Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

Hon. Khamis Mtumwa Ali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kiwengwa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020 - Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira

MHE. KHAMIS MTUMWA ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi nami nichangie Wizara hii ya Muungano na Mazingira. Pia naomba nichukue fursa hi kumpongeza kwa dhati kabisa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein kwa kuhakikisha kwamba wanaulinda, kuuhifadhi na kuutetea muungano wetu huu mpaka sasa unafika miaka 55. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha kwamba wanazikusanya kero hizi za Muungano na kuweza kuzifanyiakazi hatua baada ya hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile napenda kuchukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri wake pamoja na Katibu Mkuu kwa kuweza kuzichanganua na kuzitafuta kero hizi na hatimaye tunaona matokeo yake ya kuweza kutatuliwa moja hadi moja kwa kadri ya siku zinavyokwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nijielekeze sasa kwenye suala zima la umuhimu wa Muungano wetu. Muungano wetu huu ni wa historia na unatusaidia sana pande zote mbili ya Tanzania Bara na ya Zanzibar na hasa kwenye suala zima la kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshuhudia mambo mbalimbali ya kibiashara yanafanyika pande mbili hizi na watu hunufaika, lakini bado kuna kikwazo kikubwa cha kufanya double taxation ambayo inafanyika Zanzibar ukipeleka kitu ukileta Tanzania Bara ulipie tena ushuru mara ya pili. Hii bado ni kero na tunaipigia kelele sana na Wabunge wengi wa Zanzibar wanaipigia kelele hii kwa sababu bado inaonekana haitendi haki kwa pande zote mbili za Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumza kuhusiana na suala la ushiriki na ushirikiano mdogo kuhusu masuala ya Kitaifa na kikanda. Kama Mheshimiwa Waziri alivyoelezea katika kitabu chake hiki, amefanya juhudi za kuunda Kamati ya kuweza kuhakikisha kwamba changamoto hizi zinafanyiwa kazi za kielimu, nafasi za masomo na vilevile amezungumza kuhusiana na suala la utafutaji wa fedha kwa masuala ya mambo ya nje ya misaada na mikopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile ametuambia masuala mbalimbali yameundiwa Kamati ambayo atahakikisha kwamba soon tunaona matokeo yake. Napenda sana kumshauri Mheshimiwa Waziri tutakapokuja kwenye bajeti ya mwakani, changamoto hizi tusiwe tunazirejea tena kila siku katika Bunge letu hili Tukufu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nizungumzie kuhusiana na suala la Elimu ya Muungano. Wenzangu wametangulia kusema kwamba ipo haja ya kutoa taaluma kwa yale ambayo yanatatuliwa katika Serikali yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusiana na zile kero za Muungano, kwa sababu vijana wanaoamkia sasa hivi bado wana mentality kichwani kwamba Muungano siyo mzuri, au unatunyonya sana kule Zanzibar. Kiukweli Muungano una faida kubwa sana za kiuchumi, kisiasa na kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kukiwa na utoaji wa elimu katika maeneo mbalimbali hasa kule Zanzibar juu ya changamoto ambazo zinatatuliwa na umuhimu wa Muungano wetu, mimi nina imani kwamba muungano huu utazidi kudumu zaidi ya miaka 100 badala ya miaka 55 hii tuliyofikia sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kuzungumzia suala la ushirikiano kuhusiana na masuala mbalimbali ya Muungano hasa katika Taasisi hizi za ukaguzi. Tumeshuhudia kwamba Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu (CAG) hufanya ukaguzi katika Taasisi mbalimbali au katika Taasisi za Ubalozi bila kushirikiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu Zanzibar. Suala hili tumeshalizungumza sana kwamba wale wenzao ni vyema kwamba wakashirikiana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhali hili suala siyo la Muungano lakini ni vyema zaidi wakaenda kukagua katika Taasisi za Muungano ambazo zipo nje hasa Ubalozi wawashirikishe na wenzetu kule ili wapate exposure na mambo mengine ambayo wataweza kujifunza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri aliniahidi siku moja kwamba tutafuatana mimi naye twende kule Zanzibar, tuone, tukae na Taasisi ambayo inahusiana na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi kuangalia zile changamoto zao ambazo zinawakabili, lakini alitingwa na kazi. Naamini baada ya Bunge hili au baada ya kujibu hoja zetu hizi tutafuatana ili tuone tatizo hili pia linatatuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri; baada ya kauli ya Meshimiwa Waziri Mkuu kusema kwamba ikifiuka tarehe 1 Juni, 2019 suala la mifuko ya plastic ni marukufu, Mheshimiwa Waziri na Naibu wake na Katibu Mkuu wake wamefanya jitihada ya haraka kuonana na wadau na kuweza kuzungumzia mambo mbalimbali ambayo…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante kwa mchango mzuri. Mheshimiwa Juma Kombo, ajiandae Mheshimiwa Mtolea.

MHE. KHAMIS MTUMWA ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. (Makofi)