Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

Hon. Selemani Said Jafo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kisarawe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2019/2020

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, napenda sana kumshukuru Mwenyezi Mungu, muumba mbingu na ardhi kwa kuniwezesha kutoa hoja yangu hapa Bungeni ya hotuba ya Bajeti Ofisi ya Rais (TAMISEMI) kwa mwaka 2019/2020.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kuchukua fursa hii kukupongeza wewe Naibu Spika lakini kumpongeza Spika wetu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai kwa kazi kubwa mnayofanya. Pia niwashukuru sana Wenyeviti wote wa Kamati za Bunge kwa weledi, ufanisi na kwa kazi kubwa waliyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi kwa nafsi ya moyo wangu napenda sana kumshukuru Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani yake kubwa kwangu kunipa Wizara hii kubwa ambayo bajeti yake ni zaidi ya asilimia 18 ya bajeti yote ya nchi, Mheshimiwa Rais nakushukuru sana. Nimshukuru Makamu wa Rais, mama yetu Samia Suluhu Hassan, halikadhalika nimshukuru Waziri wetu Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa Majaliwa kwa uongozi wake mahiri sana ambao unatuwezesha kufanya kazi zetu kama Mawaziri ambapo yeye anatengeneza timu hiyo kama kiongozi wetu hapa hapa Bungeni na Serikali kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nimshukuru sana Mwenyekiti wetu wa Kamati, Mheshimiwa Jasson Samson Rweikiza, Mbunge wa Bukoba Vijijini kwa uongozi wake mahiri akisaidiwa na Mheshimiwa mama Mwanne Mchemba, Makamu Mwenyekiti, Mbunge wa Viti Maalum kutoka Mkoa wa Tabora kwa watani wangu Wanyamwezi, nawashukuru sana. Pia naishukuru sana Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na TAMISEMI kwa kazi kubwa waliyofanya katika kipindi hiki chote wakati tunaendelea na mchakato huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Capt. Mkuchika, Waziri pacha mwenzangu katika Ofisi ya Rais, kwa ushirikiano mkubwa aliotupatia. Vilevile niwashukuru Naibu Mawaziri wangu; Mheshimiwa Joseph Kandege na Mheshimiwa Mwita Waitara kwa ushirikiano mkubwa walionipatia. Pia nimshukuru Katibu Mkuu wangu Engineer Nyamhanga na Naibu Makatibu Wakuu wote Tixson Nzunda na dada yangu Dorothy Gwajima. Niwashukuru sana watendaji wote wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwa ushirikiano mkubwa na dada yangu Mheshimiwa Dkt. Mary Mwanjelwa, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nichukue nafasi hii kumshukuru Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango lakini Ndugu yangu Dotto James kwa ushirikiano mkubwa sana waliotupatia katika utekelezaji ya bajeti ya mwaka 2018/2019 na katika mpango wetu wa bajeti ya mwaka 2019/2020. Kwa hakika sisi tumejivunia, kwa kweli kazi imeenda vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika jedwali tulilowasilisha hapa, napenda kufanya marekebisho kidogo katika kiambatanisho katika ukurasa 158 hadi 159 kinachohusu ujenzi wa vituo vya afya 52 katika mwaka wa fedha 2019/2020 kama ifuatavyo: Kituo cha Mapera katika Halmashauri ya Mbinga kihamishiwe katika Kituo cha Afya Nangirikiri na Kituo cha Afya cha Kabwe kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi kihamishiwe kwenda Kituo cha Afya cha Ninde katika Halmashauri hiyohiyo ya Nkasi. Halikadhalika katika Halmashauri ya Wilaya ya Njombe, Kituo cha Afya cha Ikuna kihamishiwe kwenda Kituo cha Afya cha Kichiwa na katika Halmashauri ya Kasulu TC, Kituo cha Afya Kigadye kiende Heri Juu katika Halmshauri ya Kasulu Mji.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia Fungu 56 - Ofisi ya Rais, TAMISEMI limeongezewa shilingi bilioni 33 kwa ajili ya ujenzi wa barabara ambayo inaenda TARURA. Baada ya kusikiliza kilio cha Wabunge humu ndani, Serikali imeona vyema iongeze takribani shilingi bilioni 33 ambayo kwa kiwango kikubwa inaenda kutatua matatizo ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kutokana na hali hiyo, kuna baadhi ya mafungu katika Fungu 56 yatakuwa na mabadiliko. Kwa mfano, kutasomeka shilingi 496,563,123,910 katika Fungu la Maendeleo badala ya shilingi 463,563,123,910. Hivyo, kufanya Fungu 56 katika Miradi ya Maendeleo na Matumizi ya Kawaida kuwa na shilingi 550,200,093,910. Kwa maana hiyo, bajeti nzima ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI itakuwa na jumla ya shilingi 6,240,992,779,769. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya marekebisho hayo, sasa naomba kuwatambua Waheshimiwa Wabunge 130 waliochangia bajeti ya Ofisi ya Rais, TAMISEMI; wakiwemo Wabunge 86 waliochangia kwa kuzungumza na Wabunge 44 walichangia kwa maandishi. Naomba niwashukuru sana kwamba hoja yangu imechangiwa na Wabunge wengi na hii inanipa ishara kwamba Ofisi ya Rais, TAMISEMI ni eneo ambalo tunapata huduma kwa ujumla wake. Kutokana na maelezo yetu ya kikanuni, naomba majina hayo nisiyasome ila naomba yote yatambuliwe katika Hansard za Bunge kama Waheshimiwa Wabunge walivyochangia kuhakikisha kwamba Ofisi hii inatekeleza vizuri wajibu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hakika Ofisi yetu ilikumbana na hoja nyingi lakini hoja hizo zimegawanyika katika maeneo yafuatayo: Posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji; kujenga uwezo wa Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa; uchaguzi wa Serikali za Mitaa; mgawanyo wa fedha wa Mfuko wa Barabara zilizotengwa kwenda kwenye Halmashauri (TARURA); ushiriki wa wadau; utekelezaji wa Mradi ya Mabasi yaendayo Haraka lakini ujenzi na ukarabati wa hospitali za halmashauri pamoja na vituo vya afya na zahanati; ununuzi wa vifaa tiba katika hospitali zetu na vituo vya afya; miundombinu ya elimu; ajira za walimu wetu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa; vyanzo vya mapato vya Halmashauri na maeneo mengine kadhaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, binafsi nishukuru sana michango katika maeneo hayo yote lakini niwashukuru sana Naibu Mawaziri wangu asubuhi waliweza kujibu baadhi ya hoja na wamezitendea haki sana. Niwashukuru sana wapiganaji hawa mahiri sana hasa ndugu yangu Mheshimiwa Waitara na Ndugu yangu Mheshimiwa Kandege, kwa kweli wamefanya kazi kubwa sana. Kwa hiyo, mimi nitaenda kimuktadha, kwa upana mkubwa tu wa Ofisi hii jinsi gani inafanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo ambalo limezungumzwa ni suala la vitambulisho vya wajasiriamali, kwanza nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa nia yake njema kwa wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwa wakitaabika ambapo sehemu nyingine walikuwa wanakamatwa na Mgambo, wanapigwa virungu na kunyang’anywa vyakula vyao, hali yao ilikuwa ni taabani. Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa maono yake ya kuwajali Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili nimesikia hoja za Wabunge mbalimbali wakisema kwamba inawezekana nia ikawa ni njema lakini utaratibu uliotumika siyo sawasawa. Kwa upande wangu kazi yetu ni kuchukua maoni ya Wabunge baadaye kwenda kuyafanyia kazi jambo ambalo halijakaa vizuri. Lengo ni kwenda kulirekebisha na hasa kuangalia vitambulisho hivi vinatolewa kwa akina nani. Lengo ni kwa wale ambao hawako katika sehemu rasmi sasa wanarasimishwa ili nao waweze kushiriki katika uchumi na mwisho wa siku waweze kupata kipato chao kwa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme eneo hilo inawezekana kweli kuna upungufu lakini hili jambo linatofautiana kutoka eneo moja na lingine. Kwa mfano, ukiangalia maeneo ya Dar es Salaam na maeneo ya miji mara nyingi sana hata kama kuna changamoto siyo kubwa sana. Hata hivyo, tumechukua maoni na ushauri wote wa Waheshimiwa Wabunge ili tukaangalie jinsi ya kuboresha jambo hili ambalo nia yake ni njema lakini lifanyike kwa uzuri zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala zima la posho za Madiwani, Wenyeviti wa Vijiji na Vitongoji. Naomba nikiri kwamba Wabunge wengi walichangia hapa na Mwenyekiti wetu wa Kamati ya Bunge na Kamati yake walianza kuchangia kuanzia kwenye Kamati na hapa Bungeni. Vilevile Wabunge mbalimbali walichangia hoja, nawashukuru sana. Hoja hii ilipata michango mingi kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Niseme wazi kwamba jambo hili inaonekana lina interest kwa Wabunge wote kuona ni jinsi gani tutaangalia suala za posho za Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikiri wazi kwamba Madiwani wanafanya kazi kubwa sana, tunapopeleka fedha kule Madiwani kwa kweli wanasimamia kwa karibu zaidi. Hata posho yao kama nilivyosema iliongezwa awali lakini Wabunge wamesema kuna haja ya ku-review hizi posho. Kwa hali ya sasa kwa sababu tunaangalia muktadha wote nini kifanyike, kwa ujumla niseme kwamba tumelichukua wazo hili kwenda kulitafakari zaidi ni jinsi gani tutafanya hawa Waheshimiwa Madiwani kwa siku za usoni angalau kile kipato chao kiweze kuongezeka kwa sababu wanafanya kazi kubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna jambo ambalo limeonekana ni tete nalo ni la mwongozo wa utoaji wa posho imeonekana kwamba umekuwa ni changamoto kubwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Ofisi yangu imejipanga tutaenda ku-review tena ule mwongozo vizuri na haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lengo kubwa ni tuweze kubainisha wapi Diwani anatoka kwa mfano ukienda Jimbo la Mbinga kule Diwani mwingine anatoka kama mwezi anakwenda kwene mkutano atafanyaje na maudhui ya kazi wanayofanya. Kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba jambo hili mimi na wataalam wangu tutali-review vizuri ili Madiwani wetu wasiwe na kinyongo katika utendaji wao wa kazi ili kazi ziweze kufanyika vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine lilikuwa ni uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Kama mnavyofahamu mwaka huu tunatarajia kwenda kufanya uchaguzi wa Serikali za Mitaa na uchaguzi huu unaongozwa na Katiba yetu, Ibara 144 na 146 imezipa mamlaka Serikali za Mitaa lakini zikatungwa sheria zetu, Sura Na. 287 na 288 ambapo huko tumeenda kuhakikisha uchaguzi huo unasimamiwa katika mamlaka ya Serikali za Mitaa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza uchaguzi huu unaandaliwa na kanuni, tumeanza kuandaa kanuni,wataalam waliandaa zile kanuni kwa kina na umahiri wa hali ya juu. Pia tuliweza kuwashirikisha wadau mbalimbali kama Wakurugenzi wote wa Halmashauri; Wakuu wa Wilaya; Maafisa; Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakuu wa Mikoa. Pia tukapanua goli zaidi ikaenda kwa wadau wa kisiasa, tukaenda kufanya mkutano wa siku mbili, tarehe 1 mpaka tarehe 2 kuhakikisha kwamba vyama vya siasa vyenye usajili vinashiriki kutoa maoni yao katika rasimu hii ya kanuni. Naomba nikuhakikishie, mkutano wetu na vyama vya siasa ulikuwa mzuri sana na wadau walishiriki vizuri sana katika kuhakikisha kanuni hizi wanaziboresha na kutoa mapendekezo. Sasa jambo hili lipo katika hatua ya mwisho ya ku-accommodate yale maoni ili kuhakikisha kanuni hizi zinafanya na baadaye kwenda kuzitangaza katika Gazeti la Serikali. Tunatarajia mwishoni mwa mwaka huu tutaenda kufanya uchaguzi wetu, matarajio yetu ni Novemba 2019.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ni suala nzima la utoaji wa mikopo. Nishukuru Naibu Mawaziri wangu wamelizungumzia, ni kweli utoaji wa mikopo umekuwa na changamoto kubwa sana hasa mikopo ya asilimia 10 ya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu. Nilishukuru Bunge hili, katika Finance Bill iliyopita wajumbe hawa walifanya marekebisho ya sheria na ilielekeza mikopo hiyo sasa itolewe kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona kwamba hapa mwanzoni mikopo ilikuwa inasuasua sana lakini naomba nisiwe mchoyo wa fadhila niishukuru sana Kamati ya Bunge la TAMISEMI na Utawala Bora ilivyokutana na mikoa yote kupitisha bajeti ilikuwa ni hoja mahsusi sana na ilijadiliwa kwa kina zaidi. Naomba nitoe taarifa kwa Waheshimiwa Wabunge ndani ya siku hizi chache za wiki mbili baada ya maelekezo yenu, mwanzo zilikuwa zimetoka karibu shilingi bilioni 13 peke yake leo hii napozungumza mpaka tarehe 30 Machi, zimetoka takribani shilingi bilioni 20.7, haijawahi kutokea ndani ya kipindi kifupi ambayo ni utekelezaji wa lengo takribani asilimia 38.7.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikujulishe wazi kwamba tulipaswa Ofisi yetu itoe kanuni na kanuni hizo zimeshatoka na zimetoa maelekezo na zimeshatangazwa katika Gazeti la Serikali, hivi sasa ni kwamba ma-accounting officer ambapo Wakurugenzi wetu wa Halmashauri wanawajibu wa ku-comply na kanuni zilizotoka. Waliokuwa wanafuatialia vyombo vya habari siku ya Ijumaa asubuhi nilitoa taarifa kwa Wakurugenzi wote wa Halmashauri wahakikishe ile mikopo yote itakapofika tarehe 28 Juni, takribani asilimia 83.3 ya mikopo ya vijana, akina mama na watu wenye ulemavu lazima yote iweze kutoka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nini asilimia 83? Ni kwa sababu mwezi Juni wanakuwa bado hawajafunga mahesabu na ndiyo maana nimesema ikifika tarehe 20 Julai, bajeti ya mwaka wa fedha 2018/2019 mikopo hiyo inatakiwa itoke kwa asilimia 100. Kanuni ambazo tumezitoa zimewabana ma-Accounting Officer wale watakaoshindwa kupeleka mikopo hiyo kuna utaratibu wa kisheria ambao utaenda kuchukuliwa dhidi yao.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naamini si rahisi kwamba kuna Mkurugenzi ambaye anataka kuingia kikaangoni kwa makusudi kwa kushindwa kutoa mikopo hii ya asilimia 10 ambayo ipo kwa mujibu wa sheria. Naomba nikuhakikishie katika jambo hili tutakuwa wakali sana, hatuna masihara kwa sababu hii ni haki ya vijana ambao wengi wao wamemaliza vyuo vikuu na wamekosa ajira, huu ni mlango mwingine mbadala wa vijana kujiingiza katika suala zima la ajira kuhakikisha wanaenda kujenga uchumi wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo limezungumzwa sana humu ndani na nishukuru sana karibuni Wabunge wote walizungumza ni suala zima la elimu. Tunambiwa kwamba nchi zimegawanyika, kuna nchi zenye rasilimali mbalimbali na nyingine ni masikini zaidi lakini kuna nchi zimewekeza katika elimu. Ndiyo maana leo kuna mifano ya dhahiri kabisa, kuna nchi duniani mfano Switzerland na Nordic Countries ukiangalia rasilimali walizonazo ni chache lakini sasa hivi ndiyo watu ambao wanatawala dunia kiuchumi, ni kwa sababu wamewekeza katika maarifa ya watu. Ndiyo maana binafsi na Ofisi yangu inamshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli kwa programu ya Elimu bila Malipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kipindi hiki tokea Serikali ya Awamu ya Tano na Mheshimiwa Rais kuelekeza sasa wananchi wa Tanzania wapate elimu bila malipo, upande wa elimu ya msingi peke yake zaidi ya shilingi bilioni 374.3 zimetoka kusaidia elimu msingi bila malipo. Kwa upande wa sekondari zaidi ya shilingi bilioni 479.9 zimetoka kwa ajili ys elimu bila malipo. Jumla kuu ni zaidi ya shilingi bilioni 854.3 ambapo ni fedha nyingi haijawahi kutokea.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili tukiri wazi watoto wa maskini na voiceless people wamepata msaada mkubwa sana. Tunaona shule zingine zinafurika ni kwa sababu watoto hawa wa maskini zamani walikuwa wanakosa elimu leo dirisha limefunguliwa, kipa katoka, sasa watu wanapata fursa ya kupata elimu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie miaka ijayo dirisha la kuhakikisha tunajenga uchumi kwa pamoja itakuwa siyo kwa watu wenye uwezo peke yake bali na watoto wa maskini waliofunguliwa dirisha hili sasa tunasema tutajuwana mbele ya safari. Mheshimiwa Rais amenipa wajibu wa kulisimamia eneo hili, kwa kweli tunamshukuru sana kwa programu ya elimu bila malipo ameitendea haki nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni suala la ajira ambalo limezungumziwa na wajumbe mbalimbali. Naomba niseme, Serikali ya Awamu ya Tano kwa lengo la kuangalia changamoto iliyojitokeza mpaka sasa zaidi ya walimu 13,632 waliajiriwa na kuripoti katika shule zetu za msingi na sekondari lakini si muda mrefu tutatoa ajira zingine zaidi ya 4,549 ambazo ziko katika hatua ya mwisho kabisa ambapo tumeshatangaza na watu wameshaomba ambapo jumla ya walimu watakaoingia katika soko la ajira watakuwa ni 18,181. Hii inaonyesha commitment Serikali iliyonayo katika suala hili la ajira na lengo ni kuongeza idadi ya walimu. Naomba nikiri wazi kwamba tutaendelea kuongeza idadi ya walimu ili watoto wetu katika shule zetu waweze kupata elimu bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, hapa juzi juzi aliweza kutoa takriban shilingi bilioni 29.9 kwa lengo la kwenda kumalizia maboma. Waheshimiwa Wabunge hawa ni mashahidi, maboma zaidi ya 3,200 yote yameenda kumaliziwa ukarabati. Siyo hivyo tu, mwezi wa Pili Mheshimiwa Rais ametoa zaidi ya shilingi bilioni 56 hapa. Serikali imetoa fedha hizo, ambapo ukija kuangalia lengo lake ni kwenda kujenga madarasa mapya 934 kwa ajili ya kuongeza madarasa. Vile vile kujenga mabweni mapya 210 ili kuhakikisha kwamba watoto wakiingia Kidato cha Tano waweze kupata mazingira mazuri ya kusomea.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunaenda kujenga matundu ya vyoo yapatayo 2,141. Hiki ni kipindi tunatarajia kabla ya mwezi wa Sita kazi zote ziwe zimekamilika. Vile vile tutajenga nyumba za walimu, hali kadhalika tunajenga mabwalo yapatayo 76 katika shule zetu. Hii yote ni kazi kubwa kwa lengo kubwa la kuhakikisha kwamba elimu inasonga mbele.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikujulishe, tayari zimeshatoka shilingi bilioni 16 kwa ajili ya kununua vifaa vya zaidi ya maabara 1,280. Hii ni kazi kubwa. Lengo letu kubwa ni kwamba maabara hizi nazo ziweze kufanya vizuri sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, suala la ununuzi wa magari, takribani magari 26 kwa Maafisa Elimu Mikoa, manunuzi yameshafanyika na wiki tatu zilizopita nilitoa siku tisini nataka nione mikoa yote imeshapata magari. Lengo kubwa ni Maafisa wetu wa Elimu waweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo katika hotuba yangu nilizungumza wazi kwamba investment kubwa inaenda kufanyika hivi sasa katika suala zima la ujenzi wa miundombinu. Kwa mfano, kupitia mpango wa EP4R zaidi ya madarasa 1,200 tunaenda kuyajenga, zaidi ya matundu ya vyoo 3,000 yatajengwa na zaidi ya mabweni mengine ya ziada 300 yatajengwa, zaidi ya vyumba vya madarasa vingine vipatavyo 1,500 vingine mbadala, halikadhalika tutajenga nyumba za walimu na mambo mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie kwamba Serikali hii ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli, imejipanga kuhakikisha kwamba tunaenda kushughulikia changamoto ya kielimu na lengo letu kubwa ni kwamba Serikali inavyojielekeza kwenda katika uchumi wa kati lazima tujiwekeze vizuri katika suala zima la elimu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge, Serikali haijalala, inafanya kazi usiku na mchana. Hata hivyo niwahakikishie, mmeona jinsi gani tumefanya mabadiliko makubwa katika ujenzi wa miundombinu katika shule zetu kongwe. Tumemaliza awamu ya kwanza shule 48 ambapo sasa hivi tunaendelea na shule 25 na bajeti ya sasa hivi ina shule 15. Lengo kubwa ni nini? Shule zetu sasa zirudi katika hadhi yake ya kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge hawa ni mashahidi, hata walipokuja hapa kuapishwa, wakati Mheshimiwa Rais alipokuja kuzindua Bunge hili, shule hata ya Dodoma Sekondari haikuwa hivi. Nenda hapo Dodoma, nenda Bihawana, Kondoa, Mpwapwa, Moshi Tech, Mtwara Tech kokote unakokwenda miundombinu imeboreka kwa kiwango kikubwa. Hii ni ajenda ya Serikali ya Awamu ya Tano. Lengo kubwa, shule zote kongwe zirudi katika ubora wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nimesema shule hizi leo hii naomba na Waheshimiwa Wabunge tembeleeni maeneo yenu mkaone maajabu. Hata wale wa Dar es Salaam, nendeni Pugu Sekondari pale, nendeni Jangwani Sekondari pale, mtakuta maajabu makubwa yamefanywa ndani ya Serikali hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, nimesema bajeti hii ya kwangu sasa hivi ambayo nime-present hapa tunaenda kuboresha shule nyingine 15. Imani yetu ni nini? Tunataka shule zote ambazo zamani zilikuwa maarufu, lazima zirudi katika utaratibu wake ule ili Watanzania waweze kusoma vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ajenda nyingine ambayo kwa kiwango kikubwa imejadiliwa hapa, ni suala zima la ujenzi wa miundombinu ya afya. Namshukuru sana Naibu wangu, amezungumza kwa kina katika eneo hili la afya.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa dhati ya moyo wangu, naomba sana nilishukuru Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sana tu. Waheshimiwa Wabunge ninyi mnaingia katika historia ya mpya. Nchi yetu ilikuwa na changamoto kubwa sana katika Sekta ya Afya. Siku zote huwa nazungumza, toka Uhuru mpaka Serikali ya Awamu ya Tano tulikuwa na Hospitali za Wilaya 77 peke yake. Vituo vya afya vilivyokuwa na uwezo wa kufanya huduma ya upasuaji, vilikuwa 118 peke yake. Ninyi Waheshimiwa Wabunge mmeingia katika historia, ndani ya kipindi kifupi, vituo vya afya 352 vimeboreshwa, haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, juzi mmemwona Mheshimiwa Rais alivyokuwa Mikoa ya Mtwara na Ruvuma alituzindulia vituo vya afya kule; vya Mbonde, pale Masasi na Kituo cha Afya cha pale Madaba. Hii ni kazi kubwa, haijawahi kutokea. Naomba nirudishe heshima hii kwa Waheshimiwa Wabunge, msingekubali bajeti, vituo hivi visingepita. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika watu nchi hii wataingia katika historia ni Wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bunge la Kumi na Moja, litaingia katika historia. Pia hamkuwa watu wenye hiana, mwaka 2018 nilileta bajeti hapa kuomba tujenge hospitali mpya 67, ninyi Wabunge mliridhia ikapita shilingi bilioni 100.5 na ujenzi unaendelea huko makwenu. Hii haijawahi kutokea na ujenzi huo unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimewapa deadline, yale majengo saba, tarehe 30 mwezi Juni, nataka nione majengo yote yamesimama vizuri. Nilisema mwaka 2018, majengo yale ni kingiambago tu, yaani ni kianzio. Mwaka huu ndiyo maana katika majengo yale yale, Serikali imetenga fedha nyingine kwa ajili ya kuendelea kujenga majengo hayo. Vijana wa Tandale wanasema kampa, kampa tena. Mwanzo mmepata na mwaka huu mmepata tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, Bunge hili limekuja na vituo vingine vya afya na hospitali nyingine za Wilaya 27. Kwa interest ya Bunge hili naomba nivitaje; tunaenda kujenga Hospitali ya Wilaya ya Chalinze, Hospitali ya Wilaya ya Kondoa, tunaenda kuimarisha Hospitali ya Wilaya pale Kongwa, Hospitali ya Wilaya ya Mbogwe, Hospitali ya Wilaya ya Biharamulo, Hospitali ya Wilaya ya Msimbo, Hospitali ya Wilaya ya Kakonko, Hospitali ya Wilaya ya Liwale, Hospitali ya Wilaya ya Babati DC, Hospitali ya Wilaya ya Sengerema kwa watani wangu Wasukuma, Hospitali ya Wilaya ya Mbeya, Hospitali ya Wilaya ya Kilombero, Hospitali ya Wilaya ya Newala, Hospitali ya Wilaya Kwimba, Hospitali ya Wilaya ya Sengerema, Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Sumbawanga. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile, tunaenda kujenga Hospitali ya Wilaya ya Madaba, Hospitali ya Wilaya ya Msalala, Hospitali ya Wilaya ya Ikungi, Hospitali ya Wilaya ya Tunduma, Hospitali ya Wilaya ya Manispaa ya Tabora, Kaliua, Handeni, Mkinga; jamani mnataka nini? (Vigelegele/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana rafiki yangu Mheshimiwa Mwakajoka siku ile alipokuwa anachangia nikasema, Mwakajoka shukuru basi.

NAIBU SPIKA: Nadhani atakuwa ana ndiyo yako leo huyu. (Kicheko)

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, haitoshi. Lengo letu ni kuhakikisha tunaboresha mazingira haya. Ndugu zangu, sisi tumepewa dhamana kama viongozi. Tutakuja kuulizwa kwa hizi dhamana tulizopewa. Niwaombe sana Waheshimiwa Wabunge, hata hao wanaosema hapana, siyo mbaya, kwa sababu tunakubali wote bajeti hii kwa pamoja. Hii ni bajeti ya kwenda kuwasaidia wananchi wetu siyo jambo lingine. Bajeti ya watu wasiokuwa na sauti (a voiceless people) bajeti yao ndiyo hii hapa hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na jambo la ajenda hapa ya suala zima la ujenzi wa miundombinu. Naishukuru sana Kamati ya Bunge ya TAMISEMI na Utawala Bora, lakini nawashukuru Wabunge, kwa kazi kubwa inayoendelea kufanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wanavyosimamia miradi kule site. TAMISEMI sisi tunasimamia miradi katika maeneo makubwa manne; kuna miradi hii ya TARURA kwa ujumla wake, lakini kuna miradi inayoboresha Jiji la Dar es Salaam, DMDP ambayo thamani yake ni shilingi bilioni 660.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia tuna miradi ya TSP ambayo ukienda Mbeya unaikuta, Arusha utaikuta, Mwanza utaikuta, Ilemela, ukija Dodoma hapa unaikuta, ukienda Mikindani unaikuta na ukienda hata kwa ndugu yangu Mheshimiwa Zitto Kabwe pale Kigoma Ujiji utaikuta. Lengo la miradi hii ni kuimarisha miundombinu ya barabara. Tunajenga barabara za lami kuweka taa na madampo ya kisasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna miradi katika Halmashauri zote za Miji, ndiyo maana leo mnamwona Mheshimiwa Mwanri anasema, ukifika Tabora ni kama umefika Toronto. Hii ni kazi kubwa iliyofanyika. Tunaimarisha Halmashauri zote za Miji na Manispaa. Ndiyo maana leo ukienda Bariadi, mji ni tofauti, Musoma, Tabora, Morogoro, Iringa, Sumbawanga, Mpanda, Korogwe, Moshi, miji ni tofauti. Hii ni kazi inayofanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo, mwaka huu tutaendelea tena kujenga ujenzi wa madaraja katika maeneo mbalimbali. Nashukuru sana, baada ya kilio cha Waheshimiwa Wabunge tena, zaidi ya shilingi bilioni 33 imeongezeka; hii ni faraja kubwa sana. Nina imani jambo hili linaenda kutatua changamoto zetu katika mamlaka ya Serikali katika Serikali za Mitaa, katika ujenzi wa miundombinu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikuhakikishie zaidi ya madaraja 113 mwaka huu ambayo tunatarajia kuyajenga chini ya TARURA. Pia kuna makalavati makubwa zaidi ya 273 tutayajenga; na makaravati madogo zaidi ya 2,403 yote tunaenda kuyajenga. Hiyo ni ukiachia mifereji.

Mheshimiwa Naibu Spika, kazi kubwa inaenda kufanyika katika Jiji la Dar es Salaam. Niwashukuru sana Wajumbe wa Kamati ya TAMISEMI walivyoenda kutembelea miradi ya DMDP pale Dar es Salaam, waliona maajabu makubwa katika maeneo ambayo mwanzo yalikuwa yamejishika. Mpaka kaka yangu Mheshimiwa Selasini alipofika pale eneo la Tuangoma alishangaa kuona hawa watu wa Mbagala Kuu na Kijichi walivyounganishwa na watu wa Kibada kwa barabara ya mfano haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nenda Kijichi pale, tembelea hali ni tofauti, nenda Mbagala Kuu, hali tofauti; maeneo ya Makumbusho hali ni tofauti, maeneo ya viwandani hali ni tofauti. Hii kazi lengo lake ni kwenda kubabilisha Jiji la Dar es Salaam. (Makofi)

Ndugu zangu, naomba niwaambie, tutaendelea kuimarisha ujenzi wa vituo vya mabasi. Najua tulimaliza kule Korogwe, tumemaliza pale Songea, juzi juzi tumepita Songea lakini tunaimarisha kutokea Songea na maeneo mengine. Lengo letu ni kwamba madampo ya kisasa, magari ya kuzolea taka, lakini kila eneo lazima tuliimarishe.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine tunaloenda kulifanyia kazi, ni suala zima la ujenzi wa masoko. Ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge, mwaka 2018 niliomba bajeti hapa; ujenzi wa Stendi ya Dodoma, halikadhalika ujenzi wa Soko Kubwa la Dodoma. Wengine walikuwa wananiambia, hii Jafo Power Point Presentation ni kanyaboya? Nikawambia mtaona vitu.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo Waheshimiwa Wabunge ni mashahidi, mnapoenda pale Nane Nane mnakuta stendi ya kisasa na soko la Kisasa linajengwa. Jukumu letu kubwa ni nini? Ni kuhakikisha tunabadilisha miundombinu yetu yote, wananchi wapate faraja kwa utendaji wa umakini wa utekelezaji wa Ilani ya Chama cha Mapinduzi chini ya Serikali ya Awamu ya Tano. Katika hili mimi sina hiana, ninafahamu wazi Waheshimiwa Wabunge tutaendelea kushirikiana vya kutosha kuhakikisha miradi hii yote inaenda kufanyika kwa kiwango kikubwa sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiachia na mambo mengine yote kwa ujumla wake na hasa niwaombe Waheshimiwa Wabunge, ofisi yangu ina watu wengi, kuna suala zima la mahusiano, mkubwa wangu Mheshimiwa Mkuchika hapa atakuja na suala zima la utawala bora; hata hivyo, tunaendelea kutoa mafunzo mbalimbali kwa viongozi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nanyi mnafahamu hali tuliyotoka mwanzo na sasa hivi ni tofauti sana. Mwanzo tulikotoka hali ilikuwa siyo shwari sana, lakini baada ya mafunzo mbalimbali ambayo kupitia Chuo cha Uongozi, mnaona kidogo kwa kiwango kikubwa kama tuna changamoto ambazo tunaweza tukazitaja eneo kwa eneo, lakini kwa kiwango kikubwa sasa hivi kazi inaenda vizuri. Hata hivyo, tutaendelea kuimarisha suala zima la mafunzo na program mbalimbali kwa lengo la kujengeana uwezo.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata hivyo tufahamu kwamba watu wengine hawa ni vijana zaidi, sawa eeh, kwa hiyo, lazima kidogo kuna vitu vingine lazima training, tuwe tunapeana mawazo ili kuhakikisha kwamba mambo yanaenda vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaombe Waheshimiwa Wabunge jamani, msiwanyong’onyeshe watu wanaofanya kazi. Naomba niwaambie, katika ofisi ambayo hailali ni ofisi yangu. Hawa Manaibu wangu, mwangalie Mheshimiwa Waitara huyu, toka ateuliwe hajapumzika. Mwangalie Mheshimiwa Kandege, wanahangaika. Nimewaelekeza wafike kwenu wawasikilize waangalie changamoto. Sasa ikitokea Mbunge hapa anakuja anasema hakuna lolote, inawanyong’onyeza sana hata watendaji wetu. Tufikie wakati angalau tushukuru kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna maeneo mengine sitaki kusema tu, kaka yangu hapa alisema sijui TAMISEMI nini, ovyo kabisa. Jamani! Kulikuwa hakuna hospitali ya Wilaya kule, vituo vya afya vitatu vimeenda. Acha ukarabati wa shule na vitu mbalimbali watu wanafanya wanahangaika. Kama kuna magomvi tunashughulikia magomvi kwa magomvi, lakini sio kama unawavunja nguvu watendaji. Afadhali mimi! Mimi nina moyo mgumu, sina shida. Ila mnawapa stress watendaji wangu, hawa wasaidizi wangu. Kusema hakuna kitu TAMISEMI, jamani hii kazi yote kubwa inayofanyika. Watu hawalali kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania. Tu- appreciate kidogo jamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo maana nasema, mimi nina moyo mgumu, sina shida, lakini Serikali inafanya kazi kweli kweli. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli, naomba niwaambie, hii ni legacy anaiweka, itadumu kwa miaka mingi. Hata kama mtu hupendi lakini legacy ipo. Haya mambo yote kwa uchache niliyowaelezea, siyo haba, shughuli nzito imefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hii kazi, naomba sana nimshukuru Waziri Mkuu wetu. Waziri Mkuu wetu halali, hapumziki. Wanaopitia vyombo mbalimbali, kila siku Waziri Mkuu yuko katika assignment. Lengo kubwa ni kwamba imani waliyotoa Watanzania kwa Serikali yao ya Awamu ya Tano mambo yaende vizuri, Waziri Mkuu hapumziki. Ningekuwa katika mikutano ya kisiasa ningesema pigeni makofi kwa Waziri Mkuu kidogo. (Makofi/Vigelegele)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunasema mnyonge mnyongeni…

WABUNGE FULANI: Haki yake apewe.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Naibu Spika, kazi inafanyika ndugu zangu, kazi inafanyika na hii inafanyika bila hiana, watu wanahangaika.

Mheshimiwa Naibu Spika, namkushukuru sana Mheshimiwa Waziri Mkuu kwanza kwa kuwa kiongozi mahiri, anatuongoza vizuri. Naomba niseme kwamba Bunge hili na Serikali inaenda kwa utendaji wako chini ya usimamizi wa Dkt. John Pombe Magufuli na mama Samia Suluhu Hassan. (Vigelegele/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa utaratibu wa kanuni yetu, napenda kuwatambua wote, kwa sababu nikimtaja mmoja mmoja itakuja kuwa sokomoko. Waheshimiwa Wabunge hapa mmechangia vya kutosha katika hoja hii. Hakuna hata mtu mmoja; ndiyo maana nimesema wote kwa sababu utaratibu umewekwa kikanuni, niseme Wabunge wote mmechangia kwa kiwango kikubwa. Kwa hiyo, mmenipa nguvu.

Mheshimia Naibu Spika, naomba niwaambie, ile speed yetu ya mwanzo tuliyokuwa tunafanya, kwa michango yenu, naomba niwaahidi inshaallah kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, speed ile itakuwa mara mbili zaidi kwa mwaka wa fedha unaokuja. Tunafanya hivi ili Wabunge mfurahi na mfurahi wote. Unajua Mbunge ukifurahi, unaondoa stress. Mambo yakienda huko hakuna shida, una uhakika mambo yako yanaenda yametulia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba niwaambie, sisi jukumu letu ni kutengeneza mazingira. Tutawatengenezea mazingira kutekeleza miradi yote kwa wananchi. Ile inayowezekana yote tutaitekeleza kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu. Lile tutakaloshindwa kwa hali ya kibinadamu, basi hatuna namna, lakini kwa dhamira yetu inatuelekeza tufanye kila liwezekanalo kwa ajili ya wananchi wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikubwa zaidi naomba nishukuru familia yangu kwa malezi mazuri sana; na watoto wangu na wake zangu. Siyo kwamba nina wake wanne, yule mtani wangu katania tu, kachomekea. Watoto wangu nawashukuru sana, ni watoto wasikivu sana, wanani- encourage baba yao kufanya kazi, napata spirit kubwa ya kufanya kazi. (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia namshukuru sana mama yangu mzazi Khadija binti Mwalimu, namwombea sana mzazi wangu baba yangu Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema Peponi alipotangulia mbele ya safari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru wananchi wa Kisarawe, wapiga kura wa Kisarawe wamekuwa wakinivumilia hata wakati niko katika michaka michaka. Kwa kweli nawashukuru sana na wengine wapo humu ndani nawaona wapiga kura kule. Nawashukuru sana, wananipa nguvu. Naomba niwahakikishie kwamba commitment yangu kama kiongozi niliyepewa dhamana, ambapo Mheshimiwa Rais amenipa dhamana, lakini Mungu amenipa dhamana hii kuweza kuwatumikia wananchi, nitajitahidi kwa moyo wangu wote na nguvu zangu zote kutimiza wajibu wangu wote unaotakiwa, nikijua wazi mimi ni binadamu, nina maswali mawili; nina swali la duniani na nina swali siku nitakaporudi mbele ya mikono yake. Mungu anisaidie niendelee kutenda wema huo na kuhakikisha naweza kuwahudumia wananchi wote kwa moyo wote.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho zaidi nimshukuru Mheshimiwa Rais tena kwa mara nyingine kwa mapenzi yake, Mheshimiwa Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, lakini niwashukuru Mawaziri wote wakiongozwa na Chief Whip wetu hapa dada yangu Mheshimiwa Jenista Mhagama kwa kazi yao mahiri, dada yangu Mheshimiwa Mhagama halali, hapumziki anafanya kazi kubwa sana, huyu ndiye kiranja wa Mawaziri humu ndani, tunakushuuru sana dada yangu, Mheshimiwa Jenista Mhagama. Pia niwashukuru Wabunge wote, Wabunge wamekuwa wema kwangu wananipa moyo, hongera sana. Mungu awalipe sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, sasa naomba kutoa hoja. (Makofi)