Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. MAULID S.A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kunijalia uzima na mimi kupata fursa ya kuchangia katika Wizara hii muhimu sana. Pili, nikushukuru wewe Mwenyekiti wetu. Tatu, niwashukuru Watendaji wote Wizara ya Maji nikianza na Waziri, Naibu wake na Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yetu ya Maji ni nyeti sana kama Wabunge wengi walivyosema lakini vilevile tujikumbushe Wizara hii katika Awamu hii ya Tano tu wamepita Mawaziri wengi na wamefanya kazi kubwa. Ameanza Mzee wetu Mheshimiwa Maghembe, Mheshimiwa Eng. Lwenge, Mheshimiwa Eng. Kamwelwe na sasa tunaye Mheshimiwa Profesa Mbarawa. Kwa kweli wote wamefanya kazi nzuri lakini sasa hapa kwa Profesa kwa kweli mambo yanakwenda kweli kweli. Wakati mwingine Profesa unamkuta ananing’inia kwenye ngazi unapata raha kabisa, mzigo unapigwa kweli kweli. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati mwingine matatizo yetu yanaonekana kwa sababu ya uzito wa jambo lenyewe na umuhimu katika jamii yetu. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wenzangu tuwaunge mkono wenzetu hawa kuhakikisha kwamba tunawapa nguvu, tunawatia moyo hili jambo liende.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kwangu Kinondoni maji tunapata, yako mengi na ukichukua Mradi wa Ruvu Chini na Ruvu Juu hatuna shida sana ya maji, shida yetu ni mtandao wa maji tena kwa baadhi ya kata. Niiombe Wizara ishirikiane na watu wetu wa Dar es Salaam kwa ajili ya Kata zetu za Tandale, Mwananyamala, Makumbusho, Kigogo, Hananasifu na Mzimuni. Hizi ndiyo kata ambazo tunaamini mtandao wa maji ukiwekwa itakuwa ni vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nishukuru tu kwamba bajeti ya mwaka huu inakwenda nzuri na itatekelezeka. Kama nilivyosema pesa zimesainiwa lakini zile shilingi trilioni 1.2 ambazo hata kaka yangu Mheshimiwa Mnyika amezisema asiwe na wasiwasi mwaka huu ndiyo mwaka wa mavuno, mihela itakuwa inashuka kwenye Wizara ya Maji kwa maana shilingi bilioni 330 ipo, shilingi trilioni 1.2 zipo, wasimamizi wapo, RUWASA inakwenda kuanzishwa mwezi Julai, tuhakikishe mapanya wote wanaokula pesa za maji wanakwenda kudhibitiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nafikiri ni wakati wetu sasa, hakuna wakati mzuri ambao tunatakiwa tuungane, tushikamane kuwasaidia wenzetu hawa kwa sababu wameonyesha dhamira ya kweli.Waheshimiwa Wabunge mtakuwa mashahidi kila Mbunge ametembelewa na Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri au na Katibu Mkuu au na kiongozi yoyote. Hili jambo kwa kweli siyo dogo, ni jambo ambalo sisi kama viongozi na wawakilishi wa wananchi lazima tuwape moyo; mnyonge, mnyongeni, haki yake mpeni.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana, unga mkono hoja.

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)