Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Salma Rashid Kikwete

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Kabla ya kuanza, naomba niunge mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mungu kwa kunipa hiki kibali cha kuweza kusimama kwenye Bunge lako Tukufu ili niweze kuchangia na kutoa ushauri kwenye Wizara hii muhimu sana ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo ndiyo mhimili wa Taifa letu kwani elimu ndiyo uti wa mgongo wa Taifa letu la Tanzania. Sio Tanzania tu bali nchi yoyote duniani bila elimu hakuna kitu chochote ambacho kinaweza kikafanikiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, nitoe pongeze sana kwa Mheshimiwa Profesa Ndalichako kwa kazi nzuri, pamoja na Naibu Waziri na Katibu Mkuu na viongozi wote katika Wizara hiyo kwa kazi kubwa na nzuri ambazo wanazifanya katika kusukuma gurudumu hili la elimu katika Nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe pongezi zangu za dhati kabisa kwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, kwa kazi kubwa na nzuri ambayo anaifanya ya kuendeleza elimu na hasa ile elimu bure. Elimu bure kwa kweli tumeweza kuona matokeo yake na matokeo yake ni pamoja na kuongezeka wanafunzi wengi sana kwenye shule zetu za msingi, hii ni kwa sababu ya elimu bure ambayo inatolewa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na hilo, kila mwezi zaidi ya bilioni 23 na ushehe zinatolewa kwa ajili ya kuboresha hii elimu. Mheshimiwa Rais tunampongeza sana kwa kusimamia Ilani ya Chama chetu, Chama cha Mapinduzi, chama tawala kwa kazi kubwa anayoifanya. Endelea kufanya hivi Mheshimiwa Rais, sisi tuko nyuma yako kukuunga mkono kwa Tanzania inayowezekana, kwa Tanzania mpya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri alipotoa taarifa yako tumeona kuna dira, kuna dhima na kuna majukumu. Dira ya Wizara ni kuwa na Mtanzania aliyeelimika na mwenye maarifa pamoja na stadi, lakini sambamba na hilo kuna dhima; kuinua ubora wa elimu pamoja na mafunzo. Sambamba na hilo kuna majukumu; majukumu yapo jukumu la kwanza mpaka jukumu la 13, lakini la kwanza ni kutunga na kutekeleza sera, utafiti na huduma za maktaba na mambo mengine mbalimbali. Kwa kweli dira, dhima na majukumu ya Wizara yanaendana hasa na uboreshaji wa elimu hii tunayoitaka na tunayoitarajia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa pamoja na kuwa na dira, dhima na majukumu, nataka niende kwenye eneo la Walimu wa Sayansi. Kupanga ni kuchagua, tunataka tuboreshe elimu, hatuwezi kuboresha elimu kama hatutakuwa na Walimu wa kutosha hasa Walimu wa Sayansi. Nini tunachotakiwa tufanye kwenye eneo hili; kila kitu ni maandalizi, tuliandaa Ilani ya Chama chetu cha Mapinduzi tukasema kwamba ifikapo mwaka 2015/2020 tunataka tununue ndege; tumenunua, tunataka tujenge reli ya kisasa; tumejenga, tunataka tuwe na vitu ambavyo vitaonekana kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa nini nimesema haya; kwenye hili maana yangu ni kwamba watoto wanaanza kwenye ngazi ya awali, shule za msingi, sekondari hatimaye wanakwenda kwenye elimu ya juu; naomba tuwaandae watoto hawa tangu shule za msingi, tuwaangalie kwamba watoto hawa wanataka wawe akina nani. Hili jukumu ni letu sisi kama wazazi, vilevile ni jukumu la Walimu. Walimu tuna uwezo wa kuwajua watoto hawa wanaweza kuwa ama wanasayansi au wanabiashara na fani nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa tusipolianza hili mapema ni vigumu, hata tukianza kwenye level ya vyuo kama huku hatujawaandaa watoto hawa kuwa wanasayansi hatutaweza kupata Walimu waliokuwa bora wakaweza kuleta mabadiliko kwenye eneo la sayansi. Kwa hiyo, hili naomba lazima tuzingatie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapochagua wanafunzi tuweke malengo, malengo yetu ni nini; kuwapata Walimu wa sayansi. Basi tusichague tu ilimradi huyu anaweza kuwa Mwalimu, tuangalie sifa, tujipange, kama tunataka kuboresha tuangalie wa Division I, wa Division II basi hawa waende kwenye eneo la ualimu, sio wale ambao kwa kweli maksi zao haziridhishi ndiyo tunawachagua kwenda kufanya kazi ya ualimu, hili halitakuwa na tija kwetu. Ni lazima tuwekeze kwenye hili, sisi kama Serikali tuna uwezo wa kusema hili tunataka hili hatulitaki, sisi ndio wenye maamuzi, tukiwashawishi watoto hawa wanaweza kufuata kile ambacho tunakitaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyoandaa Mainjinia, tunavyoandaa Madaktari, hali kadhalika tuwaandae watoto hawa kwenda kwenye fani hiyo ya ualimu. Kwa kufanya hivyo tutapata Walimu wa Sayansi mahiri sana na hapo ndipo tutakapoweza kutafsiri dira, dhima na majukumu ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka twende kwenye shule za ufundi; shule hizi ni muhimu sana kwa ustawi wa Taifa letu hasa ukizingatia kwamba tunakwenda kwenye uchumi wa viwanda na tunaelekea kwenye uchumi wa kati ifikapo 2020. Hili ni muhimu kwa sababu kubwa moja; lazima tuwapate hapa mafundi wa katikati, wale mafundi mchundo, ili tuweze kuendana na hali ya sasa tuliyokuwa nayo. Kwa sababu shule zilikuwepo; kulikuwa na Tanga, Ifunda, Mtwara Technical, Dar es Salaam na zote zilikuwa zinafanya hizi kazi. Kitu kikubwa tu sasa hivi ni kufanya hayo maboresho na kurejesha hilo ili tuwe na mafundi hao wa katikati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nataka nizungumzie Bodi ya Mikopo; tunaishukuru Serikali kwa kuwashughulikia watoto yatima na wanaotoka katika mazingira magumu, watoto hawa wameweza kupata…

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Mama Salma kwa mchango mzuri.

MHE. SALMA R. KIKWETE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, mengine nitayaandika. Ahsante sana. (Makofi)