Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

Hon. Joseph Kasheku Musukuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 – Wizara ya Katiba na Sheria

MHE. JOSEPH K. MUSUKUMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia. Niseme tu kiukweli Mheshimiwa Waziri na Serikali ni vizuri wakaangalia uwezekano wa kurekebisha sheria, hasa kwenye makosa madogo madogo ambayo ndiyo yamepelekea magereza yetu mengi yamejaa mahabusu kwa kesi ambazo kiukweli zingine zinastahili tu hata makofi mtu anaenda nyumbani. Kwa hiyo, nashauri sana, hizi sheria zilitungwa Watanzania tukiwa milioni 20, leo tupo milioni 55 bado mtu anawekwa mahabusu wiki mbili kwa kesi ya kuiba kuku. Ni vitu ambavyo kiukweli lazima tufikirie adhabu ambazo zitaweza kupunguza mrundikano wa mahabusu kule ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; nimeona kwenye taarifa ya Waziri katika mahakama zilizojengwa zimo na ya Geita, Chato na Bukombe na mimi natokea Geita ambako kumejengwa mahakama hiyo. Nimwombe tu Mheshimiwa Waziri, aongeze msukumo mahakama ile iweze kukamilika. Sio kweli kwamba imekamilika kama alivyoandika kwenye kitabu chake na tunaona kesi kubwa zinakwenda kufanyika kwenye vyumba vya Wakuu wa Wilaya, sio haki. Ni vizuri tukayakamilisha yale majengo ili yaweze kutoa haki kwa wahusika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nilikuwa nasoma kwenye Kitabu cha Kambi Rasmi ya Upinzani kuhusiana na uteuzi wa Majaji pamoja na kwamba yameondolewa lakini ukiangalia kwenye Katiba, Ibara ya 109(7) na (8) pale inampa mamlaka Mheshimiwa Rais kuteua na anakuwa na jopo ambalo linamshauri. Ningewashauri tu wenzangu, ni vizuri tukamuachia Rais madaraka yake, akafanya kazi kwa mujibu wa Katiba yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho; nimeongea hapa nasikia rafiki yangu Mheshimiwa Sugu ananiita mboyoyo, nakubali, sawa, lakini Watanzania wanajua kati yangu mimi na wewe mboyoyo ni nani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili; dada yangu, Mheshimiwa Upendo nilikuwa namuuliza tu kwa nia nzuri, amesema Humphrey Polepole amesema uteuzi wa wanawake wa CHADEMA unapatikana mpaka wapitiwe na Mwenyekiti. Mimi sikuelewa Kiswahili ndiyo maana nikauliza kwa sababu ninavyofahamu Humphrey yupo sawa; yule ni Mwenyekiti wa chama lazima apitie majina ya watu wake, kuna tatizo gani analolalamika? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. (Makofi)