Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Aysharose Ndogholi Mattembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. AISHAROSE N. MATEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hotuba hii muhimu ya maji kwa maendeleo ya Watanzania. Nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na kuniwezesha kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie nafasi hii kuipongeza sana Serikali ya chama changu kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kuwaletea Watanzania maendeleo. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais, amekuwa na ziara ndefu akihamasisha maendeleo, hakika tunamwombea heri, baraka na nguvu katika kuwatumikia Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri wa Maji Profesa Mbarawa, Naibu wake Mheshimiwa Aweso, Katibu Mkuu, Kitilya Mkumbo, pamoja na watendaji wote kwa hotuba nzuri, hotuba ambayo inatoa mwelekeo wa kumtua ndoo mwanamke kichwani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji ndiyo kila kitu. Maji ni uhai, maji ni maendeleo, maji ni uchumi, lakini maji haya yamekuwa yakileta madhara makubwa, mfarakano na kusababisha ndoa nyingi kuvunjika na kuwafanya wanawake wengi kutokushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wangu wa Singida unakabiliwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji safi na salama, hususan maeneo ya vijijini na hii ni kutokana na jiografia yake. Jambo kubwa la kusikitisha ni kwamba, hata miradi mikubwa inayopangwa kutekelezwa katika Mkoa wa Singida imekuwa ikisuasua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano, Mradi wa Maji Kitinku, Lusilile katika Wilaya ya Manyoni, uliibiliwa chini ya mpango wa Matokeo Makubwa Sasa na ulianza kutekelezwa mwaka 2013, lakini hadi leo ni miaka sita mradi huu haujakamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana Waziri atakapokuja kufanya majumuisho atuambie, ni lini fedha za kutosha zitapelekwa kwa wananchi wa Manyoni ambao wanausubiri mradi huu kwa hamu kubwa na ni vijiji kumi vitakavyonufaika. Vijiji hivi ni Kintinku, Lusilile, Maweni, Chikuyu, pamoja na vijiji vingine ambavyo vipo karibu katika maeneo haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishukuru Serikali kwa kutupa miradi mikubwa miwili ya maji ya mtandao wa bomba katika Jimbo la Ikungi Magharibi. Miradi hii ni ya Ighuka na Mtunduru, lakini niombe sana, sana Serikali ipeleke fedha za kutosha ili miradi hii iweze kukamilika kwa wakati kwa sababu wananchi wa Jimbo la Ikungi Magharibi wanapata tabu sana ya ukosefu wa maji safi na salama. Pia naishukuru Serikali kwa kutupa vibali vya kuchimba visiwa 20 kwenye Jimbo la Ikungi Magharibi pamoja na Ikungi Mashariki. Naomba vibali hivi viende sambamba na kutupa fedha za kutosha ili wananchi waondokane na adha ya ukosefu wa maji safi na salama.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa maji katika Mkoa wangu wa Singida hususan maeneo ya vijijini bado ni duni sana na vijiji vingi bado havina huduma ya maji safi na salama. Mfano Jimbo la Singida Kaskazini Vijiji vya Mitula, Migugu, Ughandi B, Misinko, Mwighanji havina kabisa mtandao wa maji, maji wanayotumia ni maji ya malambo na unapofika wakati wa kiangazi, maji haya yanakauka na wananchi wanapata tabu kubwa sana ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji haya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ningependa kuchangia ni ukosefu mkubwa wa vitendea kazi yakiwemo magari, pamoja na watumishi wa Idara za Maji. Naishauri Serikali iangalie jambo hili kwa jicho la tatu; Wilaya zangu zote za Singida ikiwepo Mkalama, Manyoni, Ikungi, Iramba na Singida Vijijini wapate watumishi pamoja na magari na vitendea kazi vya kutosha. Naipongeza na kuishukuru Serikali kwa kutupa Mamlaka za Maji katika Miji Midogo ya Ikungi, Mkalama na Itigi. Tayari Bodi zimeshaundwa na mapendekezo yameshapelekwa Wizarani. Naiomba Serikali basi iharakishe upatikanaji wa bibali hivi, naamini kwamba Mamlaka hizi za Maji zitaweza kusaidia sana upatikanaji wa maji katika maeneo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, liko suala lingine ambalo ningependa kulichangia; kuna changamoto kubwa sana ya ukosefu wa maji katika Taasisi za Elimu na Afya. Watoto wetu wa shule wamekuwa wakitumia muda mrefu sana kuhangaika kutafuta maji na unategemea jambo gani la ufaulu iwapo watoto hao wanatumia muda mwingi kutafuta maji. Pia watoto wanapofika siku za hedhi, watoto wa kike wanataabika sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kubwa la kusikitisha ni kwamba wanawake wajawazito wanapokwenda kujifungua wanaambiwa waende na maji ni kwa sababu kwamba Taasisi hizi za Afya zinakuwa hazina miundombinu ya maji. Niombe sana pia Serikali iangalie jambo hili kwa jicho la tatu, iweke miundombinu katika shule zetu pamoja na Taasisi za Afya ili kuweza kuwapatia wananchi huduma ya maji katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii na nakushuru kwa muda ulionipatia. (Makofi)