Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Eng. Hamad Yussuf Masauni

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kikwajuni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuendelea kuniamini kwa nafasi hii ya Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Naomba niendelee kumhakikishia kwamba nitaendelea kutokumwangusha na kuchapa kazi inavyostahili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nachukua fursa hii kumshukuru Mheshimiwa Makamu wa Rais na Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa msaada wao mbalimbali ambao unanisadia kutekeleza majukumu yangu vizuri. Pia nachukua fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Kangi Lugola ambaye kwa kweli ni Waziri wa aina yake. Tumefanya kazi kwa ushirikiano mkubwa; pamoja na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wakuu wa Vyombo pamoja na Makamanda wote nchi nzima na Wakuu wa Taasisi mbalimbali wakiwemo NIDA na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia siyo kwa umuhimu, niishukuru sana familia yangu kwa kuniunga mkono na kuweza kunistahimilia pale ambapo natekeleza majukumu ya Kitaifa. Baada ya shukrani hizo, sasa nataka niende moja kwa moja kwenye hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la kwanza ambalo nataka nizungumze kwa sababu ya ufupi wa muda, nimeamua kuliweka hili mwanzo kwa sababu ni jambo nadhani ni muhimu sana. Jambo hili kwa bahati mbaya linaonekana kuleta taswira mbaya na kuichafua Serikali yetu adhimu ambayo wakati wote imekuwa ikifanya kazi kwa uadilifu, kwa ufanisi na kwa bidii kubwa na juhudi kubwa katika kuwatumikiwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuhuma hizi zisipojibiwa kwa uwazi kama ambavyo nataka nijitahidi kuzijibu hapa leo, zikiendelea kubakia kuzungumzwa kila siku zinaweza kusababisha kutengeneza chuki kati ya wananchi na Serikali yao, chuki ambazo madhara yake kwa mustakabali wa amani ya nchi yetu zinaweza zikawa kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa kuna tuhuma kwamba vyombo hasa Jeshi la Polisi na kwa maana ya Serikali kwa ujumla wake, tumekuwa tukifanya kazi zetu kwa kukandamiza baadhi ya raia kulingana na aina ya dini wanayoiamini au sehemu waliyotoka. Labda nitoe mfano mmoja hai ambao umekuwa ukizungumzwa miaka mingi, wamekuwa wakitoa mfano wa watu ambao wanawaita Mashehe wa Uamsho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikiri kwamba binafsi kwa kupata fursa ya kutumikia Serikali hii, najiridhisha pasi na shaka yoyote kwamba Serikali yetu hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na vyombo vyake ambavyo tunavisimamia wakati wote tumekuwa tukifanya kazi kwa kufuata misingi ya sheria. Kama ingelikuwa nimeshuhudia aina yoyote ya upendeleo, ubaguzi kwa misingi yoyote ile, leo ningelimwandikia barua Mheshimiwa Rais ya kujiuzulu nikakaa kule backbencher, nikawa mimi ndiyo miongoni mwa watu wa kushiriki kupingana na hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu naamini kabisa kwamba kwanza Serikali ya aina hiyo itakuwa ni Serikali ambayo inatenda dhambi kwa Mwenyezi Mungu, lakini ni Serikali ambayo itakuwa inaandaa misingi mibovu ya amani ya nchi hii. Tumeshuhudia Mataifa mbalimbali ambayo haikuwa na misingi mizuri kama misingi ambayo Waasisi wa Taifa hili waliojenga kwa Tanzania inayosababisha mpaka sasa hivi tuendelee kubakia na umoja na mshikamano bila kujali jambo lolote ambalo mhusika analo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi najua jambo hili bahati mbaya linazungumzwa na baadhi ya wanasiasa kwa sababu za kisiasa, jambo ambalo ni hatari sana, lakini hatuwezi kuendelea kukubali. Tuhuma hizi za hawa watu wa Uamsho zimekuwa za muda mrefu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakumbuka katika vikao vya bajeti vilivyopita ilikuja hoja ya kwamba watu hawa wa Uamsho wanafanyiwa vitendo vya udhalilishaji na tukapata maelezo kutoka vyombo vyetu tukiwasilisha Bungeni kueleza kwamba haya ambayo yanazungumzwa siyo kweli. Nami binafsi nilifanya ziara ya kwenda Gereza la Ukonga na kuzungumza nao watu hawa. Nilipofika niliwauliza kwamba je, kuna jambo lolote la kinyume na utaratibu ikiwemo udhalilishaji ambapo vyombo vyetu vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vimewafanyia? Wakaniambia hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilivyofika niliwauliza kwamba, je, kuna jambo lolote la kinyume na utaratibu ikiwemo udhalilishaji ambavyo vyombo vyetu vilivyopo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi vimewafanyia? Wakaniambia hakuna, nikawauliza je, kuishi kwenu hapa kuna mashaka yoyote ya ukiukwaji wa haki za binadamu? Wakaniambia hakuna, tuko vizuri kabisa. Baadaye wakanieleza pamoja na mambo mengine, jambo la kwanza wakaniambia kwamba sisi changamoto yetu hapa ni kuchelewa kwa kesi yetu. Concern hiyo ndiyo concern ambayo Serikali tunayo siyo kwa wao tu bali kwa Mahabusu wote nchi nzima na kila siku tumekuwa tukieleza mikakati mbalimbali ya jinsi ambavyo tunataka tuhakikishe kwamba wanaotuhumiwa kesi zao zinakwenda haraka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna mikakati mingi ya kutumia wafungwa kwa ajili ya kujiendeleza katika Jeshi la Magereza ambayo tutaizungumza baadaye; kwenye kilimo, kwenye viwanda, tunahitaji nguvu kazi. Kwa hiyo tunaamini kabisa wale ambao hawana hatia waachiwe huru, waliokuwa na hatia wafungwe ili kama hata wanaendelea kutumia rasilimali za nchi, lakini waweze kuzalisha vilevile. Kwa hiyo hakuna hata siku moja Serikali hii imekaa ikawa inapendelea kuona raia wake wanaendelea kubaki mahabusu. Jambo hili bahati nzuri tulilizungumza kwa mapana yake. Aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Profesa Kabudi alilizungumza akaeleza ni changamoto gani zinakabili tuhuma hizi, tuhuma za ugaidi ni kwa nini kesi zimechelewa na jitihada gani Serikali tunaingiza katika kuona mambo haya yanakwisha haraka, limeelezwa vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine ambalo waliniuliza, wakanipatia maandiko ambayo walieleza kwamba wao wanataka, wanaona kwamba wameshajifunza vya kutosha na kwa hiyo basi wanaomba waachiwe na kwa namna hiyo basi watakapokuwa wameachiwa hawatakubali tena kufanya siasa au kutumika kwenye siasa. Sasa nikajiuliza; kwani kesi ambayo inawakabili hawa watuhumiwa ni kesi ya siasa au kesi ya ugaidi? Ninavyofahamu ni kwamba tuhuma zile ni za ugaidi siyo za siasa, sasa unazungumza siasa imetoka wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kauli hiyo ikanikaa sana kwenye kichwa na ndiyo maana ninapokuja sasa huku kwenye Bunge na maeneo mengine, naona sasa nikishabihisha na matukio yaliyotokea kipindi cha nyuma napata mashaka. Naona hapa kuna jambo lingine na kama jambo ni siasa hivi kweli Waheshimiwa Wabunge tuko tayari kuligawa Taifa hili kwa sababu ya siasa? Kama kweli hoja ni siasa na nikashabihisha baadhi ya sera za Chama Kikuu cha Upinzani kilichokuwa Zanzibar za kuendelea kudhani kwamba wataendelea kupata popularity kwa kugawa wananchi. Sera za kusema hawa Wapemba, hawa Waunguja kwamba labda watu wa Unguja wameona kwamba sera hizo hazikufanikiwa kuwaambia watu wa Unguja ambao ni ndugu za damu na wenzao wa Pemba kwamba watu wa Unguja hawawapendi Wapemba ili kupata kura tu. Au sera za kusema kwamba hawa Watanzania Bara, hawa Wazanzibari na ndiyo haya mambo ambayo yalifanyika katika kipindi cha nyuma, nikashangaa vihi dini gani ambayo inashabihisha kugawa watu? Dini gani ambayo inazungumzia masuala ya Muungano mbaya? Hivi kweli hakuna jambo hata moja zuri la Muungano? Badala ya kuwaambia wananchi watumie fursa zilizopo nyingi za Muungano, wanatumia changamoto ambazo pengine tunazikabili kila siku na kuzipunguza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nikapata mashaka sana na hilo jambo na ndiyo maana nikasema kwamba yale mambo ambayo yalijitokeza kipindi kile na watu wengi ni mashahidi, tulishuhudia jinsi ambavyo baadhi ya Masheikh wengine mpake leo wana makovu na majeraha kwenye uso ya kumwagiwa tindikali, kuna Mapadre walipigwa risasi, kuna mabomu yalitegwa, ni kwa sababu ya kuendekeza na kuchanganya na yote yalifanyika kwa kutumia dini lakini kumbe leo nimegundua haya kumbe yalikuwa na malengo ya kisiasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni hatari na nimeona niyazungumze hivyo kwa mapana kwa sababu tumechoka kuona kwamba Serikali yeu inaendelea kuchafuliwa hali ya kuwa ukweli hawa wanasiasa wanaufahamu. Nataka niwahakikishie kitu kimoja tu kwamba, karne hii tuliyokuwanayo hatutakubali kuruhusu undumilakuwili wa kisiasa, hatutakubali kuona dini inatumika kujenga chuki, kujenga uadui kwa kupitia kwenye siasa. Yaliyotokea yamekuwa ni funzo kwetu sisi na ndiyo maana nichukue fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri kwa statement nzito na muhimu sana aliyotoa Zanzibar juzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikwenda Zanzibar pamoja na tuliona kwamba kuna hatari ya kunyemelea kwa taratibu zile zile ambazo zilitufikisha pale tulipokuwepo na tukapata kazi kubwa sana na hivyo basi naendelea kusisitiza kauli ya Mheshimiwa Waziri na hii kauli ambayo aliwaelekeza Jeshi la Polisi. Kutokana na kazi za kisiasa ambazo zimeendelea kufanywa na wale wale ambao sasa wamehamia vyama vingine kwa kisingizio kwa mikutano ya ndani halafu leo wanakuja hapa wanalalamika wanasema mikutano ya ndani inazuiliwa, mikutano ya hadhara inazuiliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikutano ya ndani ambayo itakuwa inafanywa kwa utaratibu kama ambavyo wamekuwa wakifanya wao kule Zanzibar, utaratibu wa kutumia mikutano ya ndani kueneza chuki, utaratibu wa kutumia mikutano ya ndani kutukana viongozi na kugawa wananchi, mikutano hiyo haitakuwa na uhalali, hata kama ni mikutano ya ndani. Mikutano ya ndani ambayo unafanya unaweka maturubai na mabomba nje na kuziba njia wananchi wasifanye shughuli zao, kupiga ngoma barabarani, kuchinja wanyama sijui mbuzi na kumwaga damu barabarani, mikutano hiyo marufuku.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasisitiza kauli ya Mheshimiwa Waziri kwamba kama kuna Askari ambao wanadhani kwamba baadhi yao, najua kama watakuwepo kwa Zanzibar watakuwa wachache kama wapo, kama yaliyotokea kipindi kile cha siasa na dini kwenda pamoja wakaacha mambo haya yakaenda mpaka yakafikia yalipofikia, kama wamefanya hivyo iwe kwa uzembe, iwe kwa utashi wao na mapenzi yao kwa chama chochote kile cha upinzani wachukuliwe hatua. Wasipochukuliwa hatua, wakubwa wao tutawachukulia hatua sisi na watakaokuwa nje ya mamlaka yetu tutatoa mapendekezo kwenye mamlaka husika wachukuliwe hatua. Hili jambo hatuwezi kuliruhusu, tunataka sheria ifuatwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhumuni ya mikutano hii najua Mheshimiwa Waziri atalizungumza, madhumuni ni kwamba sisi tunataka demokrasia hii iwe na tija kwa wananchi, demokrasia itafsiri hali halisi ya kupambana na umaskini ndiyo tafsiri ya demokrasia yetu na ndiyo maana tunasema kwamba wakati huu ni wakati wa kufanya kazi. Kwa hiyo mikutano ya hadhara inayofanywa itafanywa wakati husika. Hatuwezi tukafika hapa tukarithishana tu demokrasia za watu wengine. Wamarekani wanawake wameanza kuruhusiwa kupiga kura mwaka 1920, tokea karne na karne za nyuma zilizopita. Kuruhusiwa watu weusi kupiga kura, kushiriki uchaguzi imechukua miaka zaidi ya 100.

MWENYEKITI: Haya malizia Mheshimiwa Waziri.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tafsiri ya Demokrasia yetu ilete tija kwa wananchi na tunafanya hivyo kwa kufuata sheria kwa sababu Jeshi la Polisi linaposema kwamba linataka kuangalia intelijensia ikoje, intelijensia ni uwanja mpana. Kwa mfano; unapozungumzia intelijensia…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri malizia.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ikiwa intelijensia ya Polisi inaona kwamba sisi tunahitaji Askari wetu waende wakaangalie hali ya usalama ya wezi, hali ya usalama ya majambazi ili Wananchi watekeleze shughuli zao za maendeleo hatuwezi ku-deploy Polisi wetu wakalinda mikutano ya fujo na chuki.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Kwa hiyo tuko hapa tunasimamia kwa mujibu wa sharia, kwa hiyo tunataka Askari wote watambue hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwa kumalizia; nataka nichukue fursa hii kuwaambia Askari wetu kwamba kama kuna Serikali ambayo inawapenda ni Serikali ya Dkt. John POmbe Magufuli. Katika kipindi cha muda mfupi kwa haraka haraka, toka Serikali ya Dkt. Magufuli imeingia madarakani kuna mambo makubwa Jeshi letu la Polisi limefanyiwa ambayo ni ya kutolea mifano na hayajafanyika kwa miaka mingi nitataja machache:-

Mheshimia Mwenyekiti, mafao ya wastaafu ni moja ya changamoto kubwa kwa Askari wetu na takwimu hapa zinaonesha ni kwa kiasi gani tumefanikiwa. Masuala ya ucheleweshwaji wa mishahara kwenye vyeo ilikuwa ni changamoto kubwa kwa Askari wetu, sasa hivi mambo haya yamepata ufumbuzi kwa kiasi kikubwa sana. Mheshimiwa Waziri wa Utumishi amezungumza, tunatarajia kupandisha vyeo vingine zaidi mwaka huu wa fedha pamoja na kuajiri askari wapya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, posho mbalimbali ziko katika hatua za kuongezwa, mpaka hata sasa makazi ya Askari yanaboreshwa. Serikali hii ya Dkt. Magufuli inaimarisha vitendeakazi ikiwemo vyombo vya usafiri na teknolojia za kisiasa kwa ajili ya matumizi ya Jeshi la Polisi. Hali kadhalika, katika masuala…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …ya mafunzo…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Msigwa kaa.

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …masuala ya mafunzo pamoja na…

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu utaratibu.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Msigwa kaa kwanza

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: …Serikali hii imeangalia kwa karibu sana. Kwa hiyo hoja za Wapinzani hazina mashiko. Serikali hii…

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri ahsante wka mchango mzuri, ahsante nimekuongeza dakika saba.

(Hapa baadhi ya Wabunge waliongea bila kufuata utaratibu)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)