Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Labda nami niungane na wenzangu katika kutoa pole kwa Watanzania wote baada ya kuondokewa na mzee wetu, Reginald Mengi. Namkumbuka tu Tanga, baada kuanzishwa kwa ITV alituletea television kubwa sana pale katika uwanja wa Tangamano ikawa wananchi wa Tanga wanapitia taarifa na burudani mbalimbali kupitia katika television hiyo. Mwenyenzi Mungu amweke mahali panapostahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kwa kusema kwamba katika taarifa ya Kamati iliyotolewa, kuna upungufu ulielezwa kwamba Kamati ilivyotembelea miradi, miradi mingi ilikuwa haijapelekewa fedha za kutosha. Vile vile hata ukingalia katika bajeti, nayo inakuwa imetekelezwa kwa 16% badala ya 100% na 84% bado haikuweza kutimizwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile niwape pongezi Mheshimwia Waziri na Naibu wake wa kufanya kazi katika mazingira magumu. Pamoja na hivyo, naitaka Serikali nayo sasa iangalie kwamba Wizara ya Afya ndiyo kitengo au Wizara muhimu katika maisha binadamu, kwa sababu binadamu bila kuwa na afya bora hapawezi kukawa na uzalishaji mali, hapawezi pakawa na Jeshi ambalo lina ngumu kamili, lakini pia sekta mbalimbali zinaweza kufeli kama watumishi watakuwa hawana afya bora. Kwa hiyo, pamoja na mazingira magumu, lakini endeleeni kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba wakati mwingine lazima Serikali yetu nayo inapopanga bajeti, basi ihakikishe kwamba bajeti inapelekwa. Kuna jambo lingine gumu ambalo naliona katika bajeti zetu, mafungu makubwa ya fedha tunategemea katika fedha za wahisani. Wakati mwingine wahisani nao ama hawatuletei fedha kwa wakati ama wanatoa visingizo na matokeo yake fedha hizo zinakuwa haziji na matokeo yake mambo hayakamili.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, niende katika hotuba hii ya Kambi Rasmi ya Upinzani, kuna eneo limesema kwamba kwa mwaka wanakufa akina mama wajawazito 11,000,000, sawa na akina mama 30 kila siku kutokana na vifo vya uzazi. Kwa nchi kama Tanzania ambapo kuna Madaktari wasomi wakubwa, ina rasilimali nyingi; kushindwa kulishughulikia suala hili kwa kweli naona ni tatizo kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika akili za kawaida, kila siku kuna akina mama 30 wanapoteza maisha kutokana na vifo vinavyotokana na uzazi. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze, wana mkakati gani wa kupunguza vifo hifo hivi? Kwa sababu Watanzania 30 kupoteza maisha kutokana na vifo vya uzazi, hii idadi ya ni kubwa sana. Kwa mwaka watu 11,000,000. Hili siyo jambo dogo. Yakipangwa majeneza hapa 30 kwa siku au kwa mwaka kwamba ni watu 11,000,000 ni idadi kubwa sana. Naomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja atueleze wana mpango gani kuhakikisha jambo hili linakwisha? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine limezungumzwa hapa kwamba katika Mkoa wa Tabora kuna Wakunga wanaozalisha kwa kutumia mifuko ya rambo au mifuko ya plastiki. Serikali imeshapiga marufuku mifuko ya Rambo, sijui Wakunga huko Tabora watatumia vitu gani katika kuzalisha akina mama? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hilo halitoshi, kwenye ziara ya Mheshimiwa Rais alipokwenda Malawi, amepata taarifa moja ilinifariji, kwamba Malawi wameweza kuanza kutoa chanjo ya Malaria. Malawi ndiyo nchi ya kwanza Barani Afrika kuanza kutoa chanjo ya Malaria. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-wind-up naomba atueleze, nasi Tanzania tuna mpango gani wa kutoa chanjo ya Malaria ili nasi tuwe nchi ya pili Barani Afrika kwa kutoa chanjo ya Malaria? Tukumbuke kwamba kila dakika tano, Tanzania Malaria inaua Mtanzania mmoja. Sasa hili nalo naomba tuje tuelezwe, tuna mpango gani na sisi kuwa nchi ya pili kutoa chanjo ya Malaria?

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nirudi kwenye…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Kengele imeshagonga Mheshimiwa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante.