Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

Hon. Rehema Juma Migilla

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ulyankulu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi. Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia afya na uzima mpaka leo nipo humu ndani.

Mheshimiwa Spika, kwanza napenda nimpe pongezi sana Mheshimiwa Kangi na Naibu wake, kwa kweli wanafanya kazi nzuri. Mkoani kwangu Tabora yalitokea matatizo ya watoto kukamatwa, nilishirikiana na Mheshimiwa Kangi kuhakikisha hali hiyo inakuwa shwari.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo, napenda nimwambie Mheshimiwa Kangi wanafanya kazi nzuri lakini bado wanahitaji maboresho katika maeneo yafuatayo. Nitaanza na usalama barabarani, hawa watu wanafanya kazi nzuri sana, tumeona ajali za barabarani zimepungua na watu wanaendesha magari yao vizuri sana lakini eneo hili kuna shida mpaka baadhi ya Askari wa Usalama wa Barabarani wamebadilishwa majina badala ya kuitwa traffic wanaitwa MaxMalipo au TRA ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, dhana nzima ya kulinda usalama wa barabarani wa watembea kwa miguu na wa magari haipo tena badala yake wamefanya kama kile ni kitengo cha kukusanya kodi. Mtu anakamatwa badala ya kuambiwa kosa lake kwanza anaulizwa leseni. Baada ya hapo wanamwambia njoo nyuma huku. Sasa unampeleka kule nyuma kufanya nini?

MBUNGE FULANI: Nyuma wapi?

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Namaanisha nyuma ya gari. Akirudi tayari lile kosa limekwisha anaendelea na safari.

SPIKA: Mheshimiwa Rehema, nakukumbusha lugha za Kibunge. (Kicheko)

Endelea kuchangia Mheshimiwa Rehema.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, mimi napenda niishauri Serikali, tunaomba dhana nzima ya hawa Askari wa Usalama Barabarani iwe ni kuelimisha hawa watumiaji wa magari na watembea kwa miguu na isiwe ni kitengo cha kukusanya kodi. Leo hawatoi elimu wanakaa kufanya kazi ya kukusanya kodi. Mheshimiwa Kangi, tunataka utuambie hivi Kitengo cha Usalama Barabani na chenyewe ni source ya mapato ya Serikali? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini nikisalia hapo hapo kuna hawa watu wanaitwa PT, kiukweli hawa mfano kwa kule kwetu Tabora imekuwa ni shida. Badala ya kutembea mipakani mwa mji sasa wanasumbua bodaboda kila kukicha yaani bodaboda hawafanyi kazi kwa amani. Tukumbuke kwamba hawa watu wamejiajiri wenyewe na wengine pikipiki sio zao, aweze kupata hela ya tajiri na ya kuhudumia familia yake lakini hawa PT kila bodaboda akijipindua wako naye na wanataka chao na hiyo haina risiti wala nini, wanaweka mifukoni mwao. Mheshimiwa Kangi tunaomba hawa watu wa PT uwaangalie kwa jicho lingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala lingine la upoteaji wa vithibitisho pindi vinapofika Polisi. Nasema hili nikiwa na uhakika, mimi namiliki bodaboda. Kuna siku bodaboda yangu imekamatwa ilivyofika Polisi, kesho yake nakwenda kuchukua pikipiki yangu haina mafuta wala betri. Sasa tunaamini kabisa kwenye Kituo cha Polisi ni mahali salama na wana kazi ya kulinda usalama wa raia na mali zao. Kwa hiyo, nataka utuambie Mheshimiwa Kangi…

SPIKA: Mheshimiwa Mbunge, ajenda hiyo naomba uiache kwanza ni conflict of interest lakini pili biashara nyingine tuwaachie wananchi jamani, Mbunge unafanya biashara ya bodaboda inakuwaje? (Kicheko)

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, ndiyo ni katika kuongeza uchumi.

SPIKA: Endelea na ajenda nyingine Mheshimiwa Rehema.

MHE. REHEMA J. MIGILLA: Mheshimiwa Spika, naomba niendelee. Suala lingine nataka tuambiwe maana ya VTS (Vehicle Tracking System). Tunajua Jeshi la Polisi linafanya kazi na Idara nyingine kama SUMATRA na tumeona magari ya mizigo na mabasi yamefungiwa hivi ving’amuzi lakini mimi sijajua lengo halisi la kufunga hivi vidubwasha ni lipi? Kwa sababu nimepanda kwenye basi yaani dereva akiongeza spidi kinachofanyika pale ni ule mlio tu unasikia chwi, chwi, chwi lakini hakuna kusema kama ni kile kifaa kinapunguza ule mwendo wa gari. Kama lengo ni kusikiliza tu ule mlio haina haja ya kuwawekea hao wenye magari hivi vitu.

Mheshimiwa Spika, tunataka tujue, hii sauti inavyolia mule kwenye basi hatua gani zinachukuliwa dhidi yake kama hatapunguza mwendo? Atakapoamua kuongeza mwendo kwa sababu kuna magari siku hizi yana TV na music dereva akaamua tu kuchapa mwendo kwa sababu abiria hawatasikia ile sauti matokeo yake atasababisha ajali na huyu mtu bado akienda kule mbele kwa sababu ameenda spidi kubwa atakutana na tochi, je, atakuwa charged mara mbili au vipi? Maana tunaambiwa ikilia ile sauti kwa bosi na SUMATRA inasoma, je, huyu mtu atakuwa anachajiwa mara mbili?

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni ucheleweshwaji wa upelelezi wa makosa mbalimbali. Haki ya mtuhumiwa ni kupelekwa Mahakamani. Tunajua kabisa muda wa kumpeleka Mahakamani mtuhumiwa ni saa 48 au 24 lakini kuna watu leo wako mahabusu takriban miaka sita hawapelekwi Mahakamani na hata wakipelekwa Mahakamani wanaambiwa hii Mahakama haina uwezo wa kusikiliza kesi yao. Kwa nini waendelee kukaa mahabusu ilhali Mahakama ambayo itashughulia kesi zao haipo? Wanaongeza msongamano na gharama kubwa ya kuhudumia mahabusu wengine. Tunaomba tuambiwe, je, hawa watu wanaokaa mahabusu muda mrefu mfano hawa Mashekhe wa Uamsho, kuna watu walikamatwa kule Arusha mpaka leo takriban miaka sita hawajasomewa hukumu yao, ni lini upelelezi wao utakamilika? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni utumikaji wa Polisi kama sehemu ya wasimamizi wa uchaguzi. Inahuzunisha sana Polisi kutumika kama wasimamizi wa uchaguzi ilhali wao kazi yao ni kusimamia usalama wa raia na mali zao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumefanya chaguzi za marudio sehemu mbalimbali lakini unakuta Polisi anakwenda mpaka chumba cha kuhesabia kura, Polisi huyu naye anakuwa ni msimamizi. Kweli leo Polisi wanaacha kutekeleza majukumu yao wanayopaswa kufanya wamekuwa wasimamizi wa uchaguzi. Tunaomba hawa Polisi wasitumike, wafanye kazi wanazopaswa kufanya na kama wanafanya hivyo, basi wafanye kwa pande zote. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kuhusu maslahi ya Polisi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)