Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

Hon. Sonia Jumaa Magogo

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto

MHE. SONIA J. MAGOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii. Kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza watendaji wote wa Wizara hii kutokana na ugumu wa kazi yao, lakini pamoja na vile wanavyojitahidi kuendana na hizo changamoto.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali ilikuja na mpango mzuri sana wa huduma ya afya kwa wannachi na hii imekuwa ikiwasaidia sana wananchi wengi, hasa pale wanapopata matatizo mbalimbali ya afya. Hata hivyo, tumekuwa tukishuhudia mrundikano wa watu wengi kwenye madirisha zinapotolewa huduma hizi kwenye hospitali zetu, hivyo kusababisha wagonjwa kuchukua muda mrefu sana mpaka kuja kuhudumiwa. Naiomba Serikali iangalie utatuzi wa changamoto hii kwa kuongeza waajiriwa, hasa katika madirisha haya yanayotoa huduma hizi za afya kwenye hospitali zetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuongelea kuhusu watoto; tumekuwa tukizungumza sana kuhusu tatizo la lishe kwa watoto wetu na tumeona changamoto zinazojitokeza, hasa maeneo ya vijijini. Kwa upande wangu sioni kama changamoto hapa ni ukosefu wa chakula, kwa mfano, kama tunavyoongelea huko vijijini ambako ndiyo kuna vyakula vingi vinapatikana na vingi ni natural kabisa, lakini bado watoto wengi wa maeneo hayo wanapata utapiamlo na udumavu. Hivyo hapa naona tatizo ni elimu kwa hii jamii na hivyo Serikali iangalie uwezekano wa kuwapa elimu hawa wananchi hasa wa vijijini ni jinsi gani wanaweza kuwasaidia watoto wao wakapata lishe bora na kuondokana na haya matatizo ya udumavu na utapiamlo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile jamii ingefundishwa kuhusu sheria mbalimbali ambazo zinasaidia kumlinda na kumtetea mtoto anapokutana na changamoto mbalimbali huko katika jamii. Changamoto nyingi zimekuwa zikijitokeza, lakini unakuta mzazi hajui aanzie wapi, inasababisha mtoto anakosa haki yake na kuishia kuishi kwenye janga la umaskini ama kuishia kwenye matatizo ambayo baadaye yanakuwa ni changamoto kubwa sana kwake. Hivyo niiombe Serikali iendelee kutoa elimu kwa jamii kuwasaidia hawa watoto na kuwalinda ili tuweze kujenga kizazi bora cha kesho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tatizo lingine nililoliona ni katika tafiti na elimu mbalimbali. Kwenye jamii yetu sasa hivi kuna matatizo mbalimbali ya kiafya, mathalani, tunaona watu wengi hata kushika mimba limekuwa ni tatizo; pia kuna tatizo lingine la kutoka mimba kabla ya wakati; kuna tatizo la mimba kutunga nje ya kizazi; kuna vifo vya watoto wachanga; na kuna tatizo la nguvu za kiume. Haya matatizo yamekuwa ni mengi sana katika jamii na hivyo napenda kuishauri Serikali ifanye tafiti mbalimbali na kuja na majibu ambayo yataisaidia jamii yetu kuondokana na haya matatizo ambayo yamekuwa ni changamoto kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe pia Wizara iangalie hospitali zetu. Hospitali nyingi zinakuwa hazina vifaa vya kutosha, mathalani ni Kituo cha Afya cha Mombo. Kile kituo cha afya kipo katika njiapanda na kinahudumia watu wengi sana, lakini kituo kile hakina x ray, hakina ultra sound, hakina hata jenereta. Hivyo niwaombe watusaidie kwa sababu ni sehemu kubwa sana ya wananchi wanaohudumiwa na kituo kile, lakini kutokana na changamoto hizi wanashindwa kutekeleza kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. (Makofi)