Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Livingstone Joseph Lusinde

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mtera

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nimshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunipa afya asubuhi ya leo ili na mimi niweze kuchangia hili Fungu 28 la Wizara ya Mambo ya Ndani.

Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi wamempongeza sana Mheshimiwa Waziri Kangi Lugola pamoja na Naibu wake Masauni pamoja na Katibu Mkuu na watendaji wote wa vyombo vya ulinzi na usalama walioko chini ya Wizara hiyo wanafanya kazi nzuri sana. Mimi niwe shuhuda tu kuthibitisha kwamba Jeshi la Polisi, Magereza na Uhamiaji ni miongoni mwa vyombo muhimu sana kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, wakati tunajadili leo, kuna tofauti kubwa sana kati ya mjadala wa leo na mjadala wa jana Waheshimiwa Wabunge mtakubaliana nami. Jana tulifikia mahali hata kuambiwa kwa nini mnawapa pole Polisi ya kung’atwa na mbu wakati ni kazi yao. Sasa mimi nikawa napata taabu sana, hii ni kazi ya kizalendo, si tu kazi yao kazi wanayoifanya ni ya kizalendo ambayo ina mazingira magumu yanayohitaji kupongezwa.

Mheshimiwa Spika, aliyesema maneno hayo akasema ninyi wengine hamjawahi kulala hata ndani ninyi, wewe si umelala ndani kwa kujitakia mwenyewe? Kwani ukiwa hutaki kulala ndani utalala ndani jamani! Siyo rahisi, maana Polisi wanashughulika na watu waovunja sheria. Polisi hawashughuliki na kila mtu barabarani hapa, ingekuwa kila mtu basi kakamatwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nature ya chombo chenyewe tunachokijadili, kwanza ni chombo chenye mafunzo, lakini chombo kina watu wanahenya, kuna watu wanasoma na kuhenya juu.

Mheshimiwa Spika, unajua hapa Wabunge, Bunge lililopita muliamua wewe na Mheshimiwa Spika Anna Makinda, tukaenda JKT, tulikwenda na mdogo wangu Mheshimiwa Neema hapa, nadhani tulijifunza kidogo utofauti wa hivi vyombo, kwa hiyo, nataka nikupongeze Mheshimiwa Neema kwa ajili ya ukakamavu, kumaliza. Jamani counter ya jeshi la polisi haiwezi kufananishwa na counter ya hoteli, haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, counter ya polisi lazima umkute mtu ana sura ya jiwe, ametulia, anakusikiliza umasema nini, ya hoteli utamkuta mtu anatabasabu, karibu, chumba kipo, hiyo ni ya hoteli, siyo polisi! (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, polisi lazima wawe wakakamavu, siyo kitu cha mchezo.

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Tena ndiye ninayemtaka huyo.

SPIKA: Wewe unampa taarifa Lusinde, haya toa taarifa. (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, mzungumzaji anayezungumza, ni vizuri tukaweka rekodi sawa hapa, anayesema hajanitaja lakini najua ananisema kwa hiyo, lazima niweke rekodi sawasawa. (Kicheko)

Mheshimiwa Spika, na ni rafiki yangu, hoja niliyozungumza jana kwamba polisi wanatimiza majukumu yao, Serikali huwa inatoa nafasi za kazi, mtu yeyote anapokwenda kuomba kazi yoyote huwa wanajua consequences zake, anajua polisi wana kazi gani, Askari wana kazi gani.

Mheshimiwa Spika, hata wewe hapo unafanya kazi ya kizalendo, tunategemeana kama Taifa. Tulichokizungumza jana, na nilivyosema jana wengine hamjalala polisi, na nimetoa ushahidi kwamba nimesingiziwa nimelala kwa makosa. Kwa hiyo, ninachotaka kusema, kufanya kazi ngumu kisiwe kisingizio cha kuvunja sheria, hiyo ndiyo hoja tunayoizungumza, lakini siyo kwamba tunadhalilisha kazi ya polisi.

MWENYEKITI: Mbona unahutubia sasa si taarifa iwe fupi!

MHE. MCH. PETER S. MSIGWA: Mheshimiwa Spika, ndiyo hiyo.

SPIKA: Mchungaji ahsante sana, Mheshimiwa Lusinde unapokea taarifa!

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, ukipenda kachumbali upende na pilipili. Watu wote, wanaofanya upinzani kwenye maeneo yao, wote wanaingia kwenye matatizo! Mheshimiwa Zitto alijaribu kufanya upinzani ndani ya CHADEMA, kumpinga Mheshimiwa Mbowe, yupo CHADEMA? Amemalizwa, ameondoka, alijaribu Kafulila, yupo salama CHADEMA! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, muelewe kazi mnayoifanya ina hatari yake, ndiyo ninachotaka kukwambia ukweli hapa, yaani huwezi ukajiita upinzani, yuko wapi, Mheshimiwa Komu alijaribu juzi kumteta Mwenyekiti na mwenzake, wako wapi! Kwa hiyo, ninachotaka kusema, hamuwezi kuwa wapinzani, halafu mkawa salama tu, haiwezekani! (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwasaidie, kwamba kazi wanayoifanya ni kazi inayoweza kuwapa matatizo wakati wowote! (Makofi/Vicheko)

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nitulie kaka yangu kasimama amua.

SPIKA: Mheshimiwa Komu, nini tena rafiki yangu! (Kicheko)

T A A R I F A

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Haya, dakika moja bwana maana yake tunakaribia mwisho.

MHE. ANTONY C. KOMU: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa Mheshimiwa Lusinde, ambaye tuna historia nzuri sana na yeye kwa sababu tumemkuza sisi na anajua. Sasa nipo, na sijazurika, sijateteleka, nipo, maana yake yeye amesema yuko wapi, nipo hapa. (Makofi)

SPIKA: Ila jambo moja tu, hajakanusha kama alimteta Mwenyekiti wake. (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Lusinde, endelea!

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, nilichotaka kusema, kwanza namheshimu sana kaka Komu na ni mmoja wa watu waaminifu sana na alichokuwa anakisema Komu kwa kweli, naweza nikakiamini kwa upande wangu, kwamba kweli kuna matumizi mabaya ya ruzuku mle ndani. Na yeye ndiye aliyekuwa mhasibu wa chama, kwa hiyo, hata, alichofanyiwa alisema ameonewa. Nilitaka kumuonyesha Mheshimiwa Msigwa, kwamba wanaoonewa hawako huku tu, hata ndani ya chama chenu mnaonea watu, mmojawapo mmemuonea Mheshimiwa Komu! Mheshimiwa Komu amesema, kuna matumizi mabaya ya ruzuku, amevuliwa nafasi zake zote, ameonywa, yuko kwenye uangalizi hapo alipo. Sasa hii siyo sawa na Mheshimiwa Kubenea, (Makofi/Vicheko)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jeshi la polisi linafanya kazi nzuri sana. Niombe Waziri wa Mambo ya Ndani, nichukue fursa hii kumpongeza sana Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma, Mroto. (Makofi/Vigelegele)

Mroto anafanya kazi nzuri, jeshi la polisi ni beat, huwezi kucheka na waharifu, kwamba hapa kuna Bunge, Wabunge wanavaa cheni za dhahabu kama unavyowaona wengine humu, halafu Mroto acheze na maandamano maandamano hapa, Wabunge mtaporwa hizo cheni. (Kicheko)

Kwa hiyo, Mroto anaposema hataki mchezo watu watachakaa, yuko sahihi kwa ajili ya kuwalinda ninyi. (Makofi/ Vigelele)

Mheshimiwa Spika, jeshi la polisi kazi zake nyingi, kazi za operation, kwa hiyo, tunaomba Makao Makuu yamehamia hapa Dodoma na jeshi la polisi liimarishwe hapa Dodoma! Wapeni magari ya kufanyia kazi, njia nzima ya kutoka Dodoma kwenda Iringa, kuna vituo viwili tu vya polisi navyo vyote havina gari na wanapita Wabunge wengi, wanapata matatizo huko, kwa hiyo, wapeni, wapeni magari waweze kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Jimbo la Mtera tuna Tarafa tatu, tumeomba pikipiki tatu tu Mheshimiwa Kangi, mpaka leo! Tusaidieni, ili wale polisi waweze ku-move kwenda sehemu moja hadi nyingine. Majuzi hapa kuna mtu alijinyonga, ilichukua karibu siku nzima, mtu kuweza kufika pale, polisi hana pikipiki, hana nini mpaka Mbunge nimetoa gari kwa ajili ya kwenda ku-rescue hiyo situation. Kwa hiyo, sisi tunaomba jeshi la polisi liimarishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambalo limezungumzwa hapa, mikutano ya hadhara, kuna mikutano ya hadhara kama mtakumbuka Waheshimiwa Wabunge, kila mkutano ulikuwa unasababisha mauaji! Iringa alikufa mtu, Morogoro alikufa mtu, Singida alikufa mtu, ni mikutano gani hiyo, Arusha, mikutano hiyo imetuletea matatizo. Kwa hiyo, jeshi la polisi wakati mwingine linapima, hivi kama Bungeni tu tunaongea kwa mihemko hivi, Mbunge anaongea mpaka anasema rubbish, jana hapa. Sasa unajiuliza huyo Mbunge akiwa kwenye mkutano wa hadhara wa kwake binafsi ataongea maneno gani huyu! Lazima jeshi la polisi lipige marufuku, jamani uchaguzi ukishakwisha siasa zinahamia humu, nje tuache watu wachape kazi, tutakutana 2020! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimewaambia siku zote nazidi, unajua wakati mwingine huwa natema madini sijui kama huwa mnasikiliza, uchaguzi ukiisha, mnaachia washindi wafanye kazi waliochaguliwa, na washindi ni Chama cha Mapinduzi. Wapeni nafasi watekeleze Ilani, maswali mtatuuliza mwakani kama yapo, na nina uhakika yatakuwa hayapo, vituo vya afya vinajengwa, maji yanapatikana, sasa kutakuwa na maswali gani tena, hakuna! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nasema, baadhi ya Askari wachache ambao wametajwa, kwamba siyo waaminifu, hao waendelee kuchukuliwa hatua, kama sheria inavyosema, lakini tusiliharibu jeshi la polisi lote kwa sababu ya mtu mmoja kakosea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jamani ikitokea bahati mbaya Padre, au Shekhe kakamatwa ugoni, siyo dini mbaya, haiwezekani, ni huyo huyo aliyeshikwa, dini inaendelea kuaminika, dhehebu linaendelea kuaminika ila yeye aliyevunja masharti ya imani yake huyo ndiye anayechukuliwa hatua. Tusiwatukane Askari wote kwamba wote hawafai, wote wanakosea, hapana, lakini kuna mambo yamezungumzwa.

Mheshimiwa Spika, jana kilizungumzwa kitu hapa na nataka nikiseme, kwenye taarifa ya CAG iliguswa hapa jana kwamba, Mbunge wa CHADEMA alikopeshwa fedha za kununua gari. Nasema, jambo lile lina harufu ya ukwepaji wa kodi, kwa nini nasema hivyo, Wabunge tuna exemption, leo CCM wakinitumia kununua gari la chama, maana yake CCM wanataka kukwepa kodi, kwa sababu wanajua mimi nitasamehewa kodi fulani, lakini ukiniambia kwamba eti alikopeshwa na chama, halafu ameshindwa kulipa chama kimemnyang’anya, si kweli, hapo CHADEMA msikwepe mlitaka kuwepa kodi! (Makofi)

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, kuhusu utaratibu.

SPIKA: Nini tena Chief Whip!

KUHUSU UTARATIBU

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, jambo analolizungumza rafiki yangu anayeongea sasa hivi, Mheshimiwa Chenge akiwa kwenye Kiti chako, alishatolea uamuzi na hiyo hoja anayoisema haiko kwenye taarifa ya CAG! (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Selasini ni hoja gani.

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Spika, ni suala la Mbunge wa CHADEMA kukwepa kodi. Sasa CAG hakuliweka hivyo, hoja ni kwamba kuna gari lilinunuliwa kwa mkopo kutoka CHADEMA na ile gari iko kwa jina la mwanachama, haliko kwenye jina la Baraza la Wadhamini la chama. Kwa hiyo, agizo ni kwamba lile jina liondoke kutoka kwenye jina la mwanachama liende kwenye jina la Baraza la Wadhamini na siyo kukwepa kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Mheshimiwa Chenge akiwa kwenye kiti chako alitoa hiyo ruling.

SPIKA: Hivi huyo mwanachana ni nani!...

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, huyu mwanachama hatajwi, huyu mwanachama ni Mbunge, Mbunge, siyo mwanachama wa kawaida, na CHADEMA ituambie kabla ya mwaka huu, au mwaka gani iliwahi kumkopesha mtu fedha ya kununua gari, wakati Wabunge wote tunakopeshwa hapa! Jamani kuna harufu ya kukwepa kodi, ndicho ninachosema na niko wazi, niiteni popote hata kwenye maadili niiteni nithibitisha, nyie mnataka kukwepa kodi kwa kumtumia Mbunge mwenye exemption! Ninyi siyo watu wasafiki kiasi hicho! (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumze kuhusu mauaji, jeshi la polisi…

SPIKA: Mheshimiwa malizia.

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Spika, jeshi la polisi tunaliomba sana. Kuna watu wengi tu, siyo wale wanaotajwa maarufu, kwamba wameuawa taarifa zao hazipo, wako wengi, nina mjomba wangu anaitwa Nikanoli, amepotea tangu mwaka 1979 mpaka leo. (Kicheko)

Tunaomba jeshi la polisi lipewe vifaa vya kisasa vyenye weledi ili viwasaidie katika uchunguzi hasa wa mauaji, hasa wa mauaji. Watanzania wengi, siyo hawa tu wanaotajwa, wako wengi ambao wamepotea wengine wameuliwa, bila sisi kujua wala bila familia zao kuelewa.

Mheshimiwa Spika, lakini la mwisho kabisa, niombe suala la uraia limezungumzwa sana, hili suala halijawahi kujadiliwa humu Bungeni, lakini kwa kuwa limeanza kusemwa humu, tuombe mamlaka za Serikali zilifanyie kazi. Watu wamezungumza sana kuhusu wafanyabiashara maarufu, kuna siku hapa ametajwa Vedagri wa Mwanza ni mfanyabiashara mkubwa amewekeza sijui Mafya, wapi, Mwanza, hawa watu wote ambao wengine siyo maarufu wakulima ambao wanataka kuhamia nchi hii wapewe huo uraia, kama ni haki yao na kama kuna matatizo vyombo vichunguze, viangalie ubaya wao, viwakatalie kama ambavyo wengine wamewahi kukataliwa bila kusemwa Bungeni na wengine wamewahi kupewa bila kusemwa Bungeni, Serikali iendelee kuchapa kazi.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana kwa kunisikiliza. (Makofi)