Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Mussa Bakari Mbarouk

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tanga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu ambaye ametujalia kukutana katika kikao chetu hiki tukaweza kuzungumzia masuala mbalimbali ya nchi yetu. Sitaacha kuwakumbuka na kuwashukuru wapiga kura wangu wa Jimbo la Tanga Mjini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuko katika kupitisha bajeti ya Wizara ya Sheria na Katiba. Kwanza nianze kwa masikitiko kidogo kwa sababu sheria nyingi Tanzania bado ziko katika utaratibu ule ule wa kikoloni labda niseme kwa sababu zinaandikwa katika lugha ambayo kwa Watanzania siyo lugha mama kwao. Matokeo yake wengi hawaelewi na wanapata kigugumizi na wakati mwingine wanafanya makosa kwa sababu sheria hawazitambui na hawazifahamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kutoa ushauri kwa Serikali, sheria zetu ziandikwe katika lugha zote mbili iwe lugha ya Kingereza lakini pia katika lugha ya Kiswahili ambayo our mother tongue.

(Hapa baadhi ya Wabunge walizungumza bila kufuata utaratibu)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema hivyo kwa sababu nimeshuhudia kwa sababu mara nyingi…

MWENYEKITI: Eeh, umesemaje? Hebu rudia tena. (Kicheko)

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi nimeshuhudia sheria zetu hizi kutokana na kuandikwa Kingereza matokeo yake wengine wanakuwa hawazifahamu. Kwa hiyo, niseme tu kwamba kama tunavyotayarisha vipeperushi mbalimbali hasa kwa wenzetu wa vijijini au kuzifanya ziende katika makala mbalimbali za magazeti kuwe na kurasa ambazo zinatafsiriwa sheria mbalimbali ili wananchi waweze kusisoma na kuzielewa. Kwa sababu lugha inayozungumzwa katika Mahakama zetu unakuta wananchi ama washtakiwa au washitaki wengine hawaelewi na mwingine anakuwa hana Wakili wa kumuwakilisha katika kesi hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana tulipitisha sheria hapa kuwapatia Watanzania usaidizi wa kisheria kwa maana kuwapata Mawakili wa Serikali. Labda Mheshimiwa Waziri atakapokuja hapa atueleze ni kesi ngapi Watanzania wamepatiwa hawa Mawakili wa Serikali kuwasaidia kuwatetea katika kesi hizo? Kwa sababu mpaka leo bado kuna tatizo kubwa la uwakili na wananchi wetu asilimia kubwa hawana uwezo gharama za uwakili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyojua kesi ni gharama na Mawakili wana gharama kubwa. Labda niipongeze Serikali kwa ile azma nzuri ya kutoa usaidizi wa kisheria kwa wananchi lakini mpaka leo hakuna taarifa yoyote iliyotolewa kwamba wananchi kadhaa kesi zao zimesimamiwa na Mawakili wa Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri na kuweka msisitizo kwamba Serikali itumie fedha na iongeze bajeti kuhakikisha sheria zinatafsiriwa katika lugha ya Kiswahili. Pia hizo tafsiri ziwe katika vipeperushi au majarida mbalimbali ili ziende mpaka kwa wananchi. Kwa sababu wakati mwingine mtu hana usaidizi lakini amefanya kosa na utetezi hauwezi na katika sheria tunaambiwa ignorance of law is not a defense, hii ndiyo kubwa inayofanyika lakini watu wanaendelea kufungwa, kuwekwa mahabusu na wanaendelea kufanya makosa kwa sababu hawaelewi tafsiri ya kisheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuna sehemu imesemwa hapa kwamba Tanzania tumeridhia Mkataba wa Afrika kuhusu suala la demokrasia lakini leo ni mwaka wa sita sisi bado hatujaweka saini. Naomba Waziri atakapokuja hapa aeleze ni kwa sababu zipi mpaka leo sisi hatujasaini lakini tulishiriki katika kuridhia mkataba huu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu hiki kuna kipengele kinasema kwamba hivi sasa miaka sita imepita tangu Tanzania ishiriki na kupitisha Azimio kuhusu masuala ya demokrasia, chaguzi na utawala bora lililopitishwa na Umoja wa Afrika ambapo Tanzania ni mwanachama. Mkataba huo ulipitishwa na Umoja wa Afrika wakati wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Serikali za Umoja wa Afrika 30 Januari, 2007. Lengo la mkataba huu ni kuzitaka nchi wanachama kuzingatia na kutekeleza utawala bora utawala wa sheria na haki za binadamu kama ilivyoelezwa katika Ibara ya 3 na 4 ya mkataba huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme tu hili suala linatutia aibu kama Tanzania. Tanzania kama tunavyosema sisi ni kisiwa cha amani na Tanzania katika mambo mengi ndiyo mfano wa kuigwa vipi tuna kigugumizi katika suala hili la kutia saini huu Mkataba wa Demokrasia, Utawala Bora pamoja na Haki za Binadamu? Hili ni jambo kubwa na zito katika Afrika na dunia kwa ujumla, sasa Waziri atuleleze kwa nini mpaka leo miaka sita imepita bado hatujasaini mkataba huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni suala hili la kupiga marufuku mikutano na maandamano. Jambo hili lipo katika sheria ya nchi sasa inakuwaje tunapiga marufuku mikutano, maandamano hali ya kuwa ni jambo ambalo limo ndani ya sharia? Inakuwaje wananchi wakose haki yao ya kikatiba kwa sababu Katiba ndiyo sheria mama na ndiyo iliyotoa ruhusa hiyo kwa nini tuzuie mikutano ya hadhara, maandamano hali ya kuwa tunaona katika nchi za wenzetu kupitia maandamano na mikutano hata inapokuwa wananchi hawamkubali Rais anajiondoa. Kwa mfano, Rais wa Algeria, wananchi, Jeshi na wanafunzi wamefanya maandamano na hapakuwa na umwagaji damu kumetokea mapinduzi baridi Rais yule ameondoka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia katika baadhi ya nchi wananchi wanapokuwa hawaridhishwi basi wanapoandamana wanakuwa wamepeleka ujumbe wa jambo fulani. Kwa mfano, baadhi ya nchi bei ya mkate inapoongezeka au fedha yao kupungua thamani au mfumuko wa bei kuzidi wanafanya maandamano ya amani ambapo hauliwi hata sisimizi na matokeo yake Serikali inakubali na inafanya marekebisho na mambo yanakwenda vizuri. Kwa hiyo, mimi niseme suala hili la kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano tujitanzame upya ili tuweze kutoa ruhusa na ukiangalia tunaelekea katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Mimi napenda Tanzania ionekane ni mfano wa kuigwa katika mambo mengi hasa haya ya demokrasia pamoja na utunzaji wa haki za binadamu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni dhamana. Katika Bunge lililopita niliwahi kuzungumza hapa nikaiomba Serikali, tena nilimwomba Mheshimiwa Rais kupitia kwa huyu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kumtaka kwamba wale Wabunge wenzetu…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Mheshimiwa Mwenyekiti, dakika kumi tayari?

MWENYEKITI: Ndiyo.

MHE. MUSSA B. MBAROUK: Naona umeweka tano.

MWENYEKITI: Hapana, ahsante.