Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Charles Muhangwa Kitwanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Misungwi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. CHARLES M. KITWANGA: Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniweka hai. Kwa sababu leo ndiyo nasimama kwa mara ya kwanza kuzungumza Bungeni hapa baada ya kupata matatizo ya kuugua, naomba nitoe shukrani zangu za dhati kabisa kwa Wanamisungwi ambao waliacha kufanya kazi zao wakaamua kuwaomba Mapadre na Wachungaji kwa siku mbalimbali kuweza kuniombea niweze kupona. Siyo Wanamisungwi tu, nimshukuru sana Mheshimwa Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu kwa support na kwa jinsi walivyoweza kufika kuniona wakati nikiwa naumwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mheshimiwa Karume aliyefika kuniona. Namshukuru sana Makamu wa Rais wa Zanzibar, wao wanamuita Makamu wa Pili, mimi sitambui hilo kwa sababu hakuna wa kwanza, kuna Makamu wa Rais tu Zanzibar. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana wewe pamoja na Bunge lako Tukufu kwa kuniombea. Wewe mwenyewe ulifika zaidi ya mara moja kuja kuniona, nakushukuru sana pamoja na timu yako. Nawashukuru sana Wabunge wote kwa jinsi ambavyo mlifika na mliniombea na leo hii nazungumza nikiwa najidai. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwashukuru sana Watanzania wote kwa sala na maombi yao. Jamani niseme hivi, kabla hujafa hujaumbika na hapa ulipo kwa sababu unatembea mshukuru Mwenyezi Mungu na utumie dini yako uendelee kumuomba. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya shukrani hizo, niseme tu kwamba ni watu wengi sana walifika kuniona na kunitakia kheri, siwezi kuwataja wote lakini kwa sababu ya muda mfupi na nadhani huu hutauweka kwenye zile dakika zangu kumi. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, nianze kwanza kujikita kwenye hoja, leo sitaondoka hapa kwenda Ihelele kuwashawishi wananchi wa Misungwi kwenda kufunga ule mtambo unaotoa maji sehemu mbalimbali kwa sababu leo nitatoa shukrani kwamba ombi langu lilisikilizwa na wananchi wa pale Ihelele ambapo mradi mkubwa wa maji unatoka, sasa hivi kuna mradi lakini nitazungumzia matatizo yanayojitokeza. Hilo litakuwa zaidi katika kutoa ushauri wangu kwa Serikali yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tatizo kubwa katika miradi hii ni muundo. Ukiangalia muundo wa namna miradi inavyoendeshwa ni finance based, pesa zikipatikana wanaanza kusema tutapeleka kijiji hiki, wilaya hii na wilaya hii, kitu ambacho kinasababisha sasa utekelezaji wa muda mrefu unakuwa tatizo. Nitatoa mfano mdogo tu katika Mkoa wa Mwanza na particularly katika Wilaya yangu ya Misungwi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna miradi mingi ambayo utakuta meneja wa mradi, engineer wa mradi na vitu kama hivyo, yote haya yapo katika utawala wakati ambapo miradi hii ingekuwa consolidated halafu kukawa na individuals ambao wanasimamia miradi in particular, mambo ya Afisa Utumishi na Meneja wa Mradi yote yasingekuwepo. Kungekuwa na Meneja wa Mradi ambaye ni mkubwa kiwilaya au kimkoa lakini waone namna ambavyo kutakuwa na muundo mzuri.

Mheshimiwa Spika, nichukulie mfano wa Mkoa wa Mwanza. Kuna mradi wa Ukerewe, kuna mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Kwimba kupitia kwa ndugu yangu Mheshimiwa Ndassa na kuna mradi wa maji wa Misungwi; Misungwi tuna miradi minne na kila mradi una meneja, hii yote ni gharama matokeo yake sasa wakishaondoka pale uendeshaji unakuwa ni tatizo.

Mheshimiwa Spika, nichukulie mfano pale Wilayani Misungwi kuna mashine nzuri sana zinazopeleka maji Ukiliguru lakini customer base ya Ukiliguru ni watu wachache. Waki- pump maji kwa wiki mbili, bili ya umeme kwa mwezi inakuja shilingi milioni 10, shilingi milioni 10 zitalipwa na watu 200 wanaokaa Ukiliguru?

Mheshimiwa Spika, halafu siyo tu hapo katika Wilaya yangu, kuna mradi sasa wa Wilaya unaotoa maji Nyahiti kupeleka Misungwi, huo nao ni mradi. Kuna mradi huu ambao sasa hivi unaitwa mradi wa kupiga kelele Kitwanga Bungeni unaotoa maji Ihelele kuja Mbalika mpaka kufika Misasi, huo nao ni mradi unajitegemea. Sasa hivi mradi huo una matatizo, baadhi ya wakandarasi hawajalipwa na naomba tukishatoka hapa tuweze kuzungumza na wenzangu wa Wizara waweze kuniambia wamefikia wapi kuwalipa wakandarasi. Mheshimiwa Waziri nakushukuru ulifika katika Wilaya yetu ukaweza kuahidi kwamba pesa zitatolewa lakini mpaka sasa hivi hazijafika.

Mheshimiwa Spika, ushauri wangu, tujaribu kuona katika Wilaya tuweke mfumo unaoeleweka, mfumo wa Dar es Salaam na maeneo yanayoizunguka ulivyowekwa, huo ndio the best. Sijui ni DAWASA sijui nini ile ya Dar es Salaam inahudumia Dar es Salaam, Bagamoyo na sehemu kubwa zinazoeleweka na kuna mpangilio. Je, kuna tatizo gani kwa Mkoa wa Mwanza kuwa na institution moja na hizi zingine zilizopo kwenye Wilaya zikawa subsidiary za institution hiyo? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamsifia sana Mheshimiwa Eng. Sanga kwa Mkoa wetu wa Mwanza kweli anafanya kazi sana. Ukienda pale Misungwi ukiuliza hamna jibu, ukienda Ukiliguru hamna jibu, unakwenda kwa Sanga ndiyo anaanza kukuelezea, aah, mimi pale sina mamlaka jaribu kumuomba Waziri kama naweza kupewa nguvu, kwa nini asiwe na nguvu siku zote? Kwa sababu kama tungekuwa na institution moja kwa Mkoa wa Mwanza zile za Misungwi, Sengerema na Ukerewe zikawa subsidiary ya hiyo MWAUWASA tungeweza kuwa na sehemu moja inayosimamia miradi yote na hii mipangilio yote ingekuwa mizuri zaidi. Sasa nyie mkipata pesa mnaanzisha mradi na unakuwa unajitegemea, mkishaondoka kwenye mradi hamna mwendeshaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa imefikia mpaka kwenye kata, Kata ya Fera wana mashine pale wana-pump maji lakini customer base ya Kata ya Fera ni wanakijiji. Sasa wanakijiji wataweza kweli kulipia bili ya umeme waweze ku-pump maji kila siku? Mimi nadhani hapa kidogo tuna tatizo, miradi hii isiwe finance based, iwe na organization zinazojitegemea na pesa zinazofika mnasema kwamba leo hii tunaweka pesa eneo hili na inasimamiwa vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. CHARLES M. KITWANGA: Muda umeisha?

SPIKA: Ndiyo, umeisha.

MHE. CHARLES M. KITWANGA: Eeeh, naunga mkono hoja. (Makofi/Kicheko)