Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

Hon. Dr. Jasmine Tiisekwa Bunga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Vyuo Vikuu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia Wizara hii muhimu ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. Niungane na Wabunge wote ambao wamewapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Naibu Katibu na Watendaji wote pamoja na Wakuu wote wa Taasisi wa Wizara hii kwa kweli kwa kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa unyenyekevu na usikivu wako. Kwa jinsi ninavyokufahamu, kwa kweli ukisikiliza hii taarifa imesheheni na umetumia ile smart approach kwamba unasema nitafanya nini kwa muda gani, kwa hiyo, ni rahisi hata kuwa measurable tutaweza kukuuliza mbona ulisema hiki kuliko zile tulizozoea kwamba tukipata fedha, tukifanya hivi ndipo tutafanya; lakini umeonyesha. Kwa mfano, kuanzia page 134 – 213 imesheheni mambo gani yatafanyika. Hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi kama Mwakilishi wa Vyuo Vikuu nimekaa na Uongozi wa Serikali ya Wanafunzi pamoja na Viongozi wa Academic Staff takribani vyuo 10 hivi, wamenituma kwamba upeleke salamu kwa Mheshimiwa Rais wetu kwamba wana imani na Mheshimiwa Rais wetu pamoja na wasaidizi wake wote akiwemo Mheshimiwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu jinsi wanavyotekeleza mipango ya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wanasema wanapongeza sana, lakini vijana wa Vyuo Vikuu wanashukuru sana kwamba mikopo sasa hivi inapatikana kwa wakati pamoja na kwamba kuna changamoto za hapa na pale, lakini wana-support sana zoezi lile la vyeti feki. Wakifikiria jinsi wanavyo-toil halafu mwingine anapata cheti feki anapata kazi. Kwa hiyo, wanampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa zoezi hili pamoja na elimu bure. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, napenda nizungumze mambo machache kuhusu changamoto za wanafunzi. Zipo changamoto nyingi lakini kuna mambo ya msingi ambayo mwanafunzi akiyapata, akili yake itatulia na atasoma vizuri. Kuna suala la Bima ya Afya, mikopo na hosteli; na mambo mengine nitakuletea kwa maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bima ya Afya bado ni tatizo. Wanafunzi wanaingia mwaka wa kwanza kwa mfano, toka wanavyoingia mwezi wa Kumi unakuta mwanafunzi hapati kabisa Bima ya Afya, sasa tatizo ni nini? Nakumbuka nilizungumza hili tatizo wakati nikiwa kwenye Kamati ya Huduma, bado tatizo linaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri ashughulikie kwa sababu vijana hawa wanahitaji kupata afya ili waweze kusoma. Pia wakati mwingine mwanafunzi anapata Bima ya Afya mwezi wa Tano, mwezi wa Saba ina-expire, wanaomba expiring date iendane na ile date of issue.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mikopo; mikopo inakwenda vizuri lakini bado kuna changamoto. Wamepongeza sana ule mtindo wa fingerprints, wanapenda utumike huo, lakini kuna wakati vijana wanasaini mkopo wanasema fedha zimekuja, lakini wanaweza wakakaa zaidi ya hata ya mwezi fedha hizi hazijaja, kwa hiyo kuna shida. Hata hivyo, wameipongeza sana Bodi ya Mikopo Taifa kwa jinsi wanavyoshirikiana na wanafunzi hawa, tatizo bado liko kwenye kanda. Kwa hiyo kwenye kanda muweze kuelekeza nguvu waweze kuwasaidia hawa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hostels ni muhimu sana kwa vijana wetu. Wapo wanafunzi wanabakwa usiku, mfano hapa Muslim University, Mipango, wasichana wawili wamebakwa wakati wanatoka shule wanakwenda majumbani kwao, kwa hiyo hostels fedha zilizotolewa tunaomba zitolewe zote ili ziweze zikajenge kule Mzumbe, SUA, Dar es Salaam kama tunavyoona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la rushwa na maadili; wakati wa orientation nimwombe Mheshimiwa Waziri ajitahidi kwamba orientation vijana hawa wapewe namna ya maadili. Kwa mfano suala la rushwa ya ngono, suala hili mara nyingi wanaelekezwa Walimu wa kiume tu, lakini kwa jinsi nilivyokaa na wanafunzi na walimu hii ina-apply kotekote, wapo wanafunzi wa kike ambao wanawa-seduce Walimu wa kiume na meseji nimeziona. Kwa hiyo tunaomba rushwa ya ngono, hasa kwa Wahadhiri vijana ndio wanatuhumiwa zaidi, lakini hawa Seniors Professors wako vizuri, vijana wanawapongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la fieldwork; kwa mfano upande wa mining, petroleum na gesi ni shida, vijana wanapelekwa kwenye vikampuni vidogovidogo. Sasa kama tunataka tutumie wataalam wazawa, inabidi yale makampuni makubwa yasaidie kuwapokea hawa vijana wetu kwenye suala la field kwa sababu field nayo ni changamoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulipitisha humu ndani asilimia 15 kwa ajili ya kulipa mkopo. Kwa kweli asilimia 15 hii bado ni kubwa, kama inawezekana waweze ku-review, kwa sababu huyu kijana anapoanza kazi, kwanza tayari anatoka kwenye familia ya kipato cha chini, halafu bado unambebesha tena asilimia kumi ya penati akichelewa kulipa; bado alipe asilimia 15, anatakiwa alipe asilimia 30 ya tax, sijui mambo ya bima na kadhalika, please, tunaomba waangalie, asilimia 15 ni kubwa sana. Mbona mikopo ya vijana kule halmashauri tumeondoa riba; kwa nini tusiondoe na huku kwa vijana wetu ili tuweze kuwasaidia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Wahadhiri, vyuo vikuu tunategemea sana Wahadhiri wetu wafanye kazi vizuri, lakini kuna hii, Mheshimiwa Waziri anajua, yeye ni profesa ametoka kule, suala la harmonized scheme. Kule mwanzoni watu waliajiriwa wakiwa na GPA ya 3.5, wengine 3.8, baada ya harmonized scheme wanatakiwa wote kuwa na 3.8, sasa hii inaleta changamoto kwa ambao waliajiriwa kwenye 3.5, ni vizuri wakaanzia pale walipoanza hii sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, kuna suala la stahiki za Walimu kama walivyoongea Wabunge wengine. Walimu wanadai arrears zao, wanadai responsibility allowances, housing allowances, for so many years; wanasubiri nini jamani? Hawa nao ni binadamu wana majukumu yao, lakini wasije wakashawishika sasa wakaanza underground migomo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, nikiangalia kwenye bajeti yetu hii universities maana yake kuwe na research and development; fedha hazipo. Serikali wanatoa kiasi kidogo, sasa hili Taifa tutaendeleaje? Kwa mfano, sasa hivi kuna uhaba wa ajira, Walimu ni wachache, hawaaajiri lakini bado researches zenyewe hata promotion haziji. Unajua hadhi ya chuo kikuu lazima watu wapande wafikie ngazi fulani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano sasa hivi kuna hili suala la Walimu ambao ni Senior Professors kustaafu kwenye age ya 65. Sasa wale wengine sasa hivi mnasema Maprofesa waliostaafu wasipewe hata mikataba labda kama chuo kiwagharamie. Vyuo hawana fedha za kutosha, lakini tukumbuke kwamba hawa Maprofesa ambao tunawaacha, nafikiri ni kwa Tanzania tu, wangefikiria, kama suala ni gratuity wangefanya kama India, India profesa anastaafu kwenye age ya 65 lakini wanalipwa mishahara gratuity haipo. Kwa nini wasikae chini waongee? Kwa sababu vyuo vyetu vitakosa credibility, hili wanaliona, tutakwenda kwenye bomu kama la sekondari; shule za Serikali hazi-perform, private zina-perform.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hivi Serikali imetumia fedha nyingi kumuandaa Profesa, unajua kumwandaa profesa sio kazi ngumu, wanawaacha watachukuliwa huko na private sector, hata nchi za nje, baadaye tutakosa sifa tutaanza kuagiza ma-TX. Sasa kumlipa TX cha bure ni gharama, TX umsomeshee mtoto, umlipe kwa dola na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, please, nimwombe Mheshimiwa Waziri hebu wakae walifikirie…

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri. Mheshimiwa Mama Salma Kikwete.

MHE. DKT. JASMINE T. BUNGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)