtu wa kuanzia Singida hana nauli ya kuja Dar es Salaam, atakuja Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia watujengee wodi, pamoja na kwamba vifaa vipo, lakini mtu anapotaka kufanyiwa operation, hakuna wodi ya kuwalaza wale watu. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri kwa ukaribu alionao, namkushukuru sana Mheshimiwa Waziri na ninamwomba sasa awe karibu na hiyo hospitali aweze kutusadia watu wa Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunashukuru, juzi nilitembelea nikaona; mlituahidi kutujengea jengo la TB kama la Kibong’oto na lenyewe limejengwa kwa shilingi milioni 120. Ni suala ambalo kweli tunaona Serikali mpo karibu na watu wa Kanda ya Ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia waliahidi kutoa matibabu ya bure kwa wagonjwa wenye saratani. Tunaona, tunatuma watu wetu wanasaidiwa masikini bure. Tunaiomba Serikali ingalie kwa jicho la huruma, ikamilishe vitendea kazi kwenye hospitali yetu ya Bugando. Hiyo ndiyo hospitali kombozi kwenye kanda ya ziwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Ummy anakumbuka, wakati tulikuwa tunaenda, hospitali ilikuwa inakusanya shilingi bilioni mbili. Leo inakusanya shilingi bilioni tisa. Na mimi napenda huyu mtu mngempongeza Wabunge wa Kanda ya Ziwa. Kutoka shilingi bilioni mbili hadi shilingi bilioni tisa na siyo matibabu ya kugombana, ni matibabu rafiki; leo watu hawaendi hospitali za mtaani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, zamani ilikuwa ukiambiwa unaenda Bugando unajihesabu unaenda kufa, lakini leo ukifika pale unatibiwa vizuri, unakaribishwa vizuri na watu wanatoa pesa zao bila wasiwasi. Watu kama hawa, Wakurugenzi akina Makubi wangekuwa wanaalikwa kwenye Mabunge kama haya tunawapa pongezi na wao wanajisikia ili waweze kwenda kuongeza morali.

MBUNGE FULANI: Yuko hapo.

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Yuko hapa, nashukuru sana Mheshimiwa Waziri. Leo ukienda Bugando, ni kweli kabisa, hata operation za mitaani zimepungua. Watu wanapewa motisha kule ndani, Bugando imekuwa nzuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, yangu ni hayo. Nakupongeza sana Mheshimiwa Ummy; ya Jimboni kwangu unikumbuke lakini na hospitali yetu ya Bugando hatuhitaji sana kuwafuata Madaktari Dar es Salaam, tunataka tutibiwe Mwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushuruku sana. (Makofi)