Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Capt. (Mst). George Huruma Mkuchika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Newala Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA: Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushukuru kwa kupata nafasi hii ya kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa pamoja na Kamati. Kama nilivyoshukuru kwenye hotuba yangu napenda kuwashukuru viongozi wa Taifa letu. Viongozi wa kitaifa wakiongozwa na Mheshimiwa Dkt. Magufuli Rais wetu, napenda kumshukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika na Wenyeviti jinsi mnavyotuongoza humu ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda niwashukuru sana Wabunge wote, kila mtu anajua kwamba, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora ni Wizara ambayo ina uzito wa pekee ni Wizara ambayo Wabunge nawapongeza wa CCM na wa Upinzani walipokuwa wanachangia humu ndani kila mmoja nilimwona ameweka mbele maslahi ya Taifa letu. Kwa hiyo, nataka niwashukuru sana na niwaahidi kuwa sitawaangusha katika majibu niliyowaandalieni.

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa nataka niseme, nchi yetu ipo salama wala haina matatizo ya kiusalama, kikubwa niseme vita dhidi ya rushwa katika nchi yetu ina mafanikio makubwa, wachunguzi wa ndani wanasema hivyo, wachunguzi wa nje wanasema hivyo. Vile vile kubwa zaidi mimi ndio Waziri wa Watumishi wa Nchi hii. Nataka nichukue nafasi hii kuwapongeza watumishi wa umma popote walipo, mtumishi yoyote awe kwenye shirika la Serikali, awe kwenye Wizara, awe kwenye Wakala ilimradi analipwa na Serikali Waziri wao ndio mimi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kuwashukuru sana Watumishi wa Umma. Ukisikia tumenunua ndege za Serikali, ninyi ndio mmekushanya kodi, tumefanya nini, tumefanya nini, haya yote ni kwa sababu watumishi wa umma mmetekeleza wajibu wenu, huku nikizingatia wapo wachache wanaotuharibia sifa, lakini wengi mnafanya kazi nzuri na ndio maana mimi naona fahari ya kuwa Waziri wenu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka niseme jambo moja ambalo Waheshimiwa Wabunge walilizungumza hapa nisije nikalisahau, TASAF haijafika katika vijiji na shehia zote nchi zima. Kuanzia tarehe Mosi Julai tunajipanga tunataka tufike katika vijiji vyote, tunatakiwa tufike shehia zote bara na visiwani. Kwa hiyo hilo msiwe na wasiwasi, tulikuwa tunajipanga maana wanasema unajikuna pale unapofikia mkono, sasa mkono tumeurefusha. Hivyo, tuna uhakika tutakapoanza mwezi huo tutafanya vizuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nataka nichukue nafasi hii kuwashukuru Wabunge Wizara yangu imechangiwa humu ndani na Wabunge 85 orodha ninayo hapa, itaingia kwenye Hansard. Wizara yangu imechangiwa kwa maandishi na Wabunge 20, majina yenu ninayo hapa yataingia kwenye Hansard. Kama nilivyosema mambo yangu yapo mengi nikasema basi ngoja niende moja kwa moja kujibu hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamechangia.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Edwin Ngonyani anasema Serikali iangalie suala la watumishi wa afya walioajiriwa kihalali na Serikali kwa mkataba, lakini sasa wanaondoshwa. Maelezo yako hivi, Katibu Mkuu Kiongozi alitoa kibali kwamba watumishi wa afya wakati wa ajira badala ya kufuata mlolongo wa kawaida wa interview na kitu gani na kitu gani na kwa sababu walikuwa wanahitajika haraka akalegeza masharti kwamba badala ya kwenda kwenye Interview sasa waandikieni barua waende moja kwa moja wakaripoti kwenye maeneo ya kazi na ndivyo ilivyofanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kuajiriwa kwa mkataba kwa mtindo ule haikuwa sababu ya wewe kutohakikiwa kama wenzio. Kwa hiyo kwenye uhakiki wapo waliobainika pamoja na kwamba walikuja na vyeti vile hospitali, walibainika kwamba walikwenda kusoma lakini hawakuwa na elimu inayotakiwa kabla ya yeye kwenda kusoma. Hao ndio ambao baadaye waliondolewa, kwa nini? Kwa sababu walikwenda kusoma wakati hawana elimu inayotosheleza wao kwenda kusoma.

Mheshimiwa Naibu Spika, nije katika masuala ya utawala bora, ndugu yangu hapa Msemaji wa Kambi ya Upinzani, hayupo lakini mtandao wake mkubwa ndugu yangu, yanga mwenzangu, alisema hivi kumeanza kujitokeza viashiri vya ubaguzi ndani nchi yetu kwa mitazamo ya itikadi ya vyama vya siasa, aidha viongozi wamekuwa wanavunja sheria kwa kutoa kauli na mtamko kinyume cha sheria. Maelezo ya Serikali yanasema hivi hakuna ushahidi uliowasilishwa kuona kuwa kuna hali ya ubaguzi kwa misingi iliyotajwa. Hata hivyo, kupitia Bunge hili naomba viongozi wa vyama vya siasa na sisi Waheshimiwa Wabunge wote tushirikiane kukemea matendo hayo yanapojitokeza. Watu wa upinzani wanataka amani, CCM wanataka amani, asiye na chama anataka amani.

Mheshimiwa Naibu Spika, rai yangu, inapotokeza dalili kama hizo tushirikiane wote kukemea, kuna mtu mwingine akikemewa na CCM na ni wa CCM atasikiliza vizuri; kuna mtu mwingine wa upande mwingine akikemewa na Waziri wa Utumishi na Utawala Bora, anaweza asimsikilize vizuri, lakini akikemewa na Kiongozi na wa chama chake atasikia. Rai yangu wote tushirikiane linapotokea jambo kama hili wote kwa pamoja tulikemee, kila moja kwa nafasi yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, amesema Msemaji wa Kambi ya Upinzani Tanzania imejitoa katika Mpango wa Uendeshaji wa Shughuli za Serikali Kwa Uwazi (Open Government Partnership) na akasema kwamba kujitoa kule kunaweza kukaathiri uendeshaji wa Serikali yetu kwa uwazi. Maelezo ya Serikali ni kwamba Open Government Partnership ilianzishwa na Rais wa Marekani Obama na Waziri Mkuu wa Uingereza, haikuwa katika nchi zote duniani, lakini sisi Afrika Tanzania tuna mpango unaofanana huu wa kuendesha Serikali kwa uwazi unaitwa African Peer Review Mechanism na tena juzi juzi hapa Tanzania sisi, Mtanzania Balozi Sefue amechaguliwa kuwa katika Bodi ya African Peer Review Mechanism mpango wa Afrika wa kujitathimini uendeshaji wa Serikali yao kwa uwazi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukaona kwamba hizi kazi zinafanana, tukaona hakuna sababu ya kuwa katika hi na ile, lakini niseme tu kwamba hata wale ambao waliingia katika hiyo Open Government Partnership nchi zingine zimeshajitia kwa mfano Urusi imejitoa, Hungary imejitoa na nchi zingine zimejitoa. Kwa hivyo maelezo ni kwamba, sisi tuliingia kwa hiari, tumetoka kwa hiari yetu wenyewe baada ya kutosheka kwamba shughuli zile zinazofanywa na African Peer Review Mechanism, Mpango wa Afrika wa Kujitathimi wenyewe katika suala la utawala bora, tukaona inatosha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nimtoe hofu Mheshimiwa kwamba asiwe na wasiwasi Tanzania bado tunaendesha Serikali kwa uwazi na ukweli na ninataka niseme mfano ipo. Zamani tulikuwa tunaletewa hapa taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Serikali, wanapelekewa Halmashauri, wanapelekewa Mawaziri wanaambiwa watekelezwe mle, lakini leo kila mwaka taarifa ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali inaletwa hadharani hapa Bungeni, inasomwa hapa Bungeni na inajadiliwa hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekaa kidogo muda mrefu katika Serikali nimewapoteza marafiki zangu wengi waliokuwa Mawaziri kutokana na ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu wa Serikali, ilijadiliwa hapa ndani Wabunge wakasema tunaomba mtupishe. Kwa hiyo hakuna mashaka juu ya Tanzania kuendesha Serikali kimya kimya, ingekuwa tunaendesha kimya kimya tusingeleta majadala kama huu ndani ya Bunge ukajadiliwa na kila mtu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kuna maoni ya Upinzani kwamba, kutokuwa na mifumo thabiti ya uratibu, ufuatiliaji na tathmini ya utendaji kazi wa kila siku ambao unatoa fursa kusomeka moja kwa moja kwenye kitengo kinachohusika na amesema hili Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni. Maelezo ya Serikali ipo mifumo ya kielektoniki ya kukusanya mapato ya Serikali kutoka katika vyanzo mbalimbali kwenda Hazina moja kwa moja, mifumo hiyo ni pamoja na Government Electronic Payment Gateway, Local Government Revenue Collection Information System na malipo ya mshahara kwa njia ya mtandao Government Sales Payment Platform (GSPF).

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo napenda kuwaambia Waheshimiwa Wabunge kuwa, utaratibu wa kuratibu, kufuatilia na kutathmini mapato na matumizi ya Serikali kwa njia ya mtandao upo, unafanya kazi na baadaye kama nilivyosema humu ndani tuna mpango baadaye wa kubadili Wakala wa Serikali Mtandao kuufanya ni Mamlaka ya Serikali Mtandao ili tunapokuja katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali kama haya pasiwe na uhiari wa mtu kujiunga au kutojiunga ili mradi ni chombo cha Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine inasema matumizi sahihi ya dola’ kumekuwepo na matumizi mengi ya wananchi kupigwa, kujeruhiwa, kufariki kwenye vituo vya polisi ikiwa ni kubambikizwa kesi na kuwaweka mahabusu kwa makusudi hata kwa kesi zinazodhaminiwa. Maelezo ya Serikali vyombo vya dola vimekuwa vinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizowekwa, aidha kuna mifumo mbalimbali iliyowekwa kwa ajili ya kuhakikisha vyombo hivyo vinatenda haki na pale panapokuwa na ukiukwaji wa sheria hatua huchukuliwa dhidi ya wanaohusika.

Mheshimiwa Naibu Spika, matukio ambayo yamebainishwa kwa mwananchi Musa Adam Said kubambikizwa kesi ya mauaji ni upungufu wa watendaji wachache tulionaona ambao wanatia doa Serikali yetu. Hata hivyo Mheshimiwa Rais ameelekeza wote waliohusika na tukio hilo wachukuliwe hatua kukomesha tabia hiyo na hatua zinaendelea kuchukuliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine inasema Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya wanapotumia mamlaka yao ya kuweka mtu mahabusu kwa saa 48 na 28, wazingatie Sheria za Tawala za Mikoa. Maelezo ya Serikali kama nilivyoeleza huko nyuma ni kweli Sheria ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ya mwaka 1997 inawapa mamlaka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kumweka mtu ndani pale inapothibitika anahatarisha amani. Naomba Waheshimiwa Wabunge wanisikilize hii sheria inavyosema, nawaomba na huko walipo wanisikilize, mtu anawekwa ndani kama amehatarisha amani, sio watu wanadaiana madeni huko huyu hataki kunilipa, unampeleka kwa Mkuu wa Wilaya au Mkuu wa Mkoa unamweka ndani. Hawa wanadaiana, hawajahatarisha amani. Sasa hilo la kwanza, mtu asiwekwe mpaka awe amehatarisha amani, aidha Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya akitekeleza sheria kinyume na utaratibu anaweza akachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na yeye mwenyewe kushtakiwa binafsi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumekemea hili jambo, tukakemea, tukakemea, Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatamtetea mtu aliyevunja sheria makusudi kumweka mtu ndani bila sababu, Wazungu wanasema unlawful confinement umeshughulika na unlawful confinement, umetumia sheria hii vibaya utapelekwa mahakamani na huyo uliyemweka ndani na Mwanasheria Mkuu wa Serikali hatakuja kukutetea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru sana Mwanasheria Mkuu wa Serikali sisi tumeeleza kisiasa, Mwanasheria wa Serikali sasa ametoa waraka kwa wale wote waliopewa mamlaka ya kumweka mtu ndani, kila mmoja ana barua ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, nami amenipa nakala ninayo. Ikieleza ni mazingira yepi mtu anaweza kukwekwa ndani na ameeleza so emphatic, moja ujiridhishe kwamba ametenda kosa jinai; pili, uhakikishe kwamba asubuhi unaweka in writing, kwa nini unamweka ndani, nami nimesema humu ndani mara nyingi government moves on paper, hawa watu wengi wanaowekwa ndani ni kauli tu weka ndani, weka ndani. Ukimwambia hebu niandikie hawataki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo sheria inasema lazima wawekwe kwa maandishi; sheria inasema asubuhi yake afikishwe mahakamani, lakini lingine nataka nimalizie kuwaomba wenzangu wenye madaraka kama haya, utawala bora unasema kesi ikiwa mahakamani DC hasikilizi, Waziri hasikilizi, Waziri Mkuu hasikilizi, sheria inasema mahakama ya chini, uamuzi wake unaweza kutenguliwa na Mahakama ya juu. Wenzangu wengine wamejiingiza kwenye katika mambo ambayo tayari yalishahukumiwa mahakamani. Acheni, acheni acheni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine, je, Serikali huwa inafanya utafiti na kuangalia athari za maamuzi inayoyafanya? Maelezo hapa ni kwamba, Serikali inafanya tathmini kwa mfano, sisi katika Baraza la Mawaziri hatuamui kuna kikao cha wataalam wanakaa, kuna kikao cha Makatibu Wakuu wote, wao wanajadili mada ile, wanatoa ushauri, unaletwa kwenye Baraza la Mawaziri, Mawaziri tunafanya maamuzi baada ya kushauriwa na wataalam. Kwa hiyo niwatoe hofu ndugu yangu Mheshimiwa Msigwa Reverend hayupo hapa, amekosa uhondo wa majibu yake maana nilimwandalia yeye. Sisi hatufanyi maamuzi bila kutafakari, tunatafakari, tunashuriwa, lakini sio hivyo tu tunashaurika. Tukishauriwa na wataalamu ndio maana tunawasikiliza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwepo na tuhuma dhidi ya usalama wa Taifa, kuratibu na kuendesha vitendo vya utesaji wa raia wasio na hatia likitolewa mfano tukio la utekwaji wa mfanyabiashara maarufu Mohamed Dewji. Mwaka jana siku nahitimisha kama leo nilikuja hapa na Sheria ya Usalama wa Taifa, nikawasomeeni, jukumu la Usalama wa Taifa ni kukusanya habari na kuishauri Serikali full stop. Mtu ameuawa ni kesi ya polisi, mtu amepotea ni kesi ya polisi, mtu ametekwa ni kesi ya polisi. Kwa hiyo nasema, katika hili jambo tumekwishalieleza, wasiipake matope Idara yetu ya Usalama wa Taifa, hawa vijana wangu wanafanya kazi nzuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitoa mfano hapa siku moja, kiongozi wa upinzani, kiongozi wa kwenye upande wa pili wa chama cha upinzani, watu walipanga kumdhuru na wenyewe wanajua. Vijana wa Idara ya Usalama wa Taifa wakamfuata wakamwambia mzee tuondoke hapa, tuondoke hawa watu hawana nia nzuri na wewe, wakamtorosha. Sasa badala ya kuwapongeza watu wanaonusuru maisha ya mtu, ndio sasa tunawapakazia, Mohamed Dewj amepotea it is a police case. Sheria ya Usalama wa Taifa mnayo nendeni mkasome, kazi yake, ni kukusanya habari na kuishauri Serikali kwisha, kila nchi utakayokwenda, utaratibu ndio huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, iwe huru na kufanya kazi bila ya kuingiliwa na mamlaka yoyote. Jambo hili liko kwa mujibu wa kifungu cha 4 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Na.11 ya mwaka 2007. Lengo kuu ni kuhakikisha kunakuwa na ustawi wa utawala bora na kuondoa rushwa nchini. Ili kutekeleza jukumu hilo, kifungu cha 5 cha Sheria iliyotajwa hapo juu imebainisha wazi kuwa taasisi hiyo iko huru na haiingiliwi na mamlaka yoyote. Kwa hiyo, napenda kuunga mkono hapa matakwa ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani kwamba taasisi iwe huru na niseme kwamba hivyo ndivyo sheria inavyosema, pale mnapoona kwamba sheria imepotoshwa ni jukumu la Mtanzania na Mbunge yeyote kuiambia Serikali kwamba hapa mmepotoka na mimi kama Waziri mwenye dhamana ya chombo tutaunda Tume, tutafuatilia na kama ikibainika kinachosemwa kipo tutachukua hatua.

Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU kufanya kazi kwa hisia bila ya kuzingatia ushahidi dhidi ya watuhumiwa. Napenda niseme, kazi ya TAKUKURU ni kukamata na kupeleleza lakini anayefanya maamuzi Mahakamani siyo TAKUKURU. Kazi ya TAKUKURU ni kupeleleza na kupeleka mashauri Mahakamani mengine moja kwa moja, mengine kupitia kwa Mkurugenzi wa Mashtaka lakini anayeamua kwamba yule mtuhumiwa ana kosa au hana kosa ni Hakimu au Jaji anayesikiliza shauri hilo. Kwa hiyo, nafasi ya kumtia mtu hatiani TAKUKURU bila ushahidi haipo.

Mheshimiwa Naibu Spika, watendaji wa TAKUKURU wasiteuliwe na Rais. Maelezo ya Serikali yako hivi, TAKUKURU wanafanya kazi kama jeshi, Rais wa nchi cheo chake kingine ni Amiri Jeshi Mkuu, watendaji wote wa vyombo vya ulinzi na usalama kwa mujibu wa sheria tulizojiwekea wanateuliwa na Rais. Endapo Bunge hili siku moja mtaamua kubadilisha sheria mkasema wawe wanateuliwa na Waziri wa Utawala Bora na ikipita mimi nitawateua. Mimi mtumishi wa Bwana, nitatenda kama Bwana anavyotaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU itupie macho Idara ya Uhamiaji na Uwekezaji kwani zimegubikwa na rushwa na urasimu unaoathiri uwekezaji. Hoja hii imetolewa na Mbunge wa Liwale ndugu yangu Mheshimiwa Kuchauka. Sisi hapa tunasema tu kwamba taarifa tumeipokea, tutaifanyia kazi ili tujiridhishe kama yaliyosemwa ni kweli au hapana.

Mheshimiwa Naibu Spika, TAKUKURU imekuwa ikiwashtaki wafanyabiashara kwa kuwabadilishia makosa yanayohusu kiasi kidogo cha fedha na kuyafanya makosa ya uhujumu uchumi. Sisi hapa tumeeleza kwamba kwa mujibu wa aya ya 21 Jedwali la Kwanza la Sheria ya Uhujumu Uchumi ya 1984 makosa yote yanayoainishwa kwenye Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa isipokuwa tu kwa kifungu 15 ni makosa ya uhujumu uchumi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu watuhumiwa kushtakiwa kwa makosa ya utakatishaji fedha ni vyema ikafahamika kuwa kifungu cha 3 cha Sheria inayokataza kutakatisha fedha Na.12/2006 kosa la rushwa ni mojawapo ya makosa yanayosababisha mtumishi kushtakiwa kwa kosa la utakatishaji fedha. Kwa hiyo, wanashtakiwa kwa mujibu wa sheria tuliyonayo. Inaweza kubadilika mpaka hapo Bunge hili litakapoamua kufanya mabadiliko. Kwa msingi huo, watuhumiwa hushtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilisema watendaji TAKUKURU wasiteuliwa na Rais. Hili nimekwishaliezea kwamba yeye ndiyo Amiri Jeshi wao Mkuu ndiye anayeteua wakuu wote wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ni ya ndugu yangu Mheshimiwa Zitto, kwa nini fedha kwa ajili ya uendeshaji wa TAKUKURU hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wakati kila mwaka wanatengewa mabilioni ya fedha na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007 inataka wakaguliwe. Kwanza, ndugu yangu Mheshimiwa Zitto, nakupongeza siku hizi umepata wanachama wapya wengi. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, maelezo hapa ndugu yangu Mheshimiwa Zitto ni kwamba fedha zinazopokelewa kwa ajili ya utendaji wa majukumu ya TAKUKURU zinajadiliwa na Bunge lako Tukufu kupitia Fungu 30 ambalo hukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali. Kwa hiyo, nikutoe mashaka ndugu yangu kwamba fedha zao zinakaguliwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja nyingine ilikuwa kwamba Wabunge wanatunga sheria ambapo zingine zinanyima haki, kuna watu wanasingiziwa kesi za money laundering. Maelezo ya Serikali hapa yanasema TAKUKURU haina mamlaka ya kisheria kuzungumzia shauri lolote ambalo liko Mahakamani. Kwa hiyo, katika suala hili hatuna maelezo zaidi ya hapo kwa sababu jambo hili lipo Mahakamani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na swali kuhusu Sekretarieti ya Maadili linasema Serikali iingize katika mtaala elimu ya maadili katika shule na vyuo ili kuwajenga watoto wetu katika masuala ya maadili na utawala bora. Suala hili limetoka kwenye Kamati yetu ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa. Maelezo ya Serikali ni kwamba mtaala wa elimu kuhusu maadili kwa shule za msingi upo na ulianza kutumika kuanzia mwaka 2017. Kwa hiyo, kwa upande wa elimu ya msingi mtaala upo na wanaendelea kufundishwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika shule za sekondari mada kuhusu maadili imejumuishwa katika somo linaloitwa general studies, zamani tukiita uraia. Hata hivyo, tumeupokea ushauri wa Kamati kwamba tuendelee kuzungumza na Wizara ya Elimu ili sasa na vyuo vikuu navyo wapate masomo haya yanayohusu uadilifu, maadili na kupambana na rushwa wanapokuwa vyuo vikuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine iliyoletwa inahusu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), inasema utambuzi wa walengwa katika maeneo ambayo ni asilimia 30 ya vijiji, mitaa shehia nchini ufanywe mapema. Maelezo ya Serikali tunasema, utambuzi wa walengwa katika maeneo ambayo hayajafikiwa katika sehemu ya kwanza ya Mpango wa Maendeleo wa Kunusuru Kaya Maskini ambapo ni vijiji 5,693 utafanyika katika sehemu ya pili ya mpango inayotarajiwa kuanza 1 Julai, 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo la Serikali ni kuzifikia kaya maskini zote tulizonazo katika nchi hii. Kama nilivyoeleza pale mwanzoni wakati naanza kuongea kwamba tuna malengo kwamba Mbunge unapata tabu jimbo ni moja kuna vijiji wamo kwenye mpango vingine hawamo. Wewe Mbunge hawakuelewi na hata sisi Mawaziri tukienda mikoani hatueleweki, inaonekana kama kuna ubaguzi wa namna fulani lakini hoja ilikuwa ni masuala ya fedha. Sasa hivi kama nilivyosema tumejiandaa ikifika tarehe 1 Julai, 2019 tunataka tuwafikie walengwa wote ambao wanastahili kusaidiwa na mfuko huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ilisema Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini unafadhiliwa na wadau wa maendeleo lakini hakuna nia ya dhati ya Serikali kusaidia kaya maskini kwa sababu kuna tofauti ya malipo kati ya walengwa waliopo Dar es Salaam na waliopo Kaliua. Jambo la kwanza nataka nilieleze Bunge lako Tukufu na sijui kwa nini hii habari imeenea hivi, fedha za TASAF ni za Serikali ya Tanzania, tumezikopa nje na zitalipwa na Serikali ya Tanzania. Kwa hiyo, maelezo kwamba TASAF inafadhiliwa na watu wa nchi za nje si kweli, fedha zile zitalipwa na Serikali yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mpango huu tulipouanza ziko nchi marafiki wakasema katika mambo Watanzania mnayoyafanya mojawapo zuri ni hili la kuhakikisha kila mtu anapata chakula, malazi, nyumba, sisi tutawaunga mkono. Kiwango walichokiunga huwezi hata mara moja ukalinganisha na kiwango ambacho Serikali yenu italipa. Kwa hiyo, naomba Waheshimiwa Wabunge, wanufaika wa TASAF nje huko, Watanzania wenzangu wote muelewe kwamba fedha ya TASAF ni fedha inayotoka katika Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais wetu Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndugu yangu Mheshimiwa Zitto alisema Serikali inaficha nini kutokana na uamuzi wa kuhamishwa Wakala wa Ndege za Serikali kutoka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwenda Ofisi ya Rais, Ikulu tarehe 23 Aprili, 2018 kupitia Tangazo la Serikali alilolita. Majibu yake Mheshimiwa Zitto yako hivi, kwa mujibu wa sheria za nchi yetu anayegawa majukumu ya kila Wizara ni Mheshimiwa Rais na inasema Rais atapanga kazi hizo kwa Wizara mbalimbali kwa jinsi atakavyoona inafaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, humu ndani hakuna Waziri aliyejipangia kazi za kufanya wote tumepangiwa na Rais. Hata hivyo, hii si mara ya kwanza, hili mbona ni jambo la kawaida. Kwa hiyo, kwa mujibu wa sheria za mgawanyo wa kazi hufanywa na Mheshimiwa Rais, sheria inasema as he may deem it fit, kwa jinsi atakavyoona yeye inafaa, siyo kwa jinsi atakavyoona Baraza la Mawaziri au jinsi atakavyoona baada ya kukaa na Abrahman na Mussa, hapana, kwa jinsi atakavyoona inafaa, nani, Rais. Ndiyo madaraka aliyotumia Rais kufanya hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nataka niseme hajafanya hivyo kwetu, kwa mfano, Tanzania Investment Centre imehamishwa kutoka Wizara ya Viwanda, Biashana na Uwekezaji imepelekwa Ofisi ya Waziri Mkuu, haikutokea hoja, limeonekana ni jambo la kawaida tu. Basi vilevile ilivyohama Tanzania Investment Centre kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kupelekwa Ofisi ya Waziri Mkuu ndivyo alivyofanya kwa Wakala wa Ndege za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi sitaki kufafanua zaidi nisije nikaharibu lakini nataka niseme hao Air Tanzania mnaotaka wakabidhiwe ndege zote nane leo leo ndiyo wametufikisha hapa nchi hii ikawa haina ndege. Sasa tumejikusuru tumenunua ndege nane, walewale ambao tayari walishatufilisi si lazima tuwe tunawaangalia kabla hatujawakabidhi kila kitu? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana Shirika la Ndege la Tanzania hizi ndege inazikodi kutoka Wakala wa Ndege za Serikali na tuna-monitor kila mwezi kuhakikisha wanalipa hela. Kwa sababu shirika lile likifilisika tena Serikali yenu ndiyo itabeba lawama hapa, mlitafuta hela, mkanunua ndege, mkawapa wabadhirifu walewale, limefilisika tena, mimi nitakuwa mgeni wa nani tena Air Tanzania ikifilisika? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana tunasimamia ili kuhakikisha kwamba tunakwenda vizuri kibiashara na ili tusilalamike tena kwa sababu watu wengi wamefurahi sana. Nilikwenda kwenu kule ndugu yangu Mheshimiwa Zitto kutembelea Kasulu na sehemu nyingine kwa kutumia ndege hizi mpya. Miaka ya nyuma kabla ya hapo nilikuwa nakwenda na gari, mara ya mwisho nilipokuwa Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nilikwenda kwa gari nikitokea Dodoma mpaka Kaliua, ukitoka Kaliua pale pori fulani hivi mnapita, ukiharibikiwa na gari ni wewe na Mungu wako. Juzi naambiwa Mheshimiwa Waziri kwa niaba ya Shirika la Ndege la Tanzania, safari yetu kwenda Kigoma itatuchukua muda wa saa mbili, nikapewa na peremende na soda, baada ya saa mbili niko Kigoma. Mwenyewe Mheshimiwa Zitto huyu wala haji kwa gari siku hizi, wapongeze Air Tanzania. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja kuhusu Wizara yangu ni nyingi sana, nisingependa kupoteza muda wenu, tumeandaa majibu yote, tukishamaliza kikao hiki cha Bunge tutatengeneza kitabu, tulichagua tu maeneo fulani tuyasemee lakini kwa yale maeneo ambayo mmeona hatukusema siyo kwamba hatuna majibu, majibu tunayo tutayaweka katika kitabu na tutawapatia. Nataka nichukue nafasi hii tena kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa ushirikiano mliotupa Wizara yetu. Tumeweza kufanya haya kwa sababu Kamati yetu ya Utawala na Serikali za Mitaa ililiomba Bunge litupitishie makisio, mkatupitishia na leo tumekuja hapa kuomba mtuwezeshe tena ili tuweze kutekeleza majukumu tuliyokabidhiwa na Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.