Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Spika, katazo la mikutano ya Vyama vya siasa kwa mujibu wa Sheria ya Vyama vya Siasa inasajiliwa kwa kuangalia vigezo toka mwaka 1992 tulipoingia kwenye mfumo wa vyama vingi, lakini tumeshuhudia kwenye Serikali ya Awamu ya Tano kumekuwa na zuio kwa vyama vya siasa kutimiza majukumu yao. Tunaomba Serikali itujibu inatumia sheria gani kuzuia mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa.

Mheshimiwa Spika, Askari kuwaadhibu wahalifu; Je, ni sheria gani inampa mamlaka Askari anapokuwa na mhalifu ambaye hajahukumiwa kuadhibiwa? Kumekuwa na malalamiko makubwa kutoka kwa wananchi juu ya polisi pale wanapowakamata wahalifu jambo ambalo linaondoa upendo kati ya Jeshi la Polisi na raia.

Mheshimiwa Mwenyekiti; Askari wa Usalama Barabarani kugeuka kuwa wakusanya mapato; hivi sasa kumekuwa na utaratibu kwa Askari wa Usalama Barabarani wakiwa na EFD machine na risiti muda wote, je, huo ndio mpango wa Wizara ili kuweza kumaliza ajali barabarani au ndiyo chanzo cha rushwa na kupelekea ajali zaidi?

Mheshimiwa Spika, Vituo vya Polisi vinavyojengwa na nguvu ya wananchi; wananchi wamekuwa wakijitolea kujenga vituo vya polisi katika maeneo mbalimbali nchini, lakini jitihada hizi za wananchi haziungwi mkono na Serikali na kupelekea kuwavunja moyo wananchi hawa wanaojitolea.

Mheshimiwa Spika, vitambulisho vya Taifa; sio Watanzania wote ambao wamepata vitambulisho hivi, kwa hiyo jambo lolote litakalofanyika kwa sasa kwa kigezo cha kuwa na utambulisho litakuwa la ubaguzi, nashauri Serikali kwa kuwa bado kuna changamoto kwenye uzalishaji wa vitambulisho, Wizara iweke mkakati mahususi wa kuweza kumaliza changamoto hizo kwanza ili kuwapa haki wananchi wetu.

Mheshimiwa Spika, suala la askari wenye sifa na waliotimiza vigezo kupandishwa vyeo; kumekuwa na malalamiko kutoka kwa askari wanaojiendeleza kielimu kushindwa kupandishwa vyeo pale ambapo ameshajiendeleza, suala hili linashusha morali kwa askari wetu kwani nao wana stahiki kupewa haki kama watumishi wengine nchini.

Mheshimiwa Spika, pesa za likizo; pamoja na uhamisho kwa askari wetu kumekuwa na malalamiko makubwa kwa askari kuhusu pesa za likizo na pesa za uhamisho, Wizara iangalie upya utaratibu wa kuwasaidia askari kuwapatia pesa hizo kwa kuwa ipo kisheria na ni haki zao.