Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii. Nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, lakini pia nimpongeze Waziri, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara hii kwa kazi nzuri wanazozifanya katika sekta ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na pongezi za Waziri pamoja na timu yake yote, nichukue nafasi hii pia kutoa pongezi kwa Taifa Stars, Serengeti Boys, Simba Sports Club, Chimo Olympic Maalum, Mabondia na timu ya Bunge Sports kwa kutuwakilisha vyema katika mashindano mbalimbali yaliyofanyika nje ya nchi. Aidha, nichukie nafasi hii pia kuwapongeza Wabunge wote Wawakilishi wote na Madiwani wote ambao wamekuwa wakiendeleza michezo katika maeneo yao kwa gharama zao.

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ya Sanaa Bagamoyo na Chuo cha Michezo Malya, wanafanya kazi nzuri sana, naomba Wizara isisite kuwapa fedha za kutosha ili waweze kutimiza wajibu wao na kuleta tija kwa malengo yaliyokusudiwa. Sasa hivi tunawasifia wasanii wetu na wanamichezo, lakini wengi wao hawajapita kwenye vyuo, ni vizuri basi vyuo hivyo vitumike vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue fursa hii pia kuipongeza Taasisi ya Tulia kwa kuanzisha tamasha la ngoma za asili kila mwaka ambapo wameweza kutuletea burudani, kudumisha utamaduni lakini pia kutoa ajira.

Mheshimiwa Naibu Spika, msichoke kwa pongezi zangu, niwapongeze pia wasanii wote kwa ujumla. Naomba wasanii wadogo wawe wanaungwa mkono, wengi wao wana kazi nzuri, lakini wanashindwa kutuletea kwa sababu hawana fedha, aidha za kurekodi au kuziendeleza. Sasa ningefikiria itakuwa jambo zuri kama na wao wangeingizwa katika lile kundi la wajasiriamali ili wale wasanii wadogo waweze kurekodi kazi zao na kuweza kutuwasilishia.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la mavazi kwa wasanii wanawake bado halijakaa sawa. Wasanii wanaume bado wanavaa vizuri, wanapendeza lakini wanawake, naona mpaka labda vitu fulani fulani vionekane ndiyo wanaona ngoma inanoga. Hata hivyo, nimpongeze dadayangu Vicky Kamata na dada mmoja anaitwa Siza Mazongela au mama Segere, wanaimba, wanacheza lakini bado wako katika mavazi mazuri ya heshima na wanapendeza. Kwa hiyo, naomba Wizara iendelee kulifanyia kazi suala la mavazi ya wasanii wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe wasanii hao wajitahidi sana kutumia ala za asili katika nyimbo zao. Kwa sababu, hasa wasanii wa kizazi kipya, wamekuwa wakitumia sana kompyuta, wakishatengeneza ile mistari yao wanakwenda kwenye kompyuta, sasa unaweza ukamkuta mwimbaji hata ukimpa gitaa, hawezi kutumia. Sasa ni vizuri basi wasanii wetu wawe wanatumia pia na ala za asili na wajitahidi kwenda katika chuo chetu cha sanaa ili waweze kupata mafunzo zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la filamu, filamu zetu wasanii wetu wanakwenda vizuri. Kuna tatizo moja katika zile scripts, niseme yale maneno ambayo yanapita chini pale wakati picha inaendelea kuangaliwa. Maneno yale naona mengi hayajahakikiwa vizuri, kuna Kiingereza kinachotumika pale nafikiri bado hakijakaa sawa. Aidha spellings zimekosewa na matokeo yake yanapoteza maana kabisa, ni vizuri basi ziwe zinapitiwa na kuangaliwa vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika vyombo vya habari, niwashukuru wana habari wote, wanafanya kazi nzuri na wanajitahidi kutuletea habari nzuri na zile mbaya tusizozipenda zote tunazipata. Tunawashukuru sana, lakini sasa kuna suala zima la vijana wabunifu ambao wametengeneza blogs zao na wengine wako online TV, lakini masuala ya usajili, ada na nini gharama imekuwa kubwa, kwa hiyo, ubunifu wao wanashindwa kuendelea nao wamekaa nao. Tuangalie jinsi gani tunaweza tukawasaidia ili tupate vyombo vingine zaidi vya habari vya kutufanyia kazi na kutupa taarifa zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika suala la utamaduni, tusiangalie tu ngoma, tuna suala pia la lugha. Katika suala la lugha matumizi sahihi ya lugha yetu ya Kiswahili ni mazuri zaidi na hili tulichukue hata huku Bungeni, unapomwona Mbunge ambaye ni mzazi na mwenye hadhi ya kitaifa anatamka maneno ya ajabu ajabu ndani ya Bunge, basi ujue huko nyumbani kwake ngoma kubwa. Hii inabidi tujirekebishe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TBC naomba iboreshwe, kama TBC Taifa, kuna wakati inatukwaza, tunasema hebu twende kwanza kwenye TV hii tuangalie, lakini inafika katikati, picha imeganda, ukienda kwenye television nyingine, picha inaendelea. Utakuta saa nyingine hotuba nzuri inayotolewa pale, unataka usikilize hotuba, maneno yameganda. Kwa hiyo, naomba,TBC ifanyiwe marekebisho ya kweli ili tunaposema hii TBC Taifa, iwe TBC Taifa kweli. Marekebisho yanafanywa, lakini sijaona bado, naomba…..

T A A R I F A

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malembeka kuna taarifa!

MHE. AMINA S. MOLLEL: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda tu kumpa taarifa kwamba, kuganda kwa picha katika Shirika la Utangazaji la TBC ni kutokana na ubovu wa baadhi ya mitambo, vifaa vingi vimechakaa. Kwa hiyo, siyo tatizo kwa TBC bali ni umuhimu kwamba tuweze kutetea ili fedha zaidi ziweze kwenda TBC. Ahsante.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Amina Mollel, nilifikiri hiyo ndiyo hoja yake, kwamba TBC iweze kupelekewa vifaa. (Makofi)

Mheshimiwa Malembeka unaipokea taarifa hiyo!

MHE. ANGELINA ADAM MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, huyo ni pacha wangu, kwa hiyo, nikiongea na yeye akichangia si mbaya, lakini neno kuboreshwa lina maana sahihi kama alivyozungumza, labda kama anataka uchambuzi tuanze kutoa mojamoja, kitu gani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati nazungumzia hoja yangu ya kuboresha TBC Taifa, pia nishukuru Azam TV kwa channel yake ya Sinema Zetu. Imejitahidi sana kuwachukua wasanii hasa wadogo, tumewaona tulikuwa hatuwajui, tunaangalia picha zile zina maadili mazuri, waendelee hivyo hivyo. Halafu, huo mkakati wao wa kuwasaidia wasanii, basi uende vizuri ili wasanii waweze kupata haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, dakika zangu ni kumi, muda ni mchache, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na huu ndiyo utekelezaji wa Ilani ya CCM. Ahsante. (Makofi)