Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Eng. Ramo Matala Makani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tunduru Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nakushukuru kwa fursa hii. Kwa muda wa dakika tano nachoweza kusema ni haya yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza, pongezi kwa ujumla kwa Serikali lakini mahsusi kabisa kwa Wizara ambayo hoja yake iko mezani, Mheshimiwa Profesa Mbarawa na timu yake nzima, Mheshimiwa Jumaa Aweso, Profesa Kitila Mkumbo - Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu – Eng. Kalobelo, Wakurugenzi wote pamoja na wataalam kwa ujumla pamoja na wafanyakazi wengine wa kada saidizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nashukuru Serikali kwa sababu katika Jimbo la Tunduru na Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru kwa ujumla tulipata fedha kwenye bajeti hii jumla ya shilingi bilioni1.27; shilingi milioni 300 mjini na milioni 974 vijijini. Siwezi kutumia muda mrefu sana kurudia kusema kwamba fedha hizi hazitoshi lakini ieleweke tu kama ujumbe kwa Wizara kwamba hasa kwa mradi wa mjini ambao unahitaji fedha karibu shilingi bilioni 16, bajeti ya shilingi milioni 300 kwa mwaka maana yake mradi huu utachukua karibu miaka zaidi ya 50. Kwa hiyo, tutafutiwe fedha kwa kutoka vyanzo vingine na kwa style nyingine tuweze kukamilisha mradi wa Tunduru Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mji wa Tunduru uko mahali pa kimkakati hata kitaifa. Ni mji ambao uko katikati ya umbali wa kutoka Bandari ya Mtwara mpaka Bandari ya Mbambabay. Pia kule tuna zoezi maalum la kimkakati Kitaifa la Mtwara Corridor, maendeleo ya kitaifa yatakavyoweza kuchangiwa na maendeleo ya Kusini kupitia Miradi ya Ukanda wa Kusini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hotuba ya Mheshimiwa Waziri yenyewe ilishamaliza mjadala hapa Bungeni na hasa pale ilipokuwa inazungumzia changamoto. Imetaja changamoto tano lakini kila changamoto Wizara imetoa mapendekezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya kwanza upungufu wa fedha kwa ujumla katika kutekeleza miradi ya maji nchini. Wao wamesema Serikali inaendelea kutafuta fedha na mimi narudia Serikali iendelee kujipanga kutafuta fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi yote muhimu kwa ajili ya kuwapatia wananchi huduma hii ya maji ambayo ni muhimu na kila Mbunge akisimama anaeleza namna gani mahitaji ya maji ni muhimu kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ya pili muhimu kabisa kupita hata hiyo ya kutafuta fedha, wamesema hivi na hii nitaisoma kabisa, 5.2, ukurasa wa 108, anasema: “Uwezo mdogo katika utekelezaji, usimamizi na uendeshaji wa miradi ya maji”. Kitaalam hii wanaita low absorption capacity, uwezo mdogo wa kutumia fedha ulizonazo kwa tija na kutumia fedha kwa tija maana yake utekeleze mradi ufanikiwe. Mafanikio ya mradi yanatafsiriwa kitaalam kwamba ujenge mradi kwa wakati, uwe na ubora, kwa gharama zile ambazo zimekadiriwa na uwe endelevu (sustainability) utakaozingatia mazingira lakini pia uhakikishe wale walengwa (stakeholders) wanapata yale matarajio yao, ndiyo maana ya mradi uliofanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miradi ya maji ukisikiliza michango ya Wabunge wote haikidhi haya niliyoyaeleza, mambo karibu matano. Sababu kubwa ni nini? Sababu kubwa ipo muda hautoshi ningeweza kuieleza iko kwenye utaalam.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Engineer Makani.

MHE. ENG. RAMO M. MAKANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naunga mkono hoja. (Makofi)

Whoops, looks like something went wrong.