Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

Hon. Lucy Simon Magereli

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Maji na Umwagiliaji

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kupata nafasi hii kuchangia hoja ya Wizara ya Maji, lakini kabla sijaendelea nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa ajili ya uzima na uhai na kuwezesha kuwepo ndani ya Bunge hili leo kutekeleza majukumu yetu.

Mheshimiwa Spika, neno “Maji” lina herufi nne tu; (M), (A), (J), (I) lakini nadhani ndiyo Msamiati mgumu sana ndani ya Bunge hili tangu nimeingia mwaka 2015 mwishoni ndilo jambo ambalo limekuwa likileta mjadala mkubwa, mgumu na ambao hauna majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasikitika kueleza masikitiko yangu kwamba suala la maji tufike mahali labda Serikali iseme imeshindwa halafu tuwape private sector huenda tukapata jibu.

Mheshimiwa Spika, Serikali haina vipambele. Tunatekeleza miradi mingi, mikubwa kwa wakati mmoja wakati tunafahamu ya kwamba resources zetu ziko so limited, tunatekeleza miradi midogo midogo mingi sana wakati tunafahamu kabisa kwamba resources zetu ziko limited badala yake tumekuwa na vipande vingi sana vya miradi ya maji ambavyo havikamiliki, havitoi matokeo, visima vinachimbwa haina maji, pamekuwa na Misamiati tu mizuri ya usanifu wa kina, sijui Bodi, hakuna jibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 148 nimeona ametaja suala la mradi wa fedha za India ule wa Miji 29, tunashukuru. Bajeti iliyopita mradi huu ulizungumzwa na kiasi hiki cha fedha kilitajwa na kwamba kingeanza kufanya kazi tangu Bajeti ya 2018/2019.

Mheshimiwa Spika, ni kwa bahati mbaya sana kwamba mpaka sasa bado fedha hizo hazijaanza kufanyakazi katika miradi ya hiyo Miji 29 iliyotajwa. Lakini naamini bado nia na dhamira ipo kwa sababu ni fedha za mkopo ambazo tutakwenda kuzilipa kwa kodi zetu. Niwasihi Serikali katika utekelezaji wa mradi huu wa Miji 29, naamini walifanya utafiti wa kina kabla ya kuamua ya kwamba ni Mji gani na Mji gani fedha hizi zielekezwe. Basi uwiano wa ugawanyaji wa fedha hizo upelekwe kwa utaratibu kadri ya utafiti ili hatimaye basi angalau kwa mara ya kwanza tupate Miji 29 ambayo inasema sisi sasa hatuna tatizo la maji, limekwisha ili watu wengine wafikiriwe baada ya kuwa mradi huu umekwishakukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mradi huu wa Miji 29 nashukuru nimeuona Mji wa Mugumu nao umetajwa kwa Mama yangu. Umetengwa shilingi milioni 200 kwa ajili ya kutibu maji katika Bwawa la Manchira. Bwawa la Manchira Mheshimiwa Waziri ni changamoto ya muda mrefu, nimezaliwa pale nimelikuta, nalisikia watoto wanaishai kuogela tu lakini hatimaye miaka mitatu, minne nyuma likaanza kufanyakazi lakini halina ufanisi.

Mheshimiwa Spika, maji yanayotoka pale yanafanana na ile aina ya Togwa tunayokunywa inayoitwa Obhosara. Huwezi kufananisha ya kwamba haya ni maji au hii no Togwa. Kwa hiyo nikushukuru na nitajisikia vizuri ikiwa hizi milioni 200 zitapelekwa na utaratibu wa kutibu maji yale ukafanyika.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la mradi wa maji wa Kimbiji na Mpera; suala hili nimelifuatilia kwa karibu sana kwa kipindi kirefu, nimezungumza na Waziri, nashukuru amekuwa akinipa mrejesho kila nilipofika kuzungumza naye. Leo sikupanga kulizungumzia lakini nilipokwenda kwenye hotuba ya Waziri nikakuta ametaja ya kwamba pale Kimbiji kwenye visima 20, tayari wamekamilisha visima 19 kwenye ukurasa wa 80, hili linanifanya niongee.

Mheshimiwa Spika, katika mradi wa Kimbiji na Mpera, visima vilivyokamilika ni tisa tu. Waziri anaposema kumekamilika visima 19 kwenye hotuba yake anamaanisha kutoa Ujumbe gani? Bajeti ya 2016/2017 tulijadili suala hili, 2017/2018, 2018/2019 na leo ni 2019/2020 bado hoja ya visima vya Kimbiji na Mpera iko kwneye hotuba ya Waziri. Mradi huu umekuwa ukitengewa fedha lakini ufanisi wake umekuwa mdogo na umekwenda pole pole sana sijafahamu ambacho kimetokea.

Mheshimiwa Spika, kwa sababu nakumbuka Mwaka 2017 wakati huo Waziri wa Maji akiwa Mheshimiwa Eng. Lwenge alikuja mpaka pale kwenye mradi wetu wa Kimbiji na deadline ya mradi huu mkataba ulikuwa unakwisa Oktoba, 2017. Mradi haukwisha wakapewa extension mpaka Disemba na wakaambiwa baada ya hapo watalipa penalty za kuchelewesha mradi lakini ninapozungumza mpaka Disemba, 2017 ule mradi haukwisha leo tunazungumza ni Mei, 2019 bado mradi wa maji wa Kimbiji na Mpera haujatupa hata kilometa moja ya mtandao wa maji. (Makofi)

Mhshimiwa Spika, mwaka jana niliuliza swali hili hili wakati huo ni Mheshimiwa Eng. Kamwele nadhani ndiyo alikuwa Waziri. Na yeye alijibu ya kwamba tayari utaratibu wa distribution unaanza lakini bado hata distribution yenyewe haijaanza na kwa maelezo ya Waziri anasema ndiyo kwanza wametangaza tenda za ujenzi wa Matenki kwa ajili ya kuanza distribution. Kwa hiyo mradi huu umemeza fedha nyingi, umechukua muda mrefu kama ilivyo miradi mingine mingi nchi hii ambayo unajikuta kwamba mkataba umetajwa miezi 36, miezi 48 lakini mikata mingi inakwenda ina-extend mpaka miezi 60 mpka 90.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la gharama za juu za uchimbaji wa visima; sijafahamu serikali ina mpango gani baada sasa ya kusuasua kwa uwezo wake wa kuwapatia wananchi maji kuwezesha watu binafsi wanaotaka kuchimba viisma vyao kwa maana ya ku-subsidies aidha ile mitambo au hao watoa huduma wapewe aina fulani ya leave kusaidia kushusha gharama za uchimbaji visima ili watu binafsi nao ambao hawawezi kufikiwa na hii huduma ya Serikali waweze kujipatia huduma za maji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfano halisi ni Mji wa Kigamboni; Mji wa Kigamboni tangu ulipoumbwa haujawahi kuapata mtandao hata wa mita 600 za maji kwa maana ya maji ya Serikali maji ya DUWASA ama nyingine yoyote. Tumeishi miaka yote tukichimba visima wenyewe virefu na vifupi lakini kwenye mkakati ambao niliusikia kwenye ile Sheria ya usimamizi wa rasilimali za maji namba 11 ya Mwaka 2009 ambayo tulikuwa tumeomba irudishwe Bungeni kwa ajili ya mapitio kwa sababu ina mkanganyiko wa kiutekelezaji ndipo ambapo kuna ile hoja iliyoletwa ya kwamba tutatakiwa kuja kilipia gharama za kumiliki visima binafsi ikiwa tumefanya initiatives ya sisi wenyewe kuchimba vile visima.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo Mheshimiwa Waziri naomba sana mnapokuja kutekeleza suala hili, Mji wa Kigamboni muuangalie kwa sura ya peke yake. Mwenye kisima chake kama mtataka kuanza kum-charge tozo yoyote ya kulipia basi uanze leo usim-charge gharama za nyuma kwa sababau ndiye aliyefanya ubunifu wa kuhakikisha kwamba anajipatia huduma ya maji ambayo Serikali haikuweza kumpa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la ucheleweshwaji wa kukamilika kwa miradi ya maji; ni kwa bahari mbaya sana miradi mingi imekuwa na extensions za utekelezaji wa mikataba kwa hiyo hata thamani za miradi zinakuwa zinabadilika badilika kila mara wakati ambapo fedha za Wananchi zinaendelea kutumika kwa wingi na matokeo hayaonekani.

Mheshimiwa Spika, kuna suala la usanifu unafanyika kabla ya kupata fedha; miradi mingi ya maji imekuwa ikifanyiwa usanifu sijui na upembuzi n.k wakati Serikali bado haina fedha. Kwa hiyo jukumu lile la usanifu linakamilika halafu Serikali haina fedha, badala yake inapofika ule muda sasa kwamba Serikali imepata fedha, ule mradi unakuwa hauna thamani ile ile na kwa jinsi hiyo kukuta kama miradi inakuwa inafanyiwa mipango ambayo inashindwa kutekelezeka kwa utaratibu ambao unakubalika kwa sababu ya kuwa muda umekwishakupita. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la Taasisi za Serikali ambazo hazilipi ankara za maji. Sifahamu tatafanya nini, kwa sababu kama Serikali kama Wizara ya Maji inasimama leo Bungeni inalalamika katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri kwamba kuna taasisi za Serikali; siyo kuna, mimi nahisi taasisi za Serikali zote hazilipi ankara za maji. Kama ndivyo, je, kuna haja ya kuleta hoja Bungeni ya kwamba taasisi hizi zifutiwe kabisa basi utaratibu wa kulipa ankara za maji ili tujue kwamba sio wadeni, hata tunapopanga bajeti zetu, tusifikirie zile fedha za ankara zinazotokana na Taasisi za Serikali?

Mheshimiwa Spika, naomba kwa utaratibu maalum, kama Serikali ingeweza kuangalia shule zetu, wakahakikisha shule zote zinapatiwa huduma ya maji, ingekuwa vizuri. Kwa sababu fikiria watoto wa kike wanapotumia vyoo vya kawaida vya shimo katika mazingira ambayo hakuna maji wala hakuna toilet paper, suala la hygiene yao limebaki kuwa kitendawili. Labda hawa wangeweza kupewa maji na wakawa exempted, tungeweza kuliunga mkono vizuri suala hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala la mabwawa ya kimkakati. Nasikitika kuona kwamba Bwawa la Kidunda Morogoro limetajwa tena leo na likiitwa bwawa la kimkakati. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Mheshimiwa Magereli, muda hauko upande wako.

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, one minutes. Dakika moja ya kwako Mheshimiwa.

SPIKA: Unga mkono hoja. (Kicheko)

MHE. LUCY S. MAGERELI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa muda huu. Mungu akubariki. (Makofi)